Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Wayahudi wa karne ya kwanza walitayarishaje wafu kabla ya kuwazika?

Wayahudi walizika wafu muda mfupi baada ya kufa, kwa kawaida siku ileile. Kuna sababu mbili kwa nini walifanya hivyo. Kwanza, maiti huoza haraka katika mazingira ya joto huko Mashariki ya Kati. Pili, wakati huo, watu walifikiri kuacha maiti bila kuizika ni kumkosea heshima mtu aliyekufa na familia yake.

Vitabu vya Injili na kitabu cha Matendo vina rekodi nne hivi za mazishi yaliyofanyika siku ileile ambayo mtu alikufa. (Mathayo 27:57-60; Matendo 5:5-10; 7:60–8:2) Karne nyingi mapema, Raheli mke mpendwa wa Yakobo alikufa familia yake ilipokuwa safarini. Badala ya kupeleka mwili huo hadi mahali pa kuzikia pa familia, Yakobo alimzika katika kaburi “njiani kuelekea . . . Bethlehemu.”—Mwanzo 35:19, 20, 27-29.

Masimulizi ya Biblia kuhusu mipango ya mazishi yanaonyesha kwamba Wayahudi walitayarisha maiti kwa uangalifu sana kabla ya kuzika. Marafiki pamoja na watu wa familia waliosha maiti, wakaipaka manukato na mafuta mazuri, na kuifunga kwa vitambaa. (Yohana 19:39, 40; Matendo 9:36-41) Majirani na wengine walikuja ili kuomboleza na kufariji familia.—Marko 5:38, 39.

Je, Yesu alizikwa kulingana na desturi za Wayahudi?

Wayahudi wengi walizika wafu kwenye mapango au makaburi yaliyochongwa kwenye miamba laini inayopatikana katika sehemu nyingi za Israeli. Kwa kufanya hivyo, walifuata mfano wa wazee wa ukoo. Abrahamu, Sara, Isaka, Yakobo, na wengine walizikwa kwenye pango la Makpela karibu na Hebroni.—Mwanzo 23:19; 25:8, 9; 49:29-31; 50:13.

Yesu alizikwa katika kaburi lilichongwa kwenye mwamba. (Marko 15:46) Kwa kawaida makaburi kama hayo yalikuwa na mlango mwembamba. Ndani kulikuwa na sehemu zilizochongwa kwenye mwamba mfano wa rafu za vitabu, ambapo maiti ziliwekwa. Baada ya mwili kuoza, mifupa iliyokauka ilikusanywa na kuwekwa kwenye sanduku la mifupa, kama ilivyokuwa desturi wakati wa Yesu. Hivyo, familia ilipata nafasi katika kaburi ya kuzika wafu wakati ujao.

Siku ya Sabato Wayahudi hawakuruhusiwa na Sheria ya Musa kufanya mipango ya mazishi. Kwa sababu Yesu alikufa saa tatu hivi kabla ya Sabato kuanza, Yosefu wa Arimathea na wengine walimzika Yesu bila kukamilisha matayarisho. (Luka 23:50-56) Hivyo, baadhi ya rafiki za Yesu walienda kwenye kaburi lake baada ya Sabato, ili kukamilisha matayarisho hayo.—Marko 16:1; Luka 24:1.