Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dini ya Calvin Imetimiza Nini Tangu Ianzishwe Miaka 500 Iliyopita?

Dini ya Calvin Imetimiza Nini Tangu Ianzishwe Miaka 500 Iliyopita?

Dini ya Calvin Imetimiza Nini Tangu Ianzishwe Miaka 500 Iliyopita?

JEAN CAUVIN (John Calvin) alizaliwa mjini Noyon, Ufaransa, mwaka wa 1509. Alianzisha kikundi cha kidini ambacho kilikuwa na uvutano mkubwa juu ya maisha ya watu wengi katika sehemu mbalimbali za Ulaya, Amerika, Afrika Kusini, na maeneo mengine. Anaonwa kuwa mmoja kati ya viongozi mashuhuri wa marekebisho ya kidini katika historia ya Ukristo.

Leo, miaka 500 hivi baada ya Calvin kuzaliwa, baadhi ya maoni na mafundisho yake bado yana uvutano juu ya dini za Kiprotestanti kama vile kanisa la Reformed, Presbiteri, Congregational, Wapuriti, na kadhalika. Kufikia Septemba mwaka uliopita, Muungano wa Makanisa ya Reformed Ulimwenguni Pote uliripoti kuwa na wafuasi milioni 75 katika nchi 107.

Atofautiana na Wakatoliki

Baba ya Calvin alikuwa mwanasheria na mwandishi wa kanisa Katoliki huko Noyon. Kwa sababu ya kazi yake, yaelekea alishuhudia mwenendo mpotovu wa makasisi uliokuwa umeenea sana wakati huo. Hatujui kama jambo hilo lilifanya alalamike kuwahusu makasisi hao, au kuwavunjia heshima, lakini baada ya muda, baba na kaka ya Calvin walitengwa na kanisa. Baba yake alipokufa, ilikuwa vigumu kwa Calvin kulishawishi kanisa Katoliki kukubali kumzika. Yaelekea tukio hilo lilimfanya Calvin asiweze kuliamini tena kanisa Katoliki.

Vitabu vingi kumhusu Calvin havisemi mengi kuhusu ujana wake ila tu kwamba alikuwa kijana mnyamavu, asiyesema mengi. Hata alipokuwa mwanafunzi huko Paris, Orléans, na Bourges, Calvin hakuwa na marafiki wengi. Lakini alikuwa na akili na kumbukumbu nzuri sana. Sifa hizo, kutia ndani uwezo wake mkubwa wa kufanya kazi, zilimwezesha kusoma kila siku kuanzia saa kumi na moja asubuhi mpaka saa sita usiku. Kwa hiyo, akawa mwanasheria kabla ya kufikia umri wa miaka 23. Pia, alijifunza Kiebrania, Kigiriki, na Kilatini ili aweze kuichunguza Biblia. Hata hivyo, Calvin alijulikana hasa kwa bidii na nidhamu yake kazini, mambo ambayo hata leo yanahusianishwa na wafuasi wa dini yake.

Wakati huohuo, nchini Ujerumani, Martin Luther alililaumu waziwazi Kanisa Katoliki kwa ufisadi na mafundisho yasiyopatana na Biblia. Inasemekana kwamba Luther alipigilia hoja au malalamiko yake 95 kwenye mlango wa kanisa jijini Wittenberg mwaka wa 1517, akilitaka kanisa lifanye marekebisho. Wengi walikubaliana naye, na Marekebisho Makubwa ya Kidini yakaenea kwa haraka kotekote barani Ulaya. Bila shaka, jambo hilo lilichochea upinzani mkali katika maeneo mengi, na wale waliounga mkono marekebisho hayo, au Waprotestanti, wakanyanyaswa kwa kutetea maoni yao. Katika mwaka wa 1533 jijini Paris, rafiki ya Calvin, aliyeitwa Nicholas Cop, alitoa hotuba iliyomuunga mkono Luther, na kwa vile Calvin alimsaidia kuandika hotuba hiyo, wote wawili walilazimika kukimbia wasiuawe. Calvin hakurudi tena kuishi Ufaransa.

Katika mwaka wa 1536, Calvin alichapisha kitabu Institutes of the Christian Religion. Kitabu hicho kina kanuni za msingi za dini ya Kiprotestanti. Alimwandikia Mfalme Francis wa Kwanza kitabu hicho ili kuwatetea Waprotestanti wa Ufaransa, ambao baadaye waliitwa Wahuguenoti. Calvin alishtumu mafundisho ya Kanisa Katoliki na kutetea msingi wa imani yake—enzi kuu ya Mungu. Kitabu hicho cha Calvin pia kilichangia sana ukuzi wa lugha ya Kifaransa na mtindo wa uandishi. Calvin alisifika kuwa mmoja kati ya viongozi mashuhuri zaidi wa marekebisho ya kidini. Hatimaye, Calvin alihamia Geneva, Uswisi, na kuanzia mwaka wa 1541 na kuendelea, akalifanya jiji hilo kuwa kitovu cha marekebisho yake.

