Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

“Kapteni wa hekalu” alikuwa nani, na alikuwa na majukumu gani?

“Kapteni wa hekalu” alikuwa kati ya viongozi wa kidini Wayahudi waliowakamata mtume Petro na mtume Yohana walipokuwa wakihubiri. (Matendo 4:1-3) Biblia haifafanui majukumu ya kapteni wa hekalu, lakini vitabu vingine vya kihistoria vinatoa habari zaidi.

Inaonekana kwamba kufikia wakati ambapo Yesu alikuwa duniani, cheo hicho kilikuwa cha kuhani aliyekuwa wa pili kutoka kwa kuhani mkuu. Kapteni wa hekalu alihakikisha kwamba kulikuwa na utaratibu ndani na nje ya hekalu la Yerusalemu. Alisimamia ibada katika hekalu na vilevile alisimamia polisi wa hekalu. Makapteni waliokuwa chini yake waliwasimamia walinzi waliofungua malango ya hekalu asubuhi na kuyafunga usiku, wale waliohakikisha kwamba hakuna mtu aliyeingia katika maeneo ambayo watu hawakupaswa kuingia, na wale waliolinda hazina ya hekalu.

Makuhani na Walawi waliofanya kazi katika hekalu walipangwa katika migawanyo 24, kila mgawanyo ulitumikia kwa zamu ya juma moja, mara mbili kwa mwaka. Huenda kila mgawanyo ulikuwa na kapteni wake.—1 Mambo ya Nyakati 24:1-18.

Makapteni hao wa hekalu walikuwa watu wenye mamlaka. Wanatajwa pamoja na wakuu wa makuhani waliopanga njama ya kumwua Yesu na pia waliwatumia watu waliokuwa chini yao kumkamata Yesu.—Luka 22:4, 52.

Andiko la Mathayo 3:4 linasema kwamba Yohana Mbatizaji alikula “nzige na asali ya mwituni.” Je, nzige walikuwa chakula cha kawaida wakati huo?

Wengine wameshuku kwamba Yohana alikula wadudu, wakidai kwamba Mathayo alikuwa akirejelea matunda ya mti wa karuba, matunda ya mwituni, au hata samaki wa aina mbalimbali. Hata hivyo, neno la Kigiriki ambalo Mathayo alitumia linarejelea jamii fulani ya panzi wanaojulikana leo kama Acrididae. Nzige wa jangwani ndiye aliyepatikana sana huko Israeli, nao wanajulikana kwa uharibifu wao.—Yoeli 1:4, 7; Nahumu 3:15.

Nzige walionwa kuwa chakula kitamu na watu nyakati za kale kama vile Waashuru na Waethiopia na bado wanaliwa leo na makabila fulani ya Wabedui na Wayahudi wanaoishi Yemen. Katika Israeli, nzige walionwa kuwa chakula cha maskini. Baada ya kichwa, miguu, na tumbo kuondolewa, kifua kililiwa kikiwa kibichi au baada ya kuchomwa au baada ya kuanikwa juani. Nyakati nyingine nzige waliwekwa chumvi au kulowekwa kwenye siki au asali. Mwanahistoria Henri Daniel-Rops anasema kwamba ladha yao ni kama ya uduvi.

Kwa kuwa Yohana alihubiri nyikani, nzige walipatikana kwa urahisi. (Marko 1:4) Kwa kuwa asilimia 75 ya nzige ni protini, wanapoliwa pamoja na asali, kinakuwa chakula chenye lishe bora.

[Picha katika ukurasa wa 28]

Watumishi Waashuri wakibeba nzige na makomamanga

[Hisani]

From the book Discoveries Among the Ruins of Nineveh and Babylon (1853)