Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
Kabla ya kupata ujuzi wa ile kweli, mimi na mke wangu tulitamani sana kupata mtoto, hivyo tulitumia mbinu ya kutunga mimba nje ya tumbo la uzazi, yaani, “in vitro fertilization.” Baadhi ya mayai yetu yaliyotungishwa (viini-tete) hayakutumiwa; yaligandishwa na kuhifadhiwa kwenye barafu. Je, ni lazima yaendelee kuhifadhiwa au yanaweza kuharibiwa?
Jambo hili ni mojawapo ya mambo mazito ya kimaadili ambayo wenzi wa ndoa wanakabili wanapochagua kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi. Kila wenzi wa ndoa wanawajibika mbele za Yehova kuhusu uamuzi watakaofanya. Hata hivyo, inaweza kuwa rahisi kufanya uamuzi wakifahamu mambo fulani kuhusu mbinu hiyo isiyo ya asili ya kutungisha mimba.
Mwaka wa 1978, mwanamke mmoja huko Uingereza alikuwa wa kwanza kubeba mimba iliyotungiwa kwenye maabara. Hangepata mimba kwa sababu mirija yake ya uzazi ilikuwa imeziba, hivyo shahawa hazingeweza kufikia mayai yake ya uzazi. Wataalamu wa kitiba walimfanyia upasuaji na kuchukua mayai yake yaliyokomaa, wakayatia katika bakuli la kioo, kisha wakayaunganisha na shahawa za mume wake. Kiini-tete kilichotokezwa kilitiwa ndani ya virutubishi ili kikue, kisha kikapandikizwa kwenye tumbo lake la uzazi. Baadaye, mwanamke huyo alijifungua mtoto msichana. Mbinu hiyo, na mbinu nyingine za aina hiyo zinaitwa katika Kiingereza in vitro fertilization (IVF), yaani, kutunga mimba nje ya tumbo la uzazi katika bakuli la kioo (vitro).
Ingawa mbinu hiyo huwa tofauti katika nchi mbalimbali, kwa ujumla inahusisha mambo yafuatayo: Kwa majuma kadhaa, mke hupewa vidonge vya kuchochea vifuko vyake vya mayai (ovari) vitokeze mayai mengi. Huenda mume akaambiwa apige punyeto ili shahawa zitoke. Mayai na shahawa zilizosafishwa huunganishwa katika maabara. Mayai mengi yanaweza kutungishwa mimba na kuanza kugawanyika, kisha yanakuwa viini-tete vya kibinadamu. Baada ya siku moja hivi, viini-tete hivyo hukaguliwa kwa makini ili kutenganisha vile ambavyo vina kasoro na vile ambavyo vinaonekana havina kasoro na ambavyo vinaweza kujipandikiza katika tumbo la uzazi na kukua. Baada ya siku tatu hivi, kwa kawaida viini-tete viwili au vitatu vilivyo bora kabisa huingizwa ndani ya tumbo la uzazi la mke ili kuwe na uwezekano mkubwa zaidi wa kubeba mimba. Ikiwa kiini-tete kimoja au viwili vitajipandikiza katika tumbo la uzazi, basi, yeye ni mjamzito, na inatarajiwa kwamba atajifungua wakati ukifika.
Lakini namna gani viini-tete vinavyobaki, kutia ndani vile vilivyoonekana kuwa vina kasoro au dhaifu? Viini-tete hivyo vya ziada vikiachwa, havitaendelea * Au huenda mwenzi mmoja au wote wawili wakafa ama kuoa au kuolewa na mtu mwingine na hivyo kufanya hali iwe ngumu. Naam, kuna mambo mengi ya kuhangaikia, na hivyo wenzi fulani wa ndoa huendelea kugharimia hifadhi ya viini-tete kwa miaka mingi.
