Jinsi ya Kuishi Ukiwa na Pesa Kidogo
Je, umelazimika kuishi ukiwa na pesa kidogo zaidi kwa sababu hali za kiuchumi zimekuwa ngumu? Magonjwa ya kuenea, misiba ya asili, misukosuko ya kisiasa, na vita vinaweza kuathiri uchumi. Ingawa kupoteza kipato kwa ghafla kunaweza kukusababishia mkazo, kuchukua hatua zinazofaa zinazotegemea hekima ya Biblia kunaweza kukusaidia kuishi ukiwa na pesa kidogo.
1. Kubali hali yako.
Kanuni ya Biblia: “Ninajua jinsi ya . . . kuwa na wingi na pia jinsi ya kuishi bila kitu.”—Wafilipi 4:12.
Ingawa utakuwa na pesa kidogo kuliko awali, unaweza kubadilikana kulingana na hali zako mpya za kiuchumi. Ukikubali hali yako upesi na kuanza kubadilikana itakuwa rahisi kwako na kwa familia yako kukabiliana na hali hiyo.
Chunguza ni msaada gani unaoweza kupata kutoka kwa serikali au kwa mashirika ya kutoa msaada. Tenda upesi, kwa kuwa mara nyingi programu hiyo huwapa wahusika muda mfupi wa kuomba msaada.
2. Shirikianeni mkiwa familia.
Kanuni ya Biblia: “Mipango huvunjika watu wasiposhauriana, lakini mambo hufanikiwa kupitia washauri wengi.”—Methali 15:22.
Zungumzia hali yenu pamoja na mwenzi wako na watoto. Mkiwa na mawasiliano mazuri, mnaweza kumsaidia kila mtu katika familia kuelewa na kuunga mkono mabadiliko yanayohitajika. Na nyote mnaposhirikiana kubana matumizi na kuepuka kupoteza chochote, pesa mnazopata zinaweza kuwasaidia zaidi.
3. Panga bajeti.
Kanuni ya Biblia: “[Keti] kwanza na kuhesabu gharama.”—Luka 14:28.
Unapolazimika kuishi ukiwa na pesa kidogo, ni muhimu sana ujue jinsi pesa zako zote zinavyotumika. Panga bajeti kwanza kwa kuandika pesa unazofikiri utapata kila mwezi kwa kutegemea hali yako mpya. Kisha, andika gharama zako zote na matumizi yako ya kawaida, hata ingawa unajua lazima yabadilike. Unapoorodhesha matumizi ya kila mwezi, jaribu kutia ndani kiasi cha pesa unachotaka kuhifadhi kwa ajili ya gharama zisizotarajiwa au hali za dharura.
Dokezo: Unapochunguza matumizi yako, usisahau kuorodhesha matumizi madogo-madogo. Huenda ukashangaa kuona jinsi matumizi hayo yanavyogharimu pesa nyingi yanapojumlishwa baada ya muda. Kwa mfano, mwanamume mmoja alipochunguza matumizi yake, alitambua kwamba kila mwaka alikuwa akitumia mamia kadhaa ya dola kununua peremende!
4. Amua ni matumizi gani muhimu zaidi na ufanye mabadiliko.
Kanuni ya Biblia: “Mhakikishe mambo muhimu zaidi.”—Wafilipi 1:10.
Linganisha mapato na matumizi yako. Amua ni nini unachoweza kuondoa au kupunguza ili kuishi kupatana na mapato yako yaliyopungua. Chunguza mambo yafuatayo:
Usafiri. Ikiwa una gari zaidi ya moja, je, unaweza kuuza moja? Ikiwa gari lako ni la kifahari, je, unaweza kulibadili na lisilo la kifahari? Je, unaweza kutumia usafiri wa umma au baiskeli na uuze gari lako?
Burudani. Je, unaweza kufuta kwa muda maandikisho ya vituo vya Intaneti, satelaiti, au televisheni? Je, unaweza kupata njia za badala za kujiburudisha za gharama ya chini zaidi, kama vile, kupitia maktaba za sinema, vitabu kwenye mtandao, au vitabu vya kusikiliza vinavyotolewa bila malipo?
Maji, umeme, mafuta. Zungumzeni mkiwa familia jinsi ya kupunguza matumizi ya vitu hivyo. Huenda ukaona kuwa ni jambo dogo kuzima taa na kutumia maji kidogo zaidi kuoga, lakini mazoea hayo yanaweza kuokoa pesa.
Chakula. Epuka kula mkahawani. Badala yake, pika chakula nyumbani. Panga utakachopika, ikiwezekana nunua na upike chakula kingi, na utumie kinachobaki. Unapoenda dukani andika orodha ya vitu unavyotaka ili usinunue vitu ambavyo hukupangia. Nunua mazao ya shambani yaliyo katika msimu. Epuka kununua vyakula visivyo na lishe. Jaribu kuwa na shamba la mboga.
Mavazi. Nunua mavazi wakati tu unapohitaji kubadili mavazi yaliyochakaa, si ili kuendana na mtindo wa kisasa. Tafuta wakati ambapo vitu vimepunguzwa bei au mtumba ulio katika hali nzuri. Anika nguo zako kwenye kamba ikiwa hali ya hewa inaruhusu; hilo litapunguza gharama ya kukausha kwa mashine.
Ununuzi wa Wakati Ujao. Kabla ya kununua kitu, jiulize: ‘Je, nina uwezo wa kukinunua? Je, kweli ninakihitaji?’ Je, kwa sasa unaweza kuepuka kununua vifaa vipya na vya kisasa vya kielektroni au gari? Kwa upande mwingine, je, unaweza kuuza vifaa ambavyo hutumii au huhitaji tena? Kufanya hivyo kunaweza kukusaidia kurahisisha maisha na kuongeza mapato yako.
Dokezo: Mapato yako yanapopungua kwa ghafla, huenda hilo likakuchochea kuacha mazoea yenye madhara na yanayogharimu, kama vile kutumia tumbaku, kucheza kamari, au kutumia kileo vibaya. Kufanya mabadiliko hayo kutakusaidia kuboresha hali yako ya kiuchumi na maisha yako.
5. Tanguliza mambo ya kiroho.
Kanuni ya Biblia: “Wenye furaha ni wale wanaotambua uhitaji wao wa kiroho.”—Mathayo 5:3.
Biblia inatoa ushauri huu wenye usawaziko: “Hekima ni ulinzi kama pesa zilivyo ulinzi, lakini hii ndiyo faida ya ujuzi: Hekima humhifadhi hai yule aliye nayo.” (Mhubiri 7:12) Hekima hiyo inapatikana katika Biblia, na watu wengi wamegundua kwamba kufuata mwongozo wake kumewasaidia kuepuka mahangaiko yanayopita kiasi kuhusu mambo ya kiuchumi.—Mathayo 6:31, 32.