Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Nenda Ukanawe Katika Dimbwi la Siloamu”

“Nenda Ukanawe Katika Dimbwi la Siloamu”

“Nenda Ukanawe Katika Dimbwi la Siloamu”

BAADA ya kumtibu mwanamume fulani kipofu akitumia udongo laini, Yesu alimwambia hivi: “Nenda ukanawe katika dimbwi la Siloamu.” Mwanamume huyo alitii na “akarudi akiwa anaona.” (Yohana 9:6, 7) Dimbwi la Siloamu lilikuwa wapi? Ugunduzi fulani wa vitu vya kale uliofanywa hivi karibuni umefunua mambo mapya kuhusu mahali dimbwi hilo lilipokuwa.

Watalii wengi wametembelea sehemu fulani huko Yerusalemu ambayo inaitwa Dimbwi la Siloamu, wakiamini kwamba hilo ndilo dimbwi linalotajwa katika Yohana 9:7. Sehemu hiyo iko mwishoni mwa mfereji wa Hezekia—mfereji wa maji wenye urefu wa mita 530 uliochimbwa katika karne ya nane K.W.K. Hata hivyo, dimbwi hilo ni la karne ya nne W.K. Lilijengwa na “Wakristo” wa Byzantium waliofikiri kimakosa kwamba dimbwi lililotajwa katika Injili ya Yohana lilikuwa mwishoni mwa mfereji huo.

Hata hivyo, mwaka wa 2004, wataalamu wa vitu vya kale vilivyochimbuliwa, waligundua lile ambalo wamekata kauli kuwa ndilo Dimbwi la Siloamu ambalo lilikuwapo Yesu alipokuwa duniani. Liko mita 100 hivi kusini mashariki ya sehemu ambayo iliaminika kimakosa kuwa Dimbwi la Siloamu. Waligundua dimbwi hilo jinsi gani? Serikali ya jiji ilihitaji kurekebisha bomba la maji machafu katika sehemu hiyo. Hivyo, wakatuma wafanyakazi waliotumia mashine kubwa. Mtaalamu mmoja wa vitu vya kale aliyekuwa karibu, aliwatazama walipokuwa wakichimba na akaona ngazi mbili ardhini. Kazi hiyo ilisimamishwa, nayo Halmashauri ya Vitu vya Kale ya Israel ikatoa kibali cha kuchimbua sehemu hiyo. Tayari upande mmoja wa dimbwi hilo, wenye urefu wa mita 70 hivi, na pembe zake mbili zimechimbuliwa.

Baadhi ya sarafu ambazo zimepatikana wakati wa uchimbuaji huo ni za mwaka wa pili, wa tatu, na wa nne wa uasi wa Wayahudi dhidi ya Roma. Uasi huo ulitukia kati ya mwaka wa 66 na 70  W.K. Sarafu hizo zinathibitisha kwamba dimbwi hilo lilikuwa likitumiwa hata kufikia mwaka wa 70  W.K., Yerusalemu lilipoharibiwa na Waroma. Gazeti moja (Biblical Archaeology Review) linakata kauli hii: “Dimbwi hilo liliendelea kutumiwa mpaka mwishoni mwa uasi huo, na baada ya hapo halikutumiwa tena. Eneo hilo, ambalo ndilo la chini zaidi katika Yerusalemu yote, halikukaliwa tena mpaka wakati wa enzi ya Byzantium. Kila mwaka, mvua ya majira ya baridi kali ilisukuma matope kwenye dimbwi hilo. Na baada ya Waroma kuliharibu jiji hilo, dimbwi hilo halikusafishwa tena kamwe. Kadiri karne zilivyopita ndivyo matope yalivyozidi kurundamana ndani ya dimbwi hilo mpaka likafunikwa kabisa. Wataalamu wa vitu vya kale walifukua sehemu fulani za dimbwi hilo zilizokuwa zimefunikwa na matope kwa kina cha mita 3.”

Kwa nini wanafunzi wanyoofu wa Biblia wanataka kujua Dimbwi la Siloamu lilikuwa wapi? Ni kwa sababu habari hiyo itawasaidia kuelewa vizuri zaidi jinsi eneo la Yerusalemu lilivyokuwa katika karne ya kwanza, jambo ambalo linazungumziwa mara nyingi katika masimulizi ya Injili kuhusu maisha na huduma ya Yesu.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Dimbwi la Siloamu lililogunduliwa hivi majuzi

[Hisani]

© 2003 BiblePlaces.com