kuwa hai. Kwa hiyo, kabla havijafa, viini-tete hivyo vya ziada vinaweza kugandishwa katika umajimaji wa nitrojeni. Kwa nini? Endapo jaribio la kwanza la IVF halitafaulu, baadhi ya viini-tete hivyo vilivyohifadhiwa vinaweza kutumiwa katika jaribio lingine la IVF kwa bei nafuu. Hata hivyo, jambo hilo linatokeza masuala ya kimaadili. Kama wale wenzi wa ndoa waliouliza swali lililo mwanzoni, wengi hushindwa kuamua watafanyaje na viini-tete vyao vilivyogandishwa. Huenda hawahitaji watoto zaidi. Labda umri wa wazazi hao umesonga sana au hawawezi kugharimia jaribio lingine kama hilo la kupata mtoto. Huenda wanaogopa hatari zinazohusiana na kupata mimba za mapacha.Katika mwaka wa 2008, mtaalamu mmoja mkuu wa masuala ya viini-tete alisema katika gazeti la The New York Times kwamba wazazi wengi hawajui wafanye nini na viini-tete vilivyobaki. Makala hiyo ilisema hivi: “Angalau viini-tete 400,000 vinahifadhiwa katika kliniki nchini kote, na idadi hiyo inazidi kuongezeka kila siku . . . Viini-tete vinaweza kubaki hai kwa miaka kumi au zaidi ikiwa vitagandishwa vizuri lakini si vyote huendelea kuwa hai vinapoondolewa kwenye barafu.” (Italiki ni zetu.) Jambo hilo linafanya Wakristo watue kidogo na kufikiria. Kwa nini?
Wenzi wa ndoa Wakristo wanaokabili masuala yanayohusu mbinu za IVF wanaweza kufikiria athari za hali nyingine ya kitiba. Huenda Mkristo akalazimika kuamua hatua ya kuchukua kuhusu mpendwa wake aliye mahututi na anayeishi kwa msaada wa mashine ya kutegemeza uhai, kama ile ya kumsaidia mgonjwa kupumua. Wakristo wa kweli hawaungi mkono wazo la kumwacha mgonjwa afe bila kutibiwa; wanathamini sana uhai kulingana na Kutoka 20:13 na Zaburi 36:9. Gazeti la Amkeni! la Kiingereza la Mei 8, 1974, lilisema hivi: “Kwa kuwa wanaheshimu maoni ya Mungu kuhusu utakatifu wa uhai, na kwa sababu ya dhamiri zao na kwa kuwa wanatii sheria za serikali, wale wanaotaka kuishi kupatana na kanuni za Biblia hawawezi kamwe kuruhusu madaktari waharakishe kifo cha mgonjwa asiyepona,” yaani, wakomeshe kimakusudi uhai wake. Hata hivyo, katika hali fulani uhai wa mgonjwa unategemezwa tu na mashine. Ni lazima watu wa familia waamue kama mgonjwa huyo atabaki katika mashine hiyo au la.
Ni kweli kwamba hali hiyo haifanani na hali inayowakabili wenzi wa ndoa waliotumia mbinu ya IVF na ambao sasa wamehifadhi viini-tete. Lakini huenda wakapendekezewa waondoe viini-tete vilivyohifadhiwa katika nitrojeni, na kuviacha vife. Bila kugandishwa, viini-tete vinaweza kudhoofika na kufa. Wenzi hao wa ndoa watalazimika kuamua kama wataruhusu jambo hilo.—Gal. 6:7.
Kwa kuwa wenzi wa ndoa waliamua wenyewe kutumia mbinu ya IVF kupata mimba ili hatimaye wapate mtoto, huenda wakaamua kuendelea kulipia gharama ya kuhifadhi viini-tete vilivyogandishwa au kuvitumia baadaye kujaribu tena kupata mtoto. Hata hivyo, wenzi wengine wa ndoa huenda wakaamua kwamba wataacha kuvitunza viini-tete vilivyogandishwa, wakiona kuwa viko hai tu kwa sababu vimehifadhiwa kwa njia isiyo ya asili. Wakristo wanaokabili uamuzi huo wanawajibika mbele za Mungu kutumia dhamiri yao iliyozoezwa na Biblia. Wangependa kuwa na dhamiri safi, bila kupuuza dhamiri za wengine.—1 Tim. 1:19.
