Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kenya na Nchi Jirani

Kenya na Nchi Jirani

Kenya na Nchi Jirani

MIAKA mia moja na arobaini na nne iliyopita, London lilikuwa na msisimko. Johannes Rebmann, mvumbuzi Mjerumani, alikuwa ameripoti kwamba aliona mlima mkubwa sana katika Afrika Mashariki, mlima uliokuwa mrefu sana hivi kwamba kilele chao kilikuwa na theluji. Ingawa wengi walistaajabia habari hiyo ya kushangaza, wastadi wa jiografia hawakuamini. Theluji katika ikweta? Labda Rebmann anaota, wakaamua.

Katika miaka ya baadaye, wavumbuzi wengine wa Ulaya wakaja na habari walizosimulia za watu washamba ambao walikuwa wafupi kama mbilikimo, walioishi ndani ya misitu, watu ambao hawakuwa wamepata kuonwa na mzungu yeyote. Kwa mara nyingine tena, wastadi hao walitia shaka. Kwa kweli mambo hayo yalikuwa hekaya kwao.

Lakini wastadi hao walikosea katika hali zote mbili. Uvumbuzi zaidi ulithibitisha kuwapo kwa mlima Kilimanjaro ulio mrefu sana, vilele vyao vikiwa na theluji mwaka wote. Kuwapo kwa Wapigmi kulithibitishwa pia: Wanaume wakiwa na urefu wa futi nne na nusu.

Afrika Mashariki, ni bara la maajabu kama nini! Kati ya maeneo yote ya dunia, ni maeneo machache yanayosisimua, ni yenye rangi, uzuri, na uvutio kama ule wa eneo hilo la Afrika. Katika eneo hilo hamna milima yenye vilele vyenye theluji tu bali pia mna majangwa yenye joto kali sana. Si watu wafupi zaidi duniani tu ndio wanaoishi huko, bali pia watu warefu zaidi duniani, yaani Watusi (Watutsi) na Wadinka, ambao miongoni mwao si ajabu kupata wanaume wenye kimo cha futi saba.

Vikundi vya Watu na Lugha Mbalimbali

Ni bara lenye unamna-namna mwingi sana. Watu wapatao milioni 150 wanaoishi huko wamegawanywa katika makabila 350. Tanzania pekee ina makabila kama hayo 125. Kuna makabila karibu 40 katika Kenya, tokea Wakikuyu ambao ni wengi katika eneo la ki-siku-hizi la kibiashara la Nairobi, hadi Wamasai, watu wafugaji ambao chakula chao kikuu ni maziwa na damu ya mifugo yao.

Si ajabu kwamba lugha za Mashariki mwa Afrika ni nyingi pia. Ingawa lugha hizo zinaweza kugawanywa katika lugha kadha kuu, vilugha na lahaja mbalimbali zafanya kuwe na mamia ya lugha. Zaidi ya lugha mia moja husemwa katika Ethiopia pekee, kutia ndani “lugha iliyo safi” ambayo haitaunganisha Afrika ya Mashariki tu bali ulimwengu mzima pia.—Sef. 3:9.

Milima, Maziwa, na Wanyama

Ingawa sehemu kubwa ya Afrika Mashariki ni ya kitropiki, sehemu zayo za ndani zenye nyanda za juu ni baridi zikilinganishwa na maeneo ya pwani yenye joto. Bonde Kuu la Ufa, ambalo ni mpasuko wa uso wa dunia wenye urefu wa zaidi ya kilometa 6,400, hugawanya sehemu hiyo kutokea kaskazini kuelekea kusini. Kando ya bonde hili mna milima ya volkeno zimwe. Mlima Kilimanjaro ndio unaojulikana zaidi ya mingine yote. Huo ndio mlima mrefu zaidi katika Afrika, ukiwa na urefu wa kwenda juu wa meta zaidi ya 6,000. Kaskazini mwake mna Mlima Kenya. Mlima huo una hali zinazotofautiana sana kwani msingi wao u katika ikweta yenye jua kali sana, na hali vilele viwili vyao vimefunikwa na theluji nyakati zote.

Maziwa yaliyoko kati ya miinuko ya milima yana ndege wa majini aina tofauti-tofauti sana na ambao pia ni wengi mno—hao ni mwari, chopoa, bata bukini, bwenzi, kulasitara, korongo, kwarara, na korongo wenye domo-jiko, tukitaja wachache tu. Magadi nyingi inayopatikana katika maziwa hayo hutegemeza uduvi wa maji ya chumvi na majani madogo-madogo yenye rangi ya buluu na kijani ambayo heroe hutumia. Ndege hao wanaopendeza ambao ni karibu milioni mbili huishi katika Afrika Mashariki. Na kweli, mojawapo maono ya kustaajabisha zaidi katika bara nzima ni kundi kubwa la heroe wakipuruka angani, rangi nyekundu-nyeupe kwenye anga buluu.

Kila mahali unapotazama pana ndege wa ajabu, wanaosisimua, na wenye umaridadi. Chozi mwenye rangi mbalimbali akonga maji matamu kutoka kwa ua. Mnana mwenye rangi ya manjano-nyangavu afuma kiota chake tata katika funjo. Tai-mzoga apeperuka bila jitihada kati ya mawingu.

Bila shaka, kuna wanyama wakubwa pia. Njoo mbugani uwaone ndovu, punda milia, vifaru, nyati, twiga, simba, chui, na paa wa aina mbalimbali zaidi ya 60. Huko unaweza kuona kundi kubwa la nyumbu elfu kumi wakikimbia kwa kishindo kuvuka nyanda, tumbili mweusi akitazama kutoka kwenye mkakaya, au mbuni mrefu akitafuta chakula.

Naam, iwe ni katika Nyanda ya Danakil, ambayo ni mojawapo sehemu zenye joto zaidi duniani, au iwe ni katika Milima ya Mwezi, ambapo nyani-mtu hucheza, au katika fuo nyeupe za bahari, ambapo kobe wenye umri wa karne moja hutambaa, utapata kwamba Mashariki mwa Afrika ni bara lisilo na kifani.

Dini Mbalimbali

Kihistoria, watu wa Mashariki mwa Afrika wamefuata dini za kikabila, isipokuwa katika Ethiopia, ambapo Kanisa Orthodoksi la Ethiopia limedhibiti mambo kutokea karne ya nne W.K. Lakini Meka ikiwa ng’ambo tu ya Bahari Nyekundu na pepo za msimu zikiwa zinaleta majahazi ya Waarabu kutoka Ghuba ya Uajemi hadi pwani ya Afrika Mashariki, upesi Uislamu ulipata wafuasi. Biashara ya watumwa yenye ufanisi wakati wa karne za 18 na 19, na watumwa wengi waliotoka kati ya yale maziwa makuu na bandari ya Zanzibar walivutia Waislamu waende mbali kusini na barani. Karibu asilimia 40 ya idadi ya watu katika Afrika Mashariki ni wafuasi wa Uislamu, ingawa idadi hiyo ni ndogo sana katika nchi fulani-fulani za eneo hilo kama vile Uganda, Kenya, Rwanda, na Ushelisheli.

Wavumbuzi na wamishonari wa Ulaya pia walikuja katika karne ya 19, nao wakaweka msingi wa ukoloni. Milki ya Uingereza ilidai kumiliki ile iliyokuja kuitwa Sudan ya Uingereza na Misri pamoja na Afrika Mashariki ya Uingereza. Somalia iligawanywa kati ya Uingereza, Ufaransa, na Italia. Ubelgiji ilitawala Rwanda na Urundi (leo ni Burundi). Kwa muda mfupi Italia ilitawala Eritrea (Ethiopia), na Ujerumani ikatawala Afrika Mashariki ya Ujerumani, ambayo sasa ni Tanzania. * Wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo waligawanya maeneo hayo kuwa maeneo ya kumiliki, wakiruhusu “kanisa” fulani kudhibiti kila jambo katika eneo fulani. Shule zilijengwa, hospitali zikafunguliwa, na Biblia zikatafsiriwa katika lugha nyingi.

Theluthi mbili za idadi ya watu wa Kenya wanadai kuwa Wakristo leo, huku katika Afrika Mashariki nzima ni watu wanaopungua nusu tu ya idadi ya watu wote ndio wanaodai kuwa Wakristo. Makabila mengine yamedumisha imani zao za kuabudu maumbile, na leo hao ni kati ya robo na sehemu moja kwa tano ya idadi ya watu wote. Wahindi waliohamia huko waliendelea na dini zao za Mashariki.

Katika nyakati za hivi karibuni zaidi, utukuzo wa taifa katika Afrika uliongezeka sana, na katika miaka ya 1960, nchi baada ya nchi ilipata uhuru. Mara nyingi jambo hilo lilimaanisha uhuru zaidi wa ibada. Utukuzo wa taifa pia ulitokeza watu wengi wapya waliojiita eti manabii, ambao walichanganya imani za Kiafrika pamoja na imani za dini za Jumuiya ya Wakristo na kuanzisha mamia ya madhehebu mapya, kukiwa na ushindani mkubwa na mvurugo miongoni mwao. Tofauti hizo za imani zilipotokeza chuki, wafuasi wa dini nyinginezo walinyanyaswa sana.

Kwa kujihusisha sana na siasa za ukoloni na biashara, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo hayakuweka mfano ulio kama wa Kristo wala hayakuleta mabadiliko yanayodumu ya maadili miongoni mwa wengi wa wafuasi wayo. Wakati ulikuwa umefika wa kweli ya Biblia kung’aa katika Mashariki mwa Afrika.

Mapainia wa Mapema Waangaza Nuru

Karibu miaka 60 baada ya wavumbuzi mashuhuri Livingstone na Stanley kukutana katika ufuo wa Ziwa Tanganyika na wakati ambapo chanzo cha kusini ya mbali cha Mto Naili hakikuwa kimevumbuliwa, jitihada za kwanza zilikuwa zinafanywa za kuleta nuru ya kweli ya Biblia katika sehemu hii ya Afrika. Kufikia wakati huu Wanafunzi wa Biblia walikuwa tayari wamekuwa wakitenda sana katika sehemu nyingine za ulimwengu, wakifunua wazi uwongo wa kidini na kutahadharisha wanadamu juu ya umaana wa matukio ya wakati huu. Katika Afrika, kulikuwa na mwanzo katika pwani ya Magharibi na katika Cape, ukingo wa kusini mwa bara.

Katika 1931, mwaka ambao Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa, walichukua jina la Kimaandiko, Mashahidi wa Yehova, ofisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Cape Town ilitafuta njia za kupanda mbegu za kweli ya Biblia katika pwani ya mashariki mwa bara na mahali palipowezekana hata katika bara. Gray Smith na kaka yake Frank, waliokuwa wahudumu mapainia wawili wajasiri kutoka Cape Town, walifunga safari ya kwenda Afrika Mashariki ya Uingereza waone kama ingewezekana kutangaza habari njema. Walichukua gari aina ya De Soto waliyokuwa wameigeuza kuwa ya kulala pia, wakaiweka melini pamoja na katoni 40 za vitabu, na kuabiri kuelekea Mombasa, bandari ya Kenya. Reli iliyotoka tu kujengwa iliunganisha Mombasa na Uganda, ikipitia nyanda za juu za Kenya. Wakiwa Mombasa, mapainia hao wawili walipeleka vitabu vyao vya thamani kwa garimoshi hadi Nairobi, jiji kuu lililokuwa kwenye mwinuko wapata kilometa moja na nusu juu ya usawa wa bahari na ambalo miaka 20 tu iliyopita, halikuwa kitu ila vibanda vya kuweka vifaa vya reli.

Kisha ndugu hao wawili walifunga safari ya kilometa 580 kuelekea Nairobi. Wasafiri wa leo husafiri umbali huo kwa karibu saa saba katika barabara nzuri yenye lami, lakini katika siku zile safari kama hiyo katika gari lililojaa vitu ilikuwa ni kisa kwelikweli. Ripoti iliyopelekewa msimamizi wa wakati huo wa Watch Tower Society, Joseph F. Rutherford, na ambayo ilichapishwa katika Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) la Agosti 1, 1931, inatuonyesha jinsi safari yao na kutoa kwao ushahidi kulivyokuwa katika Nairobi:

“Ndugu Mpendwa Rutherford:

“Mara nyingi mimi na ndugu yangu tumekushukuru sana kwa pendeleo hili la sisi kuja kutoka Afrika Kusini hadi nchi ambayo haijapata kuhubiriwa.

“Tulisafirisha gari letu tunamoishi kutoka Cape Town hadi Mombasa kwa meli inayoitwa S.S. ‘Llamtepher’; na baada ya safari njema baharini, tulianza safari ya gari ambayo ndiyo safari yenye kuogopesha zaidi niliyopata kufunga. Ilituchukua siku nne, tukienda siku nzima, kumaliza kilometa 580, kutoka Mombasa hadi Nairobi, tukilala nyikani miongoni mwa wanyama wakali.

“Ilinibidi kutoka nje nikiwa na koleo na kulainisha miinuko kilometa baada ya nyingine, kujaza mashimo, na pia kukata nyasi na miti ili kujazia mabwawa ili magurudumu yasikwame. Tuliendelea siku nzima na sehemu ya usiku tukiwa na hamu ya kutaka kutoa ushahidi.

“Hatimaye tulifika Nairobi, jiji kuu la Kenya lililo karibu na ikweta na Afrika ya Kati; na Bwana mpendwa akabariki jitihada zetu kwa matokeo bora sana. Sisi sote wawili tulifanya kazi kwa siku ishirini na moja, kutia ndani Jumapili na Jumamosi zote, na kwa muda huo mfupi tukagawanya vijitabu 600 na seti kamili 120 za mabuku tisa. Tulitishwa kwamba tutaitiwa polisi, tukaitwa wawongo, tukatukanwa, tukafukuzwa ofisini; lakini tuliendelea tu, na sasa kazi yetu karibu inamalizika. Nuru imewashwa ambayo itang’aa katika giza tititi la kiroho la Afrika. Kulingana na yale tunayosikia, kazi yetu imeleta mvurugo miongoni mwa watu wa kidini katika Nairobi.

“Ninarudi Cape Town; lakini ndugu yangu anapanga kuendeleza ujumbe kupitia Kongo na Rhodesia Kaskazini hadi Cape Town, ambapo tutakutana tena naye tukiwa tayari kupokea pendeleo jingine.

Mimi wako katika utumishi wa Bwana,

F. W. Smith, Colporteur.”

Mawasiliano na Waafrika yalizuiwa chini ya utawala wa kikoloni, kwa hiyo ndugu hao wawili waliangushia Wagoa Wakatoliki fasihi zao nyingi, waliotoka Goa katika pwani ya magharibi mwa India ili kuja kujenga reli. Lakini makasisi Wakatoliki, wakiwa na ghadhabu kwa sababu ya kweli zilizoelezwa katika vichapo hivyo vya Biblia, walivikusanya na kuvichoma vitabu vyote ambavyo wangeweza kuvipata.

Baadaye, ndugu hao wawili walishikwa na malaria, ugonjwa uliokuwa umeua wasafiri wengi. Gray alipona baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi minne, lakini ndugu yake Frank alikufa kabla ya kufika Cape Town.

Kufuatia kwa Ujasiri

Wakati uo huo katika Afrika Kusini, mapainia Robert Nisbet na David Norman walijitayarisha kufuatia safari ya kwanza. Robert Nisbet akumbuka jinsi alipowasili kwenye ofisi ya tawi ya Cape Town kutoka Skotland, alivyoonyeshwa katoni 200 za fasihi zilizokuwa tayari kupelekwa Afrika Mashariki. Vitabu hivyo vilikuwa vingi mara tano zaidi ya vilivyochukuliwa na akina Smith!

Wakiwa wanajikinga dhidi ya malaria kwa kulala ndani ya chandarua na kwa kumeza kwinini kila siku, walianza kampeni katika Dar es Salaam, jiji kuu la Tanganyika, mnamo Agosti 31, 1931. Huo haukuwa mgawo rahisi. Ndugu Nisbet asimulia hivi: “Mwangaza mwingi wa jua kutoka kwenye barabara za mitaani, joto kali sana lenye kutosha jasho, na uhitaji wa kubeba mizigo mizito ya fasihi kutoka ziara moja hadi nyingine, yote yalikuwa baadhi tu ya magumu tuliyokabili. Lakini tulikuwa vijana wenye nguvu na tuliifurahia.”

Wakizuru maduka, ofisi, na makao, mapainia hao wawili waliangusha karibu vitabu na vijitabu elfu moja kwa muda wa majuma mawili. Miongoni mwa hivyo, vilikuwamo vile vilivyoitwa Seti za Rainbow zenye vitabu 9 mbalimbali vyenye rangi tofauti-tofauti zenye kuvutia pamoja na vijitabu 11 vinavyoeleza Biblia. Haikulichukua Kanisa Katoliki muda mrefu kutoa tangazo linalokataza Wakatoliki wote wasiweke vichapo hivyo nyumbani mwao.

Kutoka Dar es Salaam mapainia hao wawili walielekea Zanzibar, kisiwa kilichoko kilometa 40 kutoka pwani mwa bara, kilichokuwa kitovu cha biashara ya watumwa. Mji wa kale ambao pia unaitwa Zanzibar, ukiwa na barabara nyembamba za mitaa na zenye kutatanisha, ulikuwa na manukato ya karafuu nyakati zote, kwani Zanzibar ndiyo iliyokuwa ikiongoza katika kusafirisha nje karafuu. Waislamu wanaosema Kiswahili ndio waliokuwa wengi wakiwa wakazi karibu robo milioni. Vichapo vingi viliangushiwa Wahindi na Waarabu waliosema Kiingereza kwa sababu vichapo hivyo vilikuwa katika lugha ya Kiingereza.

Baada ya siku kumi katika Zanzibar, mapainia hao walipanda meli kuelekea Mombasa katika Kenya wakienda kwenye nyanda za juu za Kenya. Walisafiri kwa garimoshi kutoka Mombasa, wakihubiri eneo lililo kando-kando ya reli mpaka wakafikia Ziwa Viktoria, ambalo lipo kusini tu mwa ikweta.

Kisha wakachukua meli ndogo hadi Kampala, jiji kuu la Uganda, ambapo waligawanya vitabu vingi na kupata maandikisho ya gazeti Golden Age (ambalo siku hizi ni Amkeni!). Mtu mmoja aliyeona rafiki yake akisoma kitabu Government kwa shauku, alisafiri mwendo wa kilometa 80 kutafuta akina ndugu hao naye akajipatia vitabu vyote vilivyopatikana pamoja na andikisho la The Golden Age.

Kisha mapainia hao wawili wakipitia Jinja na Kisumu katika Ziwa Viktoria, walirudi Mombasa. Huko wakaangusha vichapo vingi tena na kutoa hotuba mbili za Biblia zilizohudhuriwa na Wagoa wengi. Kutoka huko, wakaabiri kurudi Cape Town, safari ya kilometa 4,800. Kwa ujumla, Ndugu Nisbet na Norman waliangusha zaidi ya vitabu na vijitabu 5,000 pamoja na maandikisho mengi.

Safari ya Nchi Kavu Kuvuka Nusu ya Afrika

Katika 1935, mwaka ambapo ufahamu wa Biblia wenye kuendelea ulipofunua kukusanywa kwa umati mkubwa wa kuishi katika dunia paradiso, kundi la Mashahidi wanne lilifanya kampeni ya tatu katika Afrika Mashariki. Hao walikuwa ni Gray Smith, aliyekuwa amesalimika katika kampeni ya kwanza, na mke wake Olga, pamoja na ndugu wawili wa kimwili Robert na George Nisbet. George alikuwa amewasili Cape Town wakati wa mwezi wa Machi. *

Wakati huu walikuwa na magari mawili makubwa yenye uzito wa robo-tatu za tani na yaliyorekebishwa kuwa makao ya kuishi, yenye vitanda, jiko, ugavi wa maji, tangi la ziada la petroli, na fremu zinazoweza kutolewa zikiwa na vifuniko vya kuzuia mbu. Sasa miji zaidi ingeweza kufikiwa, ingawa nyakati nyingine barabara zilifunikwa na nyasi ndefu zinazofikia meta 3. Mara nyingi mapainia hao walilala nyikani nao wangeweza kuona, kusikia, na kuhisi jinsi Afrika ilivyokuwa hasa, ikiwa na sehemu kubwa zilizo wazi na wanyama wengi: simba wakinguruma wakati wa usiku, na punda milia, swala, pamoja na twiga wakilisha pamoja kwa utulivu wakati wa mchana—pamoja na kuwapo kunakoogofya kwa vifaru na ndovu.

Walisafiri kwa gari kupitia Barabara ya kutoka Cape kwenda Cairo. Ukweli uliopo katika jina lenye fahari la barabara hiyo ni kwamba ina sehemu ndefu zenye upweke na vumbi na pia sehemu zenye mawemawe na matope, mchanga mwepesi na mito iliyokuwa lazima ivukwe. Walipofika Tanganyika, hao wanne wakaenda pande mbalimbali. Ndugu wawili Robert na George Nisbet walielekea Nairobi, huku Ndugu na Dada Smith wakihubiri Tanganyika, ambayo wakati huo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza.

Upesi polisi walishika akina Smith na kuwaamuru warudi Afrika Kusini. Badala ya kufanya hivyo, wakifuata akina Nisbet, walishika njia kuelekea kaskazini kwenda Nairobi, ambako walipewa idhini ya kukaa baada ya kulipa kwa polisi wa huko amana ya dola 160 ambazo zingeweza kurudishwa. Mapainia hao walifanya kazi kwa bidii, wakiangusha zaidi ya vitabu 3,000 na karibu vijitabu 7,000 pamoja na maandikisho mengi ya gazeti Golden Age. Hatimaye, upinzani wa kidini uliokuwa ukiongezeka ulitokeza amri wafukuzwe nchini. Baada ya kuteta sana dhidi ya kufukuzwa nchini, ambako hakukufaulu, watatu wa mapainia hao walifunga safari ya kurudi Afrika Kusini, wakimwacha Robert Nisbet nyuma katika hospitali moja ya Nairobi akiugua homa ya matumbo. Kwa uzuri, alipona na akaweza kurudi Afrika Kusini pia.

Baadaye, Robert na George Nisbet walipata pendeleo la kuhudhuria Watch Tower Bible School of Gilead na kupewa mgawo wa kutumikia kisiwa cha Bahari ya Hindi cha Mauritius katika 1951 wakiwa wamishonari. Robert Nisbet sasa yuko Australia, na ndugu yake George alitumikia katika ofisi ya tawi ya Afrika Kusini hadi kifo chake katika mwaka 1989.

Kama ilivyokuwa kwa wamishonari wa karne ya kwanza wanaotajwa katika kitabu cha Matendo, mapainia hao walionyesha upendo wenye kina kwa Yehova na wanadamu wenzao kujapokuwa magumu na hatari. Kati ya mapainia sita waliokuja Afrika Mashariki, wanne walilazwa hospitalini kwa muda mrefu, na mmoja hata alikufa. Na bado, ushahidi ulitolewa na vichapo vikazaa tunda. Kwa mfano, Shahidi mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika eneo la mashambani la Kenya miaka 30 baadaye, alipata mtu mmoja akiwa na nakala ya kitabu Reconciliation alichokipata katika 1935. Mtu huyo sasa amekuwa Shahidi yeye mwenyewe.

Painia Mwingine—Katika Milki Iliyojificha

Karibu na wakati uo huo, painia mwingine mwenye ujasiri, Krikor Hatzakortzian, alifika Ethiopia ili atoe nuru ya kiroho katika lugha yake ya Kiarmenia na vilevile katika Kigiriki na Kifaransa. Kazi yake ya kujasiria ilikuwa katika nchi isiyo ya kawaida katika njia nyingi. Sehemu kubwa ya nchi hiyo ni nyanda ya juu kubwa sana yenye umbo la pembe tatu na inayoinuka meta 2,000 kwa wastani. Kuna vilele virefu sana vya milima na milima isiyo na kitu iliyochongoka juu na kuwa tambarare yenye nyanda zenye rutuba na iliyozungukwa na mabonde. Mto Naili Buluu una chanzo chao huko na unapitia mabonde yenye magenge marefu yanayovutia sana. Mto Tekeze vilevile hupitia bonde lenye magenge marefu linalokumbusha wasafiri wengi juu ya Grand Canyon ya Amerika Kaskazini. Bara hilo lenye milima-milima hutenganisha Ethiopia na nyanda za chini za Sudan zilizoko magharibi na majangwa ya Danakil na Ogaden upande wa mashariki.

Ethiopia ilikuja kuwa milki iliyojitenga mapema katika historia; Maliki Ezono aliifanya ikubali imani za Jumuiya ya Wakristo karibu na wakati wa Baraza la Nisea katika karne ya nne. Kanisa la Orthodoksi la Ethiopia, likikazia ibada ya Mariamu na msalaba pamoja na ufungamano walo na dini ya Kiyahudi ya kale, limekuwa na nguvu sana katika historia ya Ethiopia na kufanya Ethiopia iwe milki ya “Kikristo” iliyofichika ambayo ilikinza maendeleo ya Uislamu kutoka nyanda za chini. Maliki Haile Selassie, ambaye jina lake lilimaanisha “Uwezo wa Utatu,” alikuwa na majina ya cheo kama vile “Mfalme wa Wafalme,” “Simba wa Yuda,” na “Mchaguliwa wa Mungu.” Zaidi ya hayo, katiba ilimpa wajibu wa kisheria wa kutetea masilahi ya Kanisa. Lakini watu waliwekwa katika giza la kiroho na wangeweza kuchochewa kwa urahisi watende bila akili.

Katika hali kama hiyo katika mwaka 1935, Ndugu Hatzakortzian alijikuta bila painia mwenzi lakini akiwa na tumaini kamili katika Yehova. Manukuu yanayofuata ya barua yake yanayotoa ripoti ya kazi yake, ambayo yalichapishwa katika Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) la Novemba 1, 1935, yanatusaidia tuelewe hali aliyokabili:

“Sioni kuwa ajabu kunyanyaswa kwa ajili ya uadilifu, natarajia mengi zaidi yafuate. . . . Yehova wa majeshi amenilinda nyakati zilizopita naye atafanya hivyo pia wakati ujao.

“Adhuhuri nilikuwa ninatoka katika kazi yangu, na mmoja wa mawakili wa Shetani alitoka kwa ghafula alipojificha na kunigonga kichwani mara mbili kwa fimbo kubwa; alinipiga kwa nguvu sana hivi kwamba fimbo hiyo ilivunjika vipande-vipande. Lakini kwa msaada wa Bwana na kwa mshangao wa majirani wangu, jeraha langu halikuwa baya sana. Nililala kitandani siku mbili pekee. Wakati mwingine tena, mawakili wa adui walinishambulia kwa visu; lakini mara tu walipotaka kunidunga, kwa uwezo wa nguvu fulani walitupa visu vyao na kuniacha.

“Lakini [wao] wanaendelea na mnyanyaso wao. Wakati huu walitoa taarifa za uwongo juu yangu, na kunipeleka kwenye jiji kuu (Addis Ababa) nifikishwe mbele ya maliki. Wakati wa kukaa kwangu jijini (miezi minne), nilienda kila mahali na kutoa ushahidi nyumba kwa nyumba, kutia na mahotelini na mikahawani. Mwishowe nililetwa mbele ya maliki. Alinisikiliza; na aliponipata bila hatia, aliniachilia huru na kuniamuru nirudi nyumbani. Bwana atukuzwe kwa ushindi huo!

“Watu wanaishi katika hofu na kutokujua mambo, lakini ninashangilia katika Bwana. Yehova Mweza Yote na awabariki sana, na kuwapa nguvu ya kumaliza kazi aliyowapatia.

Ndugu yenu katika Kristo,

K. Hatzakortzian.”

Hakuna habari iliyopokewa kutoka kwa Ndugu Hatzakortzian wakati wa mchafuko wa Vita ya Ulimwengu 2, lakini katika miaka ya mapema ya 1950, wakati wamishonari waliozoezwa Gileadi walipofika Addis Ababa, walisikia fununu juu ya mtu aliyeishi Diredawa (Dire Dawa) “anayesema kama nyinyi.” Haywood Ward alifika mji huo ulioko mashariki na kumpata mtu mzee-mzee ambaye hakusema Kiingereza. Mishonari huyo alipojitambulisha, mzee huyo akalia machozi, akatazama mbingu, na kutaja jambo fulani katika Kiarmenia kutia ndani jina la Yehova. Alikuwa ni ndugu Hatzakortzian. Siku aliyoitamani sana ilikuwa imefika! Alimkumbatia Ndugu Ward huku akilia kwa shangwe. Kisha Ndugu Hatzakortzian akavuta masanduku kwa fahari na kumwonyesha magazeti yaliyokunjana ya Mnara wa Mlinzi na vitabu, huku akiongea kwa furaha kwa lugha ambayo mgeni wake hakuelewa.

Ndugu Ward alifurahi sana kwa kukutana huko na alitarajia kurudi tena, lakini haikutokea hivyo. Wamishonari wengine walipoenda kumwona, walipata watu wakiomboleza. Ndugu Hatzakortzian alikuwa amekufa.

Alikuwa kama “Melkizedeki” kwa wamishonari hao. (Heb. 7:1-3) Kulibaki maswali mengi ambayo hayakujibiwa: Yeye alikuwa nani? Alitoka wapi? Alijifunza wapi kweli? Ni nini kilichompata wakati wa matatizo ya Vita ya Ulimwengu 2? Hata iweje, alikuwa painia wa mapema mwenye ujasiri katika Ethiopia.

Hatimaye, Msingi Mpya Katika Kenya

Katika Novemba mwaka wa 1949, Mary Whittington alihamia Kenya kutoka Uingereza pamoja na watoto wake watatu wachanga ili aungane na mume wake aliyefanya kazi na Reli ya Afrika Mashariki katika Nairobi. Ingawa alikuwa amebatizwa karibuni mwaka mmoja tu uliokuwa umepita, upesi alijifunza kuwa thabiti katika kweli. Akiwa mwanamke mwembamba mwenye nidhamu na roho yenye nguvu ya painia, hakuwazia sana juu ya upweke katika nchi kubwa kuliko yake ya Uingereza lakini aliona shamba hilo kubwa kuwa fursa ya kueneza kweli ya Biblia.

Hizo zikiwa nyakati za ukoloni zenye sheria zilizofikilizwa za ubaguzi wa rangi, ilimbidi Dada Whittington ahubirie Wazungu pekee alipoanza kazi ya nyumba kwa nyumba katika ujirani wake. Wenye nyumba walikuwa wenye urafiki sana; mara nyingi walimkaribisha na kuchukua fasihi za Biblia. Mara nyingi aliulizwa hivi: “Nyinyi mnafanya mikutano yenu wapi?” Alijibu kwamba kadiri alivyojua, yeye alikuwa Shahidi wa Yehova peke yake katika nchi nzima!

Upesi kukatokea jaribu la ushikamanifu. Baada ya miezi mitatu, mume wake alijulishwa na wakubwa wake wa kazi kwamba utendaji wa kuhubiri wa mke wake umeonwa na polisi ambao hawakupendelea jambo hilo. Iwapo mke wake angeendelea na kazi yake, basi angefukuzwa katika koloni. Mume wake naye akamwambia Dada Whittington awahubirie rafiki zake pekee. Alijibu kwamba hakuwa na rafiki katika Kenya na kwamba uaminifu wake wa Kikristo ulimlazimisha kuendelea na kazi yake. Mume wake akamweleza kwamba ikiwa atafukuzwa, hangemruhusu aende na watoto.

Miezi michache baadaye, polisi wa upelelezi walimzuru Bw. Whittington ofisini mwake wakidai sampuli za fasihi zilizoenezwa na mke wake. Kwa furaha Dada Whittington akatoa fasihi chache. Ofisa aliyezirudisha alisema kwamba alikuwa amefurahia kuzisoma. Hakukataza utendaji wake wa kuhubiri lakini akakazia kwamba asihubirie idadi ya Waafrika. Wakati huo jambo hilo halikuwa tatizo kwa sababu kulikuwa na kazi nyingi sana ya kufanywa miongoni mwa wakazi wa Nairobi ambao hawakuwa Waafrika.

Upesi mwandamani akatokea, lakini si kwa njia ambayo Dada Whittington alitarajia. Ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ya Rhodesia Kaskazini ilimjulisha juu ya Bi. Butler fulani aliyependezwa na mambo ya Biblia. Olga Butler, aliyekuwa Mshelisheli, alikuwa akipokea fasihi za Sosaiti katika Tanganyika kwa zaidi ya miaka kumi na alikuwa amehamia Nairobi kufuatia kifo cha mumewe. Waliwasiliana kwa barua, na wakapanga wakutane kwenye mkahawa mmoja katika Nairobi, na upesi funzo la Biblia likawa likiendelea, kwanza katika bustani ya umma kwa sababu sheria ilikataza kushirikiana kwa watu wa rangi tofauti. Olga Butler alibatizwa miaka miwili baadaye katika besheni ya kuogea ya Whittington.

Jitihada za Kusaidia

Jitihada zilifanywa za kupeleka wamishonari ili kufungua eneo hili kubwa na kusaidia Dada Whittington pia katika upweke wake, lakini serikali ya kikoloni ilikataa. Katika 1952, msimamizi wa Watch Tower Society, Nathan H. Knorr, pamoja na mwandishi wake Milton G. Henschel, walizuru Nairobi na kutumia jioni moja pamoja na kikundi kidogo cha ndugu na dada kutoka Kenya na Uganda. Ombi jingine kwa ajili ya wamishonari lilifanywa, lakini hilo lilikataliwa pia.

Magumu zaidi yakaja kutoka chanzo kingine. Vita vya Mau Mau vilitokeza kutangazwa kwa hali ya hatari, kukifanya mkutano wowote wa watu zaidi ya tisa kuwa kinyume cha sheria, isipokuwa ikiwa umeandikishwa kwa serikali. Ombi la kuandikisha mikutano ya Kikristo lilikataliwa katika mwaka wa 1956. Wakati wa miaka hiyo, idadi fulani ya Mashahidi wa kigeni walikuja Kenya kukaa kwa muda mfupi, lakini ni Mary Whittington, watoto wake, na Olga Butler ndio waliobaki kuhubiri habari njema.

Kuwasili kwa Wahitimu wa Gileadi

Hizo ndizo hali ambazo wahitimu wa Gileadi William na Muriel Nisbet walipata walipowasili Nairobi kutoka Skotland katika mwaka wa 1956. William Nisbet alikuwa ndugu ya wale mapainia wawili wa mapema waliokuja Kenya kutoka Afrika Kusini katika miaka ya 1930. Ilimbidi Ndugu Nisbet afanye kazi ili akae, lakini bado aliweza kusimamia kikundi kidogo cha funzo la Biblia. Wakati huo, Dada Nisbet pamoja na Dada Whittington walikuwa wakitumia kila asubuhi kwa utulivu katika utendaji wa nyumba kwa nyumba.

Nairobi ulikuwa mgawo mzuri sana kwa akina Nisbet. Jiji hilo lilikuwa linasitawi kuwa jiji safi la ki-siku-hizi. Hali ya hewa yenye kiasi na vilima vya Ngong vilivyoko karibu na jiji viliwakumbusha nyumbani kwao Skotland. Ukitazama kusini-mashariki katika siku nyangavu, ungeweza kuona theluji ikimeremeta katika jua kwenye vilele vya mlima mrefu zaidi katika Afrika, Kilimanjaro. Vilele vilivyochongoka vya Mlima Kenya vingeweza kuonekana upande wa kaskazini. Mlima huo ndio ulioipa nchi hiyo jina. Na kulikuwa na paradiso ya wapenda wanyama mlangoni tu mwa Nairobi—Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi, ikiwa na simba, duma, vifaru, nyati, twiga, punda milia, na paa.

Hata hivyo, akina Nisbet walipendezwa zaidi na kuanzisha mafunzo ya Biblia. Mojawapo mafunzo hayo yalifanywa na familia ya ofisa wa polisi wa upelelezi. Ingawa akina Nisbet hawakujua, ofisa huyo alikuwa amepewa mgawo wa kupeleleza Mashahidi wa Yehova. Lakini upelelezi wake ulitokeza mambo tofauti na yale aliyotarajia. Ofisa huyo hakutoa ripoti nzuri juu ya utendaji wetu tu, bali pia alipata kweli ambayo ni hazina yenye thamani kubwa zaidi. Baadaye, washiriki wote wanne wa familia hiyo walibatizwa wakawa Mashahidi!

