Je, Wajua?
Je, Wajua?
Kuna uthibitisho gani nje ya Biblia kwamba Yesu alikuwa mtu halisi?
▪ Waandikaji kadhaa wa mambo yasiyo ya dini ambao waliishi karibu na wakati wa Yesu, walimtaja katika maandishi yao. Mmoja kati ya waandikaji waliomtaja Yesu ni Kornelio Tasito, ambaye aliandika historia ya Roma chini ya utawala wa maliki mbalimbali. Kuhusu moto ulioharibu Roma mwaka wa 64 W.K., Tasito anasema kulikuwa na uvumi kwamba Maliki Nero ndiye aliyesababisha msiba huo. Tasito anasema, Nero alijaribu kukilaumu kikundi cha watu ambao waliitwa Wakristo. Tasito anaandika: “Kristo, ambaye jina Wakristo lilitokana na jina lake, aliuawa mikononi mwa gavana Pontio Pilato wakati wa utawala wa Tiberio.”—Annals, XV, 44.
Mwanahistoria Myahudi Flavio Yosefo pia anamtaja Yesu. Anaposimulia mambo yaliyotukia baada ya kifo cha Festo, ambaye alikuwa gavana Mroma wa Yudea yapata mwaka wa 62 W.K., na kabla ya Albino kuwa gavana, Yosefo anasema kwamba Kuhani Mkuu Ananu (Anania) “aliitisha kikao cha Sanhedrini na kumleta mbele yao Yakobo, ndugu ya Yesu aliyekuwa akiitwa Kristo, pamoja na wengine.”—Jewish Antiquities, XX, 200 (ix, 1).
Kwa nini Yesu aliitwa Kristo?
▪ Vitabu vya Injili vinasimulia kwamba malaika Gabrieli alipomtokea Maria na kutangaza kwamba angepata mimba, alimwambia kuwa alipaswa kumwita mtoto wake Yesu. (Luka 1:31) Hilo lilikuwa jina la kawaida miongoni mwa Wayahudi wa nyakati za Biblia. Mwanahistoria Myahudi Yosefo aliandika kuhusu watu 12 walioitwa Yesu, kando na wale wanaotajwa katika Biblia. Mwana wa Maria aliitwa “Mnazareti,” jina lililoonyesha kuwa Yesu alitoka Nazareti. (Marko 10:47) Pia aliitwa “Kristo,” au Yesu Kristo. (Mathayo 16:16) Jina Kristo linamaanisha nini?
Neno la Kiswahili “Kristo” linatokana na neno la Kigiriki Khri·stosʹ, ambalo lina maana sawa na neno la Kiebrania Ma·shiʹach (Masihi). Maneno hayo mawili yanamaanisha “Mtiwa-Mafuta.” Kabla ya Yesu, kulikuwa na watu wengine walioitwa Masihi. Kwa mfano, Musa, Haruni, na Mfalme Daudi walitajwa kuwa watiwa mafuta, ikimaanisha kwamba Mungu alikuwa amewachagua na kuwapa mamlaka na majukumu mbalimbali. (Mambo ya Walawi 4:3; 8:12; 2 Samweli 22:51; Waebrania 11:24-26) Yesu, Masihi aliyeahidiwa, ndiye mwakilishi mkuu zaidi wa Yehova. Kwa hiyo, Yesu aliitwa “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”—Mathayo 16:16; Danieli 9:25.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Picha ya Flavio Yosefo iliyochorwa