Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 HABARI KUU | NI NANI ANAYEWEZA KUTABIRI WAKATI UJAO?

Utabiri Fulani Hutimia Lakini Mwingi Hautimii

Utabiri Fulani Hutimia Lakini Mwingi Hautimii

Je, ungependa kujua wakati wako ujao? Wengi wangependa kujua. Watu wengi hutabiri wakati ujao, hata hivyo matokeo hutofautiana. Hebu chunguza mambo yafuatayo:

  • WANASAYANSI hutumia pesa nyingi na vifaa vya kisasa kutabiri mambo mbalimbali kama vile, madhara yatakayoletwa na uchafuzi wa mazingira au kutabiri hali ya hewa.

  • WACHANGANUZI hutabiri kuhusu hali ya biashara na siasa. Warren Buffett, mmoja kati ya watu matajiri zaidi ulimwenguni, amesifiwa sana kwa uwezo wake wa kuchanganua na kufanikiwa kibiashara. Mchanganuzi mwingine Nate Silver, huchanganua takwimu ili kutabiri mambo mengi kutia ndani siasa za Marekani na hata tuzo za waigizaji wa filamu za Hollywood.

  • MAANDISHI YA KALE yamefafanuliwa kuwa unabii. Watu fulani husema kwamba mambo yaliyoandikwa na Michel de Notredame (Nostradamus) katika karne ya 16 yanatimia sasa. Kalenda ya Wamaya iliyokwisha Desemba 21, 2012, ilifafanuliwa na wengi kuwa ishara ya kipindi cha msiba mkubwa duniani.

  • VIONGOZI WA KIDINI mara kwa mara hutabiri kuhusu matukio yenye kutisha ulimwenguni ili kuwaonya wanadamu na kujipatia wafuasi. Harold Camping na wafuasi wake walitangaza kwa bidii kwamba ulimwengu ungeangamizwa mwaka 2011. Lakini mpaka sasa bado mwisho haujafika.

  • WABASHIRI hudai kwamba wana uwezo wa kipekee wa kutabiri kuhusu wakati ujao. Edgar Cayce na Jeane Dixon walitabiri kwa usahihi matukio fulani ya karne ya 20. Hata hivyo, mambo mengi waliyotabiri hayakutimia. Kwa mfano, Dixon alitabiri kwamba Vita vya Tatu vya Ulimwengu vingetokea mwaka wa 1958, na Cayce alisema kwamba jiji la New York lingezama na kuingia baharini katika miaka ya 1970.

Je, kuna njia yoyote inayotegemeka ya kujua kuhusu wakati ujao? Ni vizuri kujiuliza swali hilo. Kama ungejua mambo yatakayotukia wakati ujao ungefanya marekebisho fulani maishani.