Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

INDONESIA

Mbinu za Awali za Kuhubiri

Mbinu za Awali za Kuhubiri

Matangazo ya Redio

MWAKA wa 1933, ndugu walifanya mipango ya kutangaza hotuba za Ndugu Rutherford zilizorekodiwa katika Kiingereza kwenye kituo cha redio cha Jakarta. Hotuba za ziada za Kiholanzi zilirushwa hewani kwa kusomwa na mtu aliyekuwa anapendezwa na kweli. Hotuba hizo ziliwachochea watu waliopendezwa na zilifanya akina ndugu wawaachie watu wengi machapisho.

Hotuba motomoto ya Ndugu Rutherford yenye kichwa “Matokeo ya Mwaka Mtakatifu kwa Amani na Ufanisi,” iliporushwa hewani viongozi Wakatoliki walikasirika sana. * Wakiwatumia watumishi wao, walimkamata Ndugu De Schumaker aliyekuwa akisambaza rekodi hizo na kumshitaki kwa makosa ya “uchochezi, dhihaka, na chuki.” Ndugu De Schumaker alipinga mashtaka hayo kwa uthabiti, hata hivyo, akapigwa faini ya gilda 25 (pesa za Uholanzi) * na kulipia gharama za mahakama. Magazeti matatu maarufu yaliripoti kisa hicho, jambo lililochangia kutolewa kwa ushahidi kwa kiasi kikubwa.

Mashua ya Lightbearer

Julai 15, 1935, mashua ya Watch Tower Society yenye urefu wa mita 16 iliyoitwa Lightbearer iliwasili Jakarta baada ya kusafiri kwa miezi sita kutoka Sydney, Australia. Mashua hiyo ilibeba mapainia saba wenye bidii, walioazimia kutangaza habari njema kotekote nchini Indonesia, Singapore, na Malasia.

Kwa zaidi ya miaka miwili, mapainia walitumia mashua ya Lightbearer kutembelea bandari ndogo na kubwa kotekote nchini Indonesia, wakigawa machapisho mengi ya Biblia. Mashua ilipowasili katika kila bandari ndogo, Jean Deschamp anasema: “Mapainia hao wangecheza hotuba moja ya J. F. Rutherford, aliyekuwa msimamizi wa Watch Tower Society wakati huo. Watu wa vijiji vya Malasia walishangaa sana kuona mashua kubwa ikiwasili katika bandari yao na kusikia sauti kubwa. Ni kana kwamba walikuwa katika sayari nyingine.”

Wakiwa wamekasirishwa na ujasiri wa kuhubiri wa ndugu hao, viongozi wa kidini waliwashinikiza wenye mamlaka kupiga marufuku mashua ya Lightbearer kutia nanga kwenye bandari nyingine nyingi za Indonesia. Desemba 1937, mashua ya Lightbearer ilirudi Australia, na kuacha historia nzuri ya kazi ya umishonari nchini Indonesia.

Kikosi cha Lightbearer

^ fu. 2 Hotuba ya Ndugu Rutherford ilifunua vitendo vya ufisadi, siasa na biashara, vilivyofanywa na Kanisa Katoliki.

^ fu. 2 Kiasi hicho ni sawa na dola 300 za Marekani..