Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Korintho “Jiji Linalomiliki Bandari Mbili”

Korintho “Jiji Linalomiliki Bandari Mbili”

Korintho “Jiji Linalomiliki Bandari Mbili”

UNAPOTAZAMA ramani ya Ugiriki, utaona kwamba sehemu kuu ya nchi hiyo ni rasi na sehemu ya kusini inaonekana kama kisiwa kikubwa. Sehemu hizo zimeunganishwa na sehemu nyembamba ya nchi yenye upana wa kilomita sita kwenye sehemu yake nyembamba zaidi. Eneo hilo linailoitwa Shingo ya Nchi ya Korintho linaunganisha rasi ya Peloponesia iliyo upande wa kusini na sehemu kuu ya nchi upande wa kaskazini.

Shingo hiyo ya nchi ni muhimu kwa sababu nyingine. Imeitwa daraja la bahari kwa sababu upande wake wa mashariki kuna Ghuba ya Saroniki, inayoelekea kwenye Bahari ya Aegea na sehemu ya mashariki ya Bahari ya Mediterania, na kwenye upande wa magharibi kuna Ghuba ya Korintho, inayoelekea kwenye Bahari ya Ionia, Bahari ya Adriatiki, na sehemu ya magharibi ya Bahari ya Mediterania. Katikati ya eneo hili kuna jiji la Korintho, lililokuwa kituo muhimu wakati wa safari za umishonari za Paulo, na ambalo zamani lilijulikana sana kwa ufanisi, anasa, na upotovu wa maadili.

Jiji Lililo Mahali Panapofaa

Jiji la Korintho liko karibu na ncha ya magharibi ya eneo hilo muhimu. Lina bandari mbili, bandari ya Lechaeum upande wa magharibi na bandari ya Kenkrea upande wa mashariki. Kwa sababu hiyo, mwanajiografia Mgiriki Strabo alifafanua Korintho kuwa “jiji linalomiliki bandari mbili.” Kwa sababu ya kuwa mahali panapofaa, jiji la Korintho lilidhibiti njia za biashara za kimataifa. Lilidhibiti njia za kibiashara za juu ya ardhi kutoka kaskazini hadi kusini na njia za biashara za baharini kutoka mashariki hadi magharibi.

Tangu zamani, meli kutoka mashariki (Asia Ndogo, Siria, Foinike, na Misri) na magharibi (Italia na Hispania) zilikuja zikiwa na mizigo, zikapakuliwa kwenye bandari moja na kusafirishwa kilomita chache juu ya ardhi hadi upande wa pili wa shingo hiyo ya nchi. Mizigo hiyo ilipakiwa kwenye meli nyingine na kuendelea na safari. Mashua ndogo zilivutwa kuvuka shingo hiyo ya nchi kupitia njia iliyoitwa diolkos.—Ona  sanduku kwenye ukurasa wa 27.

Kwa nini mabaharia walipenda kutumia njia hiyo ya kuvuka juu ya ardhi? Kwa sababu hilo liliwafanya waepuke safari ya kilomita 320 katika bahari iliyochafuka kwa sababu ya dhoruba zilizotokea kwenye eneo la Peloponesia ya kusini. Mabaharia waliepuka hasa Rasi ya Malea, ambayo ilisemwa hivi kuihusu: “Zunguka Rasi ya Malea na usahau nyumbani.”

Kenkrea—Bandari Iliyozama Yafunuliwa

Bandari ya Kenkrea, iliyoko kilomita 11 mashariki ya Korintho, ilikuwa ndiyo bandari iliyotumiwa na meli zilizotoka Asia. Leo, nusu ya bandari hiyo iko chini ya maji kwa sababu ya tetemeko la nchi lililokumba eneo hilo mwishoni mwa karne ya nne W.K. Strabo alifafanua Kenkrea kuwa bandari yenye shughuli na utajiri mwingi, na mwanafalsafa Mroma Lucius Apuleius aliiita “eneo maarufu na lenye fahari linalotembelewa na meli za mataifa mengi.”