Watu wengine walijifunza pia. Bado kulikuwa na Sheria za Hali ya Hatari, na yeyote ambaye angehudhuria mikutano ya watu zaidi ya tisa angefukuzwa nchini au afungwe jela miaka mitatu. Ingawa akina ndugu hawakupendezwa na jambo hilo, iliwabidi wakutane katika vikundi vidogo.

1958—Mwaka wa Kukumbukwa

Mwaka huo ulianza kwa wahitimu wengine wanne wa Gileadi kupewa mgawo wa kuja Nairobi yaani, akina Clarke na Zannet. Kama ilivyokuwa kwa Ndugu Nisbet, ilibidi waume hao wawili wafanye kazi, huku wake zao wakipainia. Kilele kipya cha wahubiri 35 kilifikiwa, wengi wakiwa si wenyeji.

Huo pia ulikuwa mwaka wa Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko la Kimataifa katika New York, lililohudhuriwa na watu zaidi ya 250,000 kutoka ulimwenguni pote. Ilikuwa ni shangwe kwa Mary Whittington kuwa miongoni mwao na kutoa ripoti fupi juu ya kazi katika Kenya. Kuongezea shangwe ya mwaka huo, ndege iliyokodiwa na iliyojaa Mashahidi kutoka Rhodesia ilitua Nairobi ilipokuwa njiani kuelekea New York, ikitoa fursa ya ushirika wa kuchocheana kiroho.

Katika mkusanyiko wa New York, ombi lilitolewa kwa Mashahidi wenye uwezo wahamie nchi zenye uhitaji mkubwa zaidi wa wahubiri wa Ufalme; Kenya ilikuwa katika orodha ya nchi hizo. Kwa hiyo, kati ya Desemba 1958 na Septemba 1959, zaidi ya akina ndugu na dada 30 walikuja kutoka Kanada, United States, na Uingereza ili kusaidia kazi katika Kenya. Baadhi ya hao wapya waliowasili walienda Mombasa, katika pwani ya Kenya, yenye fuo nzuri za bahari. Wengine walianza kuhubiri katika mji wa Bonde la Ufa wa Nakuru, wenye kujulikana zaidi kwa ziwa lenye jina ilo hilo la Nakuru, ambalo ni makao ya heroe karibu milioni moja.

“Wanaotumikia Penye Uhitaji Mkubwa Zaidi” Wachangia

Hao “wanaotumikia penye uhitaji mkubwa zaidi” walikuwa ni kikundi chenye bidii, kikiweka kiwango cha juu cha ukomavu wa Kikristo. Walikuwa wameacha marafiki, kazi-maisha, na starehe lakini wakabarikiwa sana. Kenya ilikuwa Makedonia yao ya ki-siku-hizi.—Mdo. 16:9.

Akisema kwa niaba ya wengi, Ron Edwards, kutoka Uingereza, alisema hivi: “Kutokea tu mwanzoni mwa kipindi hicho, kifungo chenye nguvu sana cha upendo na shauku-nyororo kilikuwa kimekuwa miongoni mwetu tuliokuja kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi. Bila shaka hilo lilikuwa ni kwa sababu ya umoja wa kusudi lilelile na hali zetu zilizofanana. Wengi wetu tulikuwa wa rika moja (miaka 30 hadi 40) tuliofunga ndoa, na tulikuwa tumekuwa na maisha ya familia yenye kuridhisha kabla ya kuja hapa. Hata hivyo, tuliacha makao yetu na kuanza wakati ujao usiojulikana kwa kuitikia mwito wa Sosaiti.”

Ilibidi wengi waondoke kadiri miaka ilivyozidi kupita kwa sababu ya magumu ya kibinafsi ya kiafya, kutokubaliwa kufanya kazi ya kimwili, na mambo mengine. Ingawa hivyo, wengine kama vile Alice Spencer, waliweza kubaki kwa miaka mingi. Alivumilia joto kali la Mombasa kwa miaka zaidi ya 25. Na Margaret Stephenson, ambaye ana umri wa miaka zaidi ya 80, ameishi Kenya kwa miaka zaidi ya 30 na bado anatumikia akiwa painia wa kawaida. * Wakifanya kazi kwa bidii ya kimishonari, akina ndugu na dada hao waliweka msingi ambao juu yao Wakenya wengi wamejenga upendo wao wa ibada ya kweli.

Hata hivyo, kujapokuwa mmiminiko mwingi wa “wanaotumikia penye uhitaji mkubwa zaidi,” kazi bado ilikuwa na kizuizi—kazi nyingi ya kuhubiri ilifanywa miongoni mwa Wazungu, jambo lililomaanisha kuhubiria Wazungu wageni na jumuiya ya Wahindi. Ingawa baadhi ya ndugu zetu walijifunza Kiswahili, ushahidi wao mwingi ulitolewa kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Mipango ya Upanuzi Zaidi

Ndugu Knorr alizuru Nairobi tena katika 1959. Kufikia wakati huo, kikundi kidogo cha watu tisa kilikuwa kimekuwa kutaniko lenye vikundi viwili vya wahubiri 54. Kwa vile ndugu wengi zaidi walipatikana wa kuchukua uongozi, Ndugu Knorr alifanya mpango wa kugawa vikundi hivyo viwili kuwa vinne. Ndugu Nisbet angetumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko, akizuru vikundi hivyo huku akiendelea na kazi yake ya kimwili. Idadi kubwa isivyo kawaida ya wanaopendezwa walipatikana miongoni mwa wageni nyakati hizo.

Utawala wa kikoloni ulipokaribia kukoma, Mashahidi wa Yehova ndio waliokuwa wa kwanza kuwasiliana na wakazi wenyeji, kama inavyoonyeshwa na ono hili linalofuata. Wakati dada mmoja Mzungu alipokuwa akinunua viatu mjini, aliuliza mfanyakazi wa duka hilo mahali alipoishi. Mfanyakazi huyo akasema, “Jeriko.” Dada yetu akajibu, “Najua Jeriko vizuri sana. Mimi huenda huko mara nyingi.” Mara mfanyakazi huyo akasema kwa sauti kubwa, “Oh, basi lazima wewe uwe ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova!”

Kazi ya Ufalme sasa ilikuwa inasonga mbele katika Kenya. Lakini kabla ya kuendelea zaidi, hebu tutue na kutazama nchi zilizoko karibu ambako pia jitihada za kuhubiri habari njema zilikuwa zinaanza kufanywa.

Uganda—“Lulu ya Afrika”

Uganda, jirani ya Kenya upande wa magharibi, ni nchi yenye majani mabichi ambapo mtu anaweza kutembea kistarehe kwenye fuo za kijani kibichi za Ziwa Viktoria, kupanda Milima ya Ruwenzori yenye vilele vya theluji (inayodhaniwa kuwa ile Milima ya Mwezi ya hekaya), kupanda mashua ndogo katika Mto Naili, au kuendesha gari kupitia misitu ya mvua nyingi yenye fahari. Mvua nyingi ilihakikisha mavuno mazuri ya pamba na kahawa pamoja na mboga na matunda mazuri sana. Joto lilikuwa la kiasi, na kiangazi cha mwaka mzima kilifurahisha watawala Waingereza pamoja na wafanya biashara Wahindi. Walifurahia michezo ya nje kwenye vilabu vyao, viwanja vya kuchezea gofu, vidimbwi vya kuogelea, mashindano ya magari, na viwanja vya kuchezea kriketi. Si ajabu kwamba watu waliita Uganda “Lulu ya Afrika.”

Maisha yalikuwa ya utulivu na yenye kufurahisha katika Aprili ya 1950 wakati ambapo wenzi wa ndoa wachanga waliokuwa Mashahidi walipofika Uganda kutoka Uingereza, wakiwa na tamaa ya kushiriki maarifa yao ya Biblia na wengine. Kwa mwaka mmoja walikuwa wamesaidia familia ya Wagiriki na ya Waitalia kufahamu kweli.

Kutaniko dogo lilikuwa limeanzishwa katika Kampala, jiji ambalo limejengwa juu ya vilima saba kama Roma. Kuhubiri miongoni mwa Waafrika kulianzwa polepole, na lilikuwa jambo lenye kusaidia kwamba Kiingereza ndicho kilichokuwa lugha rasmi ya Uganda. Matumizi ya kwanza ya lugha ya kienyeji yalikuwa ni katika hotuba ya watu wote iliyotafsiriwa katika Luganda kwa wahudhuriaji Waafrika wapatao 50. Kufikia 1953, kulikuwa na wahubiri sita wanaotenda.

Miaka miwili baadaye, ubatizo wa kwanza katika Uganda ulifanywa katika Ziwa Viktoria karibu na Entebbe. Miongoni mwa watano waliobatizwa alikuwa ni George Kadu mwenye shauku kwelikweli, ambaye bado anatumikia akiwa mzee mwaminifu katika Kampala.

Matatizo yalitokea wengine walipotengwa na ushirika kwa sababu ya mwenendo mbaya, wengine walipoondoka nchini, na wengine wakakwazwa. Hivyo, kufikia mwisho wa 1957, Ndugu Kadu alijipata akiwa mhubiri peke yake katika Uganda. Lakini alijua alikuwa na kweli, na alimpenda Yehova.

Maonyesho ya sinema yenye kichwa The New World Society in Action, pamoja na kutokezwa kwa kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme” katika Luganda mwaka wa 1958 kulichochea kazi tena katika Uganda. “Wanaotumikia penye uhitaji mkubwa zaidi” kutoka Kanada na Uingereza pia walikuja Uganda kusaidia, na kufikia 1961, miaka mitatu baadaye, kulikuwa na wahubiri 19 wakiripoti. Habari zaidi juu ya nchi hii itakuja baadaye.

Sudan—Nchi Kubwa Zaidi Katika Afrika

Mto Naili Mweupe, ambao ni sehemu ya mto mrefu zaidi duniani, huanzia Uganda na kuingia Sudan kupitia bara za nyasi, vichaka, mabwawa, na bara-kame. Wafugaji warefu wanaishi kando-kando ya mto huo. Baada ya mwendo wa karibu kilometa 2,000, mto huo hujiunga na Naili Buluu, unaotoka kwenye nyanda za juu za Ethiopia upande wa mashariki. Hapo, kando ya mto, pana majiji makubwa matatu: Khartoum, Omdurman, na Khartoum Kaskazini.

Mbele kidogo, Mto Naili hupitia maporomoko kadhaa na kuingia eneo lenye historia nyingi. Hapa palikuwapo milki ya Kushi, magofu yayo yangali yakionekana katika mchanga wa Sahara. Hiyo ndiyo iliyokuwa Ethiopia ya nyakati za Biblia, ambapo Ebedmeleki, pamoja na ofisa wa makao ya kifalme aliyebatizwa na Filipo walitoka.—Yer. 38:7-16; Mdo. 8:25-38.

Sudan, ambayo zamani iliitwa Sudan na Misri za Uingereza ndiyo nchi kubwa zaidi katika Afrika ikiwa na eneo lenye ukubwa wa zaidi ya robo ya lile la United States ya Amerika. Kiarabu ndiyo lugha kuu. Karibu kaskazini yote ni eneo la Kiislamu, na katika kusini mna waabudu-viumbe na wale wanaojiita Wakristo. Watu wa Sudan kwa kawaida ni wakarimu na wenye fadhili kwelikweli.

Ilikuwa ni katika 1949 kwamba Demetrius Atzemis, mhitimu wa Gileadi kutoka Misri, alipokuja Sudan kwa mara ya kwanza. Kama ilivyokuwa katika Misri, kando-kando ya Mto Naili katika Khartoum kulikuwa na rangi ya kijani kibichi kwa sababu ya mashamba ya tango-pepeta, liki, na vitunguu. Maeneo madogo-madogo yaliyokuwa karibu na maji yaliandaa vivuli vyenye kustarehesha chini ya miti mikubwa ya banyani. Lakini maeneo haya ya kijani-kibichi chenye kusitawi yalikwisha na kuwa jangwa lenye ukiwa. Rangi kuu ikiwa ni hudhurungi. Anga lilikuwa hudhurungi. Mchanga, hudhurungi. Nyumba za matope, hudhurungi. Na hata nguo nyingi zilikuwa hudhurungi.

Kisha kulikuwa na joto kali sana. Hali ya joto wakati wa usiku ikifikia Sentigredi 39. Kwenye jua kipima-joto kingeweza kurekodi Sentigredi 60. Kwa vile mabomba ya maji hayakukingwa na jua, maji “baridi” ya kuogea yangeweza kukuchoma usipoacha yatiririke kwanza.

Ndugu Atzemis alianza kazi kwa bidii chini ya hali hizo. Alihubiri sana-sana katika Omdurman, akipata maandikisho 600. Kisha akaenda kwenye mji mdogo wa viwanda ulioitwa Wad Medani, kabla ya kurudi Misri. Baadaye, familia ya washiriki watatu ilihamia Khartoum kutoka Cairo. Ndugu huyo, aliyefanya biashara ya sufu, aliwahubiria wateja wake na kuwatolea maandikisho kabla ya kuwauzia bidhaa.

Upesi kutaniko ndogo lilifanyizwa, idadi ya wahubiri ikiongezeka kila mwezi kutoka kilele kimoja hadi kingine, idadi hiyo ikifikia 16 kufikia mwisho wa Agosti 1951. Jambo kuu la mwaka uliofuata lilikuwa hotuba iliyotolewa kwa watu 32. Hotuba hiyo ilitafsiriwa katika lugha tatu kwa manufaa ya wageni waliokuwapo.

Katika 1953, Ndugu Atzemis alirudi kutoka Cairo, wakati huu kwa miezi mitano, na kupanga uenezaji wa utaratibu wa eneo katika Khartoum. Alithawabishwa wakati ndugu wa kimwili watatu wanaoitwa akina Orphanides walipokuja kwenye kweli. Mwezi mmoja tu baada ya yeye kupatikana, George Orphanides alitoa sehemu kubwa ya nyumba yake iwe mahali pa mkutano. Ndugu huyu hatimaye alikuwa mwangalizi wa kutaniko, na wakiwa pamoja na ndugu yake Dimitri, walikuwa wenye bidii sana katika kuhubiri ujumbe wa Ufalme kwa wengine. George angeweza kuwa imara sana na thabiti na wakati uo huo mwenye ukarimu sana katika kuchunga kondoo. Alitumikia kwa miaka mingi mpaka 1970, ambapo ilimbidi aondoke nchini. Dimitri alisaidia wengi katika kweli. Kujapokuwa joto kali sana isiyo na huruma na dhoruba ya upepo-mchanga ya mara kwa mara, ndugu hao walivumilia wakiwa na mwelekeo unaofaa. Wakati mmoja George alisema hivi: “Ingawa hatutambuliwi na ulimwengu, lakini tukitambuliwa mbinguni na kwa msaada wa roho ya Yehova, tulifurahia kila siku ya maisha zetu, tukijaribu kutimiza huduma yetu kulingana na maneno ya Paulo katika 2 Timotheo 4:2-5.”

Ndugu Atzemis alirudi mara kwa mara, na katika 1955 iliwezekana kwa Sosaiti kutuma mishonari mwingine Khartoum, ambaye aliitwa Emmanuel Paterakis naye aliishi kwa miezi kumi. Wahubiri kadhaa walikuwa wameondoka nchini kufikia wakati huo. Ombi la kuandikishwa kisheria lilifanywa katika Juni 1956, lakini kwa sababu ya ushawishi wa makasisi wa Koptiki na viongozi wa kidini wa Kiislamu, ombi hilo lilikataliwa. Mashahidi walichunguzwa kwa muda mfupi, lakini hakukutokea mnyanyaso mkali, na kazi ya kuhubiri haikusimamishwa.

Dada Waaminifu

Katika karne ya kwanza, wanawake waliojitoa walikuwa nguzo ya kiroho katika kutaniko. Ndivyo ilivyo pia katika karne ya 20 nchini Sudan. (Mdo. 16:14, 15; 17:34; 18:2; 2 Tim. 1:5) Katika 1952, dada Mgiriki mwenye bidii aliyeolewa na mtu wa Sudan katika Lebanoni alikuja nyumbani kwa mume wake achochee kazi ya kuhubiri. Upesi dada huyo, Ingilizi Caliopi akawa painia wa kawaida na baadaye painia wa pekee. Alikuwa mwenye nguvu, nishati na thabiti—sifa zilizohitajiwa wakati wa kuhubiria wafuasi wa Kanisa la Koptiki la Orthodoksi, ambao walikuwa ni watu wenye hisia inayochokozeka haraka na wepesi kukasirika, wenye kuwaogopa makasisi na watu wa ukoo.

Miongoni mwa wale aliosaidia kupata kweli ni Mary Girgis, ambaye pia alikuja kuwa painia wa pekee na ambaye masimulizi ya maisha yake yalitokea katika Mnara wa Mlinzi la Februari 15, 1977 (Kiingereza). Mary aliishi katika jiji la kihistoria la Omdurman, jiji kuu la kale la Sudan. Alikuwa ndipo tu amemaliza kusali wakati Dada Caliopi alipomzuru mara ya kwanza katika 1958. Dada Caliopi alipata mwanamke aliyesumbuka juu ya hayawani wanaoogofya wanaosimuliwa katika Ufunuo. Hayawani hao walimaanisha nini? Hofu kuu ya “moto wa mateso” ilimfadhaisha pia. Alitaka kujua kama hayo yangekuwa ni mapenzi ya Mungu. Lakini swali lake kubwa zaidi lilikuwa, Kweli iko wapi?

Dada Caliopi alijibu maswali hayo yote. Mary alifurahi kusikia kwamba sasa Yesu ni Mfalme. Lakini mume wake, Ibrahim, alimwambia, “Usimsikilize mwanamke huyu. Ni lazima yeye awe ni mbaya. Juzi alipoanguka kutoka kwenye basi, watu walisema, ‘amestahili kwa sababu alibadili dini yake.’”

Ijapokuwa hilo, Ibrahim bado alichukua vile vitabu viwili “Let God Be True” na “This Means Everlasting Life.” Upesi baadaye, alipokuwa akihudhuria kanisa Koptiki, Ibrahim alikasirika alipomsikiliza kasisi aliyekuwa akishutumu waume kwa kuruhusu wake zao wajifunze na kuhubiri dini tofauti. Ilikuwa ni rahisi kuona kasisi alikuwa akiongea juu ya nani! Ibrahim aliacha kanisa hilo. Sasa yeye na familia yake wakaanza kunyanyaswa. Siku moja jiwe lililotupwa kutoka upande mwingine wa ukuta lilimgonga na kuangusha miwani yake lakini bila kumdhuru sana wala kivulana wake aliyekuwa amebeba mikononi mwake!

Katika 1959, polisi walimshtaki Mary Girgis kwamba alienda kwenye nyumba za watu kwa nia ya kuiba. Jambo hilo likafikishwa mahakamani. Washtaki wawili waliwekwa dhidi yake, lakini bila shaka, hakukuwa na uthibitisho. Kesi hiyo ikatupiliwa mbali.

Katika kesi nyingine ya mahakama, makasisi walileta mashtaka ya Usayuni. Mahakamani, dada yetu alitukuza jina la Yehova mbele ya mahakimu wanne. Hakimu aliyesimamia kesi hiyo aliamua vizuri akisema, “Enda, mama, kotekote katika Sudan, ukahubiri kadiri unavyotaka. Sheria ya nchi hii inakuunga mkono na itakulinda.”

Dada Girgis na, hadi kifo chake, Dada Caliopi wamekuwa mifano mizuri sana kwa wachanga. Dada hao wawili wenye bidii wamesaidia wengi kupata kweli kwa miaka hiyo mingi. Ibrahim Girgis pia alichukua msimamo kwa ajili ya kweli na akawa mwaminifu hadi kifo chake.

Jitihada za kupata kutambuliwa kisheria hazikufaulu, kwa hiyo kazi iliendelea katika hali ya kutokutambuliwa kisheria, kukiwa na mnyanyaso mara moja moja. Hata hivyo, maongezeko yalizidi kufuata, kukiwa na 27 wakiripoti katika 1960 na 37 katika 1962. Katika 1965, kazi ilikuja chini ya uangalizi wa ofisi ya tawi mpya iliyofunguliwa Kenya, na kusanyiko la mzunguko likapangwa mara moja kila mwaka. Wakati wa mwaka uliofuata, watu 81 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo. Tutasikia kutoka nchi hii tena.

Ethiopia—“Eneo la Nyuso Zilizochomeka”

Ethiopia iko kati ya Sudan na Bahari Nyekundu, ina ukubwa wa nusu ya Sudan, na ni jirani ya Kenya ya kaskazini. Katika Kigiriki, jina hilo lamaanisha “Eneo la Nyuso Zilizochomeka,” na katika nyakati za kale jina hilo lilitumiwa kuonyesha eneo la Afrika lililokuwa kusini mwa Misri. Hivyo, Ethiopia inayotajwa na Biblia hasa ni kaskazini mwa Sudan na kisehemu cha kaskazini mwa Ethiopia ya kisasa. Kama vile Ndugu Hatzakortzian alivyokuwa amepata katika miaka ya 1930, nchi hii ilikuwa ya pekee katika njia nyingi, ikiwa na utamaduni wayo na Kanisa Orthodoksi la Ethiopia likiwa ndilo dini kuu. Huo ndio uliokuwa mgawo wa wamishonari waseja watatu waliofika jiji kuu Addis Ababa, katika Septemba 14, 1950.

Kulikuwa na mambo mengi mapya ya kuzoeleana nayo. La kwanza lilikuwa ni mwinuko wa Addis Ababa, ambao ukiwa kwenye mwinuko wa meta 2,400 ni mojawapo majiji makuu yaliyo juu zaidi ulimwenguni. Jambo jingine lilikuwa ni lugha ya Kiamhara, ikiwa na maneno yanayosikika kwa sauti ya juu ya p, t, na s, na ikiwa pia na alfabeti ya Kiethiopia yenye herufi 33 zinazoweza kutamkwa kwa njia tofauti-tofauti 250. Kwa kuongezea, kulikuwa na lugha zaidi ya 70 za kikabila na nyingine 200 na lahaja ndogo-ndogo. Zaidi ya hayo, makasisi bado walitumia lugha iliyoendelea kuisha iliyoitwa Kigiizi, kama vile wanachuo fulani wa Ulaya hutumia Kilatini.

Watu walikuwa na nyuso zenye kuvutia za rangi hudhurungi kwa sababu ya jua, mitindo ya nywele isiyo ya kawaida, mavazi yenye kutofautisha, na mavazi ya sherehe. Wengine walikuwa na misalaba iliyochorwa kwenye vipaji vya nyuso zao. Walikuwa na majina yenye kupendeza. Wanaume wangeweza kuitwa Gebre Meskal, linalomaanisha “Mtumwa wa Msalaba”; Habtemariam, linalomaanisha “Mtumishi wa Mariamu”; au Tekle Haimanot, linalomaanisha “Mmea wa Dini.” Mwanamke angeitwa Leteberhan, likimaanisha “Mtumwa wa Nuru,” au Amaresh, “Wewe ni Mrembo.”

Walimu wa Shule Huku Wakiwa Wahubiri

Katika makao yao ya kwanza ya wamishonari katika eneo la Addis Ababa la Kasa Popolari, wamishonari walishangaa kuona mbega akiwatembelea kwa ukawaida. Mbega huyo machachari angeenda kila mahali na kuharibu kitu kimoja baada ya kingine. Hakucheza tu na nyanya zilizotengenezwa zikawa umaji-maji, bali pia aliupaka sakafuni na ukutani! Wageni wanadamu walikuja pia bila shaka, na mafunzo ya Biblia yaliongozwa katika sebule ya mbele ya makao ya wamishonari.

Ili kulinda masilahi ya Kanisa la Ethiopia, sheria ilikataza kuhubiri miongoni mwa Wakristo. Kuhubiri kulikubaliwa tu miongoni mwa Waislamu na “wapagani.” Hivyo, wamishonari walikubaliwa waingie ikiwa tu wangeanzisha shule za kufundisha masomo kama Kiingereza, kupiga taipu, na kuweka hesabu.

Wakati masomo ya watu wazima yalipoanzishwa vizuri katika Addis Ababa, ilibidi wamishonari wahamie makao makubwa zaidi katika barabara ya Churchill Road, iliyokuwa njia kuu ya jiji. Ndugu hao waliamua kutochanganya mafundisho ya kidini na masomo ya shule, lakini wanafunzi walialikwa kuhudhuria mikutano ikiwa wangependa. Wakati wa mikutano, mojawapo madarasa ya masomo liligeuzwa kuwa Jumba la Ufalme.

Katika 1952, wamishonari wanane zaidi kutoka darasa la 18 la Shule ya Gileadi waliwasili Addis Ababa. Miongoni mwao mlikuwamo Harold na Anne Zimmerman, ambao walipewa mgawo wa kusaidia katika madarasa ya usiku katika jiji kuu. Wenzi wa ndoa wanne akina Brumley na Luck, walifungua shule katika mji wa kihistoria wa Harar, karibu na mpaka wa Somalia katika mashariki, ambapo hapo awali wageni hawakuruhusiwa kwenda na uliokuwa ukitembelewa sana na fisi. Kwa kweli wale waitwao watu wa fisi huandaa tamasha wakati wa usiku kwa kuwalisha fisi hao wenye nguvu kwa furaha ya watazamaji.—Ona Amkeni! (Kiingereza) la Novemba 22, 1985.

Wamishonari wa Gileadi Dean Haupt na Raymond Egilson walianzisha shule nyingine kama hiyo katika Diredawa, mji wa kibiashara karibu na Harar, ukiwa mahali panapofaa katika reli pekee ya Ethiopia inayotoka bandari ya Djibouti kuelekea Addis Ababa. Hapa ndipo Ndugu Hatzakortzian alipofia.

Maisha hayakuwa ya starehe. Ndugu Haupt aeleza hivi: “Usiku wetu wa kwanza ulikuwa ni ono tusiloweza kusahau. Bado hatukuwa na fanicha, kwa hiyo tulitumia sanduku kubwa kuwa meza nasi tulikalia masanduku ili tule chakula chetu. Tulitandika magodoro yetu chini kwa sababu vitanda vyetu havikuwa vimefika. Hali haikuwa mbaya sana, lakini tulipozima taa, kunguni walianza kuteremka ukutani watuume! Ilionekana kwamba nyumba hiyo ilikuwa imekuwa bila mtu kwa muda fulani, na kunguni walitaka damu mpya! Sidhani kama tulilala usiku huo.”

Ofisi Ndogo ya Tawi

Mishonari mmoja aeleza kwamba kazi ilifurahisha siku hizo wajapokuwako wadudu hao: “Nilikuwa natembea njiani siku moja wakati nilipokutana na kijana mmoja Mwethiopia na nikasimama niseme naye. Alipojua kwamba nilikuwa mishonari, aliuliza, ‘Tafadhali, Bwana, niambie juu ya Yesu Kristo.’ Nikamwalika kwetu siku iliyofuata, na baada ya dakika kumi za kuwasili kwake, funzo lilikuwa tayari linaendelea katika kitabu “Let God Be True.” Alirudi siku iliyofuata pamoja na kijana mwingine. Hao wawili wakawa wahubiri wa kwanza Waethiopia.”

Watu wengi wangekuja kwenye makao ya mishonari wakiomba mafunzo ya Biblia, hivyo ilikuwa ni lazima mishonari mmoja abaki nyumbani. Watu wengine walikuwa wametembea kwa saa nyingi ili waje na walitaka kujifunza kwa saa mbili au tatu kwa kikao kimoja. Upesi idadi ya wahubiri ikafika 83.

Katika 1953, ofisi ndogo ya tawi ilifunguliwa katika Addis Ababa. Tafsiri iliyoandikwa kwa mkono ya mambo ya mikutano ilitayarishwa katika maandishi ya Kiethiopia na kurudufishwa kwa mkono. Jambo hilo lilisaidia wapya wawe na msingi mzuri katika kweli. Ndugu wenyeji walijifunza kuhubiri nyumba kwa nyumba, kuongoza mafunzo ya Biblia, na kuongoza mikutano yenye kuarifu. Kwa sababu ya bidii yao, habari njema ilienezwa katika sehemu 13 tofauti-tofauti nchini humo, ambapo kulikuwa na karibu wahubiri 20 wakiripoti kufikia 1954.

Kasisi Mwanafunzi Ashika Jembe

Mmoja wa wale walioitikia vema ujumbe wa Ufalme alikuwa ni kasisi mwanafunzi ambaye hakujua hata neno moja la Kiingereza. Mazungumzo yake ya kwanza na mmoja wa wamishonari wetu yalifanywa kupitia mkalimani. Mambo yenye kutokeza ubishi yalipotokea, mwanafunzi huyo angeangalia Biblia yake katika lugha ya kale ya Kigiizi. Alishtuka kuona kwamba utegemezo wake aliopenda sana wa Utatu katika 1 Yohana 5:7, haukuwa katika Biblia yake. Upesi mafundisho mengine bandia yalifunuliwa wazi kwa Biblia hiyo.

Alikuja kwa funzo mara tatu au nne kwa juma, akileta wengine pamoja naye. Alipoacha seminari akaishi na Shahidi mmoja, karani wa seminari hiyo alikuja na polisi nao wakamburuta wakaenda naye. Baadaye, alipokuwa amefungwa katika seminari kwa siku nne, alipeleka ujumbe kwa akina ndugu akiwaambia wasimhuzunikie kwa kuwa alikuwa akishangilia kwamba alikuwa mfungwa kwa ajili ya Yehova. “Msifikiri nitarudia kanisa hilo,” akasema. “Hakuna mtu anayeshika jembe kisha akaangalia nyuma.” Alihamia jiji kuu baada ya yeye kufunguliwa, ambapo alihudhuria mikutano na akaja kuwa miongoni mwa Waethiopia wa kwanza waliobatizwa kuwa Mashahidi wa Yehova.

Hatimaye Fasihi Katika Kiamhara!

Katika 1955, baada ya hotuba ya pekee, wahudhuriaji walifurahia toleo la kwanza katika lugha ya Kiamhara, toleo hilo likiwa ni kijitabu God’s Way Is Love. Upesi baadaye, trakti ilitolewa, na katika mwaka uliofuata, kijitabu cha funzo “Habari Njema Hizi za Ufalme” kikapatikana katika Kiamhara.

Katika mwaka uliofuata wa 1956, maendeleo makubwa yalifanywa katika historia ya kitheokrasi katika Ethiopia. Ndugu walipanga kuonyesha sinema The New World Society in Action (Jamii ya Ulimwengu Mpya Katika Utendaji). Vikaratasi vya mwaliko katika Kiingereza na Kiamhara vilitangaza sinema hiyo, iliyoonyeshwa katika jumba kubwa zaidi la sinema katika Ethiopia, jumba hilo likiwa katikati ya jiji la Addis Ababa. Karatasi za kutangaza sinema hiyo ziliwekwa katika sehemu zote zenye shughuli nyingi za jiji. Tokeo lilikuwa nini? Umati mkubwa wa watu ulikuja kwenye jumba hilo la sinema. Jumba lilijaa sana hivi kwamba ilikuwa ni lazima kupanga sinema hiyo ionyeshwe mara ya pili. Usiku huo, watu 1,600 waliona sinema hiyo. Kila mmoja aliyehudhuria alipewa kijitabu bila malipo. Baadaye sinema hiyo ilionyeshwa katika Asmara, Gondar, na Dese, miji mikubwa mitatu ya kaskazini mwa Ethiopia. Jumla ya watu 3,775 waliona sinema hiyo iliyofunza juu ya kazi ya Mashahidi wa Yehova.

Mapainia wa pekee zaidi waliwekwa, na mwanglizi wa mzunguko mwenyeji alianza kutia makutaniko moyo. Ndugu walihubiri kwa ujasiri, wakiungwa mkono na katiba iliyorekebishwa iliyohakikisha haki za kibinadamu za msingi kuwa na uhuru wa kueleza itikadi za kidini, uhuru wa usemi, na uhuru wa uandishi wa habari. Idadi ya wahubiri ikafikia kilele cha 103.

Mnyanyaso! Wamishonari Wafukuzwa!

Utendaji huo wote na ufanisi wa kiroho uliamsha hasira ya makasisi wa Jumuiya ya Wakristo. Katika mji wa Debre Markos, mji mkuu wa mkoa uliokuwa karibu kilometa 280 kaskazini-magharibi mwa Addis Ababa, watu bado walikuwa washikamanifu sana kwa Kanisa la Ethiopia.

Wakati mapainia wa pekee walipowasili huko, ghasia zenye jeuri zililipuka mara hiyo. Wakuu walikusanya umati wenye ghasia katikati ya mji, wakipiga kelele kwamba watu hao wapya walikuwa wamekanyaga-kanyaga picha ya Maria na kula paka na mbwa! Ilibidi polisi waokoe ndugu hao wasipigwe hadi kufa. Umati huo, ukiwa tayari kujisukumiza ndani ya kituo cha polisi, ulizuiwa kwa kuelekezewa bunduki. Katika ghasia hizo, mapainia hao walipoteza mali yao yote.

Serikali ilitumia kisa hicho kutangaza kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa tisho kwa amani na usalama wa taifa. Serikali ilifunga makao ya mishonari na ofisi ya tawi na kuwaamuru wamishonari waondoke nchini mnamo Mei 30, 1957. Ingawa maofisa fulani walituonea huruma kwa faragha na kutaja fungu la makasisi katika jambo hilo, maombi kwa maliki mwenyewe hayakufanikiwa.

Ingawa barua nyingi za kuteta ziliandikwa kutoka ulimwenguni pote, wamishonari walilazimishwa kuondoka nchini. Visa vingi vya kushikwa na mahoji vilifuata. Sasa kukaja wakati wa kutahiniwa na kupepetwa. Wengine wakawa na hofu na kuacha kweli. Wachache wakawa wasaliti. Kazi ya painia wa pekee ilikomeshwa na mapainia kadhaa wa zamani walitengwa na ushirika. Hata hivyo, wengine walibaki waaminifu. Ndugu mmoja alifungwa miguu kwa pingu kwa siku 42 na kisha akaachiliwa na kuonywa vikali akomeshe kuhubiri kwake.

Hivyo, kazi ilianza kufanywa kisiri-siri. Mbali sana na huko, katika Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko la Kimataifa la 1958, kitabu cha kwanza katika Kiamhara, “Let God Be True,” kilitolewa, lakini ni nakala chache tu zilizopenya Ethiopia. Majaribu ya uaminifu na ushujaa ujapokuwa mnyanyaso yaliangusha wengi njiani, hivi kwamba kufikia 1962, idadi ya wale waliokuwa wakitenda ilishuka kufikia 76.

Somalia—Katika Pembe ya Afrika

Baada ya mishonari Dean Haupt kufukuzwa Addis Ababa, aliagizwa na Sosaiti aende Mogadishu, jiji kuu la Somalia. Mogadishu lilikuwa limekuwa kituo cha biashara kwa miaka elfu moja. Je! zamani jiji hilo lilikuwa sehemu ya Ofiri, iliyotokeza dhahabu ya hali ya juu ya Mfalme Sulemani? Inawezekana, ingawa wengi wanaona kwamba Arabia ndiyo iliyokuwa chanzo cha dhahabu hiyo.

Hata hivyo, wakati ndugu Haupt alipowasili katika 1957, Kisomali bado hakikuwa lugha inayoandikwa; badala ya hivyo, Kiitalia na Kiarabu zilitumiwa. Ndugu Haupt aliamua kufanya kazi katika eneo la Wazungu kwanza katika mji huo, akitoa maandikisho na kuonyesha nakala sampuli za magazeti bila kuziangusha, kwa kuwa ni chache sana zilizopatikana. Alipata maandikisho zaidi ya 90 kwa karibu miezi mitatu akitumia njia hiyo. Kisha viza yake ya kukaa huko ikakwisha na haingeweza kufanywa upya. Kwa hiyo ilikuwa ni lazima Ndugu Haupt aondoke naye ameendelea na utumishi wake katika Italia.