Wakristo wanaokabili uamuzi huo wanawajibika mbele za Mungu kutumia dhamiri yao iliyozoezwa na Biblia
Mtaalamu mmoja wa tezi za homoni za uzazi aligundua kwamba wenzi wengi wa ndoa “walichanganyikiwa na pia kuathiriwa sana na daraka la kuamua jinsi watakavyoshughulikia viini-tete vyao [vilivyogandishwa].” Alifikia mkataa huu: “Kwa wenzi wengi wa ndoa, inaonekana kwamba hakuna uamuzi mzuri.”
Ni wazi kwamba Wakristo wa kweli wanaofikiria kutumia mbinu ya IVF wanapaswa kuchanganua mambo yote mazito yanayohusiana na mbinu hiyo. Biblia inashauri hivi: “Mtu mwerevu huona hatari na kujificha, lakini wajinga wanaendelea mbele na kuumia.”—Met. 22:3, NET Bible.
Mwanamume na mwanamke ambao hawajafunga ndoa na wanaojifunza Biblia wanataka kubatizwa, lakini hawawezi kuhalalisha muungano wao kwa sababu mwanamume anaishi nchini kinyume cha sheria. Serikali hairuhusu mgeni anayeishi nchini kinyume cha sheria afunge ndoa. Je, wanaweza kutia sahihi Kiapo cha Uaminifu na kisha kubatizwa?
Huenda kufanya hivyo kukaonekana kuwa ni suluhisho, lakini si njia ya Kimaandiko ya kutatua tatizo lao. Ili tujue sababu, acheni kwanza tufikirie kusudi la Kiapo cha Uaminifu, kwa nini kiapo hicho kipo, na kinaweza kutumika kwa njia gani na wakati gani.
Kiapo hicho ni hati iliyoandikwa ambayo inatiwa sahihi na wenzi wasioweza kufunga ndoa kwa sababu inayotajwa hapa mbele. Wenzi hao hufanya hivyo mbele ya mashahidi. Katika hati hiyo, wanaapa kwamba watakuwa waaminifu katika ndoa yao na kuhalalisha muungano wao ikiwezekana. Kutaniko litaona kwamba wameapa mbele za Mungu na wanadamu kuwa waaminifu katika uhusiano wao na hivyo ni kana kwamba muungano wao umehalalishwa na wenye mamlaka.
Kiapo cha Uaminifu kinatumiwa lini na kwa nini? Yehova alianzisha ndoa na anaithamini sana. Mwana wake alisema hivi: “Kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.” (Mt. 19:5, 6; Mwa. 2:22-24) Yesu aliongeza hivi: “Mtu yeyote anayemtaliki mke wake na kumwoa mwingine, ila kwa sababu ya uasherati [mwenendo mpotovu kingono], anafanya uzinzi.” (Mt. 19:9) Kwa hiyo “uasherati,” yaani, mwenendo mpotovu kingono, ndio msingi pekee wa Kimaandiko wa talaka. Kwa mfano, ikiwa mwanamume anafanya ngono nje ya ndoa, mke wake asiye na hatia anaweza kuamua kumtaliki au kutomtaliki mume wake. Akimtaliki, basi anakuwa huru kuolewa tena.
