Kesi Iliyoendeshwa Vibaya Zaidi Kuliko Zote
Kesi Iliyoendeshwa Vibaya Zaidi Kuliko Zote
NI KESI chache za zamani zinazojulikana sana kama kesi hii. Masimulizi manne tofauti ya Biblia, yanayoitwa Injili, yanazungumzia kukamatwa, kuhukumiwa, na kuuawa kwa Yesu Kristo. Kwa nini unapaswa kujua kuhusu kesi hiyo? Kwa sababu Yesu aliwaagiza wafuasi wake wakumbuke kifo chake, jambo linalozidisha umuhimu wa kesi iliyofanya auawe; kwa sababu tunapaswa kujua ikiwa mashtaka dhidi ya Yesu yalikuwa ya kweli; na kwa sababu dhabihu ambayo Yesu alitoa kwa hiari ni muhimu sana kwetu na kwa wakati wetu ujao.—Luka 22:19; Yohana 6:40.
Wakati wa kesi ya Yesu, eneo la Palestina lilikuwa likitawaliwa na Waroma. Waroma waliwaruhusu viongozi wa dini ya Kiyahudi wa eneo hilo waongoze kesi za Wayahudi kulingana na sheria zao wenyewe lakini yaelekea hawakuwapa mamlaka ya kuwahukumu wahalifu adhabu ya kifo. Hivyo, Yesu alikamatwa na maadui wake wa dini ya Kiyahudi lakini akauawa na Waroma. Mahubiri ya Yesu yaliwaaibisha sana wakuu wa dini wa wakati huo hivi kwamba washiriki wa dini hiyo waliazimia kumuua Yesu. Hata hivyo, walitaka kuuawa kwake kuonekane kwamba kulikuwa halali kulingana *
na sheria. Utaratibu mzima uliotumika ili kutimiza jambo hilo ulimfanya profesa fulani wa sheria kuuita “uhalifu mbaya zaidi katika historia ya kesi zilizoendeshwa mahakamani.”Utaratibu wa Kisheria Wavunjwa
Sheria ambayo Musa aliwapa Waisraeli imetajwa kuwa “mfumo bora zaidi wa sheria kuwahi kuwekwa rasmi.” Hata hivyo, kufikia wakati wa Yesu, marabi ambao walipenda kutunga sheria kwa ajili ya kila jambo, walikuwa wameongeza sheria nyingi ambazo hazikuwa katika Biblia, na nyingi kati ya sheria hizo ziliingizwa katika Talmud. (Ona sanduku “Sheria za Wayahudi Katika Karne za Kwanza,” kwenye ukurasa wa 20.) Je, kesi ya Yesu iliendeshwa kulingana na sheria hizo za Biblia na zile ambazo hazikuwa katika Biblia?
Je, kukamatwa kwa Yesu kulitokana na ushahidi unaofanana uliotolewa na mashahidi wawili kuhusu kosa lilelile? Ili kukamatwa kuwe halali ushahidi ulipaswa kufanana. Huko Palestina katika karne ya kwanza, Myahudi ambaye alikuwa na hakika kwamba sheria imevunjwa alipeleka mashtaka yake mahakamani saa za kawaida za kazi. Mahakama hazingeanza kusikiliza kesi kabla ya kufanya uchunguzi wa mashtaka yaliyoletwa. Mashahidi wa shtaka lililotolewa ndio waliokuwa waendeshaji wa kesi. Kesi ingeanza kusikilizwa ikiwa kuna angalau ushahidi wa mashahidi wawili wa kosa lilelile. Ushahidi wao ungekuwa ndio msingi wa kuunda shtaka, na hivyo mshtakiwa angekamatwa. Ushahidi wa mtu mmoja haungekubaliwa. (Kumbukumbu la Torati 19:15) Hata hivyo, katika kesi ya Yesu, Wayahudi wenye mamlaka walitafuta “njia bora” ya kumwondolea mbali. Alikamatwa wakati “nafasi nzuri” ilipotokea—usiku na “bila umati kuwa karibu.”—Luka 22:2, 5, 6, 53.