Mgawo Mgumu

Baada ya Ndugu Haupt kuondoka, Sosaiti ilipanga kutuma wamishonari wanne Somalia. Walifika katika Machi 1959, na kwa sababu kuhubiri kulifanywa hasa mingoni mwa wageni, ni Vito na Fern Fraese pekee wa darasa la 12 la Gileadi waliobaki.

Upesi makasisi wa Katoliki walianza kuzuru wale walioonyesha kupendezwa katika kazi ya Mashahidi wa Yehova. Mtu mmoja aliyetembelewa hivyo na kasisi alisema hivi: “Mbona kunihangaikia sasa, na ni miaka mingi tangu nikome kuhudhuria kanisa? Je! ni kwa sababu ninajifunza Biblia?”

Katika Septemba 1959, akina Fraese waliongoza mafunzo ya Biblia 11. Wengi wa familia za Waitalia waliotembelewa hawakuwa na Biblia wala hawakuwa wameelezwa Yehova ni nani, ingawa walikuwa wamesikia juu ya Mashahidi wa Yehova magazetini. Kwa hiyo kulikuwa na kupendezwa kwingi katika ujumbe wa Biblia; lilikuwa jambo la kawaida kwa akina ndugu kukaa saa nzima au zaidi katika kila nyumba waliyotembelea.

Wanafunzi wawili wa Biblia walianza kuhubiri katika 1961. Mwaka uliofuata, mtu mwingine akajiunga na Mashahidi wa Yehova, kukifanya kuwe na jumla ya wahubiri watatu kwa kuongezea wamishonari.

Baada ya miaka minne katika Somalia, akina Fraese walipewa mgawo mwingine kwa kuwa hakukuwa na uwezekano mkubwa wa kuwafikia wakazi Waislamu wa huko. Lakini walikuwa wamevuta uangalifu kwao. Ni kama vile mchunguza mambo mmoja alivyosema: “Kati ya vikundi vyote vya Wazungu, kutia ndani wamishonari wasiohitimu na makasisi, nyinyi Mashahidi wa Yehova ndinyi pekee mliodumisha maadili mazuri!” Kati ya wahubiri watatu waliobaki, wawili baadaye walienda nchi nyinginezo, na mmoja akaacha utendaji wake. Hata hivyo, akina Fraese bado wako katika utumishi wa wakati wote katika kazi ya mzunguko katika Italia.

Tanzania—Nchi Yenye Kuvutia Zaidi ya Afrika

Tanganyika, ambayo sasa ni Tanzania, iko upande wa chini kuteremka pwani kutoka Somalia. Ni nchi yenye uzuri ambayo ni kubwa kushinda jirani yayo ya kaskazini, Kenya. Ni nchi yenye Uwanda wa Serengeti—ambayo mara nyingi huitwa nchi yenye kuvutia zaidi ya Afrika—ambapo wanyama wakubwa wenye kuvutia zaidi ya milioni mbili huzunguka-zunguka savana na misitu, ndiko kunakopatikana Kreta ya Ngorongoro, bonde kubwa mfano wa bakuli la kilometa za mraba 160 lililojaa wanyama. Wengi wa wakazi ni wakulima, ambao hutoa katani, karafuu, kahawa, na pamba.

Habari njema za Ufalme zilikuwa zimehubiriwa Tanganyika katika miaka ya 1930, na hivyo kulikuwa na idadi ndogo ya wahubiri wakitumikia katika kusini-magharibi mwa nchi hiyo kufikia 1948. Walikuwa ni akina nani? Nao walijifunzaje kweli?

Walikuwa hasa ni wa kabila la Wanyakyusa, lililo katika milima iliyo karibu na ncha ya kaskazini ya Ziwa Malawi ambapo sehemu mbili za Bonde Kuu la Ufa hukutana. Watu walitoka hapo wakaenda kufanya kazi katika migodi ya shaba ya Rhodesia. Wakiwa ni watu wenye urafiki na upole kwa asili, kwa wengine wao kazi hiyo ndiyo iliyofanya wapate kweli kutoka kwa Neno la Mungu.

Hosea Njabula, aliyezaliwa katika 1901 karibu na Tukuyu, alikuwa na shauku sana kwa imani yake ya Uprotestanti wa Kimoravia. Akawa shemasi, akifundisha shule za Jumapili katika vijiji vingi. Mmoja wa wanafunzi wake alikuwa ni Nehemiah Kalile. Siku moja katika 1930, alipokuwa akifanya kazi ya upishi katika Vawa (Vwawa) kwa masetla Wazungu, Nehemiah alijikuta katika mazungumzo mazito ya Biblia pamoja na mpishi mwingine.

Nehemiah aligundua kwamba mtu huyo alijua mambo ya ajabu kutoka kwa Biblia. Hiyo ilikuwa ndiyo kweli! Upesi baada ya hapo alivuka mpaka hadi mji wa Mwenzo akabatizwe. Huko alivutiwa sana alipoona kwa mara ya kwanza, yale mabuku saba ya Studies in the Scriptures.

Nehemiah Kalile alijaa idili. Alitamani sana kuambia mwalimu wake wa zamani wa shule ya Jumapili juu ya ugunduzi wake. Hivyo, mwaka uliofuata alikutana tena na rafiki yake, Hosea Njabula, na kumweleza juu ya kweli.

Zaidi ya miaka 60 baadaye, Hosea hukumbuka siku hiyo na kusema hivi: “Nilibisha sana, lakini aliponionyesha Maandiko kuhusu Sabato, nilijua hiyo ndiyo kweli. Nilianza kuhubiria wengine bila kukawia, kutia ndani Job Kibonde. Sisi watatu tukaanza mikutano katika nyumba yangu. Nilienda kuwaona wanafunzi wangu wengine wa Shule ya Jumapili. Niliwaalika waje kwenye mikutano yetu. Baadhi yao walikubali, miongoni mwao wakiwemo Joram Kajumba na Obeth Mwaisabila.”

Kupiga Miguu Milimani Kote

Baada ya ubatizo wa Ndugu Njabula katika 1932, ndugu hao pasipo kujua mhudumu painia ni nani, walihubiri kama mapainia. Walitembea kilometa 57 kuelekea Ziwa Malawi na kutoa ushahidi katika eneo la Kyela, ambapo Hosea Njabula na Obeth Mwaisabila walipata upinzani mkali. Walishikwa na kutupwa katika mto uliojaa mamba hata ingawa hawakujua kuogelea. Kwa njia fulani, labda kwa msaada wa Yehova, walipona. Upesi baada ya kisa hicho walijenga Jumba la Ufalme lao la kwanza karibu na kijiji cha Buyesi katika mahali walipoita Bethlehemu.

Wakati uo huo, kupendezwa zaidi kulisitawi katika Vawa, ambapo Nehemiah Kalile alipata kusikia kweli kwa mara ya kwanza, na watu kama akina Solomon Mwaibako, Yesaya Mulawa, na Yohani Mwamboneke walichukua msimamo wao. Wale waliokuwa Buyesi walifanya mpango wenye upendo wa kutuma mmoja wao kutembelea kijiji cha Ndolezi karibu na Vawa mara moja kwa mwezi ili kuwaimarisha wale wapya. Ilimaanisha kutembea kilometa 100 kwenda tu. Nyakati nyingine walitembea hata zaidi ya kilometa 190 hadi Isoka katika Rhodesia Kaskazini wapeleke ripoti zao kwa kutaniko la huko ili zipelekwe kwenye ofisi ya tawi.

Leo, miongo sita baadaye, akiwa na umri wa miaka 90, Hosea Njabula bado ni “shemasi,” sasa katika maana halisi, akiwa mtumishi wa huduma katika kutaniko la Ndolezi. Ndugu Njabula ana uradhi wa kuona mke wake mwaminifu, Leya Nsile, akiendelea kwa bidii pamoja naye, na pia wajukuu kadhaa wakiwa watendaji katika kazi ya painia.

Wengine pia walikuwa na miaka mingi ya kuhubiri kwa bidii. Miongoni mwao mlikuwamo Jimu Mwaikwaba, ambaye alivumilia kifungo cha jela kwa sababu ya habari njema; Joel Mwandembo, ambaye baadaye alitumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko; Semu Mwasakuna, aliyehubiri kwa baiskeli na nyimbo; Ananiah Mwakisisya; na Timothy Kafuko.

Ndugu mwingine aliyesaidia sana kuendeleza kazi ya kutoa ushahidi wa Ufalme alikuwa ni David Kipengere, aliyezaliwa mwaka wa 1922 na kujifunza kweli mwaka wa 1935 mjini Mbeya. Alihubiri kotekote na baadaye alitumwa kufungua kazi katika Dar es Salaam. Alikuwa painia wa kawaida katika miaka 18 ya mwisho ya maisha yake hadi kifo chake mwaka wa 1983. Alishikwa mara nyingi, lakini hakuvunjika moyo, akisema: “Kuna kazi nyingi gerezani ambayo Yehova ananitaka nitimize.” Ndugu yake anayeitwa Barnabas Mwakahabala, aliyejifunza kweli pamoja naye, bado anatumikia akiwa mzee mpaka leo. Ndugu hao walifanya yote wawezayo katika hali yao ya upweke, bila fasihi katika lugha yao na bila kujua sana kusoma.

Mawasiliano na ofisi ya tawi katika Cape Town yalitokea mara moja-moja, na ripoti hazikutegemeka. Kitabu-Mwaka cha 1943 (Kiingereza) kinaonyesha kwamba 158 walishiriki katika kazi ya kuhubiri katika eneo hili, na katika 1946, kulikuwa na 227 wakiripoti katika makutaniko saba. Wakati wa miaka iliyotangulia, utendaji wa Mashahidi katika Tanganyika yaonekana ulitiwa ndani ya ripoti za Kutaniko la Isoka katika Rhodesia Kaskazini, na labda ripoti nyinginezo zilipotea. Miaka kadhaa bado ingepita kabla ya usimamizi mzuri zaidi kutolewa kwa kazi ya kukusanya katika kusini mwa Tanganyika.

Usimamizi Kutoka Rhodesia Kaskazini

Hakika msaada ulihitajiwa kwa kuwa Mashahidi walipata upinzani mwingi kutoka kwa dini bandia, na wakati uleule walipambana na matatizo ya kuoa wanawake zaidi ya mmoja, kutumia tumbako, na desturi nyingine zisizo za Kikristo.

Katika 1948, ofisi mpya ya tawi ilifunguliwa Lusaka, katika Rhodesia Kaskazini, ambayo haingesimamia kazi katika Rhodesia Kaskazini pekee, bali pia sehemu kubwa ya Afrika Mashariki. Huo ulithibitika kuwa uongozi wa kimungu kwa sababu baada ya kituo cha muda mrefu, mianzo mingine ilikaribia kuonekana katika Kenya na Uganda. Ingawa ofisi ya tawi ilikuwa zaidi ya kilometa 2,400 za barabara mbovu kutoka Nairobi, bado ilikuwa karibu zaidi ya Cape Town, iliyokuwa umbali wa mara mbili zaidi.

Hivyo, katika 1948, ofisi ya tawi katika Rhodesia Kaskazini ilimtuma Thomson Kangale asaidie akina ndugu. Alipofika Mbeya katika Machi wa mwaka huo, alikuta kwamba kulikuwa mengi ya kufundisha na kurekebisha.

Ndugu Kangale alikuwa mwalimu mwenye subira, na ndugu zetu waliitikia kwa haraka kufanya marekebisho yaliyohitajika. Kwanza kabisa, walijifunza kujitambulisha kuwa Mashahidi wa Yehova wala si watu wa Watchtower tena. Walikuwa wamejua na kukubali jina Mashahidi wa Yehova mapema lakini hawakulitumia peupe. Ndugu zetu walijifunza pia kuwa wenye busara zaidi wanapotoa ujumbe wa Ufalme kupatana na shauri katika 1 Petro 3:15. Sasa walitoa habari njema badala ya kushambulia tu mafundisho bandia ya kidini. Na kutokuelewa njia ifaayo ya kuripoti wakati uliotumiwa shambani kulirekebishwa. Kwa kuongezea, ndugu walifanya makao yao yawe safi. Walifanya maendeleo pia katika sura zao; kadhaa walihitaji kunyoa ndevu zao zisizotunzwa.

Wote walijifunza kufuata programu yenye utaratibu mzuri na yenye kufaa na kuacha masalio ya Kibabuloni, kama vile matumizi ya kengele mikutanoni. Waliona manufaa ya kukoma kutangaza majina ya wale waliofanya vizuri katika mapitio ya kuandika wakati wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi. Iliwabidi Mashahidi wengine kuacha desturi fulani zilizohusu kuheshimu wafu. Kwa wengine ulikuwa ni wakati wa kuacha zoea la matumizi ya tumbako. Lakini kuhalalisha ndoa ili ziheshimike mbele ya wote, labda ndiko kulikokuwa rekebisho gumu zaidi.—Ebr. 13:4.

Majaribio ya Kisheria ya Kupata Kutambuliwa Rasmi

Ofisi ya tawi katika Rhodesia Kaskazini ilijaribu mara nyingi kufanya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika Tanganyika iruhusu wamishonari kuingia nchini na kutambua rasmi kazi ya kuhubiri. Ombi lilikataliwa katika 1950, sababu ikitolewa kwamba “hali zilizopo Tanganyika zilikuwa tofauti na za maeneo mengine ya Afrika.” Ombi jingine lilifanywa katika 1951 lakini tena bila mafanikio. Wakati uo huo, mkuu fulani wa wilaya alijaribu kupiga kazi marufuku katika eneo lake. Katika Septemba wa 1951, ujumbe wa akina ndugu ulitembelea wakuu wa serikali Dar es Salaam, wakiwa na hati iliyoeleza msimamo wa Mashahidi wa Yehova kuhusu mashirika ya kidini na sherehe za kizalendo. Jambo hilo lilitokeza tumaini, lakini katika mwaka uliofuata, walipata jibu lingine kwamba ombi lao lilikataliwa. Maombi zaidi yalifanywa katika 1956 na baadaye, lakini bila mafanikio.

Kujapokuwa mwelekeo usiofaa wa serikali, ibada ya wahubiri wa habari njema haikuzuiwa kihalisi. Mapainia wa pekee na waangalizi wa mzunguko kutoka Rhodesia Kaskazini waliendelea kusaidia bila matatizo.

Jitihada za Mazoezi Zaendelea

Katika 1952, Buster Mayo Holcomb, mhitimu wa Gileadi aliyetumikia akiwa mwangalizi wa wilaya katika Rhodesia Kaskazini, aliweza kuvuka na kuingia Tanganyika na kutumikia kusanyiko la mzunguko karibu na Tukuyu. Yeye alisema hivi: “Tulikuwa tumekaribia mahali pa kusanyiko baadaye sana alasiri nasi tulikuwa na matumaini ya kufika kabla ya giza kuingia; kisha mbingu zikatuangukia kihalisi kwa mvua kubwa. Hatungeweza kuendelea mbele kwa sababu hatungeweza kuona njia katika mvua kubwa. Tulisimamisha gari letu na kujitayarisha kulala hapo vizuri zaidi kadiri iwezekanavyo kwa sababu mvua ilionekana inaongezeka zaidi badala ya kupungua. Hata hivyo, mvua iliacha kunyesha asubuhi ya siku iliyofuata, na baada ya sisi kutembea majini kwa umbali fulani, hatimaye tulifika mahali pa kusanyiko na kupata ndugu fulani. Walitushangaza sana jinsi walivyostaajabu kwamba tungeweza hata kudokeza kwamba kusanyiko lisingeweza kufanywa. Akina ndugu wangekuja bila shaka!

“Na kweli walikuja, ingawa ilimaanisha kwamba iliwalazimu wengine kutembea katika hali hiyo ya hewa kwa siku mbili au tatu. Hudhurio katika alasiri ya Jumapili hiyo lilifikia 419, na asubuhi hiyo 61 walionyesha wakfu wao kwa ubatizo wa maji.”

Akina ndugu waliitikia vema mashauri, na waliopendezwa walifanya marekebisho makubwa maishani mwao. Kwa mfano, Biblia haikubali kuwa na wake zaidi ya mmoja. Inasema kwamba “kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke . . . mume wake mwenyewe” na kwamba mwangalizi Mkristo apaswa kuwa “mume wa mke mmoja.” (1 Kor. 7:2; 1 Tim. 3:2) Hivyo, chifu aliyekuwa na wake wengi aliwaacha wake wote waende isipokuwa yule mkubwa na baadaye akabatizwa. Baada ya muda akawa mzee wa kutaniko. Mtu mwingine aliyekuwa na wake wawili alimpa ndugu yake mdogo mke wake wa pili na kusema kwamba hangependa kusababisha vifo vya watu watatu nyumbani mwake kwa sababu ya ubinafsi wake. Ndipo yeye pia akastahili kubatizwa.

Mashahidi wengine walionyesha upendo wao usio na ubinafsi kwa kukataa haki zao za kimapokeo za kuomba mahari wanapotoa binti zao katika ndoa. Mahari kama hizo zingeweza kuwa za juu sana kwa vijana Mashahidi, hasa kwa mapainia. Lakini baba wengi walifurahi kuona binti zao wameolewa “katika Bwana tu.” (1 Kor. 7:39) Jambo hilo lilifanya pia mwanzo wa maisha ya kwanza ya ndoa kuwa mzuri kwa hao waliooana kwa sababu mzigo wa mahari ulikuwa umeondolewa. Tendo hilo lilishangaza mwanzoni, lakini kadiri muda ulivyopita na watu kulizoea, watu wengi zaidi na zaidi walithamini na kustahi tendo hilo la upendo wenye kujali.

Makasisi walijaribu kuleta matata katika Tanganyika pia, lakini hawakufaulu. Ndugu Kangale aliposhikwa na polisi mjini Mbeya, aliweza kueleza kwamba alikuwa anatembelea tu ndugu zake za kiroho. Basi polisi wakawa wenye kushirikiana na kumwuliza awaachie orodha ya ziara zake kwa makutaniko ili waarifu vituo vingine vya polisi juu ya kuwasili kwake, na kwa kufanya hivyo hawangehangaika juu yake. Kwa njia hiyo Ndugu Kangale aliweza kusafiri kwa uhuru ndani ya Tanganyika kwa miaka mingi. Mapainia wa pekee na waangalizi wasafirio wengine kutoka Rhodesia Kaskazini na Nyasaland waliungana naye kujenga kondoo. Wao walikuwa ni Frank Kanyanga, James Mwango, Washington Mwenya, Bernard Musinga na William Lamp Chisenga kutaja wachache. Jambo la kupendeza ni kwamba, Ndugu Chisenga alikutana na Norbert Kawala katika jiji la Mbeya mwaka wa 1957. Alikuwa na kiu ya kweli, akawa anajifunza Biblia mara mbili kwa juma, akastahili kubatizwa, na baadaye akatumikia akiwa mtafsiri katika ofisi ya tawi ya Nairobi, Kenya.

Maonyesho ya Sinema na Upanuzi Kuelekea Kaskazini

Wakati uo huo, kuanzia 1956 na kuendelea, sinema ya Sosaiti The New World Society in Action ilianza kuonyeshwa katika Tanganyika, na zaidi ya 5,000 walihudhuria. Kichocheo kingine kilikuja katika 1959 wakati Mashahidi kutoka ng’ambo walipoanza kuwasili kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi wa wahubiri wa Ufalme. Idadi ya wahubiri katika Tanganyika ikaanza kupanda tena, kufikia 507 katika mwaka wa utumishi wa 1960.

Hata hivyo, maendeleo hayakuwa yakija kwa urahisi sikuzote. Miji mingi ilikuwa na wakazi wengi Waislamu, jambo lililotahini ustadi wa kuhubiri wa wahubiri. Ndugu wageni walikuwa na tatizo jingine la hali ya hewa yenye joto na jasho. Lakini walikuwa na roho ya Isaya, wakisema hivi: “Mimi hapa, nitume mimi,” nao walithawabishwa kwa kufanya hivyo.—Isa. 6:8.

Kwenye Miteremko ya Kilimanjaro

Tanganyika ilipata uhuru katika 1961, na kufikia 1964 ilikuwa imeungana na kisiwa Zanzibar ili kufanyiza Muungano wa Jamhuri ya Tanzania. Hata hivyo, huko nyuma katika 1961 eneo jipya katika Tanzania, eneo la miteremko ya mlima mkubwa Kilimanjaro, lilisitawi kwa habari njema. Huo mlima mrefu zaidi katika Afrika ni volkeno zimwe kubwa sana unaofunikwa na theluji nyakati zote. Miteremko hiyo huinuka kwa uanana na hupata mvua nyingi kutoka mashariki au kusini. Udongo wenye rutuba na mvua nyingi hufanya miteremko ya mlima huo ifae kwa ukulima, na hivyo kuifanya iwe na watu wengi sana. Painia wa pekee alianzisha funzo la Biblia na kikundi cha watu watano waliopendezwa hapo.

Wakati wa mwaka uliofuata, katika Agosti 1962, kusanyiko la mzunguko lilifanywa Kibo Hotel karibu na Marangu, kukabili mlima huo mkubwa. Mashahidi kutoka Kenya waliunga mkono tukio hilo na kusafiri katika msafara wa magari umbali wa kilometa 400 kutoka Nairobi. Ubatizo ulifanywa katika kijito baridi cha mlimani, na ilikuwa ndiyo mara ya kwanza katika sehemu hii kwamba Mzungu, Helge Linck, alibatizwa na ndugu Mwafrika.

Helge Linck alijua kweli kutoka utoto wake katika Denmark lakini hakuifuatilia. Alikuja Tanganyika kufanya kazi katika shamba la miwa. Ndugu yake wa kimwili alizuru Afrika Mashariki katika 1959 na kuamsha kupendezwa kwake katika kweli. Painia wa pekee mmoja alipofungwa jela kwa kuhubiri katika 1961, Helge alifanya mpango aachiliwe huru. Baada ya ubatizo wa Helge katika mandhari hiyo yenye kupendeza kwenye kusanyiko la mzunguko la Kibo, alianza utumishi wa painia na baadaye akafukuzwa nchini kwa sababu ya kuhubiri kwake.

Na tuache Tanzania bara kidogo tuelekee kisiwa cha karafuu, Zanzibar (Unguja), ambacho ndicho kisiwa kikubwa zaidi cha matumbawe kilicho umbali kidogo kutoka pwani ya Afrika.

Zanzibar—Kisiwa cha Karafuu

Zanzibar, ikiwa kilometa 40 tu kutoka bara, ilitumika kuwa kituo cha kwanza cha misafara ya kuingia ndani ya bara la Afrika kwa Waarabu na Wazungu vilevile. Karibu wenyeji wote ni Waislamu na wenye uzao wa mchanganyiko wa Waafrika na Waarabu. Kiswahili, lugha ambayo ilipelekwa na biashara ya utumwa hadi mpaka wa Angola katika Afrika Magharibi, husemwa katika kisiwa hiki. Wakati wa karne ya 19, Zanzibar ilikuwa ndiyo soko kuu la biashara ya watumwa.

Mapainia wawili kutoka kusini mwa Afrika walitua kifupi katika kisiwa hiki cha karafuu mwaka wa 1932. Miaka ishirini na tisa baadaye, katika mwaka wa 1961, Roston na Joan MacPhee, wakiwa wahubiri wa habari njema waliobatizwa hivi majuzi, walihamia kisiwa hicho kutoka Kenya. Walianza kazi mara hiyo, wakaangusha fasihi nyingi ya Biblia. Upesi walikuwa wakiongoza mafunzo mawili ya Biblia. Kutaniko katika Dar es Salaam ulio karibu lilipanga kuzuru mara moja kwa mwezi katika mwisho wa juma ili kutiana moyo.

Upesi baada ya akina MacPhee kuhamishwa kurudi Kenya, familia nyingine ya Kikristo, akina Burke, waliwasili Zanzibar kutoka Amerika. Waliwatunza vizuri wale waliokuwa wamependezwa na wakaongezea kwa kuanzisha mafunzo yao wenyewe. Ghafula, katika mwisho wa 1963, mapinduzi makubwa yalienea kisiwani mwote, na ilibidi familia ya Burke ikimbie ikiacha nyuma mali yayo nyingi.

Baada ya akina Burke kuondoka, masilahi ya Ufalme kisiwani humo yakafifia. Kisha, mwanzo mpya ukafanywa wakati watu wanaopendezwa walipohamia Zanzibar katika mwaka wa 1986. Upesi kikundi kidogo cha wahubiri kikakua. Mtu mmoja aliyependezwa mwenye bidii kwelikweli alitumia wakati wake wote wa mapumziko kuongoza mafunzo ya Biblia na watu wapatao 30. Ilikuwa ni kazi ngumu kama nini kwa vile alikuwa na kazi ya kimwili ya kushughulikia vilevile! Watu wapatao 45 walikuwa wakifika mkutanoni. Ilikuwa ni mshangao kama nini kuona watano kati yao wakiwa tayari kwa ubatizo katika mkusanyiko wa wilaya wa Dar es Salaam wa Desemba 1987! Sasa msingi ulikuwa umewekwa kwa ajili ya kutaniko katika kisiwa hiki chenye kufanyiza historia.

Acha tuache kisiwa hiki cha karafuu na kurudi kwenye bara la Afrika.

Shangwe na Matatizo

Wakati wa muda wote wa miaka 30 ya kuhubiri katika Tanganyika, ndugu zetu walikuwa na matatizo machache tu na wenye mamlaka. Katika hali nyingi polisi walikuwa wenye heshima na wenye ushirikiano, wakati mwingine hata wakitoa vikuza-sauti kwa ajili ya makusanyiko yetu. Milton G. Henschel kutoka makao makuu ya Sosaiti katika Brooklyn alipozuru Dar es Salaam katika Mei wa 1963, kusanyiko lilipangwa lifanyiwe katika Jumba la Karimjee, lililokuwa ndilo jumba zuri zaidi nchini. Watu 274 walihudhuria, kutia ndani na meya wa jiji, na 16 wakabatizwa. Ofisi ya tawi ilikuwa imefunguliwa karibuni tu katika nchi jirani ya Kenya ili uangalifu bora zaidi utolewe kwa masilahi ya Ufalme katika Tanganyika, ambayo sasa ni Tanzania.

Mipango ilifanywa ya kuchapa Mnara wa Mlinzi katika Kiswahili. Toleo la kwanza lilitokea Desemba 1, 1963. Mwaka uo huo, mtaala wa Shule ya Huduma ya Ufalme ulitoa uongozi na uelekezi uliohitajiwa kwa waangalizi katika makutaniko 25 ya Tanzania. Mikusanyiko ya wilaya ilifanywa katika Septemba na Oktoba 1964 kukiwa na kilele cha hudhurio cha 1,033.

Lakini kulikuwa na matatizo. Wamishonari wa Mashahidi wa Yehova hawakuwa wamepata kukubaliwa kuingia nchini, na maombi yote ya kupata kutambuliwa kisheria yalikuwa yamekataliwa.

Mambo Yabadilika Kuwa Mabaya Zaidi

Ingawa hali ilibaki ikiwa tulivu kwa sehemu kubwa ya 1963 na 1964, habari ilipokewa kuhusu barua fulani iliyoandikiwa maofisa wote wa polisi ikiwashauri kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wamepigwa marufuku na hivyo walipaswa kushikwa. Pigo jingine likaja Januari 25, 1965. Magazeti yalitangaza kwamba Watch Tower Society haikuwa halali. Lakini bado kulikuwa na shaka kama tangazo hilo lilitolewa na serikali. Chini ya hali hizo, kusanyiko la mzunguko lilipangwa lifanywe Tanga Aprili 2-4, 1965.

Jumba lilikuwa limekodiwa, mipango ya malazi ikafanywa, na idadi kubwa ya Mashahidi ikaja kwa garimoshi kutoka kwenye mashamba ya katani. Njiani walihubiria abiria wenzao, mmoja wao akiwa ni polisi. Walipofika, aliwashika Mashahidi wote na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi, lakini upesi baadaye waliachiliwa huru.

Katika Aprili 3, siku ya pili ya kusanyiko, matangazo ya redio yalisema kwamba serikali imepiga marufuku kazi ya Mashahidi wa Yehova na mashirika yote ya kisheria yanayohusiana nayo. Hata hivyo, kusanyiko lilimalizika bila tukio lolote. Hakuna tangazo lolote la marufuku lililotokea katika gazeti la matangazo rasmi ya serikali. Habari ilitoka katika nchi jirani Malawi (iliyoitwa Nyasaland) na Zambia (Rhodesia Kaskazini zamani) kwamba marufuku ilitangazwa na kuondolewa baadaye. Jambo hilo lilithibitishwa na shirika la habari la Reuters. Lakini jambo ambalo halingeepukika lilitukia hatimaye. Katika Juni 11, 1965, gazeti la matangazo rasmi ya serikali lilitoa taarifa kwamba Watch Tower Society pamoja na mashirika yayo yote ya kisheria haikuwa halali.

Sasa polisi wakawa chonjo zaidi, na majaribio ya kuwa na kusanyiko la mzunguko katika kusini mwa nchi hiyo hayakufaulu. Kushikwa hapa na pale kulifuata. Nyakati nyingine vichapo vilitwaliwa na kurudishwa pindi kwa pindi. Akina ndugu wakaona ni hekima zaidi kukutana katika vikundi vidogo-vidogo. Hali zilikuwa mbaya zaidi katika sehemu ambazo wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo waliwachochea polisi.

Hali Yenye Kuendelea ya Kueleweka Vibaya

Kabla tu ya marufuku kutangazwa, William Nisbet kutoka Kenya alitumia majuma manane magumu akijaribu kukutana na maofisa mjini Dar es Salaam katika jitihada ya kutambua rasmi Mashahidi wa Yehova. Alipewa fursa ya kuzungumza na katibu wa Waziri wa Mambo ya Nchini. Inaonekana kwamba kwa sababu ya kampeni za misheni za Jumuiya ya Wakristo za kupashana habari za uwongo, maofisa wengi wa serikali walihusianisha Mashahidi wa Yehova na dini zenye ushupavu zilizopigwa marufuku katika Zambia na Malawi.

Hofu isiyo na sababu ya Mashahidi wa Yehova ilikaa juu ya maofisa kama mawingu ya dhoruba yasiyo na mvua. Maofisa walifikiri kwamba Mashahidi wa Yehova ndio waliokuwa vile vikundi vya wenyeji vilivyoitwa “Watchtower,” au Kitawala, ambavyo havikuwa na uhusiano wowote na Mashahidi. * Madhehebu hizo zilizoea uzinzi na uchawi na mara nyingi ziliasi serikali zilizosimamishwa. Walitumia vibaya jina la Mungu na baadhi ya vichapo vyetu pia. Hao ndio waliokuwa wa kuogopwa, si Mashahidi wa Yehova wa kweli wanaopenda amani. Ziara ya Ndugu Nisbet na hati iliyotayarishwa na Watch Tower Bible and Tract Society viliondoa kuelewa vibaya kwa maofisa fulani.

Kabla ya Ndugu Nisbet kuondoka Dar es Salaam, alitoa ombi la kuandikishwa kwa International Bible Students Association. Alishangaa jinsi gani alipopata telegramu kutoka kwa ndugu wa Dar es Salaam, miezi sita baada ya marufuku, iliyosema kwamba International Bible Students Association iliandikishwa rasmi Januari 6, 1966, chini ya Sheria ya Makampuni. Na bado Mashahidi wa Yehova pamoja na Watch Tower Society iliendelea kuwa chini ya marufuku. Katika Novemba 24, 1966, taarifa ya serikali ilisema kwamba International Bible Students Association ilikuwa imekomeshwa kuwa kampuni kwa sababu makutaniko yayo hayakujiandikisha chini ya Sheria ya Mashirika.

Iliwabidi ndugu Wazambia au Wamalawi waliokuwa wamekuja kusaidia katika Tanzania waondoke nchini. Kuondoka kwao kulihisiwa kwelikweli, lakini ibada ya kweli haikuwa imekufa kwa vyovyote nchini Tanzania. Idadi ya waliohudhuria Ukumbusho wa Kifo cha Kristo ilikuwa ni 1,720, na 836 walikuwa watendaji katika kuhubiri juu ya Ufalme mwaka wa 1966.

Ushelisheli—“Visiwa vya Paradiso”

Shime inayotangaza Ushelisheli husema kwamba hivyo “havina kifani kwa maili elfu moja.” Ushelisheli iko maili elfu hivi kutoka pwani ya Afrika Mashariki na ndiyo makao ya kobe wakubwa, wakubwa mno hivi kwamba mtu angeweza kuwapanda. Ushelisheli hufanyizwa na karibu visiwa 100 ambavyo huenea kufika karibu na Madagaska. Baadhi ya visiwa hivyo, kama kile kisiwa kikuu cha Mahé vimefanyizwa kwa mawe magumu sana, na visiwa vinginevyo vimefanyizwa kwa matumbawe. Visiwa hivyo vina kila kitu kinachofanya visiwa vya kitropiki vipendeze—milima, miamba inayopendeza, fuo za bahari za mchanga mweupe, bahari yenye rangi ya buluu na kijani, miamba ya matumbawe ya ajabu, mimea yenye kusitawi, ndege wa ajabu wakiruka katika hewa iliyojaa manukato ya viungo vyenye kunukia vizuri vya msituni na kutokuwako kwa maradhi ya kitropiki.

Idadi ya watu—ambao asilimia 90 yao huishi Mahé—husema Kifaransa cha patois kinachoitwa Kreole. Hao walitokana sanasana na Waafrika, wakoloni Waingereza na Wafaransa, Wahindi, na Wachina.

Mtu mmoja aliyependezwa na mafundisho ya Biblia kama yalivyoelezwa na Mashahidi wa Yehova aliwasili kutoka Afrika Mashariki katika 1961. Katika mwaka uliofuata, Mashahidi, kutia ndani familia ya McLuckie yenye washiriki wanne kutoka Rhodesia Kusini waliwasili na kuanza mahubiri ya vivi-hivi. Hata hivyo, hotuba za peupe za Biblia zilikuwa zimekatazwa kwa sababu ya kuwepo kwa Roma Katoliki yenye nguvu sana. Na bado, katika Aprili 1962, kwenye mkutano wa kwanza uliopangwa kitengenezo, watu 12 walihudhuria, na kufikia wakati huo 8 ndio waliokuwa wakishiriki huduma ya shambani.

Upinzani Waleta Mazuri

Lakini upesi, hali ya kawaida ya mnyanyaso wa makanisa ya Jumuiya ya Wakristo ikatokea. Idara ya Uhamiaji iliomba familia ya McLuckie iondoke nchini kufikia Julai 25, 1962. Polisi walimwambia ndugu mwingine mgeni asihubiri na kwamba hati yake ya kukaa huko haingefanywa upya. Makasisi Wakatoliki walitoa hotuba na kuandika makala ndefu katika magazeti ya huko wakionya wakazi juu ya Mashahidi.

Jambo hilo likaleta tokeo tofauti. Watu wengi hawakuwa wamejua Mashahidi wa Yehova. Lakini sasa walianza kuuliza-uliza kwa sababu udadisi wao uliamshwa. Mwendo wa kweli ya Biblia haungeweza kusimamishwa katika Ushelisheli! Katika siku ya Julai 15, 1962, juma moja kabla ya ile familia kuondoka, mume na mke ambao ni wenyeji Washelisheli, Norman na Lise Gardner, walibatizwa. Familia hiyo iliyokuwa ikihama waliona jambo hilo kuwa thawabu bora kwa fedha na jitihada walizotumia kuanzisha kazi katika visiwa hivyo vya mbali.

Miezi mitano baadaye, wastaafu wawili waliokuwa Mashahidi kutoka Afrika Kusini walikuja kuishi Mahé na kusaidia kazi ya kuhubiri. Baada ya muda mfupi, waliweka tangazo fupi magazetini lililoalika watu waliopendezwa kujifunza Biblia wawasiliane nao. Siku iliyofuata tu walipata barua iliyofuta viza zao. Lakini wakati wa miezi minne yao huko Ushelisheli, walikuwa wameangusha vichapo vingi vya Biblia na kutoa ushahidi mzuri. Lakini sasa hakukuwa na Mashahidi katika visiwa hivyo kwa vile hata akina Gardner walikuwa wameondoka pia.

