Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutafuta kwa Bidii

Kutafuta kwa Bidii

Barua Kutoka Ireland

Kutafuta kwa Bidii

ILIKUWA siku yenye manyunyu. Manyunyu hayo yalipiga kioo cha mbele cha gari langu na kunizuia nisione mandhari vizuri. Baada ya kusafiri kilomita 16, nilifika kwenye kilele cha mlima uliokuwa ukielekeana na Westport, mji mdogo wa pwani ya magharibi ya Ireland. Mwishowe, jua likaondoa ukungu na nikaona visiwa vingi vidogovidogo vilivyotapakaa kwenye ghuba hiyo kama vito vyenye kupendeza kwenye maji ya bluu. Visiwa vichache sana kati ya hivyo vinakaliwa na watu, lakini wakulima husafirisha mifugo yao kwa mashua ili ikalishe katika visiwa fulani.

Mbali zaidi kando ya pwani kwenye upande wa magharibi kuna safu za milima. Milima hiyo ilionekana kama shaba iliyong’arishwa ilipopigwa na jua. Kwa mbali ningeweza kuona vizuri mlima wenye umbo la pia unaoitwa Croagh Patrick, lakini wenyeji wanauita Reek. Nilisafiri kupitia barabara nyembamba, zilizojaa watu za Westport, nikaupita mlima huo hadi kwenye eneo ambalo halitembelewi sana na Mashahidi wa Yehova.

Mtu niliyekuwa nikienda kumwona hakujua kwamba ningefika siku hiyo. Nilikuwa nimepata barua iliyosema kwamba alikuwa amehamia eneo hilo hivi karibuni na kwamba alitaka kuendeleza mazungumzo yake ya Biblia pamoja na Mashahidi. Nilijiuliza: ‘Ana umri wa miaka mingapi? Je, yeye ni mseja au ameoa? Ana mapendezi gani?’ Niliutazama mkoba wangu na kujaribu kukumbuka ikiwa nilikuwa nimebeba Biblia na vichapo kadhaa vya Biblia. Nilifikiria ningesema nini ili kumfanya apendezwe zaidi na ujumbe wa Ufalme.

Nilikuwa nimeupita Mlima Reek. Kuta za mawe ambazo nyingi kati yake zilikuwa zimejengwa wakati wa ile Njaa Kuu ya karne ya 19, zilijengwa kando ya mashamba matupu hadi baharini. Kulikuwa na shakwe bahari aliyekuwa akielea angani. Kwenye upeo wa macho, niliona miti iliyokuwa imeinama na kujikunja kama wanaume wazee kwa sababu ya kupigwa na upepo.

Nyumba hazikuwa na namba na barabara hazikuwa na majina katika eneo hili la mashambani. Anwani ya mtu huyo ilionyesha tu jina la nyumba na jina la eneo. Hata hivyo, lengo langu la kwanza lilikuwa kuzungumza na mpeleka barua kwa kuwa yeye ndiye anayejua mahali kila mtu anaishi. Nilifika kwenye kituo cha posta dakika thelathini baadaye. Ishara mlangoni ilisema “Kumefungwa.” Kwa kuwa kulikuwa kumefungwa, niliuliza katika duka na nikaelekezwa katika eneo hilo.

Baada ya kusafiri kilomita 8 zaidi, nilipata alama niliyokuwa nikitafuta, yaani, kona kali upande wa kulia na barabara nyembamba upande wa kushoto. Nilibisha mlango mmoja uliokuwa karibu. Mwanamke mzee alifungua mlango na akaniambia kwa shangwe kwamba alikuwa ameishi katika eneo hilo maisha yake yote na akasema kwamba hakujua mahali mwanamume niliyekuwa nikimtafuta alipo. Alisema angepiga simu kisha anikaribishe.

Alipokuwa akizungumza, aliniangalia mara kwa mara kana kwamba alikuwa akijiuliza mimi ni nani na nilitaka nini. Niliona sanamu ndogo ya Bikira Maria kando ya mlango na picha kubwa ya Kristo ukutani. Kulikuwa na shanga za rozari juu ya meza. Ili nimtulize, nilimwambia, “Ningependa kumpa mwanamume huyo ujumbe muhimu kutoka kwa rafiki zake.”

Mume wake alikuja na kuanza kunieleza historia ya eneo hilo. Wakati huo, mwanamke huyo hakuwa amepata habari zozote kutokana na simu ya kwanza aliyopiga na hivyo akasisitiza kwamba nisubiri awapigie watu wengine simu. Ilionekana kwamba hakuna mtu aliyekuwa anamjua mtu huyo au nyumba yake. Nilitazama saa. Ilikuwa inakaribia jioni. Nilitambua kwamba ningehitaji kurudi siku nyingine. Niliwashukuru kwa msaada wao, nikarudi ndani ya gari, na nikaanza safari ndefu ya kurudi nyumbani.

Nilirudi juma lililofuata. Wakati huu, nilimkuta mpeleka barua naye akanielezea njia vizuri. Baada ya dakika 15, nilifika kwenye njia panda aliyokuwa amenielezea. Nilielekea upande wa kushoto na nikaenda juu chini mara kadhaa, nikitafuta alama inayofuata, yaani, daraja la zamani la mawe. Sikupata daraja hilo. Ingawa hivyo, nilipata alama ya mwisho niliyokuwa nimeambiwa nitafute na hapo, juu ya mlima, nikaona nyumba niliyokuwa nimeitafuta sana kwa muda mrefu.

Nilitua kidogo ili nifikirie jinsi nitakavyozungumza kuhusu habari njema. Mwanamume mzee alifungua mlango. “Pole,” akaniambia, “nyumba unayotafuta iko pale.” Alinielekeza kwenye nyumba iliyokuwa imefichwa na miti. Kwa hamu, nilielekea huko na kugonga mlango. Nilipokuwa nikisubiri, niliitazama Bahari ya Atlantiki iliyokuwa hatua chache kutoka niliposimama. Upepo ulikuwa umeongezeka, na mawimbi yalikuwa meupe yalipopiga fuo maridadi za eneo hilo. Hakukuwa na mtu karibu na eneo hilo au hata ndani ya nyumba hiyo.

Nilirudi kwenye nyumba hiyo mara mbili tena kabla ya kumkuta kijana mmoja. “Umefika kwenye nyumba uliyotaka,” akasema, “lakini mtu aliyekuwa akiishi hapa ambaye ndiye unatafuta, alihama, na sijui alikohamia.” Nilimweleza kilichokuwa kimenileta na nikagundua kwamba kijana huyo hakuwa amewahi kuzungumza na Mashahidi wa Yehova. Alikuwa ameibiwa na alijiuliza kwa nini Mungu aliruhusu jambo hilo na mambo mengine yasiyo ya haki yaendelee. Alikubali kwa furaha magazeti ya karibuni ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yaliyozungumza kuhusu jambo hilo.

Maandiko yanatuamuru tuwatafute kwa bidii watu wenye mioyo minyoofu wanaotafuta ukweli. Kwa kusikitisha, sikumpata mwanamume niliyekuwa nikimtafuta. Hata hivyo, sikuona kwamba jitihada zangu zilikuwa za bure. Nchini Ireland, watu wengi wanatamani kujifunza ujumbe wa Ufalme, na kwa baraka za Yehova, huenda mbegu ndogo zilizopandwa katika kijana huyo zikazaa matunda siku moja.