Aendelea na Marekebisho Yake Jijini Geneva

Calvin alikuwa na uvutano mkubwa sana jijini Geneva. Akichochewa na maoni yake kwamba watu wanapaswa kuwa waadilifu na wenye mwenendo mzuri, Calvin aliwabadili wakaaji wa Geneva “wenye mwenendo mpotovu wakawa watu wanaofuata viwango vya juu vya maadili katika maisha yao,” kinasema kitabu kimoja cha marejeo, Encyclopedia of Religion. Mabadiliko yalikuja katika njia nyingine pia. Dakt. Sabine Witt, ambaye ni msimamizi wa jumba la makumbusho (Berlin’s German Historical Museum) anasema: “Kutokana na vita vya kidini nchini Ufaransa, hesabu ya watu [jijini Geneva] iliongezeka mara mbili katika muda wa miaka michache kwa kuwa maelfu ya wakimbizi Waprotestanti walimiminika jijini humo.” Sawa na Calvin, Wahuguenoti walikuwa na bidii na nidhamu ya kazi, kwa hiyo walichangia ukuzi wa uchumi wa jiji la Geneva, na kulifanya kituo cha uchapaji na pia utengenezaji wa saa.

Wakimbizi kutoka nchi nyingine pia walihamia Geneva, wakiwamo wakimbizi wengi kutoka Uingereza, ambako Waprotestanti walikabili vitisho vya Malkia Mary wa Kwanza. Dini ya Calvin ambayo wengi wa wafuasi wake walikuwa waumini wa vikundi vidogo-vidogo vya dini waliofukuzwa katika nchi zao, walianzisha kile ambacho jarida la mambo ya kidini linaloitwa Christ in der Gegenwart (Ukristo wa Siku Hizi) lilikiita “theolojia ya watu wanaoteswa.” Katika mwaka wa 1560, wakimbizi hao walichapisha Geneva Bible (Biblia ya Geneva), ambayo ni Biblia ya kwanza yenye maandishi yaliyogawanywa kwa mistari yenye nambari. Kwa kuwa ilikuwa ndogo, ilifaa kwa usomaji wa kibinafsi wa Neno la Mungu. Yaelekea hii ndiyo Biblia ambayo Wapuriti walibeba walipohamia Amerika ya Kaskazini mwaka wa 1620.

Hata hivyo, jiji la Geneva halikuwa makimbilio salama kwa kila mtu. Michael Servetus, aliyezaliwa 1511 nchini Hispania, alijifunza Kigiriki, Kilatini, na Kiebrania. Pia alisomea udaktari na labda alikutana na Calvin wakati wote wawili walipokuwa wanafunzi jijini Paris. Servetus alitambua kutokana na uchunguzi wake wa Biblia kwamba fundisho la Utatu si la Kimaandiko. Alijaribu kuwasiliana na Calvin kuhusu fundisho hilo, lakini Calvin akamwona kuwa adui. Kwa sababu ya kuteswa na Wakatoliki nchini Ufaransa, Servetus alikimbilia Geneva, jiji la Calvin. Badala ya kukaribishwa, alikamatwa, akahukumiwa kuwa mwasi wa kidini, na kuteketezwa kwenye mti mwaka wa 1553. Mwanahistoria Friedrich Oehninger anasema: “Kuuawa kwa Servetus ni jambo ambalo bado linatia doa maisha na kazi ya [Calvin], kiongozi mashuhuri wa marekebisho ya kidini.”

Calvin alifanya kazi kubwa katika jitihada zake za kuleta marekebisho. Inasemekana kuwa aliandika vitabu vya marejeo zaidi ya 100 na barua 1,000. Pia alitoa hotuba za kidini 4,000 hivi jijini Geneva. Katika hayo yote, Calvin alionyesha jinsi Ukristo unavyopaswa kuwa na pia akajitahidi kuwalazimisha watu waishi jinsi alivyofikiri Wakristo wanapaswa kuishi, hasa katika jiji la Geneva, ambalo aliliona kama jiji la Mungu. *

Jitihada za Calvin za kuleta marekebisho jijini Geneva zilikuwa na matokeo gani? Idara ya Takwimu ya Uswisi inasema kwamba katika mwaka wa 2000, wafuasi wa Kanisa la Reformed la Calvin jijini Geneva walikuwa asilimia 16 tu, na kwamba wafuasi wa kanisa Katoliki ni wengi zaidi kuliko wafuasi wa Calvin.

Mgawanyiko wa Kidini Waenea

Kutokana na yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, majiji na nchi mbalimbali ziliunga mkono ama dini ya Katoliki, Kilutheri, au ya Calvin, na hivyo kukawa na mgawanyiko mkubwa wa kidini barani Ulaya. Ingawa viongozi wa marekebisho ya kidini waliungana kulipinga Kanisa Katoliki, kulikuwa na tofauti kati yao. Dakt. Witt, aliyenukuliwa awali, anasema: “Tofauti za kimafundisho zilitokea hata kati ya Waprotestanti wenyewe.” Ijapokuwa wote walikubali kwamba Biblia inapaswa kuwa msingi wa imani ya Kikristo, mafundisho yao yalitofautiana sana. Walitofautiana hasa kuhusu maana ya Mlo wa Jioni wa Bwana na kuwapo kwa Kristo. Baada ya muda, wafuasi wa Calvin walianzisha moja kati ya mafundisho ambayo yalileta ubishi mkubwa, yaani, maisha ya mwanadamu yameamuliwa mapema.