Baada ya miezi michache tu, kazi iliendelea tena wakati akina Gardner waliporudi kutoka Khartoum, Sudan walikopelekwa kwa muda mfupi kwa sababu ya kikazi. Muda huo ambao hawakuwepo, walikuwa na ushirika mzuri na ndugu waaminifu katika Sudan, na vilevile Kenya na Rhodesia Kusini. Walienda kuishi katika kisiwa Cerf, kilicho umbali wa muda wa nusu saa kwa mashua ndogo kutoka Mahé. Kwa vile kulikuwa na familia kumi na mbili hivi katika kisiwa hicho, hakikufaa kwa utendaji wao wa kutoa ushahidi. Na bado, wakiwa wahubiri pekee katika Ushelisheli, walitia bidii na kudumisha wastani wa saa 30 kila mwezi katika huduma ya shambani.

Ziara za kwanza za mwangalizi wa mzunguko zilipangwa katika 1965. Mambo mazuri mengine yalitukia katika mwaka huo. Sinema ya Biblia ilionyeshwa kwa watu waliohudhuria 75. Watu watatu wenye kupendezwa walijiunga na akina Gardner katika utendaji wa kuhubiri na wakabatizwa mwaka uo huo. Mipango ifaayo ilifanywa kwa ajili ya mikutano ya ukawaida.

Ijapokuwa ule upendo akina Gardner walikuwa nao kwa ajili ya Kisiwa Cerf, upendo wao kwa jirani ulikuwa na nguvu zaidi hivi kwamba katika 1966, walihamia kisiwa kikuu cha Mahé ili kuanzisha kitovu cha kuendeleza ibada ya kweli. Jumba la Ufalme lilijengwa likipakana na nyumba yao, jambo ambalo lilifungua njia ya ukuzi zaidi.

Wamishonari Waingereza waliotumikia Uganda, Stephen Hardy na mke wake Barbara, walifanya ziara kadhaa za mzunguko katika Ushelisheli. Wakati wa ziara yake moja katika Desemba 6, 1968, kulikuwa na wahubiri watendaji 6, na 23 walikuwapo kwa ajili ya programu ya kuwekwa wakfu kwa Jumba la Ufalme jipya.

Katika 1969 maombi yalifanywa ya kuandikisha rasmi kazi yetu na wamishonari kukubaliwa kuingia nchini. Maombi hayo mawili yalikataliwa mbali. Na hakuna sababu zilizotolewa.

Ukuzi ulikuwa wa polepole, kwa vile vijana wengine walihama kutafuta kazi, na wengine hawakufanya maendeleo kwa sababu ya kuhofu mwanadamu, jambo ambalo ni kawaida miongoni mwa idadi ndogo ya watu. Kutojua kusoma na kuandika, hali ya kawaida ya kutokujali, na ukosefu mkubwa wa adili pia vilizuia watu wengi. Lakini wengine—kama vile mfanyakazi wa serikali mwenye familia kubwa na ambaye alijifunza Biblia kila siku wakati wa mapumziko ya alasiri—walifanya maendeleo haraka. Hivyo, kufikia 1971, watu 40 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo, na 11 walikuwa watendaji katika huduma ya shambani. Ujumbe wa Dunia-paradiso inayokuja uliendelea kujulishwa katika visiwa vizuri vya Ushelisheli.

Burundi—Miaka ya Mapema

Kabla ya kutumikia Uganda na kuzuru Ushelisheli, akina Hardy walikuwa wamepewa mgawo katika nchi nzuri ya Burundi, nchi ndogo inayovutia yenye maelfu ya vilima, iliyoko kati ya Tanzania na Zaire. Ina watu wengi sana walio wakulima wenye bidii, mara nyingi wakikuza ndizi kwenye vilima vilivyolimwa na kusawazishwa.

Wakati wa utawala wa kikoloni wa Ubelgiji, Watch Tower Society ilipeleka ombi la kutuma wamishonari Usumbura, ambalo sasa ni Bujumbura, jiji kuu la Burundi, lakini ombi hilo lilikataliwa. Hata hivyo, uhuru uliopatikana katika 1962 ulileta hali tofauti ya kisiasa, na katika Oktoba 1963, mapainia wawili kutoka Rhodesia Kaskazini walifaulu kupata viza za kukaa miezi mitatu, ambazo zilifanywa upya bila matatizo. Miezi mitatu tu baadaye, katika Januari 1964, wahitimu wanne wa Gileadi walifika wakiwa na viza za kukaa muda usio dhahiri.

Mkazo wa Kidini

Watu waliitikia habari njema za Ufalme kwa hamu tangu mwanzoni. Wamishonari walipofika Burundi, mapainia wa pekee tayari walikuwa wanaongoza mafunzo mengi ya Biblia, na wahubiri tisa walikuwa wanahubiri habari njema. Lakini katika mwezi uliofuata, wamishonari waliambiwa kwamba ingekuwa lazima kuandikisha rasmi shirika lao ili wapewe vitambulisho vya kazi.

Akina ndugu walikuwa na uhakika kwamba wangeweza kuandikishwa rasmi. Lakini, katika majuma yaliyofuata, mkuu wa idara ya uhamiaji pamoja na maofisa wengine walionyesha mwelekeo usiofaa. Maofisa hao walikuwa wamewekewa mkazo wa kidini kwa siri. Hivyo mwanzoni mwa Mei, wamishonari walipewa siku kumi za kuondoka nchini. Ebu wazia jinsi walivyovunjika moyo kuwaacha watu 70 waliokuwa wakijifunza Biblia nao!

Kufikia mwisho wa Mei, mapainia wa pekee walilazimishwa kuondoka pia. Jambo hilo lilimwacha ndugu mmoja Mtanzania na kazi ngumu sana ya kutunza watu karibu 30 waliokuwa wakijifunza Biblia. Ingawa mapainia na wamishonari walikuwa wameondoka, wahubiri wenyeji waliendelea kuhubiri. Kilele cha wahubiri 17 kiliripotiwa katika 1967, na watu 32 walihudhuria Ukumbusho. Kwa kusikitisha, magumu yalitokea mwaka uliofuata wakati baadhi ya akina ndugu hawakukubali waangalizi waliowekwa. Jambo hilo likatokeza upungufu wa idadi ya wahubiri kuwa nane katika mwaka wa utumishi. Dawa ilikuwa ni shauri la kiroho nalo lilitolewa. Hatimaye akina ndugu walisuluhisha matatizo yao. Kwa hiyo 25 wakawa watendaji katika huduma ya shambani katika 1969 na 58 wakahudhuria Ukumbusho.

Wapya Wastahimili Mateso

Bidii ya Mashahidi hao iliamsha hasira ya makasisi ambao waliweka mkazo kwa serikali. Katika Agosti 1969, Mashahidi saba walishikwa na kuteswa kwa kulazimishwa kusimama kwa siku mbili katika maji yanayofikia kiunoni. Lakini kama ilivyokuwa kwa mitume wa mapema, wao hawakutishika. Wengine wapya tisa walibatizwa miezi miwili baadaye. Mara mbili baadaye, maofisa waliomba akina ndugu waandikishe dini yao, na mara mbili maombi ya akina ndugu yalikataliwa. Kila mmoja wa miaka iliyofuata ulikuwa na vilele vipya vya wahubiri 46, 56, 69, 70, na 98, pamoja na kuundwa kwa kutaniko katika Bujumbura mwaka wa 1969.

Vita kali ya kikabila ilifyatuka kati ya Watusi na Wahutu katika 1972. Iliripotiwa kwamba zaidi ya Wahutu 100,000 kutia na angalau Mashahidi wanne waliuawa katika vita hiyo. Mashahidi wengine walifungwa gerezani, wengine wao kwa miezi minane. Kujapokuwa ghasia, akina ndugu walikuwa wenye bidii katika utumishi wa shambani na kufikia wastani wa zaidi ya saa 17 kwa kila mhubiri kila mwezi.

Bado kulikuwa na tatizo la kudumu la kutoa uangalizi ufaao wa kitheokrasi baada ya miaka kumi ya usitawi. Ingawa idadi kubwa ya akina ndugu walikuwa imara, walionyesha kuwa wachanga kiroho katika njia nyinginezo, wakikosa uelewevu wa ndani na utambuzi. Katika sehemu fulani, wengine waliathiriwa na mkondo wa ushawishi wa Kitawala, ile “harakati ya Watchtower” ya bandia. Matatizo hayo hayakuwa ya kushangaza kwa sababu akina ndugu hawakuwa wamepata ziara ya mwangalizi wa eneo la dunia, hawakuwa wameona sinema za Sosaiti, waangalizi wa makutaniko hawakuwa wamepata mtaala wa pekee wa mafunzo, hawakupata kwenda kusanyiko, wala kuwa na kichapo chochote katika lugha yao. Kwa hiyo, uangalizi wa nchi hiyo uliwekwa chini ya tawi la Zaire katika 1976. Kwa njia hiyo, akina ndugu wenye kusema Kifaransa na Kiswahili wangeweza kutoa msaada uliohitajiwa kwa Mashahidi katika Burundi.

Jambo la kupendeza lilikuwa ni kwamba, wakati wa kuuana kwa kikabila, kiongozi wa Burundi aliyepinduliwa alitolewa ushahidi kikamili kabla ya kifo chake akiwa uhamishoni. Mishonari mmoja aliyekuwa akizuru alikutana naye Mogadishu, Somalia. Mazungumzo marefu yakafuata, huku kukiwa na maswali mengi, jambo lililovutia sana kiongozi huyo aliyepinduliwa. Mishonari huyo aligundua baadaye tu ni nani hasa aliyekuwa ametolea ushahidi.

Miaka Mizuri Ajabu kwa Wamishonari Katika Uganda

Kufukuzwa kwa wamishonari kutoka Burundi kulinufaisha sana Uganda, ambayo kufikia 1964, ilikuwa na kikundi thabiti cha wahubiri waliokuwa wakitenda. Hatimaye baada ya miaka zaidi ya 30 ya jitihada pamoja na kuwasili kwa wenzi wa ndoa wa kwanza wamishonari, ndugu na dada wakomavu walikuja kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi. Wamishonari wengine wangekuja baadaye.

Baada ya makao ya mishonari ya kwanza kufunguliwa Kampala, makao ya pili yalifunguliwa katika mji wenye viwanda wa Jinja, ambapo Mto Naili hutiririka kutoka Ziwa Viktoria kuelekea kaskazini. Kulikuwa na maendeleo ya haraka; upesi kutaniko likaundwa.

Wakati uo huo, ujumbe wa Ufalme ulikuwa umefika katika miji midogo ya wilaya kotekote Uganda, na kufikia 1967, kulikuwa na idadi ya wahubiri 53. Mwaka uliofuata, makao mengine ya wamishonari yalifunguliwa Mbale, mji unaositawi katika upande wa magharibi wa Mlima Elgon, karibu na mpaka wa Kenya. Kulikuwa na wahubiri 75 kufikia 1969 na idadi hiyo ikafikia 97 katika mwaka uliofuata, na 128 mwaka wa 1971.

Kazi ilikuwa imetambuliwa kisheria tangu Agosti 12, 1965. Na mambo yalionekana kuwa maangavu katika mwaka wa 1972. Kilele kipya cha wahubiri 162 kilikuwa kimefikiwa, na wamishonari wapya watano walikuwa wamekubaliwa hivi karibuni kuingia nchini. Mipango ya kufanya mkusanyiko mkubwa zaidi wa Mashahidi wa Yehova katika Uganda katika Uwanja wa Michezo wa Lugogo Kampala, ilikuwa inafanywa. Mashahidi walitoka nchi jirani ya Kenya na Tanzania na hata mbali sana kama vile Ethiopia. Ndugu 65 Waethiopia walisafiri kwa mabasi yaliyokodiwa, wengine wao wakisafiri karibu kilometa 3,200 kwa majuma mawili.

Mchafuko Katika Uganda

Wageni waliokuwa wakiingia Uganda walishangaa kuona misafara ya walimu wa shule wageni na familia za Wahindi wakitoroka mbio kutoka nchini. Hali ya kisiasa ilikuwa imebadilika baada ya mapinduzi, na watu walihofia wakati wao ujao. Ilionekana kana kwamba kila mtu alitaka kutoroka isipokuwa Mashahidi. Hali ilikuwa ya wasiwasi sana. Na bado, katikati ya mchafuko huo wote, matangazo yenye urefu wa meta 18 yaliwekwa toka upande mmoja wa barabara kuu ya Kampala hadi ule mwingine yakitangaza kwa ushujaa hotuba ya watu wote ya mkusanyiko. Akina ndugu walishukuru kwamba “Utawala wa Kimungu” Kusanyiko la Wilaya lilifanywa kwa mafanikio, kilele cha watu 937 wakihudhuria hotuba ya watu wote. Wale wa zamani kotekote katika Afrika Mashariki bado wanakumbuka kwa furaha kusanyiko hilo la Kampala.

Ingawa kulikuwa na kupendezwa kwingi katika kweli ya Biblia na vichapo vingi sana vilikuwa vikiangushwa, kulikuwa na ishara ya hali mbaya iliyokuwa ikisitawi. Vitambulisho vya kazi vya wamishonari wawili na wake zao havikufanywa upya ikimaanisha kwamba iliwabidi waondoke nchini kabla ya miezi mitatu kwisha. Kisha, katika Juni 8, 1973, bila onyo serikali ikapiga marufuku vikundi vya kidini 12 kutia na Mashahidi wa Yehova. Iliwabidi wamishonari 12 waliobaki waondoke nchini kufikia Julai 17, 1973. Hilo lilikuwa tukio la kuhuzunisha kwa wasaidiaji hao wote wageni, na lilitukia wakati ambapo kulikuwa na matatizo ya uhuru wa ibada hata katika Kenya.

Ilibidi wamishonari wengi warudi katika nchi za kwao, lakini wenzi wa ndoa wengine waliokuwa wametumikia penye uhitaji mkubwa zaidi katika Uganda waliweza kuishi Kenya na kusaidia huko pia. Miongoni mwao walikuwa ni Larry na Doris Patterson, na vilevile Brian na Marion Wallace. Akina Hardy walienda kutumikia katika Ivory Coast na baadaye kwenye Betheli ya London katika 1983. *

Sasa sheria na utengamano vilikuwa na maana tofauti katika Uganda. Kwa mfano, ndugu mmoja painia alishikwa na kupelekwa katika kituo cha kijeshi ili ahojiwe. Alifanya kosa gani? Kwamba alipokea fedha kutoka kwa “majasusi” Wazungu. Yeye alikuwa ametoka kuzuru makao ya wamishonari. Ijapokuwa alieleza wazi namna ya kazi yake ya kuwa mhubiri wa kujitolea, alipigwa na kisha akapewa kolego ajichimbie kaburi lake. Baada ya kumaliza kujichimbia kaburi, aliambiwa achimbe mengine mawili ya “wajasusi” Wazungu, yaani wamishonari! Alipomaliza, wanajeshi watatu wenye bunduki wakamwangusha na kumfyatulia risasi. Wote wakakosa shabaha. Risasi moja iligonga juu ya kiatu cha mwanajeshi mmoja, ikisababisha ubishi miongoni mwa wanajeshi na hivyo kuondoa fikira zao kwake. Ndugu huyo alilala hapo kwa muda fulani na akaachiliwa siku iliyofuata.

Ilibidi sasa makutaniko yakutane kwa siri na kujipatanisha na hali mpya zilizokuwako. Uhai kwa ujumla ulionwa kuwa kitu chenye thamani ndogo sana na kufanya kazi kwa ajili ya dini iliyopigwa marufuku kulihatarisha uhai hata zaidi.

Sehemu ya Kusini mwa Sudan Yafunguka

Wakati wa miaka ya mwisho ya 1960, Sudan ilikuwa na wasiwasi wayo pia, hasa kati ya watu wa kaskazini na wa kusini. Kutaniko la Khartoum liliendelea kwa bidii likiwa mbali na ofisi ya tawi katika Nairobi na likiwa mbali na akina ndugu kwingineko. Kilele cha wahubiri 54 kilifikiwa katika Agosti 1970 muda mfupi kabla ya mzee wa kutaniko mwenye ujuzi zaidi, George Orphanides kuondoka nchini.

Wakati uo huo Mashahidi kadhaa walishtakiwa kuwa Wasayuni na kuhojiwa na maofisa kwa siku mbili kamili. Pia dada mapainia wawili walishtukiwa na kasisi wa Koptiki walipokuwa wakihubiria mwanamke mmoja aliyekuwa amependezwa. Kasisi huyo aliita polisi na kuripoti akina dada kuwa majasusi wa Israeli. Dada hao walitoa ushahidi mzuri katika makao makuu ya polisi na kuachiliwa. Ingawa maono kama hayo yalifanya Mashahidi wengine waogope, kwa wengine yalithibitika kuwa yenye kutia imani nguvu.

Kufikia hapa, historia yetu yote ya Sudan imekuwa ikihusu tu Khartoum. Lakini kulikuwa na shamba kubwa ambalo halikuwa limeguswa: kule kusini, kulikojaa watu waliodai kuwa wa malezi ya Kikristo. Kweli ingepenyaje eneo hili kubwa ajabu? Fursa ilitokea wakati kijana mmoja kutoka kusini aliyekuwa mhariri wa gazeti la Katoliki alipokutana na Mashahidi mwaka wa 1970. Alifanya maendeleo ya haraka katika funzo lake la Biblia na upesi akaanzisha mafunzo na marafiki na watu wa ukoo. Mmoja wa rafiki zake alihubiri ujumbe wa Ufalme kwa ujasiri shuleni hata ingawa vikaratasi vya kupinga vilikuwa vimechapishwa.

Kulikuwa na vikundi vidogo vya watu wanaopendezwa kusini mwa nchi kufikia 1973, na wanafunzi wa Biblia 16 kutoka eneo hilo walibatizwa. Zaidi ya ile kweli iliyo wazi ya Biblia, watu hao wa kusini walivutiwa pia na dini iliyokuwa na upendo usio na unafiki, dini ambayo udugu wa kweli unashinda migawanyiko ya kikabila na rangi.

Kusini mwa Sudan kulikuwa na upendezi wa pekee katika miaka ya mapema ya 1970, labda kwa sababu ya kujitenga kwayo. Safari ya kutoka Khartoum hadi Juba kwa gari la moshi na mashua ilichukua zaidi ya juma moja. Watu kwa ujumla hawakuhangaikia matukio ya ulimwengu. Watu walikuwa wafadhili na wakarimu sana. Hoteli nyingine hata hazikuwa na funguo au makufuli kwa vyumba vya kulala vya wageni. Watu wangeongoza, wangelisha, au kukaribisha wasafiri wanaopita bila kutarajia malipo yoyote. Kwa kweli, hata malipo yalikataliwa katakata mara nyingi. Watu wengi zaidi na zaidi miongoni mwa watu hao wenye moyo wa fadhili walisikia na kukubali kweli juu ya kusudi la Yehova.

Sehemu ya kusini ikiwa imefunguliwa na vichapo vya Biblia vikiwa vinapokewa kwa urahisi zaidi, ukuzi wenye kuendelea ulifuata, na kufikia 1974 kilele cha wahubiri 100 kilifikiwa katika Sudan.

Eritrea Yawaka Moto kwa Mnyanyaso!

Eritrea iko ng’ambo tu ya mpaka wa mashariki wa Sudan. Katika miaka ya mapema ya 1960—baada ya kufukuzwa kwa wamishonari—matangazo ya redio, magazeti, na vyombo vingine vya habari vilitumiwa sana katika kampeni ya kushutumu Mashahidi wa Yehova. Mashahidi walionyeshwa kuwa wachukia maliki na kanisa na pia kuwa wakana Utatu na Bikira Mariamu chini ya vichwa kama “Manabii Wawongo” na “Ujihadhari na Ubandia wa Dini Unaoongoza Katika Kukana Imani ya Kweli.” Walisemwa kuwa wawakilishi wa maadui wa nchi za kigeni, kuwa watu waliokosa adili ambao hawapiganii nchi yao. Mateto ya kutaka hatua kali ichukuliwe ya kuondoa watu wa Yehova nchini yalisikika.

Makasisi wa Kanisa Orthodoksi la Ethiopia ndio waliokuwa wachochezi wakuu wa chuki hiyo. Katika sherehe moja ya ubatizo iliyohudhuriwa na watu zaidi ya 20,000, kasisi mkuu alitangaza azimio la kutenga na ushirika Mashahidi wa Yehova, akiamuru watu wasiwasalimu wala wasiwaajiri kazi wala wasiwasaidie kuzika wafu wao.

Wengi walikuwa na maoni ya kwamba huo ulikuwa ni “wakati wa kuwinda peupe” Mashahidi wa Yehova—sasa wangeweza kuuawa na yeyote bila hatua yoyote ya kisheria kuchukuliwa! Wenye nyumba walitakiwa wawafukuze Mashahidi wa Yehova wote waliokodisha nyumba zao. Wazazi waliambiwa kwamba ikiwa mmoja wa watoto wao alikuwa Shahidi, basi afukuzwe nyumbani, alaaniwe, na aondolewe katika urithi. Katika familia moja kubwa, vijana 18 walifukuzwa kwa kujifunza na Mashahidi wa Yehova.

Katika mji mmoja, umati wenye ghasia ulianza kumtafuta ndugu mmoja aliyejulikana sana lakini hawakumpata. Polisi walianza kushika akina ndugu, wakijaribu kuwalazimisha kutia sahihi zao kwenye taarifa kwamba wanakana imani zao na kukiri kwamba walikuwa wanafanya kazi dhidi ya usalama wa serikali. Kwa sababu ya kutokuelewa, akina ndugu wachache walitia sahihi lakini walipong’amua makosa yao, mara hiyo walikana sahihi zao kwa maandishi, bila kujali matokeo.

Wengine walikabili mtego wa ubembelezi: “Unaweza kuwa na imani yako moyoni mwako, lakini utuambie tu kwamba wewe si mmoja wa Mashahidi hawa,” maofisa wakabembeleza. Au kwa vijana Mashahidi wafungwa, maofisa wangetumia njia ya kiibilisi ya ushawishi wa werevu. Katika siku fulani, wangemtwaa kijana Shahidi mfungwa akutane na watu wa ukoo wazee-wazee. Walipofika, watu hao wa ukoo wangemtazama kwa ukimya kwanza, kisha wangeanza kulia machozi, kupiga magoti na kumsihi akane imani yake kwa Yehova. Ndugu waliokabili mikazo hiyo wakumbuka hilo kuwa jaribu ngumu zaidi walilowahi kupata. Mnyanyaso mkali na mikazo kama hiyo iliendelea kwa miaka mingi.

Pumziko na Kuimarisha Kazi Katika Ethiopia

Wakati wa miaka iyo hiyo, Mashahidi katika Addis Ababa na Ethiopia kusini walikuwa wananyanyaswa pia ingawa si kwa kadiri ileile kama katika Eritrea. Ethiopia na Eritrea ziliungana kuwa nchi moja katika 1962, jambo lililotokeza matatizo ya kisiasa yaliyofikia miaka ya 1990.

Lilithibitika kuwa jambo lenye kufaa kuhamishia uangalizi wa makutaniko yote ya Ethiopia kwenye ofisi mpya ya tawi ya Kenya katika 1964. Wawakilishi wa ofisi ya tawi kutoka Nairobi waliweza kufanya ziara za mzunguko katika Ethiopia na hata walipozuru makutaniko, walisaidia kupunguza kutokuelewana kubaya miongoni mwa wazee wa kutaniko waliowekwa. Funzo la Mnara wa Mlinzi liliongozwa kwa njia ya mabishano katika makutaniko kadhaa. Mwangalizi mmoja wa mzunguko mwenyeji alikuwa akiendeleza mawazo yake mwenyewe bali si ya Biblia, hivyo ikibidi aondolewe. Matatizo kama hayo yalirudisha nyuma maendeleo kati ya miaka ya 1964 na 1966, ambapo idadi ya wahubiri ilibaki ikiwa karibu 200.

Kweli ilienea bado. Shahidi mmoja aliyechukua likizo kwenda bandarini yenye joto ya Massawa katika Bahari Nyekundu alipata mtu mwenye kupendezwa katika posta na akaanza kujifunza Biblia pamoja naye. Waethiopia wengine waliopendezwa wakajiunga naye, na upesi kutaniko lilianzishwa. Karibu na wakati uo huo, kutaniko jingine likatokea sehemu za kusini katika Aseb, bandari nyingine ya Ethiopia.

Ingawa vichapo vilikuwa vimepigwa marufuku tangu 1957, Mashahidi walipata njia za kutoa chakula cha kiroho katika lugha za kwao. Katika 1966, mtaala wa Shule ya Huduma ya Ufalme uliongozwa kwa majuma mawili katika jiji kuu, ukifundisha waangalizi waliowekwa kuhusu tengenezo la kitheokrasi na mambo ya Biblia. Huo ulifanya ndugu wawe na mtazamo wa kitheokrasi na wa kutazama mbele, na mwaka wa utumishi wa 1967 ulionyesha ongezeko la asilimia 21, kukiwa na jumla ya wahubiri 253.

Kujapokuwa kupoa kwa mkazo wa kidini, Mashahidi bado waliendelea kukusanyika katika vikundi vidogo kwa sababu ya hali ya wasiwasi ya kisiasa nchini. Ingawa gazeti rasmi la serikali lilihakikisha uhuru wa ibada kwa wote na likaorodhesha Mashahidi wa Yehova pamoja na dini nyinginezo zilizokubaliwa, maombi yote ya kuandikishwa rasmi yalikataliwa.

Makasisi Wajifunza Juu ya Yehova

Idadi fulani ya makasisi wenye mioyo myeupe walisikiliza kweli za Biblia kama vile ilivyotukia katika karne ya kwanza katika Yerusalemu. (Mdo. 6:7) Kasisi mmoja mwenye haki alikiri kwa Shahidi mmoja hivi: “Kwa hakika unafanya kazi nipaswayo kufanya. Ziara yako leo ni pigo kwelikweli kwa wadhifa wangu wa kuwa kasisi.”

Kasisi mwingine alianza kuuliza juu ya mafundisho ya Mashahidi wa Yehova na akapata majibu yanayoridhisha kwa maswali yake ya Biblia—katika mazungumzo yaliyokuwa yakichukua muda wa saa 12 nyakati nyingine! Matokeo yakawa nini? Alihalalisha ndoa yake, akawa mwenye bidii kwa ajili ya kweli, na kutolea mtawa wa kike ushahidi. Mtawa huyo alifanya mpango wa mjadala kati ya mwanae (aliyekuwa mzee wa kanisa) na Shahidi mmoja, akiahidi kwamba ikiwa Shahidi huyo “angeshinda,” basi angeanza kujifunza Biblia.

Naam, mwanae “alishindwa.” Baadaye mtu huyo alimpata mwangalizi wa mzunguko aliyekuwa akizuru na kumsonga kwa maswali mengi yaliyoisha baada ya saa 20, kukiwa tu na pumziko la saa 4 za usingizi! Matokeo yalikuwa nini? Familia nzima ilijifunza, na 15 wakaendelea vizuri katika kweli; hata yule mtawa wa kike alibatizwa, na mwanae akawa mhudumu painia wa pekee.

Nyakati Bora Zaidi kwa Muda Mfupi

Ndugu katika Ethiopia walikuwa na sababu nyingi za kushangilia kufikia mapema mwa 1971. Ndugu Henschel wa Baraza Linaloongoza alizuru Addis Ababa na Asmara na kusema na wahudhuriaji wapatao 912. Idadi ya wahubiri nchini ilikuwa imefika wahubiri wapatao 500. Na shehena kubwa ya fasihi ilikuwa imeingia nchini.

Lakini matatizo yalikuwa mbele. Mwaka ulipoendelea, matangazo ya redio yaliendelea kushutumu Mashahidi wa Yehova. Waasi-imani zaidi ya 20 walishirikiana na makasisi, wakiwasaidia kuandika makala za uchongezi.

Katika eneo moja, polisi waliingia katika jumba la kukutania, wakanyakua Biblia 70, na kuwazuilia Mashahidi wengine kwa muda mfupi. Baada ya tukio hilo, Jumba la Ufalme katika Asmara lilifungwa, ikibidi kutaniko hilo likutane katika vikundi vidogo tena. Na bado kazi haikurudi nyuma. Katika 1971, wapya waliobatizwa walijumlika kuwa 142, na watu 2,302 wakahudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo.

Vikundi vipya vilikuwa vikifanyizwa katika maeneo yaliyo peke yayo, na waangalizi wa mzunguko wawili walizungukia makutaniko na vikundi 25 pamoja na watu waliopendezwa katika maeneo yaliyo peke yayo. Upesi wahubiri walipita idadi ya 1,000, kukiwa na kilele cha wahubiri 1,844 katika 1974.

Walinyanyaswa Lakini Hawakuachwa Kabisa

Upinzani haukukoma. Katika 1972, polisi waliita ndugu kadhaa ili wahojiwe na kuonya kwamba hatua itachukuliwa ikiwa utendaji wao hautakoma. Kisha, siku ya Agosti 27, 1972, malori makubwa yalifika penye mikutano ya kawaida ya Jumapili; polisi wakashika Mashahidi na watu wanaopendezwa 208. Katika kutaniko moja, msemaji alikuwa akizungumzia unabii wa Ezekieli wa shambulio la Gogu (Shetani) na kuuliza hivi: “Mngesemaje ikiwa polisi wangekuja hapa kutushika?” Na kwa kushangaza, jambo ilo hilo likatukia dakika chache baadaye!

Polisi waliwasongomeza ndugu 59 katika chumba kidogo cha meta 3 za mraba kilichojaa kunguni. Waliwashindilia dada 46 katika chumba kingine cha ukubwa uo huo. Wakalazimisha wengine walale katika baridi nje. Dhamana ilikataliwa. Wakazuiwa pia kuwa na wakili wa kuwatetea. Ingawa ndugu walitoa ushahidi mzuri kwa maofisa wa gereza, ndugu 96 walifungwa jela miezi sita. Siku chache baadaye waliachiliwa kwa dhamana baada ya kunyolewa nywele.

Wale waliobaki 112 walishtakiwa kuanzisha shirika la kidini lisilo halali na kufungwa jela miezi sita. Ndugu hao waliachiliwa kwa dhamana baada ya mwezi mmoja. Baadaye waliitwa tena mahakamani, wakafungwa tena na kuachiliwa kwa dhamana baada ya siku 12. Mahakama Kuu ilisikiliza rufani karibu mwaka mmoja baada ya kule kufungwa jela mara ya kwanza na ikashikilia uamuzi wa mahakama ya kwanza lakini ikawaachilia Mashahidi baada ya kuwaonya vikali. Mashahidi hao walikuwa wamenyanyaswa lakini hawakuachwa kabisa. (2 Kor. 4:9) Wakati ndugu hao walipokuwa gerezani, walihubiri kwa ushujaa na kuwasaidia wafungwa wawili waliofungwa maisha, wajiweke wakfu.

Ziara Iliyofaa na Chakula Kingi Zaidi cha Kiroho

William Nisbet kutoka ofisi ya tawi ya Nairobi alizuru Addis Ababa na kupata tatizo zaidi. Kikundi kilichokuwa kikizidi kukua cha ndugu vijana wenye hisia-hisia kilikuwa kinadai kuwa kimepakwa roho, kikiwa na tumaini la kimbingu. Walishiriki huduma ya shambani wao peke yao na kudharau shauri lililotolewa na yeyote ambaye hakukiri kuwa mpakwa-roho. Mikutano yao ilikuwa na kelele nyingi za dhihirisho la “roho takatifu.” Kwa mfano, katika sherehe ya Ukumbusho wa kifo cha Kristo, wengine wangepiga kelele, wakiwanyang’anya watumishi mifano, na kusimama ili kuitwaa, hivyo wakivuta fikira kwao wenyewe. Kushughulikia matatizo hayo kulichukua muda mrefu sana. Na katika miaka iliyofuata, idadi fulani ya wale wenye kelele zaidi na walioshikilia sana kula mifano hawakubaki kuwa Mashahidi waaminifu.

Vichapo vilivyohitajika sana vilipatikana katika 1973, vikitia ndani vitabu kama vile Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele na Amani ya Kweli na Usalama wa Kweli—Kutoka Chanzo Gani? vyote vikipatikana katika Kiamhara, na kitabu Tengenezo kwa Kuhubiri Ufalme na Kufanya Wanafunzi katika lugha ya Kitigrinya. Chakula hiki kizuri cha kiroho, pamoja na mfululizo wa makusanyiko ya mzunguko madogo yaliyohudhuriwa na watu 1,352, vilitia nguvu imani ya akina ndugu.

Kwa kuongezea, kikundi cha Mashahidi Waethiopia kilienda kupitia nchi kavu kikahudhurie “Ushindi wa Kimungu” Kusanyiko la Kimataifa katika Nairobi, ambapo Ndugu Henschel na Suiter wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova walishiriki. Lakini mabadiliko ya kisiasa yalikuwa karibu kutukia, na mapinduzi yangebadili upesi hali ya kitheokrasi katika Ethiopia.

Kutambuliwa Kisheria na Ofisi ya Tawi Katika Kenya

Ebu sasa turudi Kenya ili tujue maendeleo ya huko yamefikia wapi. Nchi hiyo ilikuwa imepata uhuru hivi karibuni kutoka kwa Uingereza, wakati kwenye kusanyiko la mwisho lililofanywa kwa mtindo wa mandari katika Februari 1962, mwangalizi wa eneo la dunia aliyekuwa akizuru, Harry Arnott alipotoa tangazo muhimu sana kwa wale 184 waliokuwapo. Hilo lingekuwa ndilo kusanyiko lao la mwisho lisiloidhinishwa na sheria katika Kenya. Mashahidi wa Yehova walikuwa wametambuliwa kisheria hivi karibuni! Sasa makutaniko madogo matano ya Nairobi yangeweza kukutana pamoja katika jumba zuri karibu na katikati ya mji. Ndugu walikuwa na shangwe jinsi gani kugundua kwamba sasa walikuwa kutaniko kubwa lenye wahubiri 80! Mkutano wao wa kwanza uliofanywa katika hali ya uhuru, yaani Ukumbusho, ulihudhuriwa na 192.

Mambo yakaanza kutendeka haraka kwa mfululizo. Peter na Vera Palliser kutoka ofisi ya tawi ya Zambia walipewa mgawo wa kusaidia katika Kenya. Akina Palliser na akina McLain waliohitimu Gileadi hivi karibuni, walienda kuishi katika makao ya mishonari ya kwanza katika Nairobi South, na ofisi ya tawi ikafunguliwa Februari 1, 1963. Wakati huo kulikuwa na wahubiri karibu 150 katika Kenya na Uganda, jambo lililohitaji kazi kidogo sana ofisini, labda siku moja au mbili kila juma. Chumba kidogo chenye ukubwa wa meta 3 kwa meta 2.5 katika gorofa hilo lilitumiwa kuwa ofisi.

Lakini upesi baadaye, nchi nyinginezo kama vile Tanzania na Ethiopia, zikaja chini ya uangalizi wa ofisi ya tawi ya Kenya, kazi ikawa zaidi ya maradufu. Mipango ilifanywa kuwe na maofisa wa kufunganisha ndoa miongoni mwa akina ndugu. Makusanyiko ya mzunguko yalifanywa katika majumba ya umma au shule, na Ndugu Henschel alizuru na kutoa mwelekezo uliohitajiwa juu ya jinsi ya kuendesha ofisi mpya ya tawi.

Shamba Lililotengwa Lafunguka

Ilichukua jitihada kushinda ubaguzi uliosalia kutoka siku za ukoloni. Ilisemwa kuwa haikuwa salama kuingia sehemu za mjini za Waafrika, hata wakati wa mchana. Lakini wamishonari wapya na ndugu wanaotumikia penye uhitaji mkubwa zaidi walikuwa na tamaa ya kupanua utendaji wao. Sehemu ya wafanyakazi wa reli ilichaguliwa kuwa eneo la kwanza.

Ilikuwa ni msimu wa mvua na matope mengi yalikwama kwenye viatu vya wahubiri hao wenye bidii. Hayo ndiyo yaliyokuwa majaribio yao ya kwanza kutumia mahubiri yao ya Biblia yaliyotayarishwa kwa uangalifu katika Kiswahili. Itikio lilikuwa nini? Wanawake wengi walisikiliza kwa mzubao, huku wakiashiria kwamba hawakuelewa Kiingereza. Lakini ikawa kitulizo kama nini kugundua kutoka kwa waume zao waliotoka kazini na ambao walizungumza Kiingereza, kwamba wake zao hawakuelewa sana Kiswahili pia!

