Je, Kweli Gharika ya Noa Ilikuwa Duniani Pote?
Wasomaji Wetu Wanauliza
Je, Kweli Gharika ya Noa Ilikuwa Duniani Pote?
Gharika ya Noa ilitukia miaka zaidi ya 4,000 iliyopita. Kwa hiyo, hakuna watu walioiona walio hai duniani leo wanaoweza kutueleza kuihusu. Hata hivyo, kuna rekodi iliyoandikwa kuhusu msiba huo, inayoonyesha kwamba maji ya mafuriko yalifunika mlima mrefu zaidi wakati huo.
Rekodi hiyo ya kihistoria inasema hivi: “Gharika ikaendelea siku 40 juu ya dunia . . . Maji yakazidi mno duniani hivi kwamba milima yote mirefu ambayo ilikuwa chini ya mbingu zote ikafunikwa. Maji yakaizidi mno milima hiyo kufikia kiasi cha mikono kumi na mitano [mita 6.5 hivi], kisha ikafunikwa.”—Mwanzo 7:17-20.
Huenda watu fulani wakajiuliza ikiwa simulizi kuhusu kufunikwa kwa dunia yote na maji ni hekaya tu au limetiliwa chumvi. Sivyo ilivyo! Kwa kweli, kwa kiwango fulani bado dunia imefurikwa. Maji ya bahari yamefunika asilimia 71 hivi ya uso wa dunia. Hivyo, kwa kweli maji ya gharika yangalipo. Na ikiwa miamba yote ya barafu ingeyeyuka, maji ya bahari yangeongezeka na kufunika majiji kama vile New York na Tokyo.
Wanajiolojia wanaochunguza eneo la kaskazini-magharibi mwa Marekani wanaamini kwamba mafuriko 100 hivi yenye kuharibu yamewahi kukumba eneo hilo. Inasemekana kwamba furiko moja lilipita juu ya eneo hilo likiwa kama ukuta wa maji wenye kimo cha mita 600, likisafiri kwa mwendo wa kilomita 105 kwa saa—furiko la maji lenye uzito wa zaidi ya tani trilioni mbili. Ugunduzi mbalimbali kama huo umefanya wanasayansi wengine waamini kwamba kuna uwezekano gharika ilikuwa duniani pote.
Hata hivyo, wale wanaoamini Biblia kuwa Neno la Mungu, hawaamini tu kwamba kuna uwezekano kulikuwa na gharika duniani pote. Wanaamini hilo ni tukio halisi. Yesu alimwambia Mungu hivi: “Neno lako ni kweli.” (Yohana 17:17) Mtume Paulo aliandika kwamba mapenzi ya Mungu ni kwamba “watu wa namna zote waokolewe na kupata ujuzi sahihi wa kweli.” (1 Timotheo 2:3, 4) Paulo angeweza jinsi gani kuwafundisha wafuasi wa Yesu kweli kumhusu Mungu na makusudi yake ikiwa Neno la Mungu lina hekaya?
Zaidi ya kuamini kwamba kulikuwa na Gharika, Yesu aliamini kwamba ilikuwa duniani pote. Katika unabii wake mkubwa kuhusu kuwapo kwake na mwisho wa mfumo huu wa mambo, alilinganisha matukio hayo na ya wakati wa Noa. (Mathayo 24:37-39) Pia mtume Petro aliandika hivi kuhusu mafuriko ya siku za Noa: “Kwa njia hizo ulimwengu wa wakati huo uliangamia kwa gharika ya maji.”—2 Petro 3:6.
Ikiwa Noa alikuwa mtu wa kuwaziwa na gharika ya duniani pote ni hadithi tu, maonyo ya Petro na ya Yesu kwa wale wanaoishi katika siku za mwisho hayangekuwa na maana yoyote. Badala ya kuwa maonyo, mawazo hayo yangepotosha uelewaji wa mtu kuhusu maonyo ya Biblia na kumfanya asiokoke dhiki iliyo kubwa kuliko ile Gharika ya Noa.—2 Petro 3:1-7.
Akizungumza kuhusu kuendelea kuwaonyesha watu wake rehema, Mungu alisema: “Kama vile ambavyo nimeapa kwamba maji ya Noa hayatapita tena juu ya dunia, vivyo hivyo nimeapa kwamba sitakuwa na ghadhabu tena kukuelekea wewe wala kukukemea.” Kama vile Gharika ya Noa ilivyoifunika dunia, ndivyo fadhili za Mungu zenye upendo zitakavyowafunika wale wanaomtumaini.—Isaya 54:9.