Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Kwa nini Yuda alipewa vipande 30 vya fedha ili amsaliti Yesu?

Yuda Iskariote alipokutana na wakuu wa makuhani ili aone wangempa pesa ngapi ili amsaliti Yesu, walimwambia “vipande 30 vya fedha.” (Mathayo 26:14, 15) Kiasi hicho kinaonyesha jinsi walivyomchukia na kumdharau Yesu.

Huenda sarafu walizotumia zilikuwa shekeli za fedha, pesa za kawaida zilizotumiwa na Wayahudi. Mtu angeweza kununua nini kwa shekeli 30? Sheria ya Musa ilisema kwamba hiyo ndiyo iliyopaswa kuwa bei ya mtumwa. Pia, shekeli 30 zingeweza kununua shamba.—Kutoka 21:32; Mathayo 27:6, 7.

Nabii Zekaria alipoomba mshahara wake kutoka kwa Waisraeli wasio waaminifu kwa ajili ya kazi yake ya kuwachunga watu wa Mungu, walimpa “vipande 30 vya fedha.” Walifanya hivyo kimakusudi ili kumfedhehesha nabii wa Mungu, wakionyesha kwamba walimwona kama mtumwa. Hivyo, Yehova akamwagiza Zekaria hivi: “Utupe ndani ya hazina—thamani tukufu ambayo nimekadiriwa kwa maoni yao.” (Zekaria 11:12, 13) Jambo ambalo Zekaria alifanya kwa kutii amri hiyo, linatukumbusha jambo ambalo Yuda angefanya kwa pesa alizopata kwa kumsaliti Yule ambaye Yehova alikuwa amemchagua awe mchungaji wa Israeli.—Mathayo 27:5.

“Cheti cha talaka” kinachotajwa katika Biblia ni nini?

Sheria Musa ilisema: “Mwanamume akimchukua mwanamke . . . awe mke wake, pia itatukia kwamba ikiwa hatapata kibali machoni pake kwa sababu amepata kitu fulani kisichofaa katika mwanamke huyo, atamwandikia pia cheti cha talaka na kukitia mkononi mwake na kumfukuza kutoka katika nyumba yake.” (Kumbukumbu la Torati 24:1) Ni nini lililokuwa kusudi la hati hii? Maandiko hayaelezi kilichoandikwa kwenye cheti kama hicho, hata hivyo, hati hiyo ingelinda haki na masilahi ya mwanamke huyo aliyekataliwa.

Katika miaka ya 1951-1952, vitu fulani vya kale vilipatikana katika mapango kwenye upande wa kaskazini wa Wadi Murabbaat, mto uliokauka katika jangwa la Yudea. Kati ya hati nyingi zilizopatikana hapo kulikuwa na cheti cha talaka kilichoandikwa katika Kiaramu na kinachosemekana kuwa cha 71 au 72 W.K. Kilisema mambo yaliyotukia kwenye siku ya kwanza ya mwezi wa Marheshvan, katika mwaka wa sita wa maasi ya Wayahudi dhidi ya Waroma. Yosefu, mwana wa Naqsan, aliyekuwa akiishi huko Masada, alimtaliki Miriamu, binti ya Yonathani kutoka Hanablata. Baada ya hapo, Miriamu angeweza kuolewa na mwanamume yeyote Myahudi ambaye angetaka. Yosefu alirudisha mahari ya Miriamu na kumlipa mara nne kwa ajili ya bidhaa zozote zilizokuwa zimeharibiwa. Cheti hicho kilitiwa sahihi na Yosefu mwenyewe na mashahidi watatu, Eliezeri, mwana wa Malka; Yosefu, mwana wa Malka; na Eliezeri, mwana wa Hanana.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mapango huko Wadi Murabbaat

[Picha katika ukurasa wa 25]

Cheti cha talaka cha mwaka wa 71/72 W.K.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Caves: Todd Bolen/Bible Places.com; certificate: Clara Amit, Courtesy of the Israel Antiquities Authority