Kujifunza Kiswahili kulikuwa ni ono kwelikweli kwa ndugu hao wageni, kwa sababu ni maneno machache sana yanayofanana na yale ya lugha yoyote ya Ulaya. Lakini kuna sarufi inayoeleweka, na upesi unaanza kukielewa. Matamshi yacho ni rahisi, na kina msamiati mwingi kushinda ule wa lugha nyingi za Kiafrika.

Bila shaka, mambo hayakuenda sawa wakati wote wakati wa kujifunza. Dada mmoja alitaka kusema “serikali ya Mungu” lakini badala yake akasema “suruali ya Mungu.” Ndugu mmoja alitatizika alipochanganya salamu ya kawaida “Habari gani?” kwa kusema “Hatari gani?” Dada mishonari aliona hangeweza kuchinja kuku na kwa hiyo alitaka kumwuliza painia wa pekee hivi, “Utanisaidia kuua kuku huyu?” Badala ya kusema “kuua,” akasema “kuoa,” yaani akasema “Utanisaidia kuoa kuku huyu?” Mishonari aliyekuwa akiongoza sehemu ya maswali kwa majibu aliita ndugu wote “Dudu” badala ya “Ndugu.”

Bila shaka wageni hao walikuwa kitu kipya kwa watoto wengi. Wengine wangegusa mikono ya akina ndugu kuona kama rangi nyeupe ingetoka. Watoto wengi wangefuata wahubiri hao nyumba kwa nyumba. Hadithi zilizosimuliwa za chuki kwa wageni kumbe hazikuwa za kweli. Badala yake watu wengi walionyesha njaa halisi kwa ajili ya kweli ya Biblia. Mara nyingi wageni wangealikwa ndani na kupewa viti, hata nyakati nyingine chai au chakula. Lilikuwa ni ono jipya kabisa!

Wahubiri wetu wageni walipaswa kujifunza pia kuwa wateuzi katika kutoa mafunzo ya Biblia—wengi sana walikuwa na hamu ya kukubali na ilikuwa vigumu kusoma na kila mmoja. Kutaniko la pili likafanyizwa katika eneo lenye matokeo la Eastlands kabla ya mwisho wa mwaka. Mashahidi walihisi wamestarehe wakiwa na maeneo yaliyotia ndani mitaa kama vile “Jerusalem” na “Jeriko,” na upesi akina ndugu walikuwa na mafunzo mengi kadiri ya uwezo wao.

Jambo la kupendeza ni kwamba, watu kumi na wawili hivi waliojifunza kweli wakati huo na kushirikiana na makutaniko mawili ya kwanza katika Nairobi bado wanatumikia kwa uaminifu miaka yapata 30 baadaye.

Kitabu cha kwanza katika Kiswahili, Kutoka Paradiso Iliyopotea Mpaka Paradiso Iliyopatikana, kilitolewa Juni 1963. Kilifaa sana watafutaji kweli wa ngazi zote za elimu. Baada ya hicho kitabu, Huduma ya Ufalme Yetu ilianza kurudufishwa katika Kiswahili, na Mnara wa Mlinzi lilichapishwa Zambia katika Kiswahili.

Wakati uo huo, Alan na Daphne MacDonald kutoka Shule ya Gileadi walienda kwenye mgawo wao mpya katika kisiwa Mombasa kwenye pwani ya Kenya, na akina McLain wakapewa mgawo kwenda Kampala, Uganda, wakiwa wamishonari wa kwanza huko. Hilo likatokeza fursa kwa William na Muriel Nisbet kuhamia ofisi ya tawi. Walifurahi jinsi gani kuwa huru tena kushiriki katika huduma ya wakati wote pamoja. Ili kukaa nchini, ndugu Nisbet alikuwa amefanya kazi ya kimwili kwa muda wa miaka saba. Akina Nisbet sasa wakaanza kazi ya mzunguko katika Kenya pamoja na ya wilaya katika nchi jirani ya Tanzania.

Mpanuko Katika Miji ya Kenya

Mjini Mombasa, akina MacDonald walipata kutaniko dogo lililofanyizwa na Mashahidi wageni waliokuja kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi, na vilevile kikundi kidogo cha Mashahidi Waafrika waliokuja kutoka Tanzania hadi Mombasa ili kufanya kazi. Kwa vile sasa utendaji wa kuhubiri ungefanywa kwa uhuru, ndugu hao walichukua hatua wakapanga mkutano wao wa kwanza. Walikuwa 30 wenye bidii. Hata hivyo, ndugu wengi Waafrika hawakuwa wamefunga ndoa kisheria. Hivyo, Jumapili moja, mmojawapo maofisa wa ndoa wa Sosaiti alifunganisha ndoa 14. Wote wakabatizwa tena Jumapili iliyofuata.

Eneo la Mombasa lilitokeza tatizo kwa akina ndugu kwa vile dini nyingi ziliwakilishwa. Wazoroastria walikuwa waabudu wa moto waliodai kwamba dini yao ilianza wakati wa Nimrodi. Madhehebu tofauti za dini ya Kihindu hayakutia ndani tu wafuasi wa dini ya Sikh wenye vilemba, bali pia yalitia ndani wale wa Jaini, ambao hawangeweza hata kukanyaga siafu wala kuua nzi. Kisha kulikuwa na idadi kubwa ya Waislamu na wale waliodai kuwa Wakristo. Mombasa ulizungukwa na mahekalu, misikiti, na makanisa makubwa. Kutoa habari njema za milele kulihitaji kubadilikana kunakofaa na ustadi.

Wamishonari wengi walifika baadaye na kupewa mgawo wa kwenda vituo vya mikoani kama vile Nakuru, Kisumu, Kitale, Eldoret, Kericho, Kisii, Thika, na Nyeri. Kufikia mwisho-mwisho wa miaka ya 1960, Wakenya kadhaa walikuwa wamekuwa mapainia wa pekee na walistahili vizuri kuweza kuhubiri katika vituo vya idadi ndogo ya watu.

Mdogo Akawa Elfu

Sasa mambo yakaanza kukua kikweli. Kulikuwa na wahubiri 130 katika Kenya wakati kazi ilipoandikishwa kisheria. Idadi hiyo ikawa karibu maradufu miaka miwili baadaye, na kufikia 1970, mdogo akawa amekuwa elfu kihalisi.—Isa. 60:22.

Watu waliokuwa wakijifunza kweli walifanya mabadiliko makubwa sana, kama vile kushinda tatizo la ukosefu wa adili, ulevi, uchawi, na kujifunza kujua kusoma na kuandika. Wengi walilelewa wakiwa na upendo wa kupita kiasi wa mashamba, mifugo, elimu, au fedha. Kiburi cha kibinafsi na kuficha mambo kwa ajili ya aibu yalikuwa ni lazima yashindwe pia. Kwa hivyo, ingawa watu walipendezwa, iliwachukua muda wa miaka mingi kuvaa utu mpya wa Kikristo kadiri inavyofaa ili wajiweke wakfu kwa Mungu Mweza Yote.

Vijana kwa kawaida waliendelea haraka kushinda wenye umri mkubwa kwa sababu wangeweza kusoma na hawakufuatilia sana mapokeo. Tineja mmoja aliyeitwa Samuel Ndambuki alikuwa mfano mmoja. Yeye alikuwa amevurugika akili na kuchukizwa sana na unafiki wa dini za Jumuiya ya Wakristo. Alianza maisha mabaya yaliyotia ndani kuvuta sigara, kuiba, kusema uwongo, kukosa adili, na matumizi mabaya ya dawa za kulevya akiwa na umri wa miaka 13. Miaka minane baadaye, katika 1967, wanadarasa wenzake wawili wa zamani walimpa habari njema kutoka kwa Biblia. Alivutiwa sana na jinsi vijana hao walivyotumia Maandiko. Mashahidi wa Yehova walikuwa tofauti kama nini wakikazia mwenendo safi! Samuel alifanya mabadiliko makubwa ambayo yalionwa na majirani pia. Hata ingawa alifanya maendeleo mazuri kwa adili zake, bado alipata upinzani mkubwa kuelekea imani yake mpya lakini aliendelea kufanya maendeleo na kubatizwa baadaye mwaka huo. Alianza utumishi wa painia wa kawaida mwaka uliofuata na akafuatilia kwa utumishi wa painia wa pekee, utumishi wa Betheli, na kazi ya mzunguko. Leo, yeye ni mtu wa familia na amesaidia watu kadhaa wapate kujua kweli, akiweka msingi kwa kutaniko linalozidi kukua katika Ukambani.

Mfano mwingine ulikuwa ni Raymond Kabue, aliyeishi Nairobi, na ambaye alijifunza kweli pamoja na ndugu yake wa kimwili na kikundi kingine cha vijana. Akiwa mwenye bidii kwelikweli, alienda nyumbani kwao katika Milima ya Aberdare na kuhubiria watu huko. Kama tokeo, kutaniko likatokea huko ambalo limetoa mapainia wengi wa kawaida na wa pekee. Mmoja wa watoto wake akawa painia na mwingine akatumikia Betheli.

Ndugu yake Leonard alimsaidia Ruth Nyambura, mwanamke aliyekuwa amesoma Biblia yote bila kupata majibu ya maswali yake. Ruth alikuwa na orodha ya maswali tayari, Leonard alipozuru. Ndugu Kabue aliweza kujibu maswali hayo kwa usaidizi wa ndugu mgeni kutia ndani umaana wa nambari 666 inayopatikana katika Ufunuo 13:18. Mwanamke huyo mnyoofu alikuwa mmojawapo watu wa kwanza wanaosema Kiswahili kukubali kweli. Huo ulikuwa ni mwaka wa 1965. Yeye ni mfano wa dada wengi waaminifu ambao waume zao si waamini katika Kenya, ambako, wanawake mara nyingi huwa wengi kushinda wanaume makutanikoni, jambo lisilo la kawaida katika nchi nyinginezo za Afrika. Alilea watoto saba katika kweli, akawa painia wa kawaida kwa muda, na bado atumikia kwa uaminifu akiwa mhubiri.

Mmoja wa mabinti zake, Margaret MacKenzie, alivumilia kifo cha kuhuzunisha cha mumewe katika aksidenti mwaka wa 1974. Aliachwa na watoto wachanga watatu. Kufuatia desturi za kikabila, watu wa ukoo wa mume wake wasioamini walipanga kumteka wakati wa maziko “aolewe” na ndugu-mkwe wake. Hata hivyo, alionywa kimbele naye akatoroka, hivyo akiacha kudai nyumba aliyosaidia kujenga, na shamba alilosaidia kusitawisha. Watu wa ukoo walifaulu kumnyang’anya mvulana wake mchanga, wakimwacha tu na mabinti zake wawili. Halikuwa jambo rahisi kulisha watoto na wakati uo huo kuwapatia uangalizi wa kiroho wa kutosha, lakini kwa msaada wa Yehova Dada MacKenzie alifaulu. Alichukua funzo la familia na huduma ya shambani kwa uzito sana. Alikuwa na shangwe kuona mabinti wote wawili, mmoja akiwa na umri wa miaka 14 na mwingine akiwa na 15, wakibatizwa katika kusanyiko la mzunguko. Mwana wake alirudi nyumbani pia baada ya kuwa mbali kwa miaka 11 na amefanya maendeleo kufikia hatua ya kumtumikia Yehova.

Kupanua Mweneo wa Kazi ya Ufalme

Ofisi ya tawi ilifanya jitihada za pekee za kupanua mweneo wa kazi ya Ufalme. Trakti na vitabu vilitafsiriwa katika lugha za Kikamba, Kikuyu, na Kiluo. Vitabu vya ziada vilitolewa katika Kiswahili, yaani, “Mambo Mawili Yasiyobadilika Asiyoweza Mungu Kusema Uongo,” Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele, na “Neno Lako Ni Taa ya Miguu Yangu.” Chapa ya Mnara wa Mlinzi katika Kiswahili ikaongezeka ikawa na kurasa 24. Hivyo, vichapo vingi vikaangushwa.

Vichapo vilipendwa sana na idadi ya Wahindi, ambao kwa kawaida walikaribisha vizuri Mashahidi Wazungu na kuchukua vichapo kwa urahisi lakini kwa kawaida waliendelea kushikamana na dini yao. Hata hivyo, kulikuwa na visa tofauti. Msichana mmoja tineja alishikilia kweli ijapokuwa upinzani mkali kutoka kwa familia yake na mikazo kutoka kwa jumuiya ya Sikh. Baba yake alimfukuza nyumbani na hata akatisha kumuua. Alienda kuishi na familia moja ya Mashahidi na baada ya funzo la Biblia kamili, akaweka wakfu maisha yake kwa Yehova, akaanza utumishi wa painia na hatimaye akahudhuria Shule ya Gileadi. Sasa akiwa ameolewa, Goody Poulsen bado ni painia wa kawaida, akiwa na matokeo mazuri, hasa katika eneo la Wahindi.

Tatizo la Ndoa Lasuluhishwa

Watu wengi kotekote katika Kenya hawakuwa wamefunga ndoa. Wengine walifunga ndoa kulingana na desturi za kikabila, zilizoruhusu talaka kwa urahisi; wengine waliishi kinyumba tu. Jambo hilo halikupatana na viwango vya juu vya Yehova.—Heb. 13:4.

Hivyo, ndugu wengi waliandikishwa kuwa maofisa wa ndoa chini ya Sheria ya Ndoa ya Kikristo ya Kiafrika. Ndugu hao walisafiri sana wakati watu waliopendezwa walipochukua msimamo wao kwa ajili ya kweli na kufikia hatua ya kutaka kuhalalisha ndoa. Mara nyingi hilo lilitukia wakati uleule walipostahili kuwa wahubiri wa habari njema. Jambo hilo liliweka msingi mzuri wa maisha ya familia kwa sababu liliondoa ile hofu kwamba ndoa ingevunjika ikiwa mke angekosa kupata watoto au ikiwa mahari haikukamilika kulipwa. Zaidi ya ndoa 2,000 zilinufaika kutokana na andalio hilo kwa muda wa miaka iliyofuata.

Ofisi Mpya ya Tawi

Ilitangazwa katika mkusanyiko wa wilaya wa 1970 kwamba Sosaiti ilikuwa imenunua kifaa kipya cha tawi katika Woodlands Road, Nairobi. Ile ofisi ya chumba kimoja katika Nairobi South ilikuwa imehamishwa kwenye nyumba nyingine katika ujirani uleule, lakini sasa kulikuwa na wahubiri karibu 3,000 waliokuwa wakiripoti kutoka nchi nane za eneo la ofisi ya tawi. Jambo hilo lilihitaji usafirishaji zaidi wa fasihi, tafsiri zaidi na uandikaji zaidi wa barua.

Jengo jipya katika ploti yenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja na nusu lililokuwa katika sehemu tulivu na bado karibu na katikati ya jiji ilifaa sana mpanuko wa baadaye. Miti mingi iliyokuwamo, na bustani inayoshuka yenye maua mengi ya rangi tofauti kwenye kingo pamoja na nyua zilipafanya hapo paonekane kuwa paradiso ndogo.

Programu ya kuiweka wakfu ilipangwa iwe siku ya Jumamosi, Juni 26, 1971. Baadaye, jengo lilirekebishwa ili kulifanya lifae zaidi likiwa ofisi na makao. Vyumba zaidi vya kulala viliongezwa. Nafasi ya kutosha katika sehemu ya chini ya uwanja ilitumiwa kujenga Jumba la Ufalme kubwa—la kwanza katika Nairobi. Jumba hilo lingetumikia makutaniko mawili, na bado kulibaki nafasi kubwa katika uwanja ambayo ingeweza kutumiwa kwa ujenzi wa ziada baadaye. Jumba la Ufalme hilo lilikamilishwa karibu na wakati wa kukamilisha mengineyo katika Mombasa, Kisumu, na Nakuru.

Ongezeko Laamsha Wivu wa Makasisi

Kadiri watu zaidi walivyoacha makanisa yao, ndivyo makasisi walivyozidi kukasirika. Majaribio yalifanywa ya kuhujumu Mashahidi wa Yehova. Akiwa amepashwa habari vibaya, Mbunge mmoja aliambia Bunge kwamba Mashahidi hawapeleki watoto wao shuleni wala hawaruhusu wafuasi wao kutibiwa hospitalini. Upesi mbunge huyo alionekana kuwa mjinga aliposahihishwa na Spika wa Bunge ambaye alipokea habari kamili kutoka kwa ofisa aliyekuwa mtu wa ukoo wa mmoja wa Mashahidi.

Hivyo, mtazamo wa kidemokrasia, wa kupenda uhuru ukaendelea kuwapo. Ndugu Knorr alizuru Nairobi tena karibu na mwanzo wa 1972, na baadaye katika mwaka huo mkusanyiko mkubwa ulifanywa Mombasa, kukiwa na hudhurio la 2,161 katika hotuba ya watu wote. Matarajio yalikuwa mazuri, na mambo yalionekana kuwa matulivu na yenye amani.

Mshtuo—Marufuku Katika 1973

Ulikuwa ni mshtuo kama nini kusikia tangazo la redio siku ya Aprili 18, 1973, kwamba Mashahidi wa Yehova walionwa kuwa hatari kwa serikali nzuri na hivyo walikuwa wamepigwa marufuku katika Kenya. Ni kweli, kulikuwa kumekuwa na visa fulani na mambo mabaya juu yetu kutangazwa katika vyombo vya habari hapa na pale lakini hakukuwa na shtaka lolote rasmi wala hakukuwa na hatua ya polisi iliyochukuliwa kutuelekea mahali popote. Kwa ghafula, elimu ya kweli ya Biblia ikawa si halali!

Jitihada zilifanywa za kuwaona maofisa wa ngazi za juu ili mambo yaelezwe wazi. Rufani rasmi ilikatwa siku ya Mei 8 lakini ilikataliwa siku sita baadaye. Wakati uo huo msajili mkuu alifuta uandikisho wa Association of Jehovah’s Witnesses. Jaribio la kumwona rais likakataliwa pia. Rufani ilikatwa dhidi ya kufutwa huko katika Mei 30. Makao makuu ya Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York, yalifuatilia jambo hilo kwa kupeleka barua kutoka kwa msimamizi wa Watch Tower Society yeye binafsi.

Mashahidi wa Yehova wakawa ndio jambo kuu la mazungumzo katika Bunge la Kenya siku ya Julai 5. Bado walionwa kimakosa kuwa madhehebu ndogo ya kisiasa na kuonyeshwa kuwa hawaheshimu serikali za kilimwengu na hukataa tiba ya hospitali. Hata waliitwa Mashahidi wa Ibilisi. Mambo hayo yote yalionyesha bila shaka jinsi watu wanavyoweza kupashwa habari vibaya, kama vile ilivyokuwa kwa wale walioshtaki Mwana wa Mungu, Yesu Kristo.—Mk. 3:22; Lk. 23:2.

Kisha serikali ikachukua hatua ya mara moja ya kuwafukuza wamishonari 36. Ilibidi hao waondoke nchini kufikia Julai 11, 1973. Ulikuwa ni wakati wa huzuni kwelikweli katika historia ya kitheokrasi ya Kenya. Ikabidi vitu vilivyokuwa katika makao kumi ya wamishonari kotekote nchini viuzwe haraka-haraka, vitu vya kibinafsi vilipasa vipakiwe katika visanduku na kuhifadhiwa ili visafirishwe hadi kwenye migawo yao mingine mbalimbali.

Hata hivyo, ofisi ya tawi iliendelea kutumika. Mipango ilifanywa ya kuanzisha kesi ya kisheria kupinga marufuku hiyo kuwa kinyume cha Katiba ya Kenya, iliyohakikisha uhuru wa ibada.

Marufuku Yaondolewa!

Maofisa wenye kufikiri waling’amua upesi kwamba jambo lililotukia halikupatana na tamaa yao kwamba Kenya ionwe kuwa nchi yenye kiasi, yenye watu wenye kufikiri, ya demokrasia, yenye kukaribisha watalii na inayoshikilia haki za kibinadamu. Hivyo, katika Agosti 1973, serikali ilichukua hatua ya kijasiri ya kuondoa marufuku. Taarifa ya serikali ilitokea ikisema kwamba hata hakukuwa kumekuwa na marufuku kamwe. Ndugu wakafurahi wee!

Kazi haikuwa rahisi kwa Mashahidi waliobaki katika ofisi ya tawi. Mashahidi kadhaa kutoka nje ya familia ya Betheli walikuja kusaidia, kutia na Helge Linck, Stanley Makumba, na Bernard Musinga. Ni wachache tu miongoni mwao ndio walielewa utaratibu wa kazi za ofisi na mambo yaliyotakikana kufanywa. Iliwabidi wajifunze namna ya kushughulikia barua na hesabu na vilevile kuweka maandishi.

Kwa kufaa makusanyiko yalionwa kuwa mambo ya lazima chini ya hali hizo. Mfululizo wa makusanyiko ya mzunguko yaliyofanywa katika Oktoba yaliwapa akina ndugu nguvu na mwelekezo mpya shambani. Pia, mipango ya mkusanyiko wa wilaya wa kimataifa ulioratibiwa ufanywe Desemba 26-30, Nairobi, ilipangwa upya. Baada ya marufuku hiyo, kichwa cha mkusanyiko “Ushindi wa Kimungu” kilifaa sana na kilikuwa cha wakati wake. Ingawa ilimaanisha kazi nyingi ngumu kwa muda mfupi wa kuarifiwa, ilikuwa ni shangwe kama nini kuwaona wasafiri wageni wakiwasili kutoa kitia-moyo zaidi kwa akina ndugu wenyeji! Kilele cha hudhurio kilikuwa 4,588 na 209 wakabatizwa.

Kulikuwako utangazaji mzuri wa magazeti pamoja na kipindi cha televisheni cha dakika 28 cha kumhoji Grant Suiter, mmoja wa wafanyakazi wa makao makuu ya Watch Tower katika Brooklyn aliyekuwa akizuru. Mambo hayo yote yalionyesha kwamba Mashahidi wa Yehova bado walikuwapo na walikuwa wakitenda. Makusanyiko zaidi ya mzunguko yalifuata, nao wazee wakachochewa kwa mazoezi waliyopokea kwenye Shule ya Huduma ya Ufalme.

Marufuku hiyo ya ghafula ilishtua sana Mashahidi na ikatahini imani yao. Hata hivyo, ilikuwa na tokeo zuri la kupepeta wale ambao hawakuwa na uhusiano wa karibu na Muumba mwenye upendo na ambao hawakuwa wamejenga imani yao katika msingi imara, yaani Kielelezo chetu, Yesu Kristo. (1 Kor. 3:11) Ikawa wazi kwamba ilikuwa ni lazima ndugu Wakenya wafanye kazi na kuchukua madaraka zaidi wao wenyewe, si kuwategemea wamishonari na ndugu wageni waliokuja kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi. Kulikuwa pia na uhitaji wa funzo zaidi la Biblia la kibinafsi na sala ya bidii.

Upesi wamishonari wengine wakaja kusaidia katika Kenya, hao walitia ndani John na Kay Jason, ambao tayari walikuwa wametumia miaka 26 katika kazi ya mishonari, mzunguko na utumishi wa Betheli katika Zambia. Yehova alikuwa ameonyesha kwamba kulikuwa kungali na kazi nyingi sana ya kufanywa katika Kenya, na Mashahidi walianza wakiwa wameazimia kuendelea na kazi.

Mpanuko Kukiwa na Nguvu Mpya

Maendeleo yalifanywa pia katika hali ya kiroho. Wahubiri walikuwa wakihubiri sanasana kwa magazeti kufikia wakati huo. Sasa mkazo wa pekee ulitiwa katika kutumia Biblia kama ilivyoonyeshwa katika Huduma ya Ufalme. Lilikuwa ni jambo la kuchangamsha moyo kama nini kuona hata watoto wadogo wakifungua Biblia na kutoa ushahidi katika huduma ya shambani, jambo lililoshangaza wenye nyumba na wahubiri wenye umri mkubwa.

Huduma ya Ufalme ilishughulikia pia kwa mara ya kwanza lile suala la mapokeo yasiyo ya Kikristo. Ilionyesha kwamba ingawa huenda kukawa na mapokeo mazuri na yanayonufaisha, mengine yametegemezwa juu ya mafundisho bandia kama vile kutokufa kwa nafsi, jambo ambalo lingeweza kuhusisha Wakristo katika dini bandia. Basi polepole ndugu na dada wakaanza kujiweka huru kutokana na mazoea machafu kama yale yanayohusiana na makesha kwa ajili ya wafu, desturi za mazishi, hofu ya kurogwa, kuvaa hirizi, sherehe za kikabila za kuwaingiza vijana jandoni na desturi za tohara.

Hatua nyingine kubwa ilikuwa ni kufanya lugha moja itumiwe kwa kila kutaniko mijini, ama Kiswahili ama Kiingereza. Hapo awali, lugha zote mbili zilitumiwa kwa mikutano ya kutaniko, ikawa kwamba ni nusu tu ya habari ndiyo ingeweza kutolewa kwa sababu ya kutafsiri daima kutoka lugha moja hadi nyingine. Sasa ndugu wangeweza kufurahia programu nzima katika mojawapo lugha hizo.

“Makedonia” Lawa Neno Maarufu kwa Wote

Wakati uo huo, ziara ya mwangalizi wa eneo la dunia Wilfred Gooch kutoka ofisi ya tawi ya London ilisaidia kupanga vizuri mambo nchini Kenya na kuweka msingi wa kampeni yenye utaratibu ya kufanyia kazi maeneo ya mbali ya Afrika Mashariki. Kwa mfano katika Kenya, robo tatu za idadi ya watu waliishi katika maeneo ya mbali.

Wahubiri waliitikia kwa idili nyingi sana, na tangu 1975 maneno kutoka Matendo 16:9 kuhusu Makedonia yamejulikana na wengi. Hata watu wasio-Mashahidi wamesikika wakisema hivi: “Leo Mashahidi wanafanya mikutano yao katika Makedonia.” Miezi mitatu kila mwaka hutumiwa kufanyia kazi Makedonia ya ki-siku-hizi.

Kwa kuongezea, ofisi ya tawi ilitia moyo wahubiri wote watumie likizo yao ya kila mwaka kutoka kazini wahubiri maeneo ya kwao. Dada mmoja alijibu hivi kwa barua: “Baada ya kufika nyumbani, nilihubiria watu habari njema za Yehova na upesi nikapata mafunzo mengi ya Biblia, wanane kati yao wakiwa watu wa ukoo, sita kati yao walianza kuhudhuria mikutano iliyokuwa umbali wa kilometa 16.”

Kazi hiyo yote ya kutoa ushahidi ilitokeza barua nyingi sana kutoka kwa watu waliopendezwa. Mamia ya barua kila mwezi za kuomba vichapo au mafunzo ya Biblia zililazimu kuongezwa kwa wafanyakazi wa kushughulikia barua katika ofisi ya tawi.

Jambo jingine la maana la mwaka huo lilikuwa ni Shule ya Huduma ya Ufalme kwa wazee katika nchi saba za Mashariki mwa Afrika. Hakukuwa na mafundisho mengi ya kiroho tu bali kulikuwa pia na mambo mengi mapya. Ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha ya ndugu wengi kufanya kazi za usafi nyumbani—kuosha vyombo na kutayarisha chakula—kazi ambazo kwa desturi ziliachiwa wanawake. Lakini wazee walikuwa wanyenyekevu na wenye nia ya kujipatanisha. Lilikuwa ni wazo jipya pia kwa wazee fulani kwamba baba angecheza pamoja na watoto wake. Ni kama vile mzee mmoja alivyosema: “Baada ya miaka hiyo yote, watoto wangu watashangaa nitakaporudi na kuanza kufurahia michezo pamoja nao.”

Hivyo, mwaka wa 1975 ukaisha kukiwa na kilele kipya cha wahubiri 1,709 nchini Kenya. Zaidi ya 300 walibatizwa. Hata hivyo, kazi ya Ufalme ilikuwa ikiendeleaje katika nchi jirani iliyo kusini ya Tanzania?

Hali Zilizobadilika Katika Tanzania

Tofauti na Kenya, ile marufuku juu ya Mashahidi, iliyokuwako tangu Aprili 3, 1965, ilikuwa bado inaendelea. Hali hiyo, pamoja na hali zilizokuwa zikibadilika za familia na za kiuchumi zilitokeza mambo mengine. Iliwabidi ndugu wageni waliokuja kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi kuondoka mmoja baada ya mwingine. Wengi wa mapainia wa pekee Wazambia pia walilazimika kurudi kwao, mara nyingi kwa sababu za kiuchumi zilizoletwa na ongezeko la haraka la ukubwa wa familia zao. Kwa mfano, painia wa pekee aliyepewa mgawo katika 1961 akiwa na watoto wawili alikuwa na familia ya watoto saba kufikia 1967.

Hali iliyo tofauti katika kuondoka kwa mapainia ni ile ya Lamond Kandama. Yeye alikubali kweli katika 1932 nchini Zambia na alishikwa na kufungwa gerezani huko kwa ajili ya imani yake katika 1940 na 1941. Alianza utumishi wa painia mwaka 1959 akiwa na umri wa miaka 47 na kutumwa Tanzania. Alishikwa huko pia. Hatimaye, alipewa mgawo kwenda Kenya, ambapo alitumikia katika migawo kadhaa, na sasa akiwa anakaribia umri wa miaka 80, yeye angali painia wa pekee na bado ni mseja. Yeye ni mfano mzuri kama nini wa uvumilivu wa uaminifu!

“Kondoo” Mahakamani

Wengi walishikwa na kulikuwa na kesi nyingi mahakamani kotekote Tanzania katika miongo miwili iliyofuata. Jambo hilo halikuwashangaza Mashahidi. Yesu alisema hivi: “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. . . . Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi.” (Yn. 15:18, 20) Kwa hiyo walivumilia kwa furaha bila kuudhika.

Mwelekeo wa akina ndugu wa upole na wa kushirikiana mara nyingi uliwasaidia washtaki wenye chuki. Wapinzani wangesingizia urafiki au kupendezwa, kisha Mashahidi wangewaalika nyumbani mwao kwa unyoofu, wakiwaonyesha kwa fahari maktaba zao za kitheokrasi. Nyakati nyingine hata waliazima wasaliti hao vitabu vyao vya kujifunza Biblia, ambavyo baadaye vilitolewa mahakamani kuwa ushahidi dhidi ya Mashahidi. Ndugu walikiri mara hiyo kuwa washiriki wa shirika la Mashahidi wa Yehova, jambo ambalo kisheria lilimaanisha kuwa waliunga mkono shirika lisilo halali. Kwa sababu ndugu wengine walikiri hatia katika kituo cha polisi, hawakukubaliwa kujitetea mahakamani. Tena, kwa sababu ya mwelekeo wao wa kushirikiana, wangeruhusu nyumba zao zipekuliwe bila hati ya upekuzi, jambo lililofanya washikwe. Wengine walifikiri kwamba ilikuwa ni lazima kujibu kila swali waliloulizwa, hivyo wakijiingiza hatiani haraka.

Mashahidi walishtakiwa kuwa washiriki wa shirika lisilo halali kwa sababu tu walihudhuria mikutano ya kujifunza Biblia au walihubiri habari njema au walikuwa na vichapo vya Biblia. Mahakama ziliwapiga faini na kuwahukumia vifungo gerezani kutokea miezi mitatu hadi miezi tisa.

Kwa mfano, ingawa Mashahidi katika Tanzania hawakuwa wengi, wakiwa mhubiri 1 kwa watu 10,000 kati ya idadi ya watu nchini katika mwaka wa utumishi wa 1973, bidii yao haikupita bila kuonwa. Siku ya Septemba 7, 1974, mkutano wa Kikristo ulipokuwa ukiendelea nyumbani mwa Isaack Siuluta mjini Dar es Salaam, polisi waliizingira nyumba hiyo ya Siuluta. Watu 46 kati ya wale waliokuwapo walishikwa kutia ndani dada wawili mapainia. Polisi waliwaacha wale wanawake wengine waende nyumbani. Kichapo chochote kilichopatikana mifukoni au mikononi mwa wahudhuriaji kilitumiwa kuwa ushahidi wakati wa kuendeshwa kwa kesi.

Kesi ilisikilizwa mahakamani siku ya Novemba 29. Ushahidi uliotolewa ulionyesha Mashahidi kuwa wenye amani na watiifu kwa sheria. Hata hivyo, hakimu aliamua kwamba kwa sababu “hali yao ya kidini ni kisingizio tu,” wote hao walikuwa na hatia. Walipigwa faini au kufungwa jela miezi sita kwa ajili ya kuwa na vichapo vya kujifunza Biblia au kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa shirika lisilo halali.

Mashahidi walitiana moyo wakiwa gerezani kwa funzo la Biblia na hotuba za Biblia kama vile “Kumfanya Yehova awe Shangwe Yako Kila Siku.” Wote waliachiliwa baada ya miezi sita. Kazi ya Ufalme haikusimama Tanzania; kilele cha wahubiri 1,609 waliripoti wakati wa mwaka wa utumishi wa 1975.

Mwanzoni ilichukua ofisi ya tawi ya Kenya muda kuja kujua matatizo ya kisheria yaliyokuwa yakiwapata ndugu hao wasiokuwa na ujuzi. Lakini ofisi ya tawi ilipojua, mashauri yanayofaa yalitolewa kwa makutaniko yote juu ya haki zao za kisheria iwapo wangeshikwa na kushtakiwa mahakamani. Mambo hayo yalichapishwa katika Kiswahili kilichoeleweka kwa urahisi na yakasaidia sana.

Katika miaka iliyofuata, kulikuwa na hesabu fulani ya kesi za mahakamani ambapo ndugu waliachiliwa huru. Mahakimu fulani walikata kesi kwamba mashahidi wa mashtaka hawakuwa na uthibitisho kuhusu ‘kuhubiri kokote kulikohusiana na shirika lililopigwa marufuku’ na kwamba “kuwa tu na vitabu hakukuwa uthibitisho wa kuwa mshiriki wa shirika lisilo halali.” Mambo hayo yote yakatoa ushahidi mzuri dhidi ya Mkinzani mkuu wa Yehova.—Mit. 27:11.

Yehova Atoa Nguvu

Wimbi la mnyanyaso dhidi ya Mashahidi wenzi katika nchi jirani ya Malawi lilikuwa na matokeo mabaya, hasa katika eneo la Tukuyu lililo karibu. Ingawa hilo lilichochea wapinzani, lilipatia wengine mwono wa ndani pia. Askari-jela mmoja alisema hivi: “Katika Malawi jitihada zao zilikuwa za bure wakinyanyasa na kuua watu hawa. Ndivyo ilivyo pia hapa. Wao hawataridhiana kamwe. Wao wataongezeka tu.”

Hata hivyo, mnyanyaso haukuwa sawa katika sehemu zote za nchi. Kulikuwa na makutaniko ambayo yangejenga Majumba ya Ufalme mapya na kukutana hadharani, hata wakiimba kwa shauku. Mara nyingi vichapo vilifikia Mashahidi vikiwa salama kupitia posta. Ofisi ya tawi ya Kenya iliendelea kupeleka waangalizi wasafirio ili kuwajenga na wawakilishi wa ofisi ya tawi ili wakutane na wazee na baadhi ya makutaniko. Vichapo zaidi vya Kiswahili vikatia nguvu imani za ndugu Watanzania. Mashahidi kadhaa walichukua utumishi wa painia na kustahili kutumikia mahali pa mapainia wa pekee Wazambia.

Jambo kuu kwa ndugu wengi Watanzania lilikuwa ni ile safari ya kila mwaka ya kuhudhuria mikusanyiko ya wilaya nchini Kenya. Mara nyingi halikuwa jambo gumu kufika Kenya kwa basi. Kwa kweli, katika Oktoba 1968 na hata miaka iliyofuata, vikundi vikubwa vya ndugu wapatao 80 wangekodi basi ili kusafiri zaidi ya kilometa 1,500 kutoka kusini mwa Tanzania hadi Kenya. Hiyo ilikuwa ni kujidhabihu kwelikweli, kwa vile ilikuwa ni lazima waweke akiba ya fedha kwa miezi mingi ili wagharamie safari ya tukio hilo kubwa la kila mwaka. Maofisa wengine wa mpaka wa Tanzania walikuwa wenye kufikiri na hata waliwaambia akina ndugu hivi: “Nendeni mkatuombee tafadhali.” Katika mwaka wa 1970 mabasi manne yakiwa na Mashahidi 350 yalitoka kusini mwa Tanzania kuelekea mkusanyiko wa Nairobi.

