Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 MATUKIO MUHIMU YA MWAKA ULIOPITA

Tengenezo Lililo Mwendoni

Tengenezo Lililo Mwendoni

Ijumaa, Julai 5, 2013, familia ya Betheli ya Marekani ilisisimka Anthony Morris wa Baraza Linaloongoza alipotangaza: “Alhamisi, Julai 4, 2013, tulitia sahihi mkataba wa kuuza majengo sita yaliyo kwenye barabara ya 117 Adams Street na barabara ya 90 Sands Street, Brooklyn. Kulingana na mkataba huo, tunapaswa kuhama jengo la 1 mpaka 5 kufikia katikati ya mwezi wa Agosti mwaka huu.”

Ndugu Morris alieleza kwamba Idara ya Dobi iliyo kwenye ghorofa ya sita na saba kwenye jengo namba 3, itaendelea kufanya kazi mpaka katikati ya mwaka wa 2014. Alisema, “Jengo lililo kwenye barabara ya 90 Sands Street huenda likahamwa mwaka wa 2017.”

Kuuzwa kwa majengo hayo makubwa sita ni sehemu ya mpango wa kuhamisha makao makuu ya Mashahidi wa Yehova kutoka New York City hadi kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 253 huko Warwick, New York. Hata hivyo, kazi ya kuchimba msingi na kazi nyingine hazingeanza hadi vibali vinavyohitajika vipatikane.

Kwa hiyo, familia ya Betheli ya Marekani ilisikiliza kwa makini tangazo lililosomwa na Mark Sanderson, mshiriki wa Baraza Linaloongoza Alhamisi Julai 18, ambalo lilisema: “Tunafurahi kutangaza kwamba jioni ya Jumatano, tarehe 17 Julai, washiriki wote wa Kamati ya Upangaji wa Mji wa Warwick, waliidhinisha ramani ya ujenzi ya makao makuu mapya ya Mashahidi wa Yehova. Hiyo ndiyo idhini ya mwisho tuliyohitaji ili kupata vibali vya kuanza ujenzi. Jambo la kupendeza ni kwamba tulipokea idhini hiyo tarehe ileile tuliyonunua uwanja wa Warwick miaka minne iliyopita. Isitoshe, matukio ya siku chache zilizopita kabla hatujapata idhini hiyo yanaonyesha wazi baraka za Yehova.” Ndugu Sanderson aliwashukuru wote kwa kufanya kazi bila kuchoka na kusali kwa bidii kwa ajili ya mradi huo muhimu. Alisema hivi: “Zaidi ya yote, sifa na shukrani zimwendee Yehova kwa ajili ya hatua hii ya kihistoria ya kuhamisha makao makuu hadi Warwick, New York.”

Ijumaa, Julai 26, Ndugu Morris alikutana na wajitoleaji 1,000 hivi kutoka Betheli na kutoka Halmashauri ya Ujenzi ya Mkoa (RBC) ambao walikusanyika kwenye chumba kipya cha kulia chakula huko Tuxedo, New York, eneo linalotumiwa kuweka mashine na vifaa kwa ajili ya ujenzi huko Warwick. Baada ya kuzungumzia habari ya kimaandiko yenye kutia moyo, Ndugu Morris alisema kwamba ana tangazo fulani. Alitangaza hivi: “Mkononi nina fomu ambayo nimepokea sasa hivi na ningependa kuwasomea. Ina kichwa: ‘Kibali cha Ujenzi.’” Kabla hajaendelea kusoma zaidi, wajitoleaji walipiga makofi kwa shangwe. Wote waliokuwepo walifurahi sana Ndugu Morris aliposoma sehemu iliyobaki ya kibali hicho muhimu cha ujenzi kilichotolewa na mji wa Warwick saa tatu tu zilizokuwa zimepita.

Ni Nini Kinachofanyika Wallkill, Warwick, na Tuxedo?

Tangu kuanza kwa mradi wa kupanua Wallkill mnamo Agosti 2009, ndugu na dada 2,800 hivi wamejitolea kutumikia huko kwa muda. Mradi huo unatia ndani jengo jipya la makao, mahali pa kuegesha magari, na jengo la ofisi. Jengo moja la makao linakarabatiwa, na marekebisho yanafanywa kwenye kiwanda cha kuchapisha, dobi, ukumbi, jengo linalotoa huduma mbalimbali, na sebule kuu. Upanuzi huo wa Wallkill unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka wa 2015.

Kwa sasa, ujenzi umeanza katika eneo litakalokuwa makao makuu huko Warwick. Miezi michache tu tangu ujenzi huo uanze, kazi ya kusawazisha ardhi, kuchimba msingi, na pia kuweka nyaya na mabomba ya chini ya ardhi inaendelea. Ujenzi wa majengo matatu ya kwanza, yaani, Gereji, Maegesho ya Magari ya Wageni, na Jengo la Udumishaji ulianza mwishoni mwa mwaka wa 2013. Majengo hayo ni muhimu kwa kuwa yatatumiwa na wafanyakazi na pia kwa ajili ya urekebishaji na udumishaji wa mashine wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Ujenzi wa majengo ya makao na Jengo la Ofisi na Huduma mbalimbali umepangwa kuanza mwaka wa 2014.

Kenneth Chernish, mshiriki wa Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi alisema kwamba uwanja wa Tuxedo wenye ukubwa wa ekari 50, ulio kilometa 10 hivi kaskazini ya Warwick, “ni kituo kitakachotegemeza ujenzi wa makao makuu mapya huko Warwick. Kitakuwa na makao ya baadhi ya wajitoleaji, kitatumiwa kuwaandalia milo, na mahali pa kuhifadhi vifaa vya ujenzi na mashine.” Ili kuharakisha mradi huo wa Tuxedo, Halmashauri za Ujenzi za Mkoa zilizoteuliwa kutoka sehemu ya mashariki ya Marekani zimekuwa zikisaidia kufanya kazi fulani katika mradi huo.

Wajitoleaji wengi wanaofanya kazi pamoja na Halmashauri za Ujenzi za Mkoa nchini Marekani wanatazamia kwa hamu kushiriki katika ujenzi wa makao makuu mapya. Tayari ndugu na dada wenye ujuzi wanajitolea kwa muda katika miradi hiyo ya ujenzi. Leslie Blondeau na mume wake, Peter, ambao wanafanya kazi katika Idara ya Mabomba anasema hivi, “Kufanya kazi pamoja kunafanya tuwe na uhusiano wa karibu sana na tunajionea mambo mengi tutakayokumbuka kwa muda mrefu sana.”

Mallory Rushmore anasema hivi: “Kwa sasa ninafanya kazi na kikundi cha umeme hapa Tuxedo. Kila siku ninafurahia kufanya kazi hapa. Kuna wajitoleaji wengi sana kutia ndani wajitoleaji wa muda, na wote wanafanya kazi kwa ushirikiano!”

Quincy Dotson anasema hivi: “Hili ni pendeleo la pekee. Nilidhani kwamba ningejidhabihu sana, lakini kwa kweli, ninafaidika sana.”

Ndugu Chernish anasema: “Inasisimua kushiriki katika mradi huu. Ndugu na dada wanafanya kazi haraka na kwa ustadi, na wanafurahia sana kazi.”