Je, Wajua?
Je, Yesu alikosea aliposema kuhusu chumvi kupoteza nguvu zake?
Katika Mahubiri yake ya Mlimani, Yesu aliwaambia wafuasi wake hivi: “Ninyi ndio chumvi ya dunia; lakini chumvi ikipoteza nguvu zake, ladha yake itarudishwaje? Haitumiki tena kwa kitu chochote bali ni ya kutupwa nje ili ikanyagwe-kanyagwe na watu.” (Mathayo 5:13) Chumvi hutumiwa kuhifadhi vitu. Hivyo, yaelekea Yesu alimaanisha kwamba wanafunzi wake wanaweza na wanapaswa kuwahifadhi wengine wasije wakaharibiwa kiroho na kiadili.
Hata hivyo, kitabu The International Standard Bible Encyclopedia kinasema hivi kuhusu maelezo ya Yesu juu ya chumvi kupoteza nguvu zake: “Chumvi iliyopatikana katika Bahari ya Chumvi ilikuwa imechanganyika na madini mengine; hivyo chumvi hiyo ilipotolewa kutoka kwenye mchanganyiko huo iliacha madini yasiyo na ladha yoyote.” Kwa hiyo, inaeleweka Yesu aliposema kwamba mabaki hayo “[hayatumiki] tena kwa kitu chochote bali ni ya kutupwa nje.” “Ingawa mchanganyiko huo ulifanya chumvi ya Bahari ya Chumvi kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na ya bahari nyingine,” kitabu hicho kinaongezea, “kwa kuwa chumvi hiyo ilipatikana kwa urahisi (iliokotwa kando-kando ya bahari) ilikuwa chanzo kikuu cha chumvi iliyotumiwa Palestina.”
Mfano wa Yesu wa kupoteza sarafu moja ya drakma ulikuwa na maana gani kwa wasikilizaji wake?
Yesu alisimulia mfano wa mwanamke ambaye baada ya kupoteza sarafu moja kati ya sarafu kumi za drakma alizokuwa nazo, alichukua taa na kufagia nyumba yake kwa makini hadi alipoipata. (Luka 15:8-10) Nyakati za Yesu, thamani ya sarafu moja ya drakma ilikuwa karibu sawa na mshahara wa siku moja, hivyo, mwanamke huyo alipoteza kiasi kikubwa cha pesa. Vilevile, hali ambayo alisimulia ilikuwa jambo la kweli katika maisha kwa sababu nyinginezo.
Vitabu vingine vya utafiti vinaonyesha kwamba wakati fulani wanawake walitumia sarafu hizo kama mapambo. Hivyo, huenda Yesu alikuwa akirejelea sarafu ambayo ilikuwa sehemu ya pambo la kike la familia lililorithiwa au sehemu ya malipo ya mahari. Iwe hali ilikuwa hivyo au la, inaeleweka kwamba mwanamke huyo alihangaika sana kupata ile sarafu moja iliyopotea kati ya zile sarafu kumi.
Hata hivyo, nyumba za watu wa kawaida nyakati za Yesu zilijengwa kwa njia ambayo ilizuia mwangaza na joto lisiingie. Nyumba nyingi zilijengwa zikiwa na madirisha machache au bila dirisha. Sakafu ilifunikwa na nyasi au matawi makavu ya miti mbalimbali. Ikiwa sarafu ingeanguka, ingekuwa vigumu kuipata. “Hivyo,” anasema msomi mmoja, “kitu kidogo, kama kipande cha pesa, kilipopotea mahali kama hapo, kuwasha taa na kufagia nyumba ndiyo iliyokuwa mbinu ya kawaida kabisa iliyotumiwa kukitafuta.”