Wakati Yesu alipokamatwa hakukuwa na shtaka lolote lililokuwa limewasilishwa. Makuhani na washiriki wa Sanhedrini, mahakama kuu ya Wayahudi, walianza kuwatafuta mashahidi baada tu ya kumkamata Yesu. (Mathayo 26:59) Hawakupata mashahidi wawili ambao ushahidi wao ulifanana. Hata hivyo, haikuwa kazi ya mahakama kutafuta mashahidi. “Kumshtaki mtu hasa kwa shtaka linalohusisha uhai, bila kutaja mapema kosa alilofanya, ni kitendo kiovu na cha kikatili,” anasema mwanasheria A. Taylor Innes ambaye pia ni mwandishi.
Umati uliomkamata Yesu ulimpeleka katika nyumba ya Anasi, ambaye zamani alikuwa Kuhani Mkuu, naye akaanza kumuuliza maswali. (Luka 22:54; Yohana 18:12, 13) Anasi alivunja sheria ambayo ilisema kwamba mashtaka yanayohusisha adhabu ya kifo yalipaswa kusikilizwa mchana, bali si usiku. Zaidi ya hayo, uchunguzi ulipaswa kufanywa katika mahakama ya wazi, bali si mahali pa faragha. Akijua kwamba hatua ya Anasi ilikuwa kinyume cha sheria, Yesu alimjibu: “Kwa nini unaniuliza? Waulize wale ambao wamesikia lile nililowaambia. Ona! Hawa wanajua lile nililosema.” (Yohana 18:21) Anasi alipaswa kuwahoji mashahidi, bali si mshtakiwa. Maneno ya Yesu yangemchochea hakimu mnyofu kufuata utaratibu uliowekwa, lakini Anasi hakutaka kufuata haki.
Maelezo ambayo Yesu alitoa yalifanya apigwe kofi na ofisa mmoja—huo haukuwa ujeuri pekee aliokabiliana nao usiku huo. (Luka 22:63; Yohana 18:22) Sheria iliyo katika kitabu cha Biblia cha Hesabu sura ya 35, kuhusu majiji ya makimbilio, inasema kwamba washtakiwa walipaswa kulindwa dhidi ya kutendwa vibaya hadi walipothibitika kuwa na hatia. Yesu alipaswa kupewa ulinzi huo pia.
Umati uliomkamata Yesu ulimpeleka nyumbani kwa Kuhani Mkuu Kayafa, ambako kesi isiyo halali iliendeshwa usiku. (Luka 22:54; Yohana 18:24) Wakivunja kanuni zote za haki, makuhani walitafuta “ushahidi wa uwongo juu ya Yesu ili wamuue,” hata hivyo, hakuna mashahidi wawili ambao ushahidi wao ulifanana kuhusiana na yale ambayo Yesu alisema. (Mathayo 26:59; Marko 14:56-59) Hivyo, kuhani mkuu alijaribu kumfanya Yesu ajifunge kwa maneno yake mwenyewe. Hivyo, akamuuliza: “Je, hujibu lolote? Watu hawa wanashuhudia nini juu yako?” (Marko 14:60) Mbinu hiyo ilikuwa kinyume cha sheria. “Kumuuliza mshtakiwa maswali, ili kutafuta nafasi ya kumnasa katika majibu anayotoa, ilikuwa ni uvunjaji wa haki ya kisheria,” anasema Innes, aliyenukuliwa awali.
