Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wafundishe Watoto Wako

Alikuwa Mkaidi Lakini Mwishowe Alitii

Alikuwa Mkaidi Lakini Mwishowe Alitii

JE, UMEWAHI kuwa mkaidi na kukataa kutii? * Labda ulitazama kipindi cha televisheni ambacho wazazi wako walikuambia usitazame. Huenda baadaye ulifikiria kuhusu jambo hilo na ukasikitika sana kwa kuwa hukutii. Kuna mtu mmoja ambaye mwanzoni alikataa kutii, mtu huyo ni Naamani. Acha tuone jinsi alivyosaidiwa ili asirudie kosa la kuwa mkaidi.

Hebu wazia tunaishi miaka 3,000 iliyopita. Naamani ni mmoja kati ya maofisa wakuu katika jeshi la Siria. Yeye huwapatia wanajeshi amri, nao humtii. Lakini Naamani anapatwa na ugonjwa mbaya wa ngozi unaoitwa ukoma. Ugonjwa huo unafanya ngozi yake ionekane vibaya, na pia huenda anahisi uchungu mwingi.

Mke wa Naamani ana msichana mdogo anayemsaidia kazi za nyumbani. Msichana huyo ametoka Israeli. Siku moja msichana huyo anamwambia mke wa Naamani kuhusu mwanamume fulani anayeitwa Elisha katika nchi ya Israeli. Anamwambia kwamba mwanamume huyo anaweza kumponya mume wake. Naamani anaposikia jambo hilo, mara moja anataka kwenda kumwona Elisha. Anabeba zawadi nyingi na kusafiri pamoja na wanajeshi wake hadi Israeli. Naamani anaenda kwa mfalme wa Israeli ili kumjulisha kusudi lake la kutembelea nchi hiyo.

Elisha anasikia kuhusu jambo hilo, naye anamtumia mfalme ujumbe wa kwamba amruhusu Naamani aende kwake. Naamani anapofika, Elisha anatuma mjumbe amwambie aende akaoge mara saba ndani ya Mto Yordani. Elisha anasema jambo hilo litamponya Naamani. Unafikiri Naamani anahisije anapoambiwa hivyo?

Anakasirika sana. Anakuwa mkaidi na kukataa kumtii nabii wa Mungu. Anawaambia wanajeshi wake: ‘Kwetu kuna mito bora ya kuoga.’ Kisha, Naamani anaanza kuondoka. Lakini unajua swali ambalo wanajeshi wake wanamuuliza?— ‘Ikiwa nabii angekuambia ufanye jambo gumu, si ungelifanya? Basi kwa nini usifanye jambo hilo rahisi analokuambia ufanye?’

Naamani anasikiliza na kutenda kama alivyoambiwa na wanajeshi wake. Anajitumbukiza ndani ya mto mara sita na kutoka. Anapotoka baada ya kujitumbukiza mara ya saba, Naamani anastaajabu sana, ugonjwa wake wa ngozi umeisha! Amepona kabisa! Mara moja anasafiri mwendo wa kilomita 48 na kurudi kwa Elisha ili kumshukuru. Anataka kumpa Elisha zawadi za bei ghali, lakini nabii huyo anakataa.

Basi, Naamani anamwomba Elisha jambo fulani. Je, unajua jambo ambalo Naamani anamwomba Elisha?— ‘Nipe udongo mzigo wa nyumbu wawili niende nao nyumbani.’ Je, unajua kwa nini anaomba udongo huo?— Naamani anasema kwamba anataka kutoa zawadi za dhabihu kwa Mungu juu ya udongo kutoka Israeli, nchi ya watu wa Mungu. Kisha, Naamani anaahidi kwamba hataabudu miungu mingine isipokuwa Yehova! Naamani ameacha kuwa mkaidi, sasa anamtii Mungu wa kweli.

Je, umeona jinsi unavyoweza kuwa kama Naamani?— Ikiwa umekuwa mkaidi kama yeye, wewe pia unaweza kubadilika. Unaweza kukubali usaidiwe na uache kuwa mkaidi.

Soma Katika Biblia Yako

^ fu. 3 Kama unasoma sehemu hii pamoja na mtoto, unapoona kistari kama hiki (—), tua na umtie moyo mtoto atoe maoni yake.