Hata hivyo, katika nchi fulani, hasa miaka ya zamani, makanisa yenye uvutano mkubwa hayakukubali maagizo hayo ya Biblia yaliyo wazi. Badala yake, yalifundisha kwamba talaka haiwezi kuruhusiwa kwa sababu yoyote. Kwa hiyo, katika sehemu fulani ambazo kanisa lilikuwa na uvutano mkubwa, sheria za serikali haziruhusu talaka, hata kwa msingi halali ambao Yesu alitaja. Katika nchi nyingine, mpango wa talaka upo, lakini utaratibu wa kuipata ni mrefu sana, haueleweki, na una masharti mengi. Huenda ikachukua miaka mingi sana kabla ya kupata talaka. Ni kana kwamba kanisa au serikali ‘inazuia’ kile ambacho Mungu anakubali.—Mdo. 11:17.
Kwa mfano, huenda wenzi wa ndoa wakaishi katika nchi ambayo haiwezekani au ni vigumu sana kupata talaka, au labda inachukua miaka mingi ili talaka iwe halali. Ikiwa wamejitahidi kadiri wawezavyo kukatisha ndoa yao ya awali iliyokuwa halali na wanastahili machoni pa Mungu kufunga ndoa, wanaweza kutia sahihi Kiapo cha Uaminifu. Huo ni mpango wa rehema wa kutaniko la Kikristo katika nchi kama hizo. Hata hivyo, hautatumiwa katika nchi ambazo mtu anaweza kupata talaka, hata ikiwa ni ghali au ni vigumu sana kupata talaka.
Kwa kuwa hawaelewi maana ya Kiapo cha Uaminifu, watu fulani wanaoishi katika nchi ambazo zinaruhusu talaka, wameuliza ikiwa wanaweza kutia sahihi hati hiyo ili waepuke matatizo au usumbufu.
Katika kisa kilichozungumziwa mwanzoni, mwanamume na mwanamke wanaoishi pamoja katika njia isiyo ya kiadili wanataka kufunga ndoa. Kila mmoja wao yuko huru Kimaandiko; wote hawajafungwa na mwenzi wa zamani. Hata hivyo, mwanamume anaishi nchini kinyume cha sheria, na serikali haiwezi kumruhusu mgeni anayeishi nchini kinyume cha sheria afunge ndoa. (Katika nchi nyingi serikali inaweza kuruhusu ndoa hata kama mmoja wao au wote wawili hawaishi kihalali nchini.) Katika kisa tunachozungumzia, nchi inaruhusu talaka. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kutia sahihi Kiapo cha Uaminifu. Kumbuka wenzi hao si kwamba yeyote kati yao alihitaji kumtaliki mwenzi wa zamani, bali wanazuiwa kuoana. Wote wawili wako huru kufunga ndoa. Lakini kwa kuwa mwanamume huyo anaishi kinyume cha sheria nchini, watawezaje kufunga ndoa? Huenda wakahitaji kwenda nchi nyingine ambayo inamruhusu mwanamume huyo kufunga ndoa. Au huenda ikawezekana kufunga ndoa katika nchi wanamoishi kwa sasa ikiwa mwanamume atachukua hatua za kuhalalisha hati zake za kuishi nchini.
Naam, wenzi hao wanaweza kupatanisha maisha yao na viwango vya Mungu na sheria ya Kaisari. (Marko 12:17; Rom. 13:1) Inatazamiwa kwamba watafanya hivyo. Kisha, wanaweza kustahili kubatizwa.—Ebr. 13:4.
^ fu. 6 Namna gani ikiwa kijusi kinachokua tumboni kinaonekana kuwa na kasoro au viini-tete kadhaa vimepandikizwa tumboni? Kuua vijusi hivyo kimakusudi ni kutoa mimba. Ni jambo la kawaida kupata mimba za mapacha (wawili, watatu, au zaidi) unapotumia mbinu ya IVF, na hilo huongeza hatari kama vile mama kujifungua kabla ya wakati na kuvuja damu nyingi. Mwanamke aliyebeba vijusi vingi tumboni anaweza kuambiwa “achague vijusi vinavyofaa,” ili kijusi kimoja au kadhaa viuawe. Huo utakuwa utoaji mimba wa kukusudia, ambao ni sawa na kuua.—Kut. 21:22, 23; Zab. 139:16.