“Ukifika Kwenye Mto Coco, Nenda Upande wa Kulia”
Barua Kutoka Nikaragua
“Ukifika Kwenye Mto Coco, Nenda Upande wa Kulia”
“UTAHITAJI gari linaloendeshwa kwa magurudumu manne, chuma cha kuinulia gari, na vibuyu vya ziada vya mafuta. Jitayarishe kukabiliana na matope mengi. Ukifika kwenye Mto Coco, nenda upande wa kulia.”
Maneno hayo niliyoambiwa na mmishonari mwenzangu hayakunipa ujasiri. Hata hivyo, Jumanne (Siku ya 2) moja asubuhi, nilianza safari yangu ya kuhudhuria kusanyiko la Kikristo huko Wamblán, mji mdogo ulio kaskazini mwa Nikaragua.
Nilianza safari asubuhi na mapema, nikiendesha gari langu lililozeeka lakini lenye nguvu katika Barabara Kuu ya Pan-American. Nilipofika Jinotega, nilifuata barabara ya udongo ambayo wenyeji waliiita feo, au sura mbaya. Kabla ya kuuacha mji huo, niliona maduka mawili. Jina la duka moja lilikuwa Muujiza wa Mungu, na lile lingine liliitwa, Ufufuo.
Barabara hiyo ilijipinda-pinda, ikapanda na kushuka. Niliendesha polepole kupitia mashimo mengi makubwa. Barabara hiyo ilipitia kando ya ziwa lililokuwa katika bonde lililo kwenye mlima mrefu. Kupitia ukungu, niliona miti kando ya barabara iliyofunikwa na okidi na kuvumwani ya Kihispania.
Nilipopiga kona moja kali, nilikuwa karibu kugonga basi lililokuwa likiendeshwa katikati ya barabara. Lilikuwa likitoa moshi mweusi, na magurudumu yake yalikuwa yakirusha mawe kandokando. Nchini Nikaragua, ni kawaida kuona kioo cha mbele cha basi kikiwa kimeandikwa majina ya utani ya madereva wakaidi kama vile: Mshindi, Nge, Chatu, au Mwindaji.
Kufikia adhuhuri nilikuwa nikivuka Nchi Tambarare ya Pantasma. Hapo nilipita nyumba ya mbao ambayo eneo lake la nje lilikuwa limefagiliwa. Kulikuwa na mwanamume mzee aliyeketi kwenye benchi, mbwa alikuwa amelala chini ya mti, na fahali wawili waliokuwa wamefungwa nira kwenye kigari chenye magurudumu ya mbao. Katika mji mmoja mdogo, niliona kikundi cha watoto wakitoka shuleni. Sare zao za rangi ya bluu ziliwafanya waonekane kama wimbi la bahari likiruka kwenye ufuo.
Jua lilikuwa kali nilipokaribia mji wa Wiwilí na niliona Mto Coco kwa mara ya kwanza. Mto huo mkubwa ulipita katika sehemu nyingi za mji huo, ukitiririka kwa kishindo. Nilikumbuka maagizo niliyopewa na hivyo nikaelekea upande wa kulia na kufuata barabara iliyotisha yenye urefu wa kilomita 37 hivi kuelekea Wamblán.
Niliendesha gari langu juu ya mawe na mashimo na kupitia kwenye vijito vinane au tisa. Nilipojaribu kuepuka mashimo katika matope yaliyokauka, nilifaulu kutifua vumbi. Ndiyo, “nilikula
vumbi,” kama wenyeji wanavyosema. Hatimaye, nilifika mwisho wa safari yangu, na mbele yangu kwenye bonde lililo na miti mingi niliona Wamblán.Kufikia saa 10:30 alfajiri siku iliyofuata, karibu kila mtu alikuwa ameamka. Kwa kuwa niliamshwa mapema zaidi na jogoo waliokuwa wakiwika bila kuacha, niliamka na kutembea kupitia barabara kuu. Harufu ya chapati za Kimexico zilizokuwa zikiokwa na meko ya mawe ilijaa hewani.
Kulikuwa na mandhari za rangi mbalimbali za kiparadiso zilizochorwa ukutani. Ishara kwenye maduka kwenye kona za barabara au pulpería, zilitangaza soda mbalimbali. Mabango yaliwakumbusha watu kuhusu ahadi za serikali tatu zilizopita. Kulikuwa na vyoo vilivyojengwa kwa mabati juu ya sakafu ya saruji.
Niliwasalimu watu kwa salamu ya Nikaragua Adiós. Watu walitabasamu na kuzungumza nami kwa uchangamfu. Tulizungumza huku kukiwa na kelele za farasi na nyumbu waliokuwa wakipita.
Kufikia Ijumaa (Siku ya 5) jioni, familia ziliwasili kwa ajili ya kusanyiko la siku mbili. Walitembea, wengine wakaja kwa farasi, na malori. Baadhi ya wavulana na wasichana wadogo walikuwa wametembea kwa saa sita wakiwa wamevalia viatu vya plastiki. Ingawa kulikuwa na mabomu ya chini ya ardhi kwenye vivukio vya mto, wao walivuka na kwa ujasiri wakapita ndani ya maji matulivu yenye ruba. Wengine kutoka maeneo ya mbali walibeba chakula kidogo tu—wali uliotiwa mafuta ya nguruwe. Walikuwa wamekuja kufanya nini?
Walikuwa wamekuja kuimarisha tumaini lao la wakati ujao mzuri. Walikuwa wamekuja kusikia Biblia ikifafanuliwa. Walikuwa wamekuja kumpendeza Mungu.
Jumamosi (Siku ya Posho) ikafika. Wasikilizaji zaidi ya 300 waliketi chini ya paa la mabati kwenye benchi za mbao na viti vya plastiki. Akina mama waliwalisha watoto wao. Nguruwe walipiga kelele na jogoo waliwika katika shamba la jirani.
Kulikuwa na joto kali na baada ya muda ilikuwa vigumu kulistahimili. Hata hivyo, wasikilizaji walikuwa makini kusikia mashauri na mwongozo uliotolewa. Walifuatana na wasemaji waliposoma maandiko ya Biblia, waliimba nyimbo zinazotegemea Biblia, na wakasikiliza kwa heshima sala zilizokuwa zikitolewa kwa ajili yao.
Baada ya programu, nilijiunga na baadhi yao na nikacheza na watoto. Kisha tukapitia mambo ambayo watoto hao walikuwa wameandika. Niliwaonyesha picha za nyota na magalaksi kwenye kompyuta yangu. Watoto hao walitabasamu na wazazi wao walifurahi.
Kusanyiko hilo lilikwisha haraka sana na kila mtu alihitaji kurudi nyumbani. Niliondoka asubuhi iliyofuata, akili yangu ikiwa imejaa kumbukumbu zenye kupendeza na moyo wangu ukiwa umejaa upendo kwa ajili ya marafiki hao wapya. Nimeazimia kuwaiga na kujifunza jinsi ya kuridhika na kumngojea Mungu.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Familia zilisafiri kilomita nyingi sana ili kuhudhuria kusanyiko huko Wamblán