Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wasomaji Wetu Wanauliza . . .

Mungu atahisije nikitumia tumbaku?

Mungu atahisije nikitumia tumbaku?

▪ Mtu mwenye mtazamo unaofaa anaweza kuuliza swali hilo, kwa sababu hakuna sheria yoyote katika Biblia inayotaja bidhaa za tumbaku. Je, inamaanisha kwamba ni vigumu kutambua maoni ya Mungu kuhusu jambo hilo? Sivyo hata kidogo.

Biblia inasema kwamba “Andiko lote limeongozwa na roho ya Mungu.” (2 Timotheo 3:16) Maandiko yana kanuni na maneno yaliyo wazi ambayo yanafunua jinsi Mungu anavyotaka tutunze afya yetu. Kwanza, acheni tuchunguze mambo ambayo watafiti wamegundua kuhusu madhara ya tumbaku kwa afya ya mwanadamu. Kisha, tutachunguza jinsi kanuni za Biblia zinavyohusiana na utafiti huo.

Tumbaku huharibu afya ya mtumiaji na ni chanzo kikuu cha kifo kinachoweza kuepukwa. Nchini Marekani, asilimia ishirini ya vifo husababishwa na tumbaku. Katika nchi hiyo, tumbaku huua watu wengi zaidi kushinda “pombe, dawa za kulevya, uuaji, kujiua, aksidenti za magari, na UKIMWI kwa kujumlishwa pamoja,” inasema ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya ya Marekani.

Wale wanaovuta tumbaku huwadhuru wengine. Kiwango chochote cha moshi wa sigara ni hatari. Watu wasiovuta sigara ambao wanapumua moshi wa wavutaji wanakabili hatari kwa asilimia 30 hivi ya kupata kansa ya mapafu na ugonjwa wa moyo. Katika miaka ya hivi karibuni, madaktari wamegundua hatari nyingine ambayo wanaiita “moshi usioonekana.” Usemi huo unarejelea kemikali zinazobaki kwenye nguo, mazulia, na maeneo mengine na zinaendelea kuwepo kwa muda mrefu hata baada ya moshi unaoonekana kwisha. Kemikali hizo zenye sumu hasa hudhuru afya ya watoto na zinaweza kuathiri uwezo wao wa kujifunza.

Tumbaku husababisha uraibu. Humfanya mtumiaji awe mtumwa wa tabia yenye kudhuru. Kwa kweli, watafiti wanaamini kwamba uraibu wa nikotini, ambayo ni kemikali kuu katika tumbaku, ni mojawapo ya uraibu mgumu zaidi kuacha.

Kanuni za Biblia zinahusianaje na mambo hayo. Ona yafuatayo:

Mungu anataka tuheshimu uhai. Katika Sheria ambayo Mungu aliwapa Waisraeli, alionyesha kwamba wale wanaotaka kumpendeza ni lazima waheshimu uhai wa binadamu. (Kumbukumbu la Torati 5:17) Waisraeli walipaswa kujenga ukuta wa ukingoni, au ukuta mfupi, kandokando ya ukingo wa dari juu ya nyumba zao. Kwa nini? Dari zilikuwa tambarare na zilitumiwa kama sebule. Ukuta ulizuia washiriki wa familia na watu wengine wasianguke na kuumia au kufa. (Kumbukumbu la Torati 22:8) Zaidi ya hayo, Waisraeli walipaswa kuhakikisha kwamba wanyama wao hawakuwaumiza watu wengine. (Kutoka 21:28, 29) Mtu anayetumia tumbaku anavunja kanuni zinazohusika katika sheria hizo. Anaharibu afya yake kimakusudi. Kwa kuongezea, tabia yake ya kuvuta sigara inahatarisha afya ya watu walio karibu naye.

Mungu anataka tumpende na pia tuwapende jirani zetu. Yesu Kristo alisema kwamba wafuasi wake wanapaswa kutii zile amri mbili kuu. Ni lazima wampende Mungu kwa moyo, nafsi, akili, na nguvu zao zote na kuwapenda jirani zao kama wao wenyewe. (Marko 12:28-31) Kwa kuwa uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu, mtu anayetumia tumbaku anaonyesha kwa njia kubwa kwamba haheshimu zawadi hiyo na hivyo hampendi Mungu. (Matendo 17:26-28) Tabia za mtu huyo zinaweza kuwadhuru sana wengine, na hivyo hawezi kamwe kudai kuwa anampenda jirani.

Mungu anataka tuepuke mazoea machafu. Biblia inawaagiza Wakristo wajisafishe wenyewe kutoka kwa “kila unajisi wa mwili na roho.” (2 Wakorintho 7:1) Ni wazi kwamba utumiaji wa tumbaku humchafua mtu. Wale wanaotaka kuacha kuvuta tumbaku ili wamtumikie Mungu wanakabili hali ngumu. Lakini kwa msaada wa Mungu wanaweza kuacha uraibu huo wenye kuchafua.