Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mchapishaji wa Kale Asaidia Kuenezwa kwa Biblia

Mchapishaji wa Kale Asaidia Kuenezwa kwa Biblia

Mchapishaji wa Kale Asaidia Kuenezwa kwa Biblia

VITABU na vitabu vya kukunjwa vilianza kuandikwa kwa mkono maelfu ya miaka iliyopita. Hata hivyo, vitabu vilivyochapishwa si vya zamani. Vitabu vya kwanza kuchapishwa vilichapishwa nchini China mnamo 868 W.K. kwa kutumia vipande vya mbao vilivyokuwa na herufi zilizochongwa ili kutokeza maandishi. Huko Ujerumani, katika mwaka wa 1455 hivi, Johannes Gutenberg alivumbua mashine ya kuchapisha yenye herufi mojamoja zilizopangwa na akaitumia kutokeza Biblia ya kwanza iliyochapishwa katika Kilatini.

Hata hivyo, kuenezwa kwa Biblia na vitabu vingine kulianza kuwa biashara kubwa miaka kadhaa baada ya hapo. Jiji la Nuremberg likaja kuwa kituo cha biashara ya uchapishaji nchini Ujerumani, na huenda Anton Koberger, mzaliwa wa jiji hilo, akawa ndiye mtu wa kwanza kuchapisha Biblia kwa wingi ulimwenguni pote.

Watu katika tamaduni zote wanapaswa kuwashukuru sana wachapishaji hao wa kwanza wa Biblia, kutia ndani Anton Koberger. Acheni tuzungumze kwa undani zaidi kumhusu Koberger na kazi yake.

Biblia Ilipewa Uangalifu wa Pekee

Mnamo 1470, Koberger alifungua matbaa ya kwanza huko Nuremberg. Kiwanda chake kilikuwa na matbaa 24 zikifanya kazi wakati uleule, kukiwa na jumla ya wachapishaji, wasanii, na wafanyakazi 100 huko Basel, Strasbourg, Lyon, na katika majiji mengine ya Ulaya. Koberger alichapisha maandishi mengi ya Kilatini ya Enzi za Kati na vitabu vingi vya kisayansi vya wakati wake. Alichapisha vitabu 236 tofauti-tofauti katika muda wa maisha yake. Vitabu vingine vilikuwa na kurasa nyingi sana, kila ukurasa ukichapishwa kwa matbaa ya mkono.

Uchapishaji wa Koberger wa hali ya juu ulifanya vitabu vyake viwe maarufu kwa sababu ya umaridadi wake na ilikuwa rahisi kuvisoma. “Sikuzote Koberger alisisitiza kwamba matbaa zenye herufi mpya ndizo tu zitakazotumiwa,” akaandika mwanahistoria Alfred Börckel. “Hakuruhusu herufi zilizofifia zitumiwe.” Isitoshe, vitabu na Biblia nyingi za Koberger zilitia ndani picha zilizonakiliwa kutoka kwenye michoro iliyochongwa kwenye mbao.

Kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kazi ya uchapishaji ya Koberger, “kitabu kimoja ndicho kilipewa uangalifu wa pekee zaidi—Biblia,” akaandika Oscar Hase, mwandishi wa maisha ya Koberger. Koberger na wenzake walijitahidi sana kupata maandishi sahihi zaidi ya Biblia. Haikuwa rahisi kufanya hivyo kwa kuwa hati nyingi za mafunjo zilionwa kuwa hazina za makao fulani ya watawa na ikiwa mtu angeruhusiwa kuzinakili angepewa ruhusa kwa muda mfupi tu.

Biblia za Kilatini na za Kijerumani

Koberger alichapisha Biblia Latina (Biblia ya Kilatini) mara 15 tofauti-tofauti, toleo la kwanza likitokea katika mwaka wa 1475. Matoleo fulani yalitia ndani picha za safina ya Noa, zile Amri Kumi, na hekalu la Sulemani. Mnamo 1483, Koberger alichapisha Biblia Germanica (Biblia ya Kijerumani) na alitokeza nakala 1,500 hivi katika uchapishaji wa kwanza—idadi kubwa sana wakati huo. Biblia hiyo ilitia ndani zaidi ya picha 100 zilizonakiliwa kutoka kwenye michoro iliyochongwa kwenye mbao ili kuwavutia wasomaji, kuwasaidia waelewe, na kuwakumbusha watu ambao hawakujua kusoma hadithi za Biblia zinazojulikana. Picha zilizokuwa katika Biblia hiyo zilikuja kuwasaidia sana wachoraji wa picha za Biblia, hasa wale waliochora picha kwa ajili ya Biblia za Kijerumani.

Biblia ya Kijerumani ambayo Koberger alichapisha mnamo 1483 ilikuwa maarufu, lakini hakuchapisha tena toleo lingine la Kijerumani. Ingawa wahariri wake walikuwa wamebadili maandishi yake kwa uangalifu sana ili yapatane na Vulgate ya Kilatini iliyokubaliwa na kanisa, Koberger alikuwa ametumia tafsiri iliyopigwa marufuku ya Wawaldo ya karne ya 14, kuwa msingi wa toleo lake. * Mwaka uliofuata, Papa Innocent wa Nane alianza kuangamiza jamii za Wawaldo. Baada ya hapo, upinzani wa kanisa kuelekea Biblia za lugha za kienyeji uliendelea kuongezeka. Machi 22, 1485 (22/3/1485), Askofu Mkuu Berthold wa Mainz, Ujerumani, alitoa taarifa akishutumu kutafsiriwa kwa Biblia katika Kijerumani. Januari (Mwezi wa 1) 4, mwaka uliofuata, Berthold alirudia tena taarifa hiyo. Kwa sababu ya upinzani huo, Koberger hakujaribu tena kuchapisha Biblia katika Kijerumani.

Hata hivyo, Anton Koberger hakufanya kazi ya bure. Alikuwa mstari wa mbele katika kutumia mbinu mpya za kuchapisha na kufanya vitabu vya aina nyingi vipatikane kwa urahisi na kwa bei ya chini huko Ulaya. Kwa sababu ya jitihada zake, Koberger alisaidia watu wa kawaida waweze kuipata Biblia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Ona habari yenye kichwa “Wawaldo—Waacha Uzushi na Kuwa Waprotestanti,” katika toleo la Machi 15, 2002, la Mnara wa Mlinzi.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kushoto hadi kulia: Nakala ya picha ya Danieli katika shimo la simba; Herufi kubwa iliyotengenezwa kwa dhahabu; Herufi zinazoweza kuonekana waziwazi

[Picha katika ukurasa wa 26]

Koberger

[Picha katika ukurasa wa 26]

Picha ya Biblia ya Koberger ya Kilatini na ya Kijerumani, zenye mapambo ya rangi nyangavu na maelezo fulani ya Mwanzo 1:1

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

All Bible photos: Courtesy American Bible Society Library; Koberger: Mit freundlicher Genehmigung der Linotype GmbH