Kulikuwa na ubishi mwingi kuhusu ufafanuzi wa fundisho hilo. Kikundi kimoja cha wafuasi wa Calvin kilidai kwamba kabla ya wanadamu kufanya dhambi, Mungu alikuwa ameamua kuwa watu wachache tu waliochaguliwa ndio wangepata wokovu kupitia Kristo, hali wengine wote wangeukosa. Kwa hiyo, kikundi hiki kiliamini kwamba wokovu ni mpango wa Mungu na kwamba hakuna usawa kati ya wanadamu. Kikundi kile kingine kiliamini kwamba wokovu umeandaliwa kwa ajili ya wanadamu wote, na mtu mwenyewe ndiye anayeamua kama ataukubali au hataukubali. Hilo lilimaanisha kwamba kukubali au kukataa wokovu ni uamuzi wa mtu mwenyewe. Kwa muda mrefu hata baada ya kifo chake, wafuasi wa Calvin waliendelea kupambana na mafundisho kama vile mpango wa Mungu kuhusu wokovu, hiari au uhuru wa mtu wa kuchagua, na usawa kati ya wanadamu.

Matendo Yasiyofaa Yaitia Doa Dini ya Calvin

Katika karne ya 20, kanisa la Dutch Reformed la wafuasi wa Calvin lilitumia fundisho la kwamba maisha ya mwanadamu yameamuliwa mapema kama msingi wa kuunga mkono ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Kuhusu sera ya serikali kwamba mtu mweupe ni bora kuliko mtu mweusi, Nelson Mandela, aliyekuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini, alisema: “Sera hiyo iliungwa mkono na Kanisa Dutch Reformed, ambalo lilitetea ubaguzi wa rangi kwa kusema kuwa Waafrikana ni watu waliochaguliwa na Mungu nao watu weusi ni jamii ya hali ya chini. Kulingana na maoni ya Waafrikana, ubaguzi wa rangi uliungwa mkono na kanisa.”

Katika miaka ya 1990, Kanisa Dutch Reformed liliomba msamaha waziwazi kwa kuunga mkono ubaguzi wa rangi. Katika ripoti rasmi inayoitwa Azimio la Rustenburg, viongozi wa kanisa walikiri hivi: “Baadhi yetu tulitumia Biblia vibaya kutetea ubaguzi wa rangi, na kufanya wengi waamini kwamba Mungu anaukubali.” Kwa miaka mingi, msimamo wa kanisa hilo kuhusu ubaguzi wa rangi ulichangia mateso ya kibaguzi na hata likadokeza kwamba Mungu ndiye wa kulaumiwa!

John Calvin alikufa jijini Geneva mwaka wa 1564. Alipokaribia kufa, inasemekana kwamba aliwashukuru watu wa kanisa lake “kwa heshima nyingi waliyompa; heshima ambayo hakustahili.” Pia aliwaomba msamaha kwa udhaifu wake wa muda mrefu wa kutokuwa mvumilivu na tabia yake ya kuwaka hasira. Ingawa alikuwa na udhaifu huo, hakuna shaka kwamba maoni yanayofaa ya Waprotestanti kuhusu kazi—kuwa wenye bidii, nidhamu, na kujitolea kazini—yanapatana sana na viwango vya maadili vya John Calvin.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kwa habari zaidi, ona kitabu Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu, ukurasa wa 322-325, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Blabu katika ukurasa wa 21]

Kutokana na yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, majiji na nchi mbalimbali ziliunga mkono ama dini ya Katoliki, Kilutheri, au ya Calvin, na hivyo kukawa na mgawanyiko mkubwa wa kidini barani Ulaya

[Picha katika ukurasa wa 18]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

HISPANIA

UFARANSA

PARIS

Noyon

Orléans

Bourges

USWISI

GENEVA

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kitabu cha Calvin “Institutes” (1536) kiliandaa kanuni za msingi za dini ya Kiprotestanti

[Hisani]

© INTERFOTO/Alamy

[Picha katika ukurasa wa 20]

Kuuawa kwa Servetus bado ni jambo linalotia doa maisha na kazi ya Calvin

[Hisani]

© Mary Evans Picture Library

[Picha katika ukurasa wa 21]

Tafsiri ya “Geneva Bible” (Biblia ya Geneva) (1560) ndio Biblia ya kwanza ya Kiingereza ambayo ina mistari yenye nambari

[Hisani]

Courtesy American Bible Society

[Picha katika ukurasa wa 18]

French town: © Mary Evans Picture Library