Hatimaye watu hao waliamua kutumia maneno ambayo Yesu alisema. Alipoulizwa: “Wewe ndiye Kristo Mwana wa yule Mbarikiwa?” Yesu alijibu: “Mimi ndiye; nanyi mtamwona Mwana wa binadamu akiwa ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu akija pamoja na mawingu ya mbinguni.” Makuhani walisema kuwa Yesu amekufuru, na “wao wote wakamhukumu kwamba anastahili kufa.”—Marko 14:61-64. *
Kulingana na Sheria ya Musa, kesi ilipaswa kuendeshwa mahali palipo wazi. (Kumbukumbu la Torati 16:18; Ruthu 4:1) Kwa upande mwingine, kesi hii iliendeshwa kisiri. Hakuna mtu aliyejaribu au kuruhusiwa kumtetea Yesu. Hakuna uchunguzi uliofanywa kuthibitisha madai ya Yesu kwamba alikuwa Masihi. Yesu hakupewa nafasi ya kuita mashahidi wa kumtetea. Waamuzi hawakupiga kura ili kuamua ikiwa Yesu alikuwa na hatia au hakuwa na hatia.
Apelekwa Mbele ya Pilato
Kwa sababu yaelekea Wayahudi hawakuwa na mamlaka ya kutekeleza hukumu ya kifo, walimpeleka Yesu kwa gavana Mroma, Pontio Pilato. Swali la kwanza la Pilato lilikuwa: “Ni shtaka gani ambalo mnaleta juu ya mtu huyu?” Wakijua kuwa shtaka lao la kukufuru halingekuwa na maana yoyote kwa Pilato, Wayahudi walijaribu kumchochea Pilato amhukumu Yesu bila kufanya uchunguzi wowote. Wakasema: “Kama mtu huyu hangekuwa mkosaji, hatungemtia mkononi mwako.” (Yohana 18:29, 30) Pilato alikataa hoja hiyo na kuwalazimu Wayahudi kutunga shtaka jipya: “Tulimkuta mtu huyu akipindua taifa letu na kuwakataza watu wasimlipe Kaisari kodi na kusema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo mfalme.” (Luka 23:2) Hivyo, kosa la kukufuru likabadilishwa kwa ujanja na kuwa kosa la uhaini.
Shtaka la “kuwakataza watu wasimlipe Kaisari kodi” halikuwa la kweli, na watu waliomshtaki walijua hilo. Yesu alifundisha kinyume kabisa cha jambo hilo. (Mathayo 22:15-22) Kuhusu shtaka la kwamba Yesu alijifanya mwenyewe kuwa mfalme, Pilato aliona kuwa mtu huyo aliyesimama mbele yake hangehatarisha hata kidogo utawala wa Roma. Hivyo akasema: “Mimi sioni kosa lolote ndani yake.” (Yohana 18:38) Pilato aliendelea kushikilia maoni hayo muda wote wa kesi hiyo.
Mara ya kwanza Pilato alijaribu kumwachilia huru Yesu kwa kutumia desturi ya kumwachilia huru mfungwa wakati wa Pasaka. Hata hivyo, Pilato alimwachilia Baraba, ambaye alikuwa amepatikana na hatia ya mauaji na uchochezi.—Luka 23:18, 19; Yohana 18:39, 40.
Pilato alijaribu mara ya pili kumwachilia Yesu kwa kuwaridhisha makuhani. Alifanya hivyo kwa kuagiza Yesu apigwe, avikwe vazi la rangi ya Luka 23:22) Hata hivyo, hilo halikusaidia.
zambarau, avishwe taji la miiba, na kudhihakiwa. Kisha, akatangaza tena kwamba Yesu hana hatia. Ni kama Pilato alikuwa akisema: ‘Je, ninyi makuhani hamjatosheka hata sasa?’ Huenda alifikiri kuwa kwa sababu Yesu alikuwa amepigwa sana na Waroma hilo lingeridhisha tamaa yao ya kutaka kulipiza kisasi au wamwonee huruma. (‘Pilato alizidi kutafuta jinsi ya kumfungua Yesu. Lakini Wayahudi wakapaaza sauti, wakisema: “Ukimfungua mtu huyu, wewe si rafiki ya Kaisari. Kila mtu anayejifanya mfalme anasema vibaya juu ya Kaisari.”’ (Yohana 19:12) Wakati huo, Kaisari alikuwa Tiberio, maliki ambaye alikuwa na sifa ya kumuua mtu yeyote ambaye alionekana kuwa si mshikamanifu—hata maofisa wenye vyeo vya juu. Tayari Pilato alikuwa amewakasirisha Wayahudi, hivyo hakutaka kuendelea kuvutana nao, hasa kwa kosa la kutokuwa mshikamanifu. Umati ulisema maneno yaliyomtisha Pilato naye aliogopeshwa na vitisho hivyo. Kwa hiyo, akakubaliana na matakwa yao na kumtoa Yesu, mtu asiye na hatia, auawe.—Yohana 19:16.
Kuchunguza Ushahidi Uliotolewa
Wafafanuzi wengi wa mambo ya kisheria wamechanganua masimulizi ya vitabu vya Injili kuhusu kesi ya Yesu. Wamefikia mkataa kwamba kesi hiyo ilikuwa ya uwongo, na haikuendeshwa kwa haki. “Kesi hiyo ilikuwa kinyume kabisa cha utaratibu wa sheria za Waebrania na pia kanuni za haki kwa sababu ilianza kusikilizwa na kumalizwa, na hukumu ikatangazwa kabla hakujapambazuka,” akaandika mwanasheria mmoja. Profesa mmoja wa sheria anasema: “Kesi yote iliendeshwa kwa njia isiyo ya haki na isiyo ya kawaida, jambo lililofanya wale waliohusika katika kesi hiyo wawe na hatia ya kumuua Yesu.”
Yesu hakuwa na hatia. Hata hivyo, alijua kwamba kifo chake kilikuwa muhimu kwa ukombozi wa wanadamu watiifu. (Mathayo 20:28) Alipenda sana haki hivi kwamba alikubali kufanyiwa kesi iliyoendeshwa vibaya kuliko zote. Alifanya hivyo kwa ajili yetu sisi watenda dhambi. Hatupaswi kusahau hilo.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Makanisa ya dini zinazodai kuwa za Kikristo yanalaumiwa kwa kutumia masimulizi ya vitabu vya Injili yanayoeleza kuhusu kuuawa kwa Yesu ili kuwachochea watu wawapinge Wayahudi, lakini waandikaji wa Injili hawakuwa na mtazamo huo ingawa wao wenyewe walikuwa Wayahudi.
^ fu. 11 Kosa la kukufuru lilitia ndani kulitumia jina la Mungu bila heshima au kujitwika uwezo au mamlaka ambayo ni ya Mungu pekee. Watu waliomshtaki Yesu hawakuthibitisha kuwa alitenda kosa lolote kati ya hayo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]
Sheria za Wayahudi Katika Karne za Kwanza
Mapokeo ya Wayahudi yaliyopitishwa kwa mdomo ambayo yaliandikwa katika karne za mapema W.K. na yanayoaminika kuwa ya zamani sana, yanatia ndani kanuni zifuatazo:
▪ Katika kesi ambazo adhabu yake ni kifo, hoja za kutokuwa na hatia zilisikilizwa kwanza
▪ Waamuzi walipaswa kufanya kila jitihada ili kumwokoa mshtakiwa
▪ Waamuzi wangeweza tu kutoa hoja za kumtetea mshtakiwa bali si za kumtia hatiani
▪ Mashahidi walionywa kuhusu uzito wa daraka lao
▪ Mashahidi walihojiwa kila mmoja akiwa peke yake, bali si wakiwa pamoja
▪ Ushahidi ulipaswa kufanana katika mambo yote muhimu, kama vile, tarehe, mahali, wakati ambapo tukio lilitokea, na kadhalika
▪ Mashtaka katika kesi ambazo adhabu yake ni kifo yalipaswa kusikilizwa mchana na kumalizwa mchana
▪ Kesi ambazo adhabu yake ni kifo haikusikilizwa siku ya kuamkia Sabato au sherehe fulani
▪ Kesi ambazo adhabu yake ni kifo zingeweza kuanza na kumalizwa siku hiyohiyo ikiwa uamuzi ungempendelea mshtakiwa; ikiwa uamuzi haungempendelea mshtakiwa, kesi ingeamuliwa siku iliyofuata, wakati ambapo uamuzi ungetangazwa na adhabu kutekelezwa
▪ Kesi ambazo adhabu yake ni kifo zilisikilizwa na angalau waamuzi 23
▪ Waamuzi walipiga kura kwa zamu ili kumwachilia au kumhukumu mshtakiwa, wakianza na aliyekuwa mdogo zaidi kwa umri; waandishi waliandika maneno ya wale waliotaka mshtakiwa aachiliwe huru na ya wale waliotaka ahukumiwe
▪ Mshtakiwa angeweza kuachiliwa huru kwa kura 12, lakini ili mtu ahukumiwe kifo, kura 13 zilihitajika; ikiwa kura za kumhukumu mtu kifo zilikuwa 12, waamuzi wawili waliongezwa mara kwa mara ilipohitajika hadi uamuzi sahihi ulipofikiwa
▪ Uamuzi wa kwamba mshtakiwa ana hatia bila angalau mwamuzi mmoja kumtetea ulionwa kuwa si halali; ikiwa waamuzi wote walikubaliana kuwa mshtakiwa ana hatia, hiyo “ilionwa kuwa ni njama”
Jinsi Sheria Zilivyovunjwa Wakati wa Kesi ya Yesu
▪ Mahakama haikusikiliza hoja au mashahidi ambao wangemtetea Yesu
▪ Hakuna mwamuzi hata mmoja aliyejaribu kumtetea Yesu; walikuwa maadui wake
▪ Makuhani walitafuta mashahidi wa uwongo ili wamhukumu Yesu kifo
▪ Kesi iliendeshwa usiku kisiri, hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia
▪ Kesi ilifanywa siku moja, usiku wa kuamkia sherehe
▪ Hakukuwa na tuhuma, au mashtaka, kabla ya kukamatwa kwa Yesu
▪ Dai la Yesu kwamba yeye ndiye Masihi lilisemwa kuwa ni ‘kukufuru,’ lakini halikuchunguzwa
▪ Mashtaka yalibadilishwa kesi ilipopelekwa kwa Pilato
▪ Mashtaka yalikuwa ya uwongo
▪ Pilato hakumpata Yesu na hatia, hata hivyo, alimtoa ili auawe
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Mashahidi na Hatia ya Damu
Kabla Mashahidi hawajatoa ushahidi wao, mahakama za Wayahudi zilitoa onyo hili kuhusiana na thamani ya uhai katika kesi ambayo huenda hukumu yake ingekuwa kifo:
“Huenda una nia ya kutoa ushahidi kwa msingi wa mambo ya kuwaziwa, kukisia, au kile ambacho shahidi mmoja amemwambia mwingine; au huenda ukawa unafikiri, ‘Tumesikia jambo hilo kutoka kwa mtu anayeaminika.’ Au huenda hujui kwamba hatimaye tutakuhoji tukitumia maswali na uchunguzi unaofaa. Unapaswa kujua kwamba sheria zinazotumika katika kesi zinazohusu mali ni tofauti na sheria zinazotumika katika kesi za zinazohusu hukumu ya kifo. Katika visa vya kesi zinazohusu mali, mtu atalipa pesa na hivyo kujikomboa. Katika kesi ambazo adhabu yake ni kifo damu [ya mshtakiwa] na hata ile ya watoto wake ambao angewazaa [ambao walihukumiwa kimakosa] itadaiwa dhidi yake [yule aliyetoa ushahidi wa uwongo] hadi milele.”—Talmud ya Babiloni, Sanhedrini, 37a.
Ikiwa mshtakiwa angepatwa na hatia, mashahidi walipaswa kutekeleza hukumu ya kifo.—Mambo ya Walawi 24:14; Kumbukumbu la Torati 17:6, 7.