Sirakusa Kituo Katika Safari ya Paulo
Sirakusa Kituo Katika Safari ya Paulo
KARIBU mwaka wa 59 W.K., meli fulani ilisafiri kutoka kisiwa cha Malta huko Mediterania kwenda Italia. Meli hiyo ilikuwa na sanamu ya “Wana wa Zeu,” miungu iliyoonwa kuwa walinzi wa mabaharia. Luka, mwandikaji wa Biblia, anasema kwamba meli hiyo iliegeshwa katika “bandari ya Sirakusa” katika pwani ya kusini-mashariki ya Sisili na ‘kukaa hapo siku tatu.’ (Matendo 28:11, 12) Luka, Aristarko, na mtume Paulo, ambaye alikuwa akipelekwa mahakamani huko Roma, walikuwa katika meli hiyo.—Matendo 27:2.
Hatujui ikiwa Paulo aliruhusiwa kutoka ndani ya meli walipokuwa huko Sirakusa. Ikiwa yeye au waandamani wake walishuka, wangeona nini?
Katika enzi za Wagiriki na Waroma, jiji la Sirakusa lilikuwa muhimu karibu kama Athene na Roma. Inaaminika kwamba, lilianzishwa na Wakorintho mwaka wa 734 K.W.K. Sirakusa lilikuwa maarufu pindi fulani na baadhi ya watu mashuhuri sana wa nyakati za zamani kama vile mwandishi wa michezo ya kuigiza Epicharmus na mwanahisabati Archimedes walizaliwa huko. Mwaka wa 212 K.W.K., Waroma walilishinda jiji la Sirakusa.
Ukitembelea jiji la Sirakusa leo huenda ukaelewa jinsi jiji hilo lilivyokuwa katika siku za Paulo. Jiji hilo liligawanywa mara mbili—sehemu moja ilikuwa kisiwa kidogo cha Ortygia, ambapo meli ya Paulo ilitia nanga, na sehemu nyingine ilikuwa bara.
Leo, katika kisiwa hicho utapata mabaki ya hekalu la kale zaidi huko Sisili lililojengwa kwa muundo wa Kigiriki—hekalu la Apolo, la karne ya sita K.W.K. Pia kuna nguzo za hekalu lililowekwa wakfu kwa Athena, ambalo ni la karne ya tano K.W.K., lakini likafanywa kuwa sehemu ya kanisa kuu.
Jiji la kisasa liko barani, ambako unaweza kutembelea uwanja wa akiolojia wa Neapolisi. Jumba la maonyesho la Ugiriki liko karibu na lango la uwanja huo. Jumba hilo la maonyesho ni mojawapo ya majumba bora zaidi ya kale yaliyojengwa kwa muundo wa Kigiriki. Jumba hilo linaloelekea upande wa bahari, lilikuwa na mandhari maridadi sana kwa ajili ya maonyesho. Upande wa kusini wa uwanja huo kuna jumba kuu la maonyesho la Waroma la karne ya tatu W.K. Jumba hilo lina umbo la yai, lina urefu wa mita 140 na upana wa mita 119, nalo ndilo la tatu kwa ukubwa nchini Italia.
Ukipata nafasi ya kutembelea jiji la Sirakusa, unaweza kuketi kwenye ufuo wa bahari huko Ortygia na kufungua Biblia yako kwenye andiko la Matendo 28:12, kisha uwazie mtume Paulo akiwa kwenye meli inayoingia bandarini.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 30]
Malta
Sisili
Sirakusa
ITALIA
Regiamu
Roma
Puteoli
[Picha katika ukurasa wa 30]
Mabaki ya jumba la maonyesho la Kigiriki huko Sirakusa