Katika nyakati za Waroma, bandari hiyo ilikuwa na gati mbili zilizoingia baharini kama kiatu cha farasi, na hivyo eneo la kuingia likawa na upana wa mita 150 hadi 200. Meli zenye urefu wa mita 40 zingeweza kutia nanga katika bandari hiyo. Uchimbuaji katika upande wa kusini-magharibi umefunua sehemu za hekalu linalofikiriwa kuwa la mungu wa kike Isisi. Majengo mengine mengi kwenye mwisho mwingine wa bandari hiyo yanaonekana kuwa kama hekalu la mungu wa kike Afrodito. Ilisemwa kwamba miungu hiyo miwili iliwalinda mabaharia.

Huenda shughuli za meli za kibiashara katika bandari hiyo zilichangia katika kumfanya mtume Paulo afanye kazi ya kutengeneza hema huko Korintho. (Matendo 18:1-3) Kitabu kimoja (In the Steps of St. Paul) kinasema hivi: “Majira ya baridi kali yalipokaribia, watengenezaji hema wa Korintho ambao pia walitengeneza matanga, walikuwa na kazi nyingi kupita kiasi. Kwa kuwa bandari zote mbili zilijaa meli zilizokuwa zikijikinga majira hayo na mabaharia wakijitahidi kurekebisha meli zao wakati huo, kila mtu katika Lechæum na Kenkrea ambaye angeweza kushona matanga hata kwa kiasi kidogo alipewa kazi hiyo.”

Baada ya kukaa Korintho kwa zaidi ya miezi 18, Paulo alisafiri kutoka Kenkrea hadi Efeso katika mwaka wa 52 W.K. hivi. (Matendo 18:18, 19) Wakati fulani katika miaka minne iliyofuata, kutaniko la Kikristo lilianzishwa huko Kenkrea. Biblia inatuambia kwamba Paulo aliwaomba Wakristo huko Roma wamsaidie mwanamke Mkristo anayeitwa Fibi “wa kutaniko lililo katika Kenkrea.”—Waroma 16:1, 2.

Leo, watalii wanaotembelea eneo la Kenkrea wanaogelea kwenye maji safi kabisa katikati ya magofu ya bandari hiyo iliyozama. Wengi wao hawatambui kwamba karne nyingi zilizopita eneo hilo lilikuwa na utendaji mwingi wa Kikristo na wa kibiashara. Hali ilikuwa hivyo pia kwenye bandari ile nyingine ya Korintho, bandari ya Lechaeum, kwenye upande wa magharibi wa shingo hiyo ya nchi.

Lechaeum —Mwingilio wa Magharibi

Barabara iliyofunikwa kwa mawe inayoitwa Barabara ya Lechaeum ilitoka kwenye soko la Korintho hadi kwenye bandari ya magharibi iliyokuwa kilomita 2 iliyoitwa Lechaeum. Wajenzi walichimba sehemu fulani ya ufuo ili kujenga bandari hiyo na wakajaza mawe na mchanga waliochimba kwenye ufuo ili kuzuia meli zilizotia nanga zisipigwe na upepo mkali uliotoka kwenye ghuba hiyo. Wakati mmoja, hiyo ndiyo iliyokuwa bandari kubwa zaidi kwenye Bahari ya Mediterania. Wachimbuaji wa vitu vya kale wamechimbua mabaki ya mnara wa taa, sanamu ya Poseidon akiwa ameshika mwenge.

Kwenye Barabara ya Lechaeum ambayo ilikingwa na kuta mbili, kulikuwa na njia za wapita-njia, majengo ya serikali, mahekalu, na maduka. Huenda Paulo alikutana na wanunuzi wenye shughuli nyingi, watu waliosimama kupiga gumzo, wenye maduka, watumwa, wafanyabiashara, na wengine—watu ambao aliwahubiria.

Lechaeum haikuwa tu bandari ya kibiashara bali ilikuwa pia bandari kubwa ya kijeshi. Watu fulani wanadai kwamba meli ya vita yenye safu tatu za makasia, ambayo ilikuwa meli bora zaidi ya vita katika nyakati za zamani, ilibuniwa na Ameinocles mjenzi wa meli wa Korintho katika viwanda vya meli vya Lechaeum katika mwaka wa 700 K.W.K. hivi. Waathene walitumia meli hiyo katika ushindi muhimu dhidi ya jeshi la wanamaji la Uajemi huko Salamisi mnamo 480 K.W.K.

Bandari hiyo ambayo wakati mmoja ilikuwa yenye shughuli nyingi sasa ni “nyangwa zenye matete meusi.” Hakuna kitu kinachoonyesha kwamba karne nyingi zilizopita eneo hilo lilikuwa moja kati ya bandari kubwa zaidi katika Bahari ya Mediterania.

Wakristo Wapata Magumu Korintho

Zaidi ya kuwa bandari za kibiashara, bandari za Korintho zilitumika kama njia ambazo zilileta uvutano mbaya sana kwa watu wa jiji hilo. Bandari hizi zilileta biashara na utajiri. Korintho lilipata utajiri kwa kutoza ada kubwa za bandarini kutia ndani zile za kusafirisha mzigo na vilevile za kutumia njia iliyoitwa diolkos. Pia jiji hilo lilitoza kodi kwa ajili ya kupitisha bidhaa juu ya ardhi. Karibu na mwisho wa karne ya saba K.W.K., pesa zilizokusanywa kutokana na biashara zilizoendeshwa katika soko la jiji na kutoka bandarini ziliwezesha serikali kufutilia mbali malipo ya kodi ya raia wake.

Korintho lilikusanya pesa za ziada kutokana na wafanyabiashara walioishi huko. Wengi wao walijihusisha katika anasa na karamu zilizogharimu sana na zilizokuwa na upotovu wa maadili. Pia mabaharia walimiminika Korintho na kulitajirisha jiji hilo. Pia kama Strabo anavyosema, walitumia pesa nyingi. Wakaaji wa jiji hilo walitoa huduma nyingi, kama vile kurekebisha meli.

Katika siku za Paulo, ilisemekana kwamba jiji hilo lilikuwa na watu 400,000 hivi na idadi hiyo ilipitwa tu na Roma, Aleksandria, na Antiokia ya Siria. Wagiriki, Waroma, Wasiria, Wamisri, na Wayahudi waliishi Korintho. Kupitia bandari zake, wasafiri wengi, watu waliokuwa wakija kwa ajili ya michezo, wasanii, wanafalsafa, wanabiashara, na watu wengine waliingia katika jiji hilo. Wageni hao walitoa zawadi na dhabihu kwa miungu ya huko. Yote hayo yalifanya Korintho liwe jiji lenye shughuli nyingi, lakini pia yalisababisha matatizo mengi.

Kitabu (In the Steps of St. Paul) kilichotajwa awali kinasema hivi: “Korintho, iliyokuwa kati ya bandari mbili, likawa jiji la kisasa na likaiga maadili mapotovu ya mataifa ya kigeni ambayo meli zao zilitia nanga katika bandari zake.” Watu kutoka Mashariki na Magharibi walikutana na wakaleta maadili yao mapotovu. Kwa sababu hiyo, maadili ya Korintho yakaharibika kabisa, watu wakapenda anasa, na hivyo likawa ndilo jiji lililokuwa na upotovu wa maadili zaidi katika Ugiriki ya kale. Watu walisema kuwa kuishi kama Mkorintho kulimaanisha kuishi maisha ya anasa na yenye upotovu wa maadili.

Mazingira kama hayo ya ufuatiaji wa vitu vya kimwili na upotovu wa maadili yalihatarisha hali nzuri ya kiroho ya Wakristo. Wafuasi wa Yesu huko Korintho walihitaji kukumbushwa umuhimu wa kudumisha mwenendo mzuri mbele za Mungu. Kwa kufaa, katika barua zake kwa Wakorintho, Paulo alishutumu vikali pupa, upunjaji, na ukosefu wa maadili. Unaposoma barua hizo zilizoongozwa kwa roho, unaweza kutambua uvutano mbaya ambao Wakristo walihitaji kukabiliana nao.—1 Wakorintho 5:9, 10; 6:9-11, 18; 2 Wakorintho 7:1.

Hata hivyo, kulikuwa na faida kwa sababu ya kuwa na mchanganyiko huo wa watu wa mataifa mbalimbali. Jiji hilo lilipata mawazo mapya kila wakati. Wakaaji wake walikuwa na akili zilizofunguka zaidi kuliko watu wa majiji mengine ambayo Paulo alitembelea. “Watu kutoka mashariki na magharibi walikutana katika jiji hilo la kale lenye bandari,” akasema mchanganuzi mmoja wa Biblia, “na hivyo kuwafanya wakaaji wake wapate mawazo, falsafa, na dini za kila aina ulimwenguni.” Kwa sababu hiyo, kulikuwa na dini tofauti-tofauti na hilo lilirahisisha kazi ya Paulo ya kuhubiri.

Bandari mbili za Korintho, yaani, Kenkrea na Lechaeum, zilichangia ufanisi na umaarufu wa jiji hilo. Bandari hizo pia zilifanya iwe vigumu kwa Wakristo kuishi Korintho. Ulimwengu wetu wa leo unakabili hali kama hizo. Hali zenye kupotosha, kama vile ufuatiaji wa vitu vya kimwili na upotovu wa maadili, yanahatarisha hali ya kiroho ya watu wanaomwogopa Mungu. Hivyo, sisi pia tunapaswa kusikiliza na kutii maneno yaliyoongozwa na roho ambayo Paulo aliwaandikia Wakristo walioishi Korintho.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

 DIOLKOS—NJIA YA KUPITISHIA MELI NCHI KAVU

Kufikia mwishoni mwa karne ya saba K.W.K., mipango ya kujenga mfereji iliposhindwa kufaulu, Periander, mtawala wa Korintho, alijenga njia ya kusafirisha meli kuvuka shingo hiyo ya nchi kwa ustadi mwingi. * Njia hiyo iliyoitwa diolkos, jina linalomaanisha “kokota-ng’ambo,” ilikuwa njia yenye mawe ya mraba na mbao zilizowekwa kwenye nafasi zilizoachwa na mawe hayo ambazo zilikuwa zimepakwa mafuta. Mizigo kutoka kwa meli zilizotia nanga katika bandari moja ilipakuliwa, ikatiwa juu ya mikokoteni yenye magurudumu, na kuvutwa na watumwa juu ya njia hiyo na kupelekwa upande ule mwingine. Meli ndogo ambazo nyakati nyingine zilikuwa na mizigo zilivutwa kupitia njia hiyo.

[Maelezo ya chini]

^ fu. 29 Ili kupata habari kuhusu historia ya ujenzi wa mfereji wa kisasa, ona makala yenye kichwa “The Corinth Canal and its Story,” katika Amkeni! la Desemba 22, 1984, ukurasa wa 25-27 la Kiingereza au Amkeni! la Machi 22, 1985 la Kifaransa.

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UGIRIKI

Ghuba ya Korintho

Bandari ya Lechaeum

Korintho ya kale

Kenkrea

Shingo ya Nchi ya Korintho

Ghuba ya Saroniki

Peloponesia

BAHARI YA IONIA

Rasi ya Malea

BAHARI YA AEGEA

[Picha katika ukurasa wa 25]

Meli za mizigo zikipita katika Mfereji wa Korintho leo

[Picha katika ukurasa wa 26]

Bandari ya Lechaeum

[Picha katika ukurasa wa 26]

Bandari ya Kenkrea

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Todd Bolen/Bible Places.com