Toa Ushahidi Unapofanya Kazi

Ndugu Watanzania hawakuogopa na walikuwa werevu katika utendaji wao wa kuhubiri. Mashahidi waliokuwa wakifanya kazi ya jumuiya pamoja na watu wengi wasio-Mashahidi wangepanga miongoni mwao ndugu mmoja ajifanye kuwa mtu anayependezwa na kuanza kuuliza Mashahidi wengine maswali ya Biblia kwa sauti kubwa, ambao walifurahi sana kujibu. Jambo hilo lilifanywa kwa sauti kubwa hivi kwamba, upesi wafanyakazi wengine walijiunga pia, na saa nyingi za kutoa ushahidi wa Biblia zingetolewa—pasipo kukatiza kazi, bila shaka.

Wakati kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele kilipotolewa kwa Kiswahili, kilikuja kujulikana sana hivi kwamba hata maadui wa habari njema upesi wakaja kukijua vizuri sana kwa jalada lacho la buluu. Kwa sababu hiyo Sosaiti iliamua kutoa chapa tofauti ya kitabu Kweli yenye jalada la rangi isiyovutia sana.

Kweli Yawaweka Huru

Matatizo yalitoka kwa makasisi wa Jumuiya ya Wakristo katika sehemu nyinginezo za nchi. Kikundi cha watu sita kilijifunza Biblia kwa bidii katika eneo la miinuko ya Mlima Meru, ulio magharibi tu mwa Kilimanjaro. Walipokuwa wakimalizia funzo moja, kasisi Mlutheri alikusanya umati wenye ghasia wafanye kelele za fujo nje ya mahali walipokuwa wakijifunza. Siku kadhaa baadaye, hao waliopendezwa walirudi nyumbani kutoka mkutano wa kutaniko uliokuwa umbali wa kilometa 20 na kupata matatizo yakiwangoja. Baba ya mmoja wao alikuwa nyumbani kwa huyo mwanafunzi akizungusha-zungusha shoka na kutisha kumuua. Mwanafunzi mwingine alipata nyumba yake imeharibiwa, mbuzi wake ameibwa na mtoto wake ametoweka. Mwanafunzi wa tatu alipigwa na kunyang’anywa ng’ombe wake. Je! watu hao waliopendezwa walivunjika moyo wasifuatie kweli ya Biblia? La, hasha! Wote waliandika barua za kujiuzulu waliache kanisa.

Wote waliendelea upesi kufikia hatua ya kuwa wahubiri wasiobatizwa ila tu jambo moja liliwazuia; walihitajiwa kwanza watoe vyeti vyao vya ndoa. Lakini vyeti vilikuwa bado mikononi mwa makasisi ambao walikataa kuvitoa. Jambo hilo likapelekwa mahakamani. Makasisi walibisha kwamba watu hao walikuwa washiriki wa shirika lisilo halali, lakini hakimu akawakasirikia makasisi, akawatoza faini na kuamuru wenyewe wapewe vyeti hivyo.

Ushelisheli Yapata Msaada

Je! unawakumbuka wale wahubiri 11 waliokuwa peke yao wakiishi mbali na bara la Afrika katika visiwa Ushelisheli? Walitamani sana kupata msaada kutoka nje. Mapema katika 1974, Ralph na Audrey Ballard wakiwa na watoto wao walitoka Uingereza kuja kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi na walipata kibali cha kuwa wakaaji. Idili yao na bidii yao shambani ilisaidia kuanzisha mafunzo mapya mengi ya Biblia. Ingawa wamishonari walikatazwa kuingia nchini mwaka wa 1969 na 1972, International Bible Students Association ilitambuliwa kisheria siku ya Agosti 29, 1974, na jambo hilo lilichochea kazi zaidi.

Kulikuwa na wahubiri 32 wakiripoti wakati huo, na katika mwaka uliofuata hesabu hiyo iliongezeka ikafikia 51. Lilikuwa ni jambo gumu kwa wenyeji kuchukua msimamo upande wa Yehova kwa sababu makasisi Wakatoliki wangewatisha watu kufukuzwa kazini au kufukuzwa nyumbani. Lakini kadiri miaka ilivyozidi kupita, ndivyo na uvutano wa makasisi ulivyozidi kwisha, na wapendao kweli walianza kuchukua hatua za ujasiri.

Pia katika mwaka wa 1974, baada ya habari njema kuhubiriwa katika kisiwa kikuu cha Mahé, Mashahidi waliabiri muda wa saa tatu kwenda kisiwa cha pili kwa ukubwa cha Praslin, ambacho kimejulikana sana kwa Vallée de Mai yenye mawese. Miti hiyo ya mawese hutoa ile nazi iitwayo eti nazi mapacha, au coco de mer, ambayo yawezekana ndiyo kubwa zaidi ulimwenguni (kilo 14-18), na hupendwa sana na wakusanyaji vitu kwa sababu ya umbo layo lisilo la kawaida. Kwa vile kuna idadi ya watu wanaopungua 5,000, bila shaka kila mtu alijua kila mtu mwingine. Ingehitaji watu wenye nguvu kusimama imara kwa ajili ya kweli dhidi ya mkazo kama huo wa marika. Na wengine walifanya hivyo, ingawa ilichukua muda kuwazoeza kuhubiri habari njema kwa busara zaidi badala ya kushambulia tu ibada ya sanamu au kuhubiri uharibifu wa waovu kwenye Har–Magedoni.

Hatimaye katika 1976, mume na mke wamishonari wakapata makao Viktoria katika Mahé. Walisaidia kusawazisha kutaniko kiroho na kusaidia watoto wengi wa familia za Mashahidi kutembea katika kweli. Hilo halikuwa jambo rahisi kwa sababu wengine walikuwa wamezoea maisha ya anasa yasiyo ya adili. Ni Mashahidi wachache tu wenyeji waliotia bidii katika funzo la kibinafsi na utumishi wa shambani. Kwa hiyo wengine walipeperushwa huku na huku kwa kila mtindo mpya wa ulimwengu, mambo yaliyofanya wengi waache kweli. Pia, hesabu fulani ya wale waliokuwa wakishirikiana na kutaniko walikuwa wameweka siku fulani akilini mwao kuwa mwisho wa ulimwengu mwovu badala ya kutumikia wakiwa na umilele akilini mwao. Mambo hayo yote yalipunguza maendeleo ya kiroho.

Wasimama Imara Pasipo Msaada Kutoka Nje

Siku ya Juni 5, 1977, mapinduzi yaliingiza serikali mpya na ono jipya kwa visiwa hivi vilivyokuwa vitulivu hapo awali. Bunge jipya lilijadili juu ya Mashahidi wa Yehova na msimamo wao wa kutokuwamo kuelekea serikali zote za dunia. Mbunge mmoja alidokeza kwamba Mashahidi wapigwe marufuku, lakini wengine kwa hekima wakatetea haki za kikatiba za uhuru wa dini.

Hata hivyo, katika 1978, makao ya mishonari yalifungwa na wamishonari hao wakapewa mgawo kwenda Kenya. Familia ya Ballard ilikuwa imehama pia. Sasa ilikuwa ni lazima ndugu wenyeji wasimame peke yao. Hata hivyo, sasa walikuwa wameimarishwa kwa njia bora zaidi kushughulikia kazi ya Ufalme kwa vile walikuwa wamenufaishwa na ushirika wa ndugu wenye ujuzi katika kweli na wazee walikuwa wamehudhuria Shule ya Huduma ya Ufalme mara kadhaa. Ingawa wengi hawakujua kusoma wala kuandika na walishikamana na uwasiliano na roho waovu, wenye mfano wa kondoo bado walipatikana. Kwa mara nyingine tena kulikuwa na wahubiri 50 katika Ushelisheli kufikia mwaka wa 1982, na wengine walianza utumishi wa painia wa kawaida, mmoja wao akiwa Lise Gardner. Hatimaye kusajiliwa kwa Association of Jehovah’s Witnesses kulikubaliwa katika Ushelisheli mnamo Januari 1987, lakini ombi la kuingia kwa wamishonari bado lilikataliwa.

Mavuno Katika Visiwa Hivyo

Mkusanyiko wa wilaya wa kwanza ulifanywa Januari 16-18, 1987. Kufikia wakati huo mikutano yote na makusanyiko ya mzunguko yalifanywa katika Jumba la Ufalme; mkusanyiko huo ungekuwa wa kwanza kufanywa mahali tofauti.

Ulifanywa wapi? Katika kibanda kilichokuwa mahali pazuri pa hoteli kubwa ya watalii. Jengo hilo lililokuwa wazi nusu, lenye paa iliyoezekwa, lilikuwa katikati ya miamba na lilielekea mojawapo ghuba ya Mahé inayopendeza zaidi. Wahudhuriaji hawakufurahia programu ya kiroho tu bali pia walifurahia sauti ya mawimbi ya bahari yenye kutuliza na pia pepo tulivu zenye kuburudisha zilizokuwa zikipitia ndani ya jumba.

Hudhurio la siku ya kwanza lilikuwa hesabu yenye kusisimua ya watu 173. Mahali hapo palijaa siku ya Jumapili kukiwa na hudhurio la 256. Uwezekano wa ukuzi ni mkubwa kama nini kukiwa na wahubiri 80 tu katika visiwa hivyo!

Miongoni mwa wale waliobatizwa kwenye mkusanyiko alikuwa mwanamke mmoja aliyekuwa mpinzani hapo awali. Ni nini kilichobadili maoni yake? Ni kuhudhuria kwake Ukumbusho wa kifo cha Kristo. Siku hiyo ndiyo aliyoona jinsi Mashahidi wa Yehova walivyo hasa. Hata hivyo alihitaji kufanya marekebisho fulani katika maisha yake. Ili ajiruzuku, alikuwa na duka dogo kando ya barabara ambapo aliuza vitu kutia ndani na tumbako. Alionywa kwamba kuacha kuuza bidhaa za tumbako kungeharibu biashara yake. Bila kujali, akamtumaini Yehova na kuacha kuuza tumbako. Biashara yake haijaathiriwa. Kwa kweli, aliandika kwenye ubao saa za kufungua na kufunga duka hilo ili apate wakati zaidi kwa ajili ya kazi muhimu zaidi ya kuhubiri Ufalme na kupanga kuhubiri wakati wengi zaidi wanapopatikana.

Jitihada za kuhubiri za wahubiri hao zinavuna mavuno mazuri. Jumba la Ufalme liliwekwa wakfu katika kisiwa Praslin mwaka wa 1990. Hesabu fulani ya mafunzo ya Biblia yanaongozwa katika kisiwa cha tatu kwa ukubwa cha La Digue. Pia, katika Septemba 1990, uangalizi wa Ushelisheli ulihamishwa uwe chini ya ofisi ya tawi ya Maurishasi, ambapo lugha ya Kikreole kinachofanana na cha Ushelisheli husemwa.

Rwanda—Uswisi Iliyofichika ya Afrika

Sasa turudi barani. Ikiwa kaskazini mwa Burundi, na ikiwa na uzuri na vilima kama Burundi, na ikiwa kati ya Tanzania, Uganda, na Zaire, Rwanda ni nchi yenye watu wengi zaidi katika Afrika. Ina ukubwa wa kilometa mia na sitini kutoka mashariki hadi magharibi na kutoka kaskazini hadi kusini, lakini katika miaka 20 iliyopita, idadi ya watu imeongezeka kutoka milioni tatu hadi zaidi ya milioni saba. Rwanda ina baadhi ya chai bora zaidi ulimwenguni na wengi wa gorila wa milimani wa ulimwengu. Ni bara la milima, maziwa ya maji, na zaidi ya vilima 10,000, na lina chemchemi za kusini zaidi za Mto Naili.

Kama ilivyo nchi jirani ya Burundi, Rwanda pia ina Wahutu wengi na kabila la watu warefu la Tusi lenye watu wachache. Watu wengi huishi sehemu za mashambani za mbali katika makao yaliyozingirwa na migomba ya ndizi katika ‘Uswisi hii iliyofichika ya Afrika.’ (Ona Amkeni! [Kiingereza] la Februari 22, 1976.) Wakaaji wote husema Kinyarwanda; na wenye elimu zaidi wanajua Kifaransa pia.

Kweli inayotoa uhai kutoka Neno la Mungu ingefikaje nchi hii ya mbali yenye milima-milima? Baraza Linaloongoza lilipatia mgawo wamishonari wanne waliofuzu Gileadi waje Rwanda katika mwaka wa 1969, lakini maombi yao ya kuingia nchini yalikataliwa, labda kwa sababu ya uvutano wenye nguvu wa Kanisa Katoliki uliokuwa wakati huo.

Hata hivyo, mapainia wa pekee wawili kutoka Tanzania, Oden na Enea Mwaisoba, walikuja mwaka uliofuata na kupata makao katika jiji kuu la Kigali na kuanza kuhubiri. Walianza kuzuru watu waliosema Kiswahili waliotoka sanasana Zaire na Tanzania kwa vile bado hawakujua Kinyarwanda. Kufikia Februari 1971 wahubiri wanne wa kutaniko walikuwa wakiripoti wakati katika huduma ya shambani. Badiliko la serikali lilitoa fursa ya kuwa na uvumiliano zaidi wa kidini lakini tatizo la lugha lilifanya ukuzi uwe wa polepole kwa vile hakukuwa na vichapo vyovyote katika lugha ya Kinyarwanda.

Mapainia wengine kutoka Zaire na Tanzania walikuja kusaidia. Kulikuwa na wahubiri 19 waliokuwa wakitenda kufikia 1974. Katika mwaka wa 1975 waliangusha vitabu zaidi ya elfu moja. Mambo mengine ya maana yalitendeka pia katika mwaka huo: Ndugu mmoja alizuru kutoka ofisi ya tawi ya Nairobi, watu sita walibatizwa, na mtaala wa Shule ya Huduma ya Ufalme ukanufaisha ndugu saba Wanyarwanda. Kwa kweli, msingi mzuri ulikuwa ukiwekwa kwa ajili ya mpanuko. Vikundi vidogo vya kujifunza Biblia vilianza kuchipuka nje ya Kigali.

Mhamaji Arudi

Wakati uo huo, Mnyarwanda mmoja aliyeitwa Gaspard Rwakabubu, alijifunza kweli alipokuwa akifanya kazi katika migodi ya shaba ya Kolwezi kusini mwa Zaire. Alisaidia katika kusimamia kutaniko la hapo, hivyo akapata ujuzi wa kiroho uliohitajika. Na bado mawazo yake na sala zake zilielekea nyumbani kwao Rwanda ambako hakuna mtu aliyekuwa anasikia habari njema.

Angefanya nini juu ya jambo hilo? Gaspard alisema na mishonari aliyekuwa mfunzi wa Shule ya Huduma ya Ufalme. Mfunzi huyo akamwuliza hivi: “Namna gani ukianza utumishi wa wakati wote wa painia na kurudi Rwanda?”

Alifurahia sana uwezekano huo na wala kupandishwa cheo wala mabembelezo ya watu wa ukoo hayangemzuia. Msaada wa Yehova ulionekana wazi pia. Si kwamba tu fomu zilizohitajiwa zilijazwa haraka isivyo kawaida bali pia kampuni ya migodi iliyomwajiri hata ilimpatia tiketi za ndege za kurudi Rwanda. Alifika Kigali Juni 1975. Kuhama huko kulimaanisha kwamba Ndugu Rwakabubu angedhabihu vitu vya kimwili; hakuwa tena na nyumba kubwa ya kampuni ya kuishi, bali nyumba sahili tu iliyojengwa kwa matope.

Shauku yake na uelewevu wake wa utu wa Wanyarwanda ulisaidia katika kusogeza mbele maendeleo ya kitheokrasi. Wanyarwanda wengine wakaja katika kweli kwa bidii ileile ya Ndugu Rwakabubu. Hudhurio la mikutano lilipanda juu katika Kigali, na hesabu ya wahubiri ikapanda kutokea 29 katika 1975 kufikia 46 katika 1976, kisha 76 katika 1977. Watu arobaini walihudhuria kusanyiko la mzunguko la kwanza, lililofanywa katika sebule yake.

Kichapo cha kwanza katika Kinyarwanda kilitokea mwaka wa 1976 nacho kilikuwa ni “Habari Njema Hizi za Ufalme.” Kisha jaribio jingine lilifanywa katika mwaka wa 1977 la kuwaleta wamishonari mjini Kigali. Ndugu wawili na wake zao walikubaliwa kukaa kwa muda mfupi tu. Walipata makao ya mishonari yenye kufaa sana baada ya kutafuta sana. Kumbe ingawa nyumba ilikuwa kubwa, hakukuwa mfumo wa kuleta maji, wamishonari walilazimika kuoga chini ya mabati ya kuchukulia maji ya paa. Walikimbia huku na huko kutafuta vyombo vyovyote vilivyopatikana ili kuteka maji ya mvua wakati mvua iliponyesha. Siku moja walijikaza sana kujaza besheni kubwa la kuogea wakaja kung’amua baadaye tu kwamba kizibio kilikuwa kinavuja na hivyo kumwaga maji yao yote yenye thamani!

Wasema Lugha ya Wenyeji

Wamishonari hao walijua kwamba ili kufikia mioyo ya wenyeji wakiwa na habari njema, ilikuwa ni lazima wajue lugha yao na kwa hiyo mara moja walianza kujifunza Kinyarwanda. Walifanya maendeleo mazuri hata wakawavutia maofisa wa huko ambao wengi wao walipendelea ujumbe wa Ufalme. Hata hivyo, uvutano wa watu wa dini bandia ulianza kuhisiwa upesi; wamishonari hawakupewa viza mpya. Na hivyo baada ya miezi mitatu tu ya kuwa nchini waliondoka kwenda Zaire.

Mapainia wa pekee wageni waliondoka Rwanda pia kwa sababu tofauti-tofauti. Ndugu wenyeji walijazia uhitaji kwa kuanza kupainia na kupanua utendaji wa kuhubiri katika wilaya zote nchini. Matokeo yalikuwa nini? Mashahidi walihubiri ujumbe wa Ufalme katika masoko ya mashambani zaidi ya mia moja. Ilikuwa vizuri kama nini kuona maendeleo hayo baada ya kazi kuanza ikiwa imechelewa sana!

Wakiwa na shauku kwa ajili ya kweli, Mashahidi hao Wanyarwanda walitamani kuwa na shangwe ya kushirikiana na ndugu zao kutoka sehemu nyinginezo. Kwa hiyo katika 1978, kulikuwa na watu 30 waliotoka Rwanda kuelekea Nairobi, ambao ni umbali wa kilometa 1,200, wahudhurie Mkusanyiko wa “Imani Yenye Ushindi.” Ilikuwa ni safari ngumu kwa sababu kadhaa. Tatizo moja lilikuwa ni njia ya usafiri usiotegemeka. Tatizo jingine lilikuwa kwamba kusafiri kupitia Uganda iliyokuwa na matatizo ya kisiasa kulimaanisha kupekuliwa mara nyingi kwa kushikiwa bunduki katika vituo vya kukagua magari, hata kushikwa na kutishwa kuuawa. Magari kuharibika mara nyingi na magumu ya kuvuka mipaka yaliongezea matatizo hayo. Safari hiyo ya kwenda Nairobi ilichukua jumla ya siku nne. Lakini ndugu hao walifurahi kama nini kuona maelfu ya Mashahidi wenzi kutoka mataifa tofauti-tofauti wakiwa wameungana kwa amani katika mkusanyiko wa Nairobi!

Miaka ya Misukosuko Katika Uganda

Kelele za shangwe hazikusikiwa katika nchi jirani ya Uganda wakati wa miaka ya katikati ya 1970. Hali zenye mkazo zilienea pote. Si kwamba tu wamishonari wote na ndugu wageni wote walilazimishwa kutoka nchini bali pia watu wote walihofia uhai wao kila siku. Matatizo ya kiuchumi na marufuku iliyowekwa tena juu ya Mashahidi wa Yehova katika mwaka wa 1975 yaliongezea taabu za akina ndugu. Ombi la kuondoa marufuku lilikataliwa, hata ingawa hapo awali serikali ilikuwa imehakikisha uhuru wa kidini.

Katika miaka hiyo, kuvunja sheria hakukuelekeza mahakamani bali kulielekeza kwenye mateso na kifo. Watu waoga hawangedumu katika nchi hiyo. Ilihitaji moyo mkuu sana ili kuendelea kuwa shahidi wa Mungu wa kweli. Na kwa sababu uchumi ulikuwa ukizorota, watu walianza kuhangaikia mali zaidi na zaidi, na mielekeo ya kukosa adili haikuwa imekwisha pia. Mashahidi walikuwa na matatizo mengi ya kukabili: Woga wa mwanadamu, kufuatilia mali, ukosefu wa adili, uwasiliani-roho, yalikuwa ni matatizo machache waliyopata. Kukawa na upungufu wa wahubiri, kutoka 166 katika 1976 hadi 137 katika 1979. Bila shaka sehemu ya upungufu huo ilisababishwa na wale waliotoroka nchi hiyo. Zaidi ya mhubiri 1 kwa kila 4 aliondoka. Lakini bado watu walioheshimu sana Mungu na ambao waliwapenda Mashahidi walibaki nchini.

Hii ilikuwa ni miaka ya majaribu kwa kila mtu nchini Uganda na hasa Mashahidi kwa sababu ya marufuku. Lakini kwa kufaa, marufuku hiyo haikufikilizwa sana kila mahali. Kazi ya upainia wa pekee iliendelea na hata kupanuka katika maeneo kadhaa. Mapainia wa pekee walipewa mgawo kwenye miji iliyokuwa kaskazini mwa nchi, na upesi makutaniko mengine yakaanzishwa. Katika mji wa Soroti uliokuwa kaskazini-mashariki, mkuu wa wilaya hata aliruhusu matumizi ya mojawapo shule bora zaidi mjini kwa mikutano ya kutaniko ijapokuwa ile marufuku!

Na bado katika Kampala, ndugu wawili walishikwa wakihubiri na kutupwa ndani ya jela mbaya zaidi nchini. Marafiki walihofu hawatawaona tena lakini kwa kushukuru, waliachiliwa baada ya juma moja. Mashahidi watatu walifungwa gerezani miezi mitatu mjini Lira kwa sababu ya kuhubiri.

Ilikuwa ni kawaida kwa watu kuona watu wa ukoo na majirani wakitoweka, kusikia mifyatuo ya bunduki usiku, kuwa na maduka matupu, kuona infleshoni ikipanda kwa kiasi cha 1000 na zaidi, na kukosa namna ya usafiri. Mamia ya watu wangengoja gari katika kituo cha basi wakiwa tayari kung’ang’ania gari linalobeba watu wanane pekee. Nauli zilizowekwa na serikali zilipwe zilipuuzwa kabisa. Watu walilipia “tiketi” wakati gari liliposimamishwa katika sehemu ya pekee ya barabara na kila abiria kulazimishwa kutoa chochote alichodai dereva.

Fasihi kutoka Nairobi na ziara za ndugu kutoka ofisi ya tawi zilikuwa kama mana kutoka mbinguni—chakula cha kiroho kwa wakati unaofaa na chanzo cha kitia-moyo chenye kuburudisha kwa Mashahidi nchini Uganda. Vijapokuwa vizuizi hivyo vyote, wengine waliweza kuhudhuria mikusanyiko ya wilaya katika Kenya. Makusanyiko madogo pia yaliendelea nchini; na katika moja la makusanyiko hayo, mwanamke mmoja alibatizwa siku moja tu baada ya kujifungua mtoto.

Wategemezwa na Yehova

Mashahidi walioendelea kuhubiri wakati wote chini ya misukosuko kama hiyo walikuwa mifano mizuri sana ya imani. Miongoni mwao alikuwa Anna Nabulya, dada mzee-mzee kutoka mji wa Masaka. Jambo kuu maishani mwake lilikuwa wakati alipohudhuria Shule ya Utumishi wa Painia nchini Kenya. Angekuja darasani akiwa amevaa vazi refu la mtindo wa kiganda lililochorwa maua makubwa na kufurahia sana kina cha mambo ya kiroho na habari zinazotumika zilizotolewa.

Watu wa ukoo wa dada Nabulya walimkaza asirudi Uganda bali akae nao Kenya na kuepuka magumu ya kiuchumi, hatari nyinginezo, na mambo mengine yasiyofaa. Lakini alikataa katakata; alitaka kuhubiri Uganda, ambapo watu walihitaji ujumbe wa habari njema unaofariji. Alisema hivi: “Ujapokuwa udhaifu wa uzee, nitatumia ile nguvu kidogo niliyo nayo kusaidia watu wenzangu wawe na uhusiano mzuri na Yehova.” Hivyo alirudi Uganda na kutumikia watu wake na Mungu wake kwa uaminifu mpaka kifo chake.

Mfano mwingine wa imani ulikuwa ni ndugu painia aliyehubiri kwa ushujaa kwa wanajeshi wote na maofisa wa polisi wote katika mgawo wake wa mbali. Alipokosa fedha za kununua kuni za kupikia, basi angechoma viti na fanicha nyingineyo mpaka fedha na vichapo vya Biblia vilivyohitajika sana vifike. Watu katika eneo lake walikuwa na njaa sana ya chakula cha kiroho hivi kwamba angeangusha kwa urahisi vitabu 40 au 50 kwa siku moja.

Mashahidi waliendelea kutaabishwa, kushikwa na kuhojiwa, lakini walivumilia. Yehova aliwapa watu wake “ulimi wa hao wafundishwao,” nao walihubiria wenye mamlaka bila kuogopa.—Isa. 50:4.

Dada wajane walikuwa chanzo cha kitia-moyo kwa Mashahidi wengi mjini Kampala. Hawakuwa wamepitia magumu ya kupoteza waume zao tu bali pia walikuwa wamepoteza mali yao. Na bado waliweka masilahi ya Yehova kwanza, wakifanya kazi kwa bidii katika huduma na kukaza ndani ya watoto wao viwango vya kimungu. Walisaidia jirani zao wajifunze kweli pia, na baadaye wakawa na shangwe ya kuona baadhi ya watoto wa wanafunzi wao wa Biblia wakiwa wahudumu mapainia. (Ona toleo la Mnara wa Mlinzi la Februari 15, 1985, kurasa 27-31, Kiingereza) Yehova alibariki kazi ya bidii ya waaminifu kama hao na idadi ya wahubiri wa Ufalme iliongezeka.

Djibouti—Yenye Joto na Ukame

Nchi ndogo ya Djibouti ambayo hapo zamani iliitwa Somali ya Ufaransa, iko ng’ambo ya kisehemu cha mwisho kilicho kusini magharibi mwa Peninsula ya Arabia kati ya Ethiopia na Somalia. Ina kituo kikuu cha kijeshi cha Manowari za Ufaransa. Jiji kuu la nchi hiyo ambalo pia linaitwa Djibouti linaorodheshwa na vitabu fulani vya takwimu kuwa jiji lenye joto zaidi ulimwenguni. Ijapokuwa hali za jangwa, nchi hiyo ndogo ina mambo ya kupendeza hasa baharini ambamo mna matumbawe yaliyojaa samaki na wanyama wengi wa baharini.

Hapa ndipo Bonde Kuu la Ufa, likitanuka tokea Lebanoni na kupitia Bahari Nyekundu, laingia bara la Afrika. Kuna mambo ya kiasili ya ajabu katika Ziwa Assal na Ziwa Abbé—mifanyizo ya chumvi na chaki, minara ya chokaa iliyochongoka juu, chemchemi moto, na maji yenye rangi nyingi.

Zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini ni wa kabila la Afar, ambao eneo lao lafika ndani ya Jangwa la Danakil nchini Ethiopia. Kabila jingine la Waissa ambao ni watu wa Kisomali huishi katika jiji kuu, ambalo liko karibu na Somalia. Joto jingi sana hufanya watu wawe walegevu, na wakati mwingine wao hupanda basi ili kusafiri umbali wa meta 90 tu. Wengi wamezoea kutafuna khat, dawa ya kulevya yenye nguvu kidogo ya kuchochea inayopatikana katika majani ya miti inayokua katika nyanda za juu za Yemen, Ethiopia na Kenya. Kwa kweli, alasiri yote hutumiwa katika kutafuna khat; mambo mengine yote hukoma wakati huo. Watu wengi ni Waislamu na husema Kifaransa, Kiarabu, Kisomali, na Kiafar.

Claudine Vauban, dada Mfaransa aliyeolewa na mwanajeshi alikuwa ndiye mhubiri wa kwanza wa habari njema nchini Djibouti. Ilikuwa ni hatari kwa mwanamke mzungu kwenda hadharani peke yake katika nchi hiyo ya Kiislamu. Jambo hilo halikuzuia utendaji wa Dada Vauban. Aliendelea kutenda katika huduma ya shambani na kuongoza mafunzo mawili ya Biblia muda wa miaka mitatu aliyoishi Djibouti. Karibu miaka miwili baadaye, katika mwisho wa 1977, Mdjibouti kijana aliyekuwa amejifunza kweli nchini Ufaransa aliwasili. Hata hivyo, akawa na matatizo ya kiroho na hatimaye akatengwa.

Dada mmoja aliyekuwa mkimbizi kutoka Ethiopia alihamia Djibouti katika 1978. Baadaye alijifunza lugha ya Kifaransa na akaendelea kuwa mwaminifu ajapokuwa mbali sana na Mashahidi wengine. Ndugu waliozuru kutoka Ufaransa na Ethiopia walimtia moyo kiroho. Hata hivyo, ziara hizo zilikuwa za mara kwa mara mpaka mwaka wa 1981, ambapo kijana mtumishi wa huduma kutoka Ufaransa, Jean Gabriel Masson na mke wake Sylvie walipofika kutumikia penye uhitaji mkubwa zaidi. Hiyo ilikuwa hatua ya uhodari kwa akina Masson kwa kufikiria upweke, kuwa wapya katika kweli, hali ya hewa isiyopendeza, na gharama ya juu ya maisha.

Upesi mahubiri yao yaliyopangwa vizuri yakaanza kuzaa tunda. Wakimbizi kadhaa kutoka Ethiopia walikubali kweli kabla ya kuondoka Djibouti kuelekea nchi nyinginezo. Kulikuwa na wahubiri watendaji 6 kufikia 1982; na 12 walihudhuria Ukumbusho. Watatu walibatizwa miezi miwili baadaye wakati wa ziara ya mwangalizi wa mzunguko kutoka Ufaransa.

Mikutano ilikuwa inafanywa kwa ua wa nyumba ndogo ya Ndugu Masson nyakati hizo, wakati mwingine chini ya hali zisizo za kawaida. Wakati mmoja ndugu mmoja kutoka Nairobi alikuwa akitoa hotuba ya Biblia wakati paka walipoanza kupiga kelele, kulia kwa nguvu na kupigana kwenye mimea mitambaazi iliyokuwa imefungwa kwa ufito juu ya ua. Sauti hiyo ikawa ya kupita kiasi na bila shaka yenye kukengeusha akili sana mpaka paka hao wenye kupigana walipoanguka mbele ya msemaji kutoka kwa ufito uliokuwa juu! Isitoshe, umeme ukapotea upesi baadaye, hivi kwamba wote waliachwa katika giza jeusi tititi. Hata hivyo, mkutano uliisha kwa mafanikio. Hudhurio la mikutano likaongezeka likawa 18. Ni jambo la kushangaza kwamba ingawa hudhurio lilikuwa dogo, mikutano ilikuwa ikifanywa kwa lugha nne: Kiingereza, Kifaransa, Kiamhara, na Kisomali.

Mtawa Achukua Msimamo Wake

Haikuwa rahisi kwa Ndugu Masson kupata kazi, lakini hatimaye alipata kazi ya ualimu. Kule shuleni alikutana na Louis Pernot mtawa Mkatoliki na mwalimu mkuu wa shule hiyo, ambaye alikuwa ameishi hapo kwa karibu miaka 20. Wakati Louis alipoonyesha kupendezwa sana na kweli ya Biblia, Ndugu Masson alimwalika ahudhurie Ukumbusho wa kifo cha Kristo. “Haiwezekani,” Louis akasema. “Kila mtu ananijua hapa Djibouti na wanajua mimi ni mtu wa aina gani. Naweza kudhubutuje kuhudhuria mkutano wa Mashahidi wa Yehova?”

Hata hivyo, Ndugu Masson alikuwa na wazo. Alidokeza kwamba Louis aje nyumbani mwake wakati wa pumziko la alasiri ambapo wote katika Djibouti wangekuwa wanalala kwa sababu ya jua kali. Kisha angeketi nyuma ya pazia katika chumba cha kulala cha Ndugu Masson na kungojea mkutano uanze. Hakuna mtu angejua kwamba yupo, na baadaye angerudi nyumbani akiwa salama akifichwa na giza baada ya mkutano.

Basi hivyo ndivyo alivyofanya—Louis alihudhuria mkutano wake wa kwanza akiwa ameketi nyuma ya pazia ya chumba cha kulala cha Ndugu Masson! Ingawa hakuelewa mambo mengi ya Kibiblia, alivutiwa sana na kina cha mazungumzo ya Biblia.

Kisha Ndugu Masson akamtia moyo achague kimoja cha vitabu vyake akakisome nyumbani. Kwa vile Louis alikuwa mwalimu, aliichagua kitabu Kupata Faida Zote za Ujana Wako. Alikuwa amejiuliza mara nyingi ni kwa sababu gani dini yake haikuwa imetoa habari hususa ya kusaidia vijana kukabiliana na matatizo yao katika ulimwengu wa leo. Alifikiria kwamba dini ya kweli ya Mungu inapasa kutoa uongozi unaofaa kwa watu bila kupuuza maneno Yake. Louis alianza kusoma kitabu Ujana Wako usiku huo. Hakuacha kukisoma. Kesho yake akamwambia Ndugu Masson kwamba alikuwa amepata kweli. Akajiuzulu utawa wake na pia kuwa Mkatoliki juma ilo hilo!

Jambo hilo bila shaka lilileta upinzani na upesi baadaye Ndugu na Dada Masson wakaambiwa watoke jamhuri hiyo ndogo. Hilo likawa pigo baya kwa Mashahidi wenyeji, kwa vile watu 44 walikuwa wamehudhuria Ukumbusho. Ndugu Masson akaomba serikali imruhusu kubaki na akaongezewa mwezi mmoja zaidi; baadaye alihamia eneo la Ufaransa la Mayotte, katika Bara Hindi.

Kabla ya akina Masson kwenda, walikuwa wakiongoza mafunzo ya Biblia ya kila siku na Louis, ambaye aling’amua kwamba ilikuwa ni lazima ajisimamie mwenyewe. Baada ya akina Masson kuondoka, mhudumu painia aliweza kwenda Djibouti kumsaidia Louis kiroho.

Lakini kwa sababu mbalimbali, Mashahidi wangekuja na kuondoka. Hivyo, ilikuwa ni lazima Louis aliyebatizwa karibuni asimame imara ijapokuwa miaka ya upweke wa kiroho. Mara kwa mara aliitwa na wenye mamlaka, akahojiwa, na kuonywa juu ya utendaji wake wa kuhubiri. Yeye alibaki imara; hata alitumikia akiwa painia msaidizi. Ingawa hivyo, hatimaye alinyang’anywa kazi yake kwa sababu ya imani yake. Louis aliacha mambo mikononi mwa Yehova na kuendelea mbele hadi alipopata njia nyingine ya kujiruzuku.

Leo, kikundi kidogo cha wahubiri katika Djibouti wanaendelea kutoa kweli za Biblia kwa wakazi. Mashahidi kutoka nchi za nje wamehamia Djibouti hivi karibuni, hivyo wakitoa kichocheo kipya.

Jitihada Mpya Nchini Somalia

Miaka mingi baada ya wamishonari Vito na Fern Fraese kupewa mgawo mwingine katika mwaka wa 1963, hakuna ushahidi wa wazi wa Ufalme uliotolewa katika Somalia. Hatimaye ndugu mmoja Mzungu aliyezaliwa Somalia alienda likizo ya miezi kadhaa katika nchi hiyo ya pwani mwishoni mwa 1980. Akiwa huko, alipata watu waliopendezwa na habari njema. Watu hao wenye mfano wa kondoo walisaidiwa zaidi na Mashahidi mbalimbali waliokuwa wakizuru nchi hiyo kila mara.

Baadaye, ndugu Mwitalia akaja kufanya kazi katika jiji la bandari na ambalo pia ni jiji kuu, Mogadishu, kwa kondrati ya ujenzi. Ujuzi wowote ambao alikosa, ulisawazishwa na idili. Hakujali kusema habari njema kwa yeyote ambaye angekutana naye, kutia ndani na Waislamu. Miongoni mwa Waislamu, mtu mmoja wa makamu alisikiliza kwa makini. Akaona nuru ya kweli. Kwa vile mtu huyo alikuwa amesafiri sana, alikuwa na akili iliyofunguka naye akakubali funzo la Biblia. Muda wa kukaa nchini kwa sababu ya ile kazi ukaisha na hivyo ikambidi ndugu yule aondoke. Hata hivyo, familia moja ya Waitalia ilihamia Somalia, nao wakaendelea kumsaidia mtu huyo aliyependezwa.

Kisha mwanamke aliyekuwa amependezwa na kweli akiwa Ulaya alirudi Somalia pamoja na mume wake. Akatatufa Mashahidi. Hivyo, kutaniko dogo likaanzishwa. Mikutano ilifanywa, na hata kukawa na ziara za mwangalizi wa mzunguko. Hatimaye, mwanamke huyo alibatizwa mwaka wa 1987. Alikuwa na shangwe sana. Ilikuwa imemchukua miaka mingi kufikia hatua hiyo. Kwa sababu ya kusafiri kwake nchi moja baada ya nyingine na kulazimika kujifunza lugha mpya kila wakati, kulipunguza maendeleo yake ya kiroho, lakini sasa hakuna chochote ambacho kingeweza kumzuia. Upesi alikuwa anaongoza mafunzo ya Biblia na watu wengine na alishangilia sana wakati wenzi wa ndoa walipojiunga naye katika kumsifu Mungu. Mke huyo akawa Shahidi wa kwanza Msomali.

Kwa kusikitisha, hali ya uchumi na usalama wa nchi hiyo ikawa mbaya sana hivi kwamba wageni wengi na hata wenyeji waliondoka nchini. Kufikia mwisho wa 1990, wahubiri wote walikuwa wameenda pia. Jambo hilo labda lilikuwa na uongozi wa kimungu, kwa sababu vita ya wenyewe kwa wenyewe ya 1991 iliharibu nchi hiyo, watu wakiuawa ovyoovyo mjini Mogadishu.

Mapinduzi hayakukumba Somalia pekee. Karibu miongo miwili mapema, dhoruba za vita ya wenyewe kwa wenyewe ilikuwa ikiendelea Ethiopia.

Mapinduzi Katika Ethiopia

Ile milki ya kihistoria ya Ethiopia ilianguka mwaka wa 1974. Wanajeshi walinyakua mamlaka kutoka kwa maliki aliyezeeka na kuanzisha marekebisho mengi wakiwa na tamaa ya kuendeleza mawazo yao mapya. Kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yao, vijana hao wa mapinduzi waliona uwezo unaotoka kwa silaha zinazoweza kuua mara hiyo. Kafyu ziliwekwa, shime zilisemwa, kama vile “Ethiopia Kwanza!” Na Upinzani wowote wa kisiasa haukuvumiliwa.

Matukio hayo yalitukia wakati ambapo kulikuwa na maendeleo mazuri kwa watu wa Yehova nchini Ethiopia. Kilele cha wahubiri 1,844 kilifikiwa mwaka wa 1974, na kitabu Kweli kilikuwa kimetafsiriwa katika Kiamhara. Hudhurio la Ukumbusho lilikuwa limefikia 3,136. Kazi ya kutoa ushahidi ilikuwa imeenea katika mikoa yote ya Ethiopia kwa mara ya kwanza, kwa msaada wa mapainia wa pekee wapya waliokuwa wamewekwa. Lakini bado ulikuwa ni wakati wa hali tofauti. Makutaniko mengine yangeweza kukutana waziwazi, na katika sehemu nyinginezo mapainia wa pekee walitiwa gerezani.

Vita vya kuvizia viliendelea katika mkoa wa kaskazini wa Eritrea. Kutaniko lililokuwa mjini Cheren (Keren) lilikuwa limetengwa na ulimwengu wa nje. Hakukuwa na maji, chakula, wala umeme. Ukumbusho wa kifo cha Kristo, ambao hauwezi kufanywa hadi jua litue ungeweza kuadhimishwaje kukiwa na kafyu ya usiku kucha? Mwadhimisho huo wa kidini ukawa tukio lisilo la kawaida, kwa vile ilikuwa ni lazima Mashahidi wote wafike mapema, kabla ya jua kushuka, na kisha wajitayarishe kulala hapo mahali pa mkutano mpaka kafyu iondolewe asubuhi. Ulikuwa ni usiku wa ushirika mzuri kama nini!

Mambo mengine mazuri yalifuata kwa ajili ya Mashahidi. Shule ya Huduma ya Ufalme ilifanywa mara ya kwanza katika 1975 baada ya miaka tisa ili inufaishe wazee wa kutaniko wa Ethiopia. Programu ya kusanyiko la mzunguko ilitolewa kwa watu zaidi ya 2,000. Cheti cha ruhusa kilitolewa kikiidhinisha fasihi zetu ziingie nchini. Shehena ya tani saba, kutia ndani vitabu 40,000 vilifika Addis Ababa kutoka ng’ambo. Katika mwaka uliofuata wa 1976, jiji la Asmara lilitulia isivyo kawaida kutokana na vita vya kuvizia, na hivyo kuruhusu Shule ya Huduma ya Ufalme ifanywe. Mashahidi wa hapo waliripoti kwamba baada tu ya shule kwisha, mifyatuo na milipuko ya roketi ilianza upya.

Mnyanyaso wa Ukatili!

Mabadiliko mabaya zaidi yalikuwa yakija kwa Mashahidi. Mapema katika mwaka wa 1976, mamlaka ilitoa tangazo dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Karibu na katikati ya mwaka huo, Kampeni ya Mnyanyaso wa Ukatili ilianzishwa dhidi ya maadui wa mapinduzi. Waabudu wa Yehova wakawa shabaha pia. Walishtakiwa kimakosa kuwa maadui. Wakaanza kushikwa.

Ni lazima Kanisa Orthodoksi la Ethiopia liwe lilifurahi kama nini! Walitumia hali hiyo ili kushambulia Mashahidi. Katika kusini mwa jiji kuu, katika mji mdogo wa Mojo, makasisi walichochea umati wenye ghasia wa zaidi ya watu 600 kushambulia na kuua Mashahidi, lakini polisi walizuia wasifanye madhara mabaya. Utendaji wa umati wenye ghasia kama huo ulitokea katika Bahir Dar vilevile, katika chanzo cha Mto Naili Buluu.

Nyumba zilipekuliwa kikamilifu isivyopata kufanywa kotekote nchini. Hata mashamba yalilimwa na vibao vya sakafu kutolewa katika jitihada za kutafuta vichapo vya Biblia, taipureta, na vifaa vingine vinavyohusiana.

Katika Asmara, polisi walimsimamisha painia wa pekee aliyekuwa ametoka mashambani kulikojaa wapiganaji wa kuvizia. Walimpekua na kupata fomu yake ya ripoti ya utumishi wa shambani. Katika fomu hiyo kulikuwa na ufupisho wa maandishi ya mkono yaliyowafanya washuku sana. Kisha wakamlazimisha painia huyo awapeleke kwa mwangalizi wa jiji, Gebregziabher Woldetnsae. Wakitumaini kumshika kiongozi wa vita vya kuvizia, malori kadhaa yaliyojaa wanajeshi yalipelekwa mahali pa kazi pa Ndugu Gebregziabher. * Walizingira ofisi yake na kisha kuivamia bunduki zao zikiwa tayari. Walimwita Ndugu Gebregziabher, wakamshika na kwenda naye. Wafanyakazi wenzi walijua kwamba hawangemwona tena.

Wanajeshi walimhoji Ndugu Gebregziabher katika makao makuu ya wanajeshi. Alijibu maswali yao waziwazi, akitoa ushahidi juu ya kazi yetu ya kuhubiri na kueleza yale mafupisho ya maneno “mag, zk, Maf. B.”, na kadhalika. Yalikuwa tu maandishi yasiyo na madhara yanayoonyesha yale ambayo painia wa pekee huyo alikuwa ametimiza shambani mwezi huo, yaani magazeti aliyokuwa ameangusha, ziara za kurudia alizokuwa amefanya, na mafunzo ya Biblia aliyokuwa ameongoza. Walimwuliza mfululizo wa maswali: “Nini! Unamaanisha mambo hayo hayahusiani na silaha, risasi? Ni nani anaweza kuamini hayo? Kwa sababu gani maneno ya fumbo yametumiwa?”

Unyofu na hali ya kushirikiana ya Ndugu Gebregziabher iliwavutia ingawa bado walikuwa na shaka. Hatimaye ofisa mkuu akamwuliza hivi: “Tunaweza kuhakikishaje kwamba kwa kweli wewe ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova?” Ndugu huyo akatafuta ndani ya vitu vyake lakini hakupata chochote kinachoweza kumtambulisha vizuri kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Lakini ebu ngoja kidogo!—alikuwa na kadi iliyoandikwa maneno haya: “Usinitie Damu” miongoni mwa vitu vyake vingine. Ofisa mkuu alipoona hiyo akasema: “Naam, hiyo inathibitisha. Waweza kwenda.” Ndugu yetu aliporudi ofisini, wafanyakazi wenzake walifikiri alikuwa amefufuliwa!

Mambo Yasiyotazamiwa Yatokea

Katika Asmara idadi fulani ya akina ndugu walikuwa wamekusanyika katika nyumba fulani. Kikundi cha vijana wakapeleleza hapo na kuarifu polisi mara moja juu ya mahali hapo pa mkutano. Walieleza kwamba kulikuwa na nyumba mbili na kwamba kulikuwa na msichana akicheza mbele ya nyumba moja. Hiyo ilikuwa ndiyo nyumba ambayo ndani yake Mashahidi walikuwa wanakutania!

Polisi wakaondoka kutafuta Mashahidi. Kumbe wakati huo yule msichana alikuwa ametoka pale. Alienda kucheza mbele ya nyumba ile nyingine. Polisi wakavamia nyumba hiyo na kupata tu kikundi kidogo cha watu katika kikao cha familia. Polisi wakaona aibu na kurudi kwenye kituo chao huku wakiwa wamekasirikia wale vijana wakiamini kwamba walikuwa wamewadanganya.

Hali ya kisiasa na ya kijamii haikuwa nzuri kwa Mashahidi. Watu walitiwa moyo warudie kusema shime za kisiasa, washiriki katika kupiga kura, na kuchanga fedha, chakula, na vifaa vya kusaidia vita. Lakini katikati ya mambo hayo, fasihi ya thamani kutoka ng’ambo iliingia nchini Ethiopia bila kutambuliwa kwa msaada wa ndugu wajasiri.

Wachungaji Wenye Kujidhabihu

Wapiganaji wa kuvizia walikuwa wametenga makutaniko kadhaa katika Eritrea na ulimwengu wa nje. Na bado kulikuwa na wachungaji wenye upendo wa kutia moyo akina ndugu huko. Mwangalizi mmoja wa mzunguko alipanga kusafiri kilometa 92 hadi Cheren akisafiri na msafara wa magari ya kusafirisha bidhaa. Ebu wazia akiwa miongoni mwa malori 100 yanayolindwa na vifaru 5 vya kijeshi na magari mengine 30 ya ulinzi ya kijeshi.

Vita vikali vikazuka njiani, huku wapiganaji wa kuvizia wakizingira msafara huo. Washambulizi hao walitaka kuchukua bidhaa zote kama vile walivyokuwa wamefanya mbeleni. Baada ya nusu saa ya vita vikali, msafara huo ukapata nafasi ya kutokea nao ukaponyoka. Hivyo, yule mwangalizi wa mzunguko aliweza kuzuru makutaniko hayo yaliyo peke yayo na kujenga akina ndugu.

Hata hivyo, hakukuwa na msafara wowote wala njia nyingine ya usafiri wakati wa kurudi kwa huyo mwangalizi wa mzunguko. Njia pekee ya kurudi ilikuwa ni kutembea mwendo wote. Jambo hilo lilikuwa hatari sana. Alitembea siku tatu kutia ndani na kutembea usiku wote.

Wahubiri fulani kutia ndani na wengine wenye madaraka walijitenga na ushirika wakati huo wa mchafuko wa kuogofya. Wengine wakawa wasiotenda, na bado wengine wakatoroka kutoka nchi. Kukawa na mshuko kwa idadi ya wahubiri.

Kufikia 1979, kulikuwa ndugu 80 gerezani kwa sababu ya msimamo wao wa kutokuwamo. Katika mwezi wa Aprili wa mwaka huo, mwangalizi wa jiji la Asmara, Gebregziabher Woldetnsae, kwa msiba, aliuawa katika aksidenti alipokuwa akienda kuzuru akina ndugu katika sehemu za mashambani zenye mchafuko. Zijapokuwa habari hizo zote za kuhuzunisha, wale waliovumilia kwa uaminifu hawakukosa kuona utegemezo wenye upendo wa Yehova.

Kupepeta na Kutahini Zaidi Imani

Wakati sehemu ya kwanza ya mapinduzi ilipokuwa imekwisha na nchi ikaanza kutulia, wananchi waliona ni kama wako katika hali tupu ya kiroho. Walijionea wenyewe makanisa yakiridhiana na kuona kuungwa mkono kwa makanisa kukiisha. Baadhi ya Mashahidi pia wakawa wasiosawazika kiroho. Ilikuwa ni uchungu, ingawa ilikuwa ni lazima, kuona wazee na watumishi wa huduma 23 wakipoteza mapendeleo yao ya utumishi katika mwaka wa 1981. Walikuwa wamekuwa wasio wa kawaida katika huduma yao ya shambani. Yakafuata mabadiliko ya makutaniko, na kwa furaha wengi zaidi wa wale waliopoteza mapendeleo yao ya kutaniko waliyapata tena.

Mitihani mingine, kutia ndani pindi za ukosefu mkubwa wa chakula ilifuata. Kwa hakika, miaka mingi ya jaribu imetokeza imani thabiti, iliyotahiniwa kwa ndugu Waethiopia.—1 Pet. 1:6, 7.

Sudan—Ukuzi Chini ya Magumu

Ilikuwa imechukua miaka miwili, kutokea Agosti 1974 hadi 1976, kufikia kilele kipya cha wahubiri 101 nchini Sudan. Ulikuwa ni wakati wenye wasiwasi mwingi. Majaribio ya mapinduzi ya serikali yalikuwa mengi, na kushukiwa kisiasa kulikuwa kwingi. Wahubiri na wazee walihojiwa na polisi nyakati nyingine. Magumu ya kiuchumi, bei za bidhaa zilizopanda na ukosefu wa bidhaa ulisababisha mahangaiko ya vitu vya kimwili na kunasa wengi. Hivyo, ukuzi wa idadi ya wahubiri ukawa wa pole. Kilele kilikuwa 102 tu kufikia Aprili 1981.

Matatizo mawili yalifanya ziara za kawaida za waangalizi wa mzunguko kwa makutaniko ya upande wa kusini ziwe ngumu: Vita vya kuvizia au ukosefu wa mafuta, ambao ungeweza kutatiza usafiri wakati wowote ule, na matatizo ya njia ya kusafiri. Ingeweza kutia ndani kujipenyeza nyuma ya lori lililojaa watu na kurushwa-rushwa huku na huku kwa siku nzima kwa sababu ya hali ya barabara au kusafiri kwa mwendo wa pole sana wa kilometa 10 kwa saa ndani ya gari la moshi lililojaa, likiwa na abiria wawili kwa kila kiti na maskwota wakikaa juu ya mabehewa. Kusafiri kwa ndege hakukuwa jambo rahisi pia. Kungeweza kumaanisha kungoja kwa juma nzima ndipo ndege iwasili, na kisha kujulishwa tu kwamba ndege itaondoka kwa muda unaopungua saa moja. Lakini jinsi makutaniko yalivyothamini ziara za waangalizi wa mzunguko! Shangwe yao na ukaribishaji wao hata hauelezeki.

Roho ya upainia iliamshwa katika 1982. Hilo likatokeza baraka nyingi sana. Idadi ya mapainia ikaongezeka kutoka 7 hadi 86 katika muda wa miaka mitano. Katika mwezi mmoja, asilimia 39 ya wahubiri wote walikuwa katika utumishi wa wakati wote, na mwezi huo ndio uliokuwa mojawapo miezi yenye joto zaidi katika mwaka, wastani wa joto la adhuhuri ukiwa zaidi ya sentigredi 40. Zaidi ya wahubiri 300 walikuwa watendaji kufikia mwaka wa 1987, na karibu 1,000 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo. Wahubiri wa kutaniko wakawa wanafikia wastani wa saa 20 kila mwezi katika huduma ya shambani.

Wengi wa ndugu vijana walifanya maendeleo ya kiroho ya haraka na kustahili kuwa watumishi wa huduma na baadaye kuwa wazee, jambo lililoongezea makutaniko nguvu zaidi. Hatimaye, katika 1987, kutaniko lilianzishwa ng’ambo ya Naili katika mji wa kihistoria wa Omdurman. Kutaniko hilo lilikuwa na eneo la watu milioni moja. Kikundi cha Mashahidi kikachipuka pia katika jiji la Port Sudan.

Hata hivyo, ukuzi mwingi ulitoka kwa watu wa kusini waliokuwa warefu, weusi, wenye afya na ambao mara nyingi huwa na alama nyingi zilizochanjwa na mapambo mengine usoni au mwilini. Wasudani wa kaskazini au wale wa jadi ya Wamisri wamekubali kweli pia, na wakimbizi wengi wameona nuru ya tumaini la Mungu kwa ainabinadamu. Vikundi vyote vimeonyesha bidii na uvumilivu katika utumishi wa Yehova. Kazi ya kutoa ushahidi mara nyingi huhitaji kutembea mwendo mrefu chini ya jua kali sana. Inabidi kutumia mbinu katika kupanga mikutano, kwa sababu kazi bado haijatambuliwa kisheria.

Kuonja Mkate wa Uhai wa Mungu

Katika 1983, Waislamu wenye siasa kali walianzisha Shari‛a, sheria ya Uislamu, nchini Sudan. Maadui wa watu wa Yehova walitumia hali hiyo ya kidini kukazia fikira Mashahidi, ambao sasa iliwabidi wafanye mikutano yao ya kutaniko katika vikundi vidogo zaidi.

Katika miaka ya hivi karibuni, ukame mkubwa uliotangazwa sana ulipiga eneo kubwa la Sahel ya Afrika, kutia na Sudan. Ukame huo ulitokea wakati ambapo vita ya wenyewe kwa wenyewe ilipofyatuka tena, ukileta njaa kali na kuteseka kwingi. Lakini ukame huo ulitokeza pia hali nyingine yenye kupendeza: Vijana wengi walihamia jiji kuu kutoka maeneo ya mbali sana ya Sudan. Huko jijini walipata kuonja Mkate wa Uhai wa Mungu, ambao huenda hawangalipata katika maeneo yao ya mbali ya hapo awali. (Yn. 6:35) Jambo hilo liliongezea mwendo wa ukuzi.

Njaa Kali ya Kimwili, Lakini Utele wa Kiroho

Katika 1988, hali ya hewa isiyo ya kawaida ilileta mvua kubwa sana katika eneo la Khartoum, ikiacha maelfu ya watu bila makao na kuua wengine. Mashahidi wengi na watoto wao waliathiriwa vibaya sana. Baba mmoja alisimama nje katika giza tititi, akiwa amenyanyua mtoto wake juu katika mvua kubwa huku maji yakizidi kupanda kufikia nyonga zake. Nguzo za umeme zilianguka, nyumba za matope zilianguka, na choo zilizochimbwa za nje zilianguka zikiacha mashimo marefu yaliyofunikwa na maji yaliyochafuliwa. Barabara zilifurika maji, zikisababisha sehemu za mjini zisiweze kufikika. Magari yalikwama katika matope mengi bila tumaini la kuondolewa. Ilichukua siku nyingi kabla ya “maziwa ya maji” mapya kukauka.

Wazee wenye kujali walikuwa wenye bidii chini ya hali hizo. Mara hiyo waliwasiliana na kondoo zao waliokuwa wakiteseka. Mipango ya msaada ikaanzishwa upesi. Baraza Linaloongoza lilihakikisha kwamba maandalizi ya ziada yalifanywa. Na kwa kustaajabisha, chini ya magumu hayo yote, huduma ya shambani iliendelea kuwa juu.

Dhoruba ya aina nyingine ikatokea pia kote katika Sudan. Mapinduzi ya serikali yalileta serikali mpya na umashuhuri mpya kwa jumuiya ya Kiislamu. Vita ya wenyewe kwa wenyewe yenye kuendelea, ukame mwingi, na vizuizi vya kuingiza vitu nchini viliathiri sana uchumi. Njaa kali bado huua watu katika majiji makubwa.

Wengi walipotoroka njaa kali na vita, idadi ya watu ikazidi kuongezeka kufikia zaidi ya robo milioni katika Juba, mji mkuu wa kusini. Ingawa hivyo, wapiganaji wa kuvizia nao wakazidi kushikilia Juba. Hivyo, kwa vipindi virefu vya wakati, mawasiliano ya mji huo na ulimwengu wa nje yalikatizwa. Misaada kwa akina ndugu mara nyingi huwafikia kwa wakati ufaao kabisa, kabla tu ya ugavi wao kwisha kabisa.

Na bado, mazoezi kwa mapainia waliokuwa wakiongezeka yaliendelea, kutia na ushirika wa kawaida wa kiroho. Ugavi wa chakula cha kiroho haukuisha. Kadiri kweli ilipozidi kuenea ndani zaidi na zaidi kusini, vikundi vipya na makutaniko nayo yakazidi kutokea katika mji baada ya mji.

Kujapokuwa na mikazo hiyo yote, mambo fulani ya kushangaza yalitukia katika 1990. Kwanza, mkoa mmoja wa kusini ulitoa utambulisho wa kisheria kwa Mashahidi wa Yehova.

Ushahidi Ukitolewa na Mtu Asiyekuwa Shahidi

Kisha, mnamo Novemba 2, mhadhiri Mwislamu anayejulikana kimataifa, alitoa hotuba nzuri sana juu ya Mashahidi wa Yehova kwa kikundi kikubwa cha maofisa wa serikali waliokuwa wamehudhuria semina. Aliwaeleza imani zetu, kutokuwamo kwetu katika mambo ya kisiasa, jitihada zetu za kufundisha umma, na manufaa ya kazi yetu kwa jumuiya yote. Isitoshe, hotuba yake yote ilitangazwa katika televisheni Jumapili iliyofuata, hivyo ushahidi ukitolewa kwa aina zote za watu na kwa upana mkubwa zaidi. Matokeo ya ushahidi huo mkuu yalikuwa nini? Wengi walisema vizuri juu yao, kuelewa vibaya kukaisha, na kupendezwa zaidi kuelekea kweli kukatokea. Hata maofisa wa serikali walitiwa moyo waige ile roho ya kujidhabihu inayoonekana katika Mashahidi wa Yehova.

Kwa kweli Mashahidi katika Sudan wanaendelea kutafuta Ufalme wa Mungu kwanza na kwa furaha kila mhubiri hutumia karibu saa 20 katika huduma ya shambani kila mwezi. Kwa hiyo, zijapokuwa dhiki nyingi, kutia njaa kali yenye kuendelea, kweli ya Ufalme wa Mungu kuwa ndio suluhisho pekee la kudumu kwa matatizo ya wanadamu inaendelea kuhubiriwa nchini Sudan zaidi ya wakati mwingine wowote.

Yemen—Njia ya Uvumba

Katika miaka ya hivi karibuni, dada mmoja aliyejitoa sana kutoka Sudan alikuwa na fursa isiyo ya kawaida ya kuangaza nuru yake katika nchi hii iliyo peke yake ya Yemen, nchi ambayo iko katika pembe ya kusini-magharibi mwa Peninsula ya Uarabu. Katika siku za Mfalme Sulemani mwenye hekima, njia ya misafara ya uvumba ilianzia huko, na kupitia ile iliyokuwa labda ndiyo milki ya malkia wa Sheba. Sasa, pamoja na dada yetu Msudani, kulikuwa na Mashahidi wengine wachache waliokuwa wameenda Yemen kikazi. Kwa msaada wa Yehova waliweza kukutana. Walihubiria wengine kuhusu imani yao kwa njia ya busara na hata wakapata watu waliotaka kujifunza Biblia.

Uislamu ungali una nguvu sana katika eneo hili la milima-milima, ambako desturi za kale bado zinafuatwa. Wanawake wengi hujifunika kabisa kwa utaji, na wanaume wengi huonyesha kwa fahari sime katika mishipi yao. Ilisikitisha kusikia kwamba ndugu mmoja wa makamo kutoka Afrika aliyekuwa na afya nzuri alikufa ghafula jioni moja. Kilichosababisha kifo chake hakikujulikana. Lakini kazi ya kuhubiri yaendelea.

Katika mwaka wa 1986, Ukumbusho wa kifo cha Kristo ulihudhuriwa na watu 15. Tangu wakati huo, baadhi yao wameondoka nchini. Hivyo, ripoti za huduma ya shambani na za mikutano zimekuwa chache, lakini mikutano inaendelea kufanywa. Dada mmoja kutoka nchi nyingine, ingawa yuko mbali na wahubiri wengine, anaongoza mafunzo ya Biblia kadhaa. Hivyo, kwa utimizo wa Mathayo 24:14, hata katika nchi hii ushahidi fulani unatolewa.

Ng’ambo tu ya Yemen, kuvuka Bahari Nyekundu, kuna nchi ambayo kutoa ushahidi kulikuja kuwa jambo la kufa au kupona katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1970.

Washika Ukamilifu Katika Ethiopia

Upinzani wa Serikali ukawa mkali sana katika Ethiopia. Wenye mamlaka waliwapa Mashahidi wawili hukumu ya kifo, lakini hawakuuawa. Mashahidi wamekazwa waende kinyume cha dhamiri zao, wanyanyasi wao hata wakishindilia bunduki vichwani mwao.

Mikazo ya kiuchumi karibu ilete utimizo halisi wa unabii wa Ufunuo unaosema kwamba “mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.” (Ufu. 13:17) Biblia zikawa zinapatikana kwa shida. Serikali ikazidi kuwa na uthibiti wa maisha za watu. Viza zilihitajika ndipo mtu asafiri sehemu za ndani za nchi. Wanaume, wanawake, na watoto walipangwa katika vyama vya kisiasa.

Katika Machi 1978, Wubie Ayele alipigwa hadi kufa kwa sababu alishikilia kanuni za Kimaandiko. Katika miezi iliyofuata, Ayele Zelelew, aliyekuwa painia na pia mzee, na Hailu Yemiru, aliyekuwa mhubiri, waliuawa na miili yao ikaachwa katika barabara ya Addis Ababa siku nzima, ili wote waweze kuona.

Mikazo iliendelea. Matangazo ya redio, magazeti, na polisi waliwashambulia Mashahidi. Kulikuwa na nyakati ambazo ndugu zaidi ya mia moja walikuwa gerezani. Wengine waliachiliwa, kutia ndani wale ambao walikuwa wamekaa gerezani miaka miwili na nusu chini ya mateso makali. Idadi fulani hata walikuwa wamekuwa mapainia wasaidizi gerezani!

Kisha mpango mkatili ukabuniwa—kufutilia mbali Mashahidi wa Yehova. Mashahidi wengine walipopata kujua jambo hilo, woga wa mwanadamu ukawashinda. Kwa kuongezea hayo, kulikuwa na magumu ya kiuchumi; kukawa na uhaba wa nyama na nafaka, kutia na tairi za magari, petroli, na vitu vingine vya lazima.

Zaidi ya Mashahidi mia moja waliendelea kuwa waaminifu hata baada ya kupoteza kazi zao—jaribu kwelikweli kwa imani za wanaume ambao walikuwa na familia kubwa za kulisha. Lakini ilichangamsha moyo kama nini kuona Mashahidi wenye kazi wakisaidia kiuchumi wale waliokuwa na uhitaji, wonyesho wa upendo kwa kuiga Wakristo wa mapema! (Mdo. 4:32) Katika hali hizo zote za kuogofya, Mashahidi walihitaji uongozi zaidi wa kiroho na kitia-moyo, na huo ulitolewa chini ya mwelekezo wa Yehova.

Wenye Moyo Mkuu Daima

Kushikwa kwingi na kuhukumiwa kuliendelea kama jipu lenye kutunga usaha. Painia wa pekee mmoja ameshikwa mara 15 tangu mwaka wa 1972. Watoto wenye umri wa miaka 14 walitiwa gerezani pia, wengine wakikaa humo zaidi ya miaka 4. Hawakuridhiana! Kisha kukaja kuandikishwa kwa jeshi. Sasa hata wanawake vijana walitiwa ndani. Mashahidi wengi walitumia wakati wao katika jela wakitumikia wakiwa mapainia wasaidizi, wakiwasaidia wafungwa wengine kujifunza kweli ya Biblia. Dada mmoja alikubaliwa kuondoka jela kwa muda mfupi ili ajifungue mtoto na baadaye alilazimika kurudi katika chumba chake cha gereza.

Ndugu mmoja mwenye moyo mkuu alikuwa akisafiri kwa gari kwenda sehemu za mashambani wakati alipong’amua ghafula kwamba alikuwa amesahau kuficha furushi la fasihi ya Biblia lililofungwa kwa karatasi. Lilikuwa katika dashbodi ya gari, mahali palipo wazi. Alisali apate mahali pafaapo pa kulificha, lakini hapakuwapo mahali pa kutosha furushi hilo kubwa. Ilimbidi aliache mahali lilipokuwa akimtumaini Yehova. Ebu wazia jinsi alivyoshangaa wakati ambapo alipita vituo tisa vya kupekua magari, vingine vikiwa na upekuzi mkali wa magari, na bado hakuna hata ofisa mmoja aliyeshuku furushi lile!

Katika Desemba 1982, Mashahidi sita walishikwa kwa sababu ya hali yao ya kutokuwamo kwa Kikristo. Wao pia walikuwa watu wenye moyo mkuu na walisaidia wafungwa wengi wenzao kupata tumaini la Ufalme. Baada ya miaka mitatu, waliondolewa gerezani na kutoweka kabisa. Wote waliuawa.

Katika Dese, sehemu ya kaskazini ya kati ya nchi hiyo, Demas Amde, mwalimu mmoja wa shule aliyekuwa baba ya watoto watano alifungwa gerezani miaka mitano ya mateso makali: Kwanza, kazi ngumu; kisha miezi sita ya kifungo cha upweke akiwa amefungwa hali ameinama, kikifuatwa na ugonjwa bila tiba; kisha, akaachwa uchi kwa miezi miwili, akiwa ameambukiwa chawa; baada ya hapo alihamishwa kupelekwa katika chumba ambamo wafungwa wengine walikaribia kufa kwa ambukizo la homa ya matumbo. Hatimaye, alifunguliwa ili akafie nyumbani baada ya afya yake na mwili wake kuharibiwa vibaya sana na kansa. Alikufa, mnamo Februari 4, 1991, akiwa mwaminifu hadi mwisho na akiwa na tumaini thabiti la ufufuo.—Linganisha Waebrania 11:37-40.

Mashahidi wengine walipona. Ndugu mmoja aliyekuwa akisafiri kwenda sehemu za mashambani alishukiwa kuwa mmoja wa wapiganaji wa kuvizia na akashikwa. Hangeweza kunyamaza na ingawa alijihatarisha sana, alijulisha wazi kwamba yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Hakuna mtu aliyemwamini na hivyo akatupwa gerezani pamoja na wafungwa wengine.

Alifanyaje usiku huo? Badala ya kulalamikia hali mbaya iliyompata, alitwaa fursa ya kutangaza habari njema kwa wengine. Jinsi alivyoshangaa asubuhi kuona wafungwa wenzake wakitolewa nje na kuhojiwa. “Ni mtu wa aina gani tuliweka katika chumba chenu usiku wa jana?” Maofisa hao wakauliza.

“Ah, wamaanisha yule aliyetuhubiria usiku kucha, akitufanya tusilale?” wao wakajibu. Ilikuwa ni rahisi kwa maofisa hao kuona kwamba mtu huyo kwa kweli alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Kujulisha kwake imani peupe kulimfungulia milango ya jela; akaachiliwa huru!

Katika sehemu ya kusini ya nchi, mtu aliyependezwa alivumilia kifungo cha jela kwa zaidi ya miaka minne. Miguu yake ilifungwa kwa minyororo katika mwaka wa kwanza; akatumia miezi sita katika kifungo cha upweke. Wakati vitu vyake vya kibinafsi viliporudishwa kwa watu wake wa ukoo, wao walidhani kuwa ameuawa. Alipewa chakula kidogo sana na katika hali hiyo ya kudhoofika kimwili, alikatiwa adhabu ya kifo. Lakini adhabu hiyo iliondolewa na maofisa wa juu zaidi.

Nyakati nyingine malaya waliletwa chumbani mwake ili wamshawishi. Miaka mitatu baadaye, alitiwa moyo alipoweza kushiriki imani yake na mtu mwingine aliyependezwa, ambaye alikuwa mfungwa mwenzake. Hakukuwa na tumaini lolote la kufunguliwa kwake. Siku moja, kwa mshangao wake mkubwa sana, aliambiwa kwamba alikuwa huru! Hatimaye, alikuwa na fursa sasa ya kuonyesha wakfu wake kwa Yehova kwa ubatizo!

Ahukumiwa Kifo Mara Nane!

Katika Debre Zeit, mji ulio karibu na eneo la kati la Ethiopia, painia mmoja, Worku Abebe, alishikwa kwa sababu ya msimamo wake wa kutokuwamo. Hukumu—kuuawa usiku uo huo. Hata hivyo, kabla ya kuuawa, ndugu na dada wengine 20 wakashikwa katika mji uliokuwa karibu. Wenye mamlaka waliamini kwamba hao 20 wangekana imani yao iwapo wangemwona Ndugu Worku akiuawa. (Maofisa waliamini kwamba yeye ndiye aliyekuwa “kiongozi.”) Hivyo maofisa katika mji huo wa karibu walitaka wapewe Ndugu Worku ili wamuue huko.

Uhamisho huo wa jela ulimwezesha Ndugu Worku kueleza imani yake mbele ya watu 300. Akitumia vizuri ile desturi ya huko kwamba mtu asikatizwe anapoongea, Ndugu Worku alitumia saa nne kueleza hadithi yake, akisimulia historia ya Mashahidi wa Yehova tokea Habili kufika wakati wetu huu. Alipomaliza, ofisa mmoja alisema hivi: “Huyu mtu asiwekwe pamoja na wengine. Karibu anisadikishe!”

Jioni moja, askari-jela walimchukua pamoja na wafungwa wengine Mashahidi hadi kando ya mto ili wauawe. Wakielekeza bunduki zao kwa Mashahidi hao, waliuliza hivi: “Mtakana imani yenu au la?” Mashahidi hao wakajibu pamoja, kwa sauti isiyokuwa na shaka kwamba hawangeweza kamwe kumkana Yehova. Hawakuuawa; bali walianza kupigwa vibaya sana kwa muda wa saa nyingi. “Mapigo yalikuwa machungu sana hivi kwamba tuliwasihi watuue badala ya kutupiga, lakini hawakuacha kutupiga,” akina ndugu wakasema.

Kisha, Ndugu Worku akateuliwa auawe peke yake. Risasi moja ikafyatuka. Akapumbaa kwa muda. Hakuanguka wala kujeruhiwa. Kisha akafahamu—ile risasi haikumpiga. Wanyanyasi hawakukawia. Walimpiga kwa ukatili kwa tako la bunduki. Alianguka akazirai naye akarudishwa katika seli yake.

Kule gerezani, walinzi wakapokea maagizo ya kwamba wahakikishe Mashahidi wote wamekana imani yao usiku huo. Upesi milio ya bunduki ikasikika katika vyumba vya gereza. Mashahidi waliambiwa hivi: “Mlisikia milio hiyo ya bunduki? Naam, ndugu zenu wameuawa. Kesho mtaona maiti zao barabarani. Na msipokana imani zenu, nyinyi mtauawa vilevile.”

Mashahidi hao wakajibu hivi: “Kikombe walichokinywea ndugu zetu, sisi nasi tuna nia ya kukinywea.”

Usiku huo, walinzi walianza kumpiga Ndugu Worku na Mashahidi wengine kwa kutumia fimbo. Mlinzi mmoja mjeuri sana alifunga mikono ya Ndugu Worku kwa kukaza sana hivi kwamba ngozi ya vidole vyake ilipasuka na damu ikaanza kutiririka. Ndugu Worku alificha vidole vyake vilivyokatwa-katwa ili ndugu wengine wasivunjike moyo. Mambo yalipotulia kidogo, Mashahidi hao walisali kabla ya kulala. Lakini kufikia saa saba za usiku, wanyanyasi wenye ghadhabu waliingia mbio na kuwapiga sana hadi saa kumi za usiku. Baada ya hilo Mashahidi hao walisali tena, wakimshukuru Yehova kwa ajili ya uwezo wake na kumwomba aendelee kuwategemeza.

Wanyanyasi wengine zaidi walikuja gerezani asubuhi. Hao walianza kuwapiga mateke Mashahidi. Alasiri hiyo, Ndugu Worku aliteuliwa tena, na jumla ya watu 20 wakampiga na kumkanyagia chini. Na bado hakukana imani yake. Ikaamuliwa tena kwamba auawe. Walinzi wengine 20 walikuja saa 4:00 za usiku na kumpiga hadi saa 8:00 za usiku. Mtesi mmoja alikuwa na ghadhabu sana hivi kwamba alishika Shahidi mwingine aliyekuwa nyuma yake na kumwuma kikatili, akimwacha Shahidi huyo na alama yenye kudumu. Mashahidi hao walifungwa katika chumba chenye giza kwa siku nne bila chakula wala maji na walipigwa tena na tena. Wote walikuwa wamevunjika mifupa mbalimbali ya mwili, kutia ndani mbavu na fuvu la kichwa. Wakawa dhaifu sana kimwili.

Ofisa mmoja mkuu alipozuru gereza hilo, aliwahurumia alipoona hali yao na kuamuru kwamba wapewe chakula. Hata hivyo, mlinzi mmoja, yule mjeuri zaidi, alikasirika kuona kwamba Mashahidi wanapewa chakula na kinywaji. Alitunga hila na kuwashtaki Mashahidi kwamba walikuwa wanataka kutoroka. Wakuu waliamini hila yake, hivyo wakafanya mpango mwingine wa kuwaua Mashahidi. Akina ndugu walisali kwa bidii waokolewe, hasa kwa sababu ya mashtaka hayo ya aibu na ya uwongo. Ofisa mmoja mkuu zaidi alizuia wasiuawe, lakini akina ndugu walipigwa kwa fimbo usiku kucha.

Baada ya siku chache, ofisa mwingine alikuja akitangaza kwamba Ndugu Worku angeuawa na wengine waachiliwe. Kwa kushangaza, ndugu hao hawakuachiliwa tu bali Ndugu Worku aliambiwa siku chache baadaye kwamba angeweza kwenda pia.

Mara hiyo alichukua fursa ya kukutana na kuwatia moyo ndugu wengine katika nyumba moja ya mtu binafsi. Hakujua kwamba alikuwa amefuatwa na kuripotiwa. Kwa hiyo siku iliyofuata, alishikwa na kuhukumiwa kifo.

Jaribio jingine tena lilifanywa la kumdanganya ili akane imani yake. Alifikiwa kwa njia ya kirafiki na kuombwa kwa fadhili aseme shime fulani. Ndugu Worku alikataa; yeye alirudia tu shime zake za Biblia za kupendelea Mungu wa kweli. Sasa “marafiki” hao waligeuka kuwa watesi wa kinyama.

Siku chache baadaye, maofisa wa jela walitaka kuzungumza mambo pamoja naye. Mazungumzo hayo yalichukua saa nne. Aliambiwa atapewa cheo kikubwa cha kisiasa. Akakataa. Maneno yao yakawa hivi: “Utapigwa risasi uwe chakula cha mabuu.”

Hatimaye, maofisa wengine wenye haki walipendezwa na kesi ya Ndugu Worku na kupendekeza aachiliwe. Alihesabu mateso yake yote kuwa shangwe; hakuwa ameshindwa. (Ebr. 12:2) Kabla ya majaribu yake kuanza, sikuzote alichukua funzo la familia la ukawaida na sala kwa uzito. Bila shaka jambo hilo lilimsaidia kuvumilia. Alisimulia yale pasta mmoja wa Jumuiya ya Wakristo aliyekuwa kama “Nikodemo” alisema juu ya Mashahidi: “Tuliogopa na tukakana imani yetu. Tulikosa kumtetea Mungu, lakini nyinyi mlisimama imara kwa ajili yake, bila hata kuogopa kifo. Mlifanya vema.” Hivyo, kwa ujumla, Ndugu Worku alikuwa amehukumiwa kifo mara nane, lakini Yehova alimhifadhi hai!

Wajifunza Somo Kubwa

Wakati wa miaka hiyo ya majaribu ya kikatili, Mashahidi katika Ethiopia waliona kwamba maneno ya mtume Paulo yalitimizwa juu yao: “Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu.” (Ebr. 11:34) Dada mmoja mnyenyekevu, aliyekuwa mtumishi wa kike nyumbani, na ambaye alikuwa akijifunza kusoma, alijikuta amefungwa gerezani na kikundi cha Mashahidi wenye elimu. Ingawa Mashahidi wengine waliofungwa walisali waachiliwe huru, sala za dada huyo zilikazwa juu ya kupata nguvu za kuendelea akiwa mwaminifu. Siku moja wanyanyasi walileta mafuta yanayochemka katika bakuli na kutisha kuingiza ndani vidole vya kila mfungwa. Mashahidi fulani waliogopa, lakini dada huyo mnyenyekevu aliendelea kuwa imara. Vidole vyake havikuumizwa. Baadaye aliachiliwa.

Jambo hilo likawa somo kubwa kwa wale waliochukua hadhi yao ya kijamii na kielimu kuwa mambo ya maana sana. Waling’amua sasa kwamba jambo muhimu zaidi lilikuwa uaminifu.

Hawakuacha Kabisa

Lilikuwa jambo lenye kuthawabisha kama nini kuona ukomavu, usawaziko, tumaini katika Yehova, na roho kubwa zaidi ya kujidhabihu ikikuzwa miongoni mwa Mashahidi hao waliovumilia mengi sana! Kama ilivyo na sehemu nyinginezo, hawakuachwa kabisa. Ibada ya kweli ilishinda.

Katika wakati huo, watu walikuja upande wa Yehova kwa njia zisizo za kawaida. Kwa mfano, mzee mmoja wa kutaniko alitolea ushahidi mwanamke mwingine kutoka Ulaya Mashariki mahali pake pa kazi. Na kwa sababu ya mwanamke huyo kupendezwa sana, alimwazima kichapo cha Biblia kilichokuwa cha thamani sana kwake. Alifadhaika wakati mwanamke yule alipoondoka nchini bila kukirudisha kichapo kile. Miaka mingi baadaye, alipokea barua iliyomfurahisha kutoka kwa mwanamke yule. Mwanamke yule alimweleza kwamba kichapo kile kilimfanya abadilishe maisha yake na sasa alikuwa dada yake wa kiroho aliyebatizwa!

Mfano mwingine ulikuwa wa mtumishi wa kike mwenye haya aliyekuwa akisikiliza wakati mwajiri wake ambaye alikuwa mwalimu alipokuwa akifunzwa Biblia. Alihisi kwamba hastahili, lakini alitamani sana kuziamini zile kweli za ajabu. ‘Ni lazima mafunzo hayo ya Biblia yawe yanagharimu pesa nyingi sana,’ yeye akafikiria. Hivyo, aliacha kumfanyia yule mwalimu kazi ili atafute kazi yenye mshahara mzuri ili alipie mafunzo hayo ya Biblia. Alipokuwa ameweka akiba ya pesa alizodhani kuwa zitatosha kulipia mafunzo ya Biblia, alienda moja kwa moja hadi kwenye nyumba ya yule Shahidi aliyekuwa akijifunza na mwajiri wake wa awali, yule mwalimu. Alishangaa kama nini kugundua kwamba mafunzo hayo yalitolewa bila malipo! Alifanya maendeleo mazuri katika mafunzo yake na baadaye akaolewa na yule mwalimu; sasa wote wawili ni watumishi waliojiweka wakfu kwa Yehova.

Vijana Mashahidi wa Yehova hasa walitiwa chini ya mikazo mingi katika nchi hii. Kwa sababu ya kutokuwamo kwao, walinyimwa mambo mengi ambayo ni ya lazima kwa maisha, kama vile matibabu ya hospitalini, mitihani ya shule, na kazi za kuajiriwa. Je! hayo yote yaliwafanya wahisi wameachwa? La! Wakiwa na imani thabiti kwamba dhiki zao ni za muda tu, waliendelea mbele kwa nguvu ambazo Yehova huwapa.—Flp. 4:13.

Suluhisho Halisi

Matatizo yanayopata Ethiopia yanafanana na yale yanayopata ulimwengu wote. Mashahidi wanaamini kwamba wamepata suluhisho na wanafurahi kwamba tangu 1990, mingi ya mikazo iliyowekwa juu yao imelegezwa, hivi kwamba wanaweza kueleza wengine juu ya suluhisho hilo.

Kwa mfano, katika Asmara, jiji kuu la Eritrea, wenye mamlaka wameamuru kwamba Mashahidi wa Yehova wasibaguliwe. Mfano mwingine: Zaidi ya ndugu 50 kutoka Ethiopia walipewa hati zote zinazotakikana za kusafiri ili wahudhurie mkusanyiko wa wilaya katika Nairobi, Kenya. Mifano mingine miwili: Mapainia wa pekee wanaweza kutumwa tena kwenye maeneo mbalimbali kuhubiri habari njema. Na makutaniko mengine yameanza kuhubiri nyumba kwa nyumba tena, yakipata matokeo mazuri. Hata hivyo bado kuna matatizo mengi yanayobaki nchini Ethiopia.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilizidi sana katika mwaka wa 1990, baada ya kutekwa kwa mji wa bandari wenye umaana mkubwa wa Massawa. Mji wote ulikuwa magofu ya uharibifu. Shukrani ni kwamba hakuna Shahidi aliyeishi huko aliyeumia. Njaa kali ilipiga Asmara na sehemu nyinginezo za mashambani. Baraza Linaloongoza liliongeza msaada katika sehemu hiyo ya ulimwengu yenye msiba. Mapainia wa pekee wawili walihatirisha maisha zao kwa kupitia eneo la vita kwa werevu ili wafike Mekele, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Tigre, na kutoa kitia-moyo kilichohitajiwa sana na Mashahidi waliokuwa wakiishi huko. Katika Mei 1991, vikundi vya wapiganaji wa kuvizia viliangusha serikali ya wanamapinduzi na kutia sahihi mkataba ulioahidi uhuru zaidi. Eritrea sasa ikawa na serikali tofauti na mawasiliano na ulimwengu wa nje yakakatizwa kwa sehemu kubwa. Katika mchafuko huo wote, Mashahidi wamedumisha kutokuwamo kabisa, kwa vile wanajua kwamba suluhisho la kudumu la matatizo ya wanadamu litakuja kupitia tu Ufalme wa Mungu. Lakini kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi, kulikuwa kumekuwa siku za kusanyiko la pekee kwa uhuru katika miji kadhaa ya Ethiopia. Matayarisho yalikuwa yanafanywa kwa ajili ya makusanyiko ya mzunguko na mkusanyiko wa wilaya, na shehena kubwa ya fasihi, na kuandikishwa kisheria. Nchini Ethiopia, kama sehemu nyinginezo, “mandhari ya ulimwengu huu inabadilika” haraka, na akina ndugu wana mtazamio wa idili kwa ajili ya kukusanywa ndani mavuno makubwa ya mwisho.—1 Kor. 7:31, NW.

Lakini ni mambo gani zaidi yalitukia katika bara la Afrika Mashariki tangu miaka ya katikati ya 1970? Ebu tuone.

Uvumilivu Wajaribiwa Nchini Tanzania

Msamaha wa watu nchini Tanzania katika mwaka wa 1976 uliruhusu baadhi ya Mashahidi waliofungwa waachiliwe. Lakini kwa kusikitisha, bado kulikuwa na maofisa fulani serikalini walioona ndugu zetu kuwa hatari. Kwa nini? Walifikiria Mashahidi wa Yehova kuwa ndio wafuasi wa kikundi cha mapinduzi cha Kitawala kilichokuwa Sumbawanga. Akina ndugu walichunguzwa sana, na mapainia wa pekee wengi ‘walifungwa kama watenda mabaya,’ kama ilivyokuwa kwa mtume akiwa Roma.—2 Tim. 2:9.

Kulikuwa na matatizo zaidi. Katika Februari 1977, mpaka wa Tanzania na Kenya ulifungwa, na ulibaki hivyo kwa miaka sita. Ikawa vigumu kwa muda fulani kupeleka barua na nyingi zilipotea. Ukame ukaleta matatizo katika maeneo fulani na ziara za waangalizi wa mzunguko zilikatishwa kwa sababu ya maambukizo ya kipindupindu. Vita kati ya Tanzania na Uganda katika mwaka wa 1979 vilileta mikazo mingine. Uchumi uliokuwa ukizorota ulileta mahangaiko ya vitu vya kimwili. Matatizo hayo yote yalileta mikazo mingi kwa wazee wa kutaniko hivi kwamba katika makutaniko fulani hawakuweza kufanya kazi ya ziara za uchungaji kadiri ilivyotakikana.

Lakini kulikuwa na mambo mazuri pia. Sehemu ya kusini mashariki mwa nchi hatimaye ilifunguliwa mwaka wa 1979 kwa ajili ya kazi ya kuhubiri, jambo lililofanya Mashahidi wawe watendaji kotekote tokea Kilimanjaro upande wa kaskazini hadi mpaka wa Msumbiji upande wa kusini.

Mahakimu walianza kufanya maamuzi mazuri kuelekea Mashahidi. Askari-jela kutoka Tukuyu akawa Shahidi, kupendezwa kwake kulitokana na mwenendo mzuri wa Mashahidi. Katika Julai 1981, kile kilele cha wahubiri 1,609 cha mwaka wa 1975 kilipitwa hatimaye wakati wahubiri 1,621 waliporipoti.

Ustahimilivu Wathawabishwa

Katika 1979 na pia 1981, akina ndugu waliendea wenye mamlaka ili kujaribu kufanya kazi itambuliwe rasmi. Majaribio hayo hayakufanikiwa. Jitihada za kutambuliwa kisheria ziliendelea kukiwa na barua iliyopelekwa kutoka kwa Baraza Linaloongoza yenye tarehe ya Mei 5, 1983. Majaribio zaidi baadaye katika Agosti 1984, yaliyofanywa na Ndugu Faustin Lugora na Elikana Green yalikataliwa bila ukali.

Mashahidi walistahimili na kupeleka ombi tena. Maombi katika Wizara ya Mambo ya Nchini yalikataliwa tena katika 1985. Ilionekana kana kwamba hakuna tumaini katika jambo hilo, na bado kulikuwa na ishara za kwamba makutaniko fulani yalikuwa yakichunguzwa. Labda kulikuwa na maofisa wenye kufikiri kwa njia yenye haki waliotaka kupata mambo ya hakika juu ya Mashahidi.

Ndugu zetu waliendelea na jitihada za kutaka kutambuliwa kisheria mwaka wa 1986. Walitendewa vizuri na kwa heshima. Hatimaye ustahimilivu wao ulithawabishwa. Baada ya uchunguzi mwingi sana, mawazo yenye kosa ya muda mrefu yalisahihishwa, na siku ya Februari 20, 1987, wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova walipewa barua ya serikali iliyotambua kisheria ile Association of Jehovah’s Witnesses katika Tanzania. Ulikuwa wakati wa kushangilia baada ya miaka 22 chini ya marufuku!

Paradiso ya Wamishonari

Shangwe ilienea kotekote Tanzania. Makusanyiko ya mzunguko yalipangwa. Miongoni mwa wale waliotaka kubatizwa katika makusanyiko hayo, wengine walipatikana ambao walikuwa wakihubiri kufikia saa za mapainia wa kawaida na kuongoza mafunzo ya Biblia tisa au zaidi. Kwa kweli, ndugu mmoja mpya alibatizwa pamoja na mwanafunzi wake wa Biblia!

Idhini ya wamishonari kuingia Tanzania iliombwa na kukubaliwa mwaka wa 1987. Mwaka uo huo wahitimu wa Gileadi waliwasili Dar es Salaam, wakati huo likiwa jiji la watu zaidi ya milioni 1.5. Eneo kubwa kama nini kwa makutaniko mawili tu ambayo yalikuwa na jumla ya wahubiri wanaopungua 200!

Eneo la kuhubiri lilikuwa paradiso ya wamishonari. Wenye nyumba waliwaalika ndani na kukubali vichapo kwa furaha. Makao ya mishonari yalifunguliwa mjini Mbeya ambao ulikuwa ndio kitovu cha zaidi ya nusu ya wahubiri wote nchini. Miezi michache baadaye, wamishonari wengine wakaja Arusha na Dodoma.

Mazoezi mengi ya kitengenezo yanahitajiwa ili kuweka msingi wa kusaidia Watanzania wenye mioyo minyofu kumwabudu Mungu wa kweli. Uwezekano wa ongezeko ni mkubwa sana, na bidii iko, kama inavyoonyeshwa na ulinganisho huu unaofuata: Katika mwaka wa 1982, kulikuwa na mapainia 160—katika 1991, kulikuwa na mapainia 866; katika 1982, Mashahidi walitumia saa 374,831 katika utendaji wa kuhubiri ikilinganishwa na saa 1,300,085 katika 1991; katika 1982, hudhurio la Ukumbusho lilikuwa 5,499—katika 1991, lilikuwa 10,441; katika 1982, waliobatizwa walikuwa 41 ikilinganishwa na wale 458 waliobatizwa mwaka wa 1991.

Maswali ya kisheria yalizuka tena katika mwaka wa 1988, na hayo yamefanya maombi ya wamishonari kuingia nchini yasikubaliwe hadi kufikia wakati huu. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza, serikali ilikubali ombi la Mashahidi la kufanya wazee wa kutaniko wawe maofisa wa kufunganisha ndoa.

Mafuriko kadhaa na ukame ulifanya msaada upelekwe katika sehemu ya kusini zaidi na pia karibu na Ziwa Viktoria, na jitihada hizo zimekuwa zikiendelea kufikia mwaka wa 1991. Lakini yajapokuwa magumu na hali isiyo ya uhakika, watu wa Yehova wanafuatilia kukusanywa kwa watu wa mfano wa kondoo kwa roho ya bidii.

Wafagiliwa Mbali Katika Kenya

Miaka iliyofuata 1975 ilifagia makutaniko sana. Wale waliokuwa katika kweli wakiwa na wazo kwamba mwaka wa 1975 ndio uliokuwa mwisho wa mfumo mwovu wa mambo waliacha kweli walipoona mwaka huo umepita. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba katika kipindi hiki wahubiri wapya 49 kati ya 77 walikuja kuwa wasiotenda. Wale waliokosa mikutano na funzo la kibinafsi walinaswa na mitego ya Shetani ya ukosefu wa adili, ulevi, na tamaa ya mali. Inasikitisha kwamba katika miaka fulani, zaidi ya asilimia 3 ya wahubiri wote walikuwa wakitengwa.

Bila shaka, makutaniko mengi yalikuwa madogo na yalikosa uelekezi mzuri. Kwa kweli, katika mwaka wa 1978, kati ya makutaniko 90 yaliyokuwa nchini Kenya, makutaniko 49 yalikuwa na wahubiri chini ya 10, na makutaniko 12 pekee yalikuwa na wahubiri zaidi ya 40. Jambo hilo lilifanya kazi nyingi ya kitheokrasi ifanywe na ndugu mmoja au wawili. Misiba ya kiasili iliongezea mzigo wa wazee. Eneo la mashariki mwa Nairobi lilipatwa na ukame mbaya sana hivi kwamba ilikuwa lazima msaada upangwe.

Hata hivyo, kila kitu hakikuwa bila tumaini na huzuni tu. Mambo mengi mazuri na yanayofaa yalitendeka pia. Hudhurio la Ukumbusho katika 1977 lilikuwa 5,584. Kulikuwa na uhitaji mkubwa wa fasihi. Ziara ya Lloyd Barry wa Baraza Linaloongoza ilichochea bidii ya Ufalme ya wote. Na ule mpango mpya wa Halmashauri ya Tawi, ulioanza kufanya kazi tangu 1976, ulichochea kazi hata zaidi.

Betheli Kubwa Zaidi

Kilele kipya cha wahubiri 2,005 kilifikiwa Februari 1979. Idadi ya wahubiri ilifanya familia ya Betheli iwe kubwa kushinda jengo la ofisi ya tawi, hivi kwamba Halmashauri ya Tawi iliomba kibali kutoka kwa Baraza Linaloongoza cha kuongeza vyumba vinne kwenye Betheli. Halmashauri ya Tawi ilishangaa wakati ilipopokea bahasha kubwa iliyokuwa na plani za jengo jipya kabisa la ziada lenye vyumba vya kulala 16 zaidi!

Uchimbuzi kwa ajili ya jengo jipya la tawi ulianza Desemba 1978, na kufikia Juni 1979, sehemu ya jengo hilo lenye kuvutia ilikuwa tayari imeanza kutumiwa. Januari 1980, Don Adams kutoka makao makuu ya ulimwengu alizuru kwa ajili ya programu ya kuwekwa wakfu, akahutubia watu 2,205 katika Nairobi City Stadium. Baadaye, kukiwa na manyunyu ya mvua, karibu watu 1,000 walizuru jengo jipya la Betheli, wengi wakiona kwa mara ya kwanza jinsi kazi inavyofanywa katika ofisi yao ya tawi. Mwaka huo uliisha kukiwa na mikusanyiko midogo, kutia ndani mkusanyiko mmoja wa Kiingereza mjini Nakuru uliohudhuriwa na ndugu kutoka Uganda yenye vita.

Mwaka uliofuata ulileta maendeleo mengine makubwa. Vifaa vya uchapishaji vya ki-siku-hizi vilifika ofisi ya tawi ya Kenya. Sasa fomu, programu, mihuri, na Huduma ya Ufalme, na hata magazeti yangeweza kuchapwa humo. Sasa ugavi huo haungengojewa kwa muda mrefu uwasili kutoka ng’ambo! Ingawa vichapo 120,000 vilichapwa mwaka wa 1980, miaka miwili baadaye jumla ya fasihi iliyochapwa ilifikia 935,000 na kufikia 1990 ikawa 2,000,000.

Nairobi ilipita kiwango cha wahubiri 1,000 katika 1983, na nchi yote ya Kenya ikafikia 3,005. Asilimia 28 ya wahubiri walikuwa katika utumishi wa wakati wote katika mwezi wa Aprili. Pia, wamishonari wengi zaidi pia walikuwa wamekuja kusaidia.

Vichapo Vyasaidia Neno Kusonga kwa Haraka

Vichapo vya Sosaiti vinapendwa sana nchini Kenya. Baadhi ya shule hutumia Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia katika masomo ya kidini. Magazeti yakawa ya kuvutia zaidi kwa sura hivi kwamba katika miaka miwili ya 1984-85, uangushaji ulipanda kwa zaidi ya asilimia 50, nyakati nyingine wahubiri wakifikia wastani wa magazeti kumi kila mwezi. Matoleo fulani yalikuwa na matokeo makubwa kwa umma mara hiyo. Mfano mmoja ni wa mtu aliyesema na mhubiri mmoja aliyekuwa akitoa ushahidi barabarani. Mtu huyo alielekeza kwa gazeti lililokuwa na makala yenye kichwa “Je! Kuvuta Sigareti Kutadumu?” na kutangaza hivi: “Mimi nilikuwa mvutaji.” Ni nini kilichomfanya aache? Ni makala hiyo ambayo alikuwa amesoma siku kadhaa zilizopita!

Mwaka wa 1982 ukawa wa maana kwa sababu ya kufika kwa broshua Furahia Milele Maisha Duniani! kichapo kilichokuja kufaa sana eneo hili la Afrika. Hata watu waliosoma sana walikitaka, wengine wakikichukua kihalisi kutoka kwa mifuko ya wahubiri. Hilo lilimpata Shahidi mmoja ambaye alikuwa na broshua hiyo moja tu imebaki mfukoni mwake. Alikuwa akiiweka kwa ajili ya mwanafunzi wake mpya wa Biblia. Msafiri mmoja akaiona broshua hiyo. Akaitaka. Na akakataa kuchukua kichapo kingine chochote. Shahidi huyo akaeleza kwamba broshua hiyo iliwekwa akiba kwa yule tu atakayekubali kujifunza Biblia kwa ukawaida. “Hiyo si shida,” akasema msafiri yule mwenye kuazimia. “Hiyo ni sawa kwangu.” Matokeo yakawa nini? Funzo jipya la Biblia kwa yule mhubiri!

Broshua hiyo hutoa ushahidi wa wazi juu ya Yehova na makusudi yake, ile serikali ya Ufalme, na viwango vya uadilifu vya Biblia. Kwa sababu broshua hiyo ilifaa sana, ilitafsiriwa kwa lugha nyingine 35 zinazotumiwa katika eneo la Afrika Mashariki, lugha 14 za Kenya na 21 za nchi zilizo karibu. Katika baadhi ya lugha hizo, broshua hiyo pekee ndiyo kichapo kinachopatikana isipokuwa Biblia. Hata mmoja wa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo alisema hivi juu ya broshua ya Kimasai: “Hili ndilo jambo bora zaidi ambalo limewahi kuwapata Wamasai.”

Roho ya Upainia

Jambo jingine lilibadilisha hali ya shamba katika Kenya: roho ya painia inayozidi kukua miongoni mwa Mashahidi. Wakati ambao mapainia walionwa kuwa watu wenye maisha mageni au walioshindwa kufaulu maishani ulikuwa umepita. Ikawa wazi kwamba Yehova alikuwa anabariki mapainia kwa maono ya kuleta shangwe na mazao ya Ufalme. Wengine walipainia hata ingawa walikuwa vipofu au kuwa na mguu mmoja tu. Ilikuwa ni kawaida kuona mzazi mwenye watoto wanane au zaidi wa kutunza akiwa mmoja wa mapainia.

Katika Aprili 1985, asilimia 37 ya wahubiri wote walikuwa katika utumishi wa wakati wote. Kwa msaada wa mapainia hao wengi, zaidi ya saa milioni moja zilitumiwa katika utumishi mwaka huo.

Warwanda Wenye Bidii Wakomboa Wakati

Mambo yalikuwa yakiendelea vizuri nchini Rwanda pia. Kweli ya Biblia ilikuja ikiwa imechelewa sana kwa kulinganisha na maeneo mengine, na bado wengi waliona njaa ya ujumbe wenye kutoa uhai. Kutokea kwa kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele kwa Kinyarwanda katika Februari 1980 kulichochea sana wahubiri, ambao wakati huo walikuwa na kilele cha 165. Jumba la Ufalme kubwa lakini sahili lilijengwa Kigali wakati wa mwaka wa 1980 na upesi watu zaidi ya 200 wakawa wanahudhuria mikutano, wakijaa mpaka nje uani.

Kupendezwa huko kwingi kwa Wanyarwanda hakukupendeza maadui wa habari njema. Orodha iliyotolewa Oktoba 1979 ya dini zilizokubaliwa nchini haikutia ndani Mashahidi wa Yehova. Jitihada zikafanywa ili Mashahidi watambuliwe kisheria. Katika mwezi wa Machi 1980, Ernest Heuse wa Ubelgiji na ambaye alikuwa ametumikia nchini Zaire, alikuja Kigali kuona wenye mamlaka. Ingawa alitoa hati nyingi, walikataa kutambua Mashahidi kisheria.

Ingawa hivyo, kutoa ushahidi juu ya Ufalme kuliendelea kusonga mbele. Hudhurio la mkusanyiko wa wilaya likawa 750 katika mwaka wa 1982, na 22 wakabatizwa, na katika Machi, wahubiri 302 waliripoti wakati waliotumia katika utumishi wa shambani. Katika makusanyiko ya mzunguko manne yaliyofanywa, jumla ya hudhurio likawa zaidi ya 1,200, na 40 wakabatizwa. Shule ya Huduma ya Ufalme ilifanywa na kuwapa mazoezi yaliyohitajiwa kwa wenye madaraka katika makutaniko madogo. Bidii haikupoa; wahubiri wakawa na wastani wa saa 20 kila mwezi shambani. Dada wawili mapainia wa pekee walifungua eneo jipya na kwa muda wa miezi mitatu pekee walikuwa wakiongoza mafunzo ya Biblia 20, wote wakiwapo kwenye mikutano. Rwanda ilijaa shughuli ya kuhubiri!

Watu wengi zaidi na zaidi waliuliza maswali juu ya kweli za Biblia. Mengi ya maswali hayo yakitokezwa na habari iliyokuwa katika gazeti la Amkeni! ambalo lilikuwa likisomwa kwa ukawaida katika redio. Mawimbi ya redio yalijaa kweli ya Biblia iliyofunua wazi mafundisho bandia yanayofundishwa na dini mbalimbali. Si ajabu kwamba upesi baadaye, magazeti ya kidini, yenye uvutano mkubwa sana nchini Rwanda yalishambulia Mashahidi wa Yehova. Na kama kawaida jambo hilo lilivuta wengi katika kweli. Ingawa hivyo, karibu na wakati huo, Mashahidi walianza kusimamishwa na kuhojiwa, na wakawa wakitozwa faini kwa kuendesha shirika lisilo halali.

Madhara kwa Njia ya Sheria

Katika Novemba 1982, wale mapainia wa pekee watatu waliotia sahihi ombi la kutaka kutambuliwa kisheria waliitwa Kigali, wakashikwa mara walipofika na kufungwa jela bila hukumu ya mahakamani wala bila kufuata njia yoyote ya kisheria. Jumba la Ufalme lilifungwa. Kazi ya kuhubiri ikaanza kufanywa kisiri-siri.

Barua kutoka kwa waziri wa sheria kwa wilaya zote ilipiga Mashahidi marufuku. Wengine zaidi wakashikwa. Mapainia wengi wageni wakalazimika kuondoka nchini. Ilikuwa ni pindi ya kutahiniwa, wakati wa kupepeta kwa akina ndugu wenyeji. Na kwa wakati unaofaa, Mnara wa Mlinzi lilianza kuchapwa katika Kinyarwanda, likitoa chakula zaidi cha kiroho.

Kulikuwa na kazi kubwa ya kufanywa katika gereza kubwa la Kigali kwa wale mapainia wa pekee watatu, Gaspard Rwakabubu, Joseph Koroti, na Ferdinand I’Mugarula. Waliongoza mafunzo ya Biblia kwa ukawaida na wafungwa wengine, na idadi fulani yao wakajifunza kweli kwa njia hiyo. Miezi ikapita bila wao kuhukumiwa mahakamani. Hatimaye, katika Oktoba 1983, walijaribiwa mahakamani. Ndugu hao watatu walishtakiwa kuiba pesa za watu, kuasi dhidi ya serikali na mashtaka mengine bandia kabisa. Hakuna tarakimu yoyote au hata hati za kifedha zilizotolewa kuwa uthibitisho wakati wa kesi yote wala hakukuwa na mashahidi wa mashtaka waliotolewa kuthibitisha mashtaka hayo.

Ndugu hao walihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani bila hata siku moja kupunguzwa. (Wakati huohuo wauaji wa kukusudia waliachiliwa.) Katika Gisenyi, Mashahidi wengine watano walivumilia kwa uaminifu kifungo cha karibu miaka miwili bila kuhukumiwa mahakamani.

Kupoa kidogo kwa mambo katika 1985 kuliruhusu baadhi ya akina ndugu katika Rwanda kuhudhuria mkusanyiko wa wilaya Nairobi na kukutana na ndugu wa Baraza Linaloongoza. Lakini kufikia Machi 1986, kukamatwa kulikuwa kumekuwa jambo la kawaida nchini kote. Wengi walishikwa wakiwa nyumbani mwao. Wanawake waja wazito pamoja na watoto walishikwa pia. Katika maeneo fulani, Mashahidi waliwindwa baada ya majina yao kuwekwa katika orodha ya watu wanaotafutwa. Hatimaye zaidi ya Mashahidi 140 wakatupwa gerezani—karibu theluthi moja ya Mashahidi wote watendaji nchini!

Kumtegemea Mwanadamu au Kumtumaini Mwenye Enzi?

Siku ya Oktoba 24, 1986, suala la Mashahidi hatimaye likaja mahakamani. Kufikia wakati huo, wengine walikuwa wamefungwa kwa miezi zaidi ya sita. Hata mtoto alizaliwa gerezani na akaitwa jina linalofaa yaani Shikama Hodari (Dumu ukiwa Imara). Walihukumiwa vikali sana, kuanzia miaka 5 hadi 12 gerezani. Mwanamke mmoja aliyependezwa na ambaye hakuwa mhubiri bado alifungwa gerezani miaka kumi.

Kesi hizo zikaja kujulikana sana kimataifa na hata zikawa mambo ya kuzungumzwa na wakuu wa mataifa ya Ulaya na Afrika. Watu wengi nje ya Rwanda walipeleka barua za kuteta kwa maofisa waliohusika. Tangazo la redio lilitaja kwamba katika siku fulani-fulani, barua 500 kwa niaba ya Mashahidi wa Yehova zilifikia serikali.

Mambo hayo yote yalitoa fursa nzuri za kutoa ushahidi gerezani. Mashahidi walionyesha mfano wenye kutokeza wa umoja: wakisali pamoja na kujifunza Neno la Mungu pamoja. Wafungwa wengine wengi wakawa na udadisi na kuanza kujifunza Biblia, na sasa wale waliokuwa wahalifu na malaya wanafanya maendeleo mazuri katika njia ya uhai wa milele.

Mashahidi hao walidumisha roho yenye shangwe zijapokuwa hukumu ndefu walizopewa. Wao walikuwa wakisema hivi: Tulifungwa miaka 12, lakini Shetani atafungwa miaka 1,000!” Pia walikuwa wakisema: “Tuna uhuru zaidi hapa ndani kushinda ndugu zetu ambao wako nje kwa sababu tunaweza kuimba katika mikutano yetu, na wao hawawezi.”

Mambo Mazuri Yasiyotazamiwa

Siku ya Julai 1, 1987, wakati wa kusherehekea mwaka wa 25 wa uhuru wa Rwanda, rais wa Rwanda aliomba radhi katika hotuba aliyotoa kwa redio juu ya kuvunjwa kwa haki za kibinadamu, na akatangaza kwamba wale wote waliofungwa siku ya Oktoba 24, 1986 wangeachiliwa. Kwa kweli huo ulikuwa uamuzi wa ujasiri na wenye kusifika kama nini! Siku chache baadaye, ndugu na dada wote 49 waliokuwa wamefungwa waliachiliwa.

Lakini swali lilibaki juu ya ingekuwaje kwa wale waliokuwa hawajahukumiwa. Majuma kadhaa yakapita, lakini hatimaye wote waliitwa mahakamani na kuambiwa kwamba wangefanya mema mengi kwa nchi yao kwa kurudi nyumbani na kulima na kufanya kazi nyingine inayofaa.

Kwa wazi, hiyo ilileta shangwe nyingi sana. Baada ya kuachiliwa kwao, zaidi ya wahubiri wasiobatizwa na wanafunzi wa Biblia 30 waliofanya maendeleo ya haraka gerezani walijitoa wabatizwe. Baada ya “shule” hiyo ya gerezani, wote wamekomaa haraka. Mara tu baada ya ubatizo wao, wengi wao walianza utumishi wa painia msaidizi! Na Mashahidi wote