Je, Wajua?
Je, Wajua?
Ni lango gani la jiji linalotajwa mara nyingi sana katika masimulizi ya Biblia?
▪ Katika nyakati za Biblia, majiji mengi yalizungukwa na kuta za ulinzi. Ndani ya malango mengi kulikuwa na maeneo ambayo watu walikutana, walifanya biashara, na kuzungumza. Matangazo ya umma yalifanywa katika maeneo hayo, na huenda manabii walitangaza ujumbe wao huko. (Yeremia 17:19, 20) Kitabu The Land and the Book kinasema kwamba “karibu shughuli zote za umma zilifanyiwa huko au karibu na malango ya jiji.” Katika Israeli la kale, malango ya jiji yalitumiwa kama vile ambayo vituo vya jamii vinatumiwa katika miji ya kisasa.
Kwa mfano, Abrahamu alinunua shamba la kuzikia watu wa familia yake kutoka kwa Efroni “masikioni mwa wana wa Hethi pamoja na wale wote waliokuwa wakiingia lango la jiji.” (Mwanzo 23:7-18) Naye Boazi aliwaomba wazee kumi wa Bethlehemu waketi langoni mwa jiji, huku wakishuhudia, akafanya mipango kwa ajili ya Ruthu na urithi wa mumewe aliyekuwa amekufa, kulingana na sheria kuhusu ndoa ya ndugu-mkwe. (Ruthu 4:1, 2) Wanaume wazee wa jiji walipotenda wakiwa waamuzi, waliketi kwenye lango la jiji kusikiliza kesi, kutoa maamuzi, na kutekeleza hukumu.—Kumbukumbu la Torati 21:19.
Ofiri, ambako Biblia inataja kuwa chanzo cha dhahabu bora zaidi, ilikuwa wapi?
▪ Kitabu cha Ayubu ndicho cha kwanza kuilinganisha “dhahabu ya Ofiri” na “dhahabu safi.” (Ayubu 28:15, 16) Miaka 600 hivi baada ya siku za Ayubu, Mfalme Daudi alikusanya “dhahabu ya Ofiri” kwa ajili ya ujenzi wa hekalu la Yehova huko Yerusalemu. Sulemani, mwana wake, pia aliagiza dhahabu kutoka Ofiri.—1 Mambo ya Nyakati 29:3, 4; 1 Wafalme 9:28.
Kulingana na Maandiko, Sulemani alikuwa na kundi la meli zilizoundwa katika Esion-geberi, kando ya Bahari Nyekundu, ambazo zilileta dhahabu kutoka Ofiri. (1 Wafalme 9:26) Wasomi wanasema kwamba eneo la Esion-geberi liko upande wa juu wa Ghuba ya Aqaba karibu na eneo la Elat na Aqaba ya leo. Kutoka huko, meli zingefika katika sehemu yoyote ya Bahari Nyekundu au mbali zaidi katika bandari za kibiashara kwenye pwani za Afrika au India, maeneo ambayo huenda Ofiri ilikuwa. Hata hivyo, watu fulani waliamini kwamba Ofiri ilikuwa Arabia, ambapo migodi ya kale ya dhahabu imepatikana na mabaki yamechimbwa hata katika nyakati za kisasa.
Iwe migodi ya dhahabu ya Sulemani ni hekaya tu kama wengine wanavyoamini, mtaalamu wa vitu vya kale vya Misri Kenneth A. Kitchen aandika: “Ofiri yenyewe ni halisi. Kigae cha udongo chenye maandishi ya Kiebrania ambacho huenda ni cha karne ya nane [K.W.K.] kimeandikwa waziwazi maneno haya mafupi: ‘Dhahabu ya Ofiri kwa ajili ya Beth-Horoni—shekeli 30 [gramu 340].’ Hapa Ofiri inatajwa kuwa chanzo halisi cha dhahabu, kama vile tu Dhahabu ya ‘Amau,’ au ‘Dhahabu ya Punt’ au ‘Dhahabu ya Kushi’ katika maandishi ya Misri—dhahabu katika visa hivi vyote, ilitolewa katika nchi inayotajwa au kutokana na aina au ubora wa dhahabu ya nchi hiyo.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Abrahamu akiwa kwenye lango la jiji, akitaka kununua shamba
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kigae chenye maandishi ya kiebrania kilicho na jina Ofiri
[Hisani]
Collection of Israel Antiquities Authority, Photo © The Israel Museum, Jerusalem