Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

mustafahacalaki/DigitalVision Vectors via Getty Images

ENDELEA KUKESHA!

Teknolojia ya Akili Bandia—Ni Baraka au Laana?​—Biblia Inasema Nini?

Teknolojia ya Akili Bandia—Ni Baraka au Laana?​—Biblia Inasema Nini?

 Hivi karibuni, viongozi wa ulimwengu, wanasayansi, na wanateknolojia wamekuwa wakijadili uwezo wa teknolojia ya akili bandia, inayofahamika kwa Kiingereza kama artificial intelligence (AI). Ingawa wamesema kwamba ina faida, wanahofia pia uwezekano wake wa kutumiwa vibaya.

  •   “AI ni mojawapo wa teknolojia zenye nguvu zaidi leo, na ina uwezo wa kuboresha maisha ya watu . . . Wakati huohuo, AI ina uwezo wa kuongeza kwa kadiri kubwa hatari za kiusalama, hatari kwenye mifumo ya ulinzi, kuingilia haki na faragha za binadamu, na kuwafanya watu wapoteze imani katika serikali za kidemokrasia.”​—Kamala Harris, makamu wa rais wa Marekani, Mei 4, 2023.

  •   Kikundi cha kimataifa cha madaktari na wataalamu wa afya kilichoongozwa na Dakt. Frederik Federspiel kiliandika hivi katika makala iliyotolewa Mei 9, 2023, katika jarida BMJ Global Health a: “Ingawa teknolojia ya akili bandia (AI) inaweza kusaidia sana katika utunzaji wa wagonjwa, inatokeza pia hatari kadhaa kwa afya na hali njema ya wanadamu.”

  •   “Huenda tayari AI inatumiwa kueneza habari za uwongo. Hivi karibuni, huenda ikaanza kuwafanya watu wapoteze kazi. Watu wanaohofia madhara yanayotokezwa na teknolojia wanasema kwamba kadiri muda unavyopita, huenda AI ikawa hatari kwa jamii ya wanadamu.”​—The New York Times, Mei 1, 2023.

 Muda utaonyesha ikiwa teknolojia ya AI itatumiwa kwa njia nzuri au mbaya. Biblia inasema nini?

Kwa nini jitihada za wanadamu zinatokeza hali ya sintofahamu?

 Biblia inaonyesha kwa nini wanadamu hawawezi kuwa na uhakika kwamba maendeleo yao ya kiteknolojia yatatumiwa tu kwa njia nzuri.

  1.  1. Hata watu wanapokuwa na nia nzuri, hawawezi kuona mbele na kutambua madhara ya matendo yao.

    •   “Kuna njia inayoonekana kuwa sawa machoni pa mtu, lakini mwishowe inaongoza kwenye kifo.”​—Methali 14:12.

  2.  2. Mtu hawezi kudhibiti ikiwa wengine watatumia kazi yake kwa njia nzuri au mbaya.

    •   “Ni lazima nimwachie [kazi yangu] mtu atakayekuja baada yangu. Na ni nani anayejua ikiwa atakuwa mwenye hekima au mjinga? Lakini bado atamiliki vitu vyote nilivyotafuta kwa jitihada nyingi na hekima chini ya jua.”​—Mhubiri 2:18, 19.

 Hali hiyo ya sintofahamu inakazia kwa nini tunahitaji mwongozo wa Muumba wetu.

Tunaweza kuweka wapi tegemeo letu?

 Muumba wetu anaahidi kwamba hatawaruhusu wanadamu au teknolojia yoyote iliyobuniwa na wanadamu iangamize dunia au wanadamu.

  •   “Dunia inadumu milele.”​—Mhubiri 1:4.

  •   “Waadilifu wataimiliki dunia, nao wataishi humo milele.”​—Zaburi 37:29.

 Katika Biblia, Muumba wetu ametupatia mwongozo ambao hatimaye utatokeza wakati ujao wenye amani na usalama. Ili ujifunze mengi zaidi kuhusu kile ambacho Biblia inasema, soma makala zenye kichwa “Je, Kuna Mwongozo Unaotegemeka wa Kuwa na Maisha Bora ya Wakati Ujao?” na “Tumaini Bora la Wakati Ujao.”

a Kutoka kwenye makala “Hatari ya Teknolojia ya Akili Bandia kwa Afya na Uwepo wa Wanadamu,” iliyoandikwa na Frederik Federspiel, Ruth Mitchell, Asha Asokan, Carlos Umana, na David McCoy.