Maisha Katika Nyakati za Biblia—Mchungaji
“Atalichunga kundi lake mwenyewe kama mchungaji. Atawakusanya pamoja wana-kondoo kwa mkono wake; naye atawabeba katika kifua chake.”—ISAYA 40:11.
WACHUNGAJI wanatajwa mara nyingi katika Biblia, kuanzia kitabu cha kwanza, Mwanzo, mpaka kitabu cha mwisho, Ufunuo. (Mwanzo 4:2; Ufunuo 12:5) Wanaume maarufu kama vile Abrahamu, Musa, na Mfalme Daudi walikuwa wachungaji. Mtunga-zaburi Daudi alieleza vizuri wajibu na mahangaiko ya mchungaji mzuri. Na zaburi iliyoandikwa na Asafu inamtaja Daudi kuwa mchungaji juu watu wa kale wa Mungu.—Zaburi 78:70-72.
Miaka ya baadaye, katika siku za Yesu, bado uchungaji ulikuwa kazi muhimu. Yesu alijirejezea kuwa “mchungaji mwema” na mara kwa mara alitumia sifa za mchungaji mwema kufundisha mambo muhimu. (Yohana 10:2-4, 11) Hata Mweza-Yote, Yehova Mungu, anafananishwa na “mchungaji.”—Isaya 40:10, 11; Zaburi 23:1-4.
Wachungaji walitunza wanyama wa aina gani? Kazi ya mchungaji ilihusisha nini? Na tunaweza kujifunza nini kutokana na wafanyakazi hao wenye bidii?
Kondoo na Mbuzi
Inaelekea wachungaji katika Israeli la kale walichunga kondoo wa jamii tofauti-tofauti kutia ndani aina mbalimbali za kondoo kutoka Siria wenye mikia minene na manyoya mengi. Kondoo dume wa jamii hiyo wana pembe, lakini kondoo jike hawana pembe. Wanyama hao watulivu huongozwa kwa urahisi na hawawezi kujilinda kutokana na mazingira na wanyama hatari.
Wachungaji pia walitunza mbuzi. Mbuzi hao walikuwa wa rangi nyeusi au kahawia. Masikio yao marefu yaliraruliwa kwa urahisi na miiba na vichaka walipokuwa wakipanda kwenye milima yenye miamba na kulisha vichakani.
Sikuzote wachungaji walikabiliana na tatizo la kuwafundisha kondoo na mbuzi watii maagizo yao. Hata hivyo wachungaji wema walitunza kwa wororo wanyama waliokuwa wakiwachunga, na hata kuwaita kwa majina.—Yohana 10:14, 16.
Majira ya Mchungaji
Katika majira ya kuchipua, huenda kila siku mchungaji alichukua wanyama kutoka katika zizi lililokuwa karibu na nyumba yake ili awalishe majani kwenye maeneo ya malisho yaliyokuwa karibu na kijiji. Katika majira hayo, kondoo na mbuzi walizaana na hivyo kuongeza idadi ya kundi. Wakati huo, wafanyakazi wangewanyoa kondoo manyoya, na hiyo ilikuwa pindi ya sherehe!
Huenda mwanakijiji angekuwa na kondoo wachache. Hivyo, angekodisha mchungaji ambaye angeunganisha kundi lake dogo na kundi lingine. Wachungaji waliokodishwa walikuwa na mazoea ya kutowajali sana wanyama wa watu wengine huku wakiwajali wanyama wao.—Yohana 10:12, 13.
Baada ya mashamba yaliyokuwa karibu na kijiji kuvunwa, mchungaji angewaruhusu kondoo wake wale mimea iliyochipuka na nafaka iliyoachwa kwenye makapi. Majira ya joto yalipoanza, wachungaji waliwapeleka wanyama wao kulisha katika maeneo ya juu yaliyokuwa na baridi. Kwa siku nyingi, wachungaji wangefanya kazi na kulala nje, na kuwaruhusu wanyama walishe kwenye miinuko yenye nyasi nyingi huku wakiwalinda kondoo wakati wa usiku. Nyakati fulani, mchungaji angewaingiza wanyama wake ndani ya pango usiku kucha ambamo wangelindwa kutokana na mbweha na fisi. Ikiwa kondoo wangeshtuka usiku kwa kusikia mlio wa fisi, sauti ya mchungaji ingewatuliza.
Kila jioni, mchungaji alihesabu kondoo na kuhakikisha walikuwa na afya nzuri. Asubuhi angewaita na kundi zima lingemfuata kwenda malishoni. (Yohana 10:3, 4) Wakati wa mchana, wachungaji wangewapeleka wanyama kwenye vidimbwi vya maji baridi ili wanywe. Vidimbwi hivyo vilipokauka, wachungaji hao wangewapeleka kwenye visima na kuwachotea maji.
Karibu na mwisho wa kiangazi, mchungaji angewapeleka kondoo kwenye maeneo tambarare na mabonde ya pwani. Majira ya mvua yalipoanza, angewarudisha nyumbani ili wakae
ndani ya mazizi wakati wa majira ya baridi kali. Kama hangefanya hivyo, wanyama wangekufa kutokana na mvua kubwa ya mawe na theluji. Kuanzia mwezi wa Novemba mpaka majira ya kuchipua, wachungaji hawangelisha wanyama wao nje.Walikuwa na Vifaa vya Kazi
Mavazi ya mchungaji yalikuwa mepesi lakini thabiti. Ili kujilinda kutokana na baridi ya usiku, huenda alivaa nguo ya kujitanda iliyotengenezwa kwa ngozi, yenye manyoya upande wa ndani. Juu ya mwili wake, angevaa vazi refu. Viatu vyake vilimlinda asidungwe na miiba na mawe, na kichwani alijifunga kitambaa kilichofumwa kwa sufu.
Kwa kawaida, vifaa vya mchungaji vilitia ndani vitu vifuatavyo: Mkoba uliotengenezwa kwa ngozi, uliokuwa na vyakula, kama vile mkate, zeituni, matunda yaliyokaushwa, na jibini (1); rungu, ambayo ilikuwa silaha muhimu, kwa kawaida ilikuwa na urefu wa mita moja na nundu yake ilikuwa na vigae vilivyochongoka (2); kisu (3); fimbo, ambayo mchungaji angetumia kuegemea alipokuwa akitembea au kupanda mlima (4); chombo cha kibinafsi cha kubebea maji (5); ndoo ya kuchota maji kwenye visima virefu iliyotengenezwa kwa ngozi na ambayo ingeweza kukunjwa (6); kombeo, alilotumia kurusha mawe ili kuwarudisha kondoo na mbuzi kwenye kundi na kuwafukuza wanyama mwitu waliokuwa karibu (7); na filimbi ya utete, ambayo alipiga ili kujitumbuiza na kuwatuliza wanyama (8).
Kutokana na wanyama, mchungaji alipata vyakula muhimu kama vile maziwa na nyama. Alitumia manyoya na ngozi kutengeneza mavazi na chupa na vilevile alibadilishana bidhaa hizo ili apate vitu vingine. Manyoya ya mbuzi yalisokotwa na kuwa vitambaa, na kondoo na mbuzi walitumiwa kama dhabihu.
Mfano wa Kuigwa
Wachungaji wema walikuwa wenye bidii, wenye kutegemeka, na wajasiri. Hata walihatarisha maisha yao ili kulinda makundi yao.—1 Samweli 17:34-36.
Haishangazi kwamba Yesu na wanafunzi wake walitumia wachungaji kama mfano wa kuigwa na waangalizi Wakristo. (Yohana 21:15-17; Matendo 20:28) Kama mchungaji mwema wa nyakati za Biblia, leo waangalizi wa makutaniko wanajitahidi ‘kulichunga kundi la Mungu lililo chini ya uangalizi wao, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupenda; wala si kwa kupenda pato lisilo la haki, bali kwa hamu.’—1 Petro 5:2.
(Ona nakala iliyochapishwa)