Mpendwa Anapokufa
Mpendwa Anapokufa
Jumanne (Siku ya 2), Julai 17, 2007 (17/7/2007), karibu saa moja jioni, ndege ya abiria iliteleza kwenye uwanja wa ndege wa Brazili wenye shughuli nyingi zaidi huko São Paulo. Ndege hiyo ilivuka barabara yenye shughuli nyingi na kugonga depo ya mizigo. Watu 200 hivi walikufa katika aksidenti hiyo.
TUKIO hilo linalosemekana kuwa msiba mbaya zaidi wa ndege nchini Brazili halitawahi kusahauliwa na wale waliowapoteza wapendwa wao. Mmoja wao ni Claudete. Alikuwa akitazama TV aliposikia habari kuhusu aksidenti hiyo ya ndege. Mwana wake, Renato, alikuwa ndani ya ndege hiyo. Alikuwa na umri wa miaka 26 tu. Alikuwa akipanga kufunga ndoa mnamo Oktoba (Mwezi wa 10). Claudete alijaribu juu chini kuwasiliana naye kwenye simu ya mkononi, lakini hakufaulu. Alianguka kwenye sakafu na kulia sana.
Antje alimpoteza mchumba wake katika aksidenti mbaya ya gari mnamo Januari (Mwezi wa 1) 1986. Aliposikia habari hizo, alipatwa na mshtuko wa akili. “Kwanza sikuamini. Nilihisi kana kwamba ni ndoto mbaya na ningeamka na kukuta mambo yako tofauti. Nilitetemeka na kuhisi uchungu mbaya ni kama mtu alikuwa amenigonga tumboni.” Antje alipatwa na mshuko wa moyo kwa miaka mitatu iliyofuata. Ingawa zaidi ya miaka 20 imepita tangu aksidenti hiyo, bado anatetemeka anapokumbuka yaliyotokea.
Hatuwezi kueleza hisia za mshtuko, kutokuamini, na kupoteza tumaini zinazoweza kuletwa na misiba mibaya kama hiyo isiyotarajiwa. Hata hivyo, hata tunapotarajia kwamba mpendwa atakufa, kama vile kutokana na ugonjwa wa muda mrefu, bado huzuni inaweza kuwa nyingi sana jambo hilo linapotendeka. Hakuna mtu ambaye huwa tayari kabisa kwa ajili ya kifo cha mpendwa. Mama ya Nanci alikufa mnamo 2002 baada ya ugonjwa wa muda mrefu. Hata hivyo, siku ambayo mama yake alikufa, Nanci aliketi kwenye sakafu ya hospitali akiwa katika hali ya mshtuko. Kwake ni kana kwamba maisha yalipoteza maana. Miaka mitano imepita, lakini bado analia anapofikiri kumhusu mama yake.
“Uchungu wa kumpoteza mpendwa hautoweki kabisa, watu huzoea tu kwamba mpendwa wao hayupo,” akasema Dakt. Holly G. Prigerson. Ikiwa umempoteza mpendwa katika kifo, iwe ni bila kutarajia au la, huenda ukajiuliza: ‘Je, ni kawaida kuomboleza? Mtu anaweza kukabiliana na kumpoteza mpendwa wake jinsi gani? Je, nitawahi kumwona tena mpendwa wangu?’ Habari inayofuata itajibu maswali haya na mengine ambayo huenda ukajiuliza.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
EVERTON DE FREITAS/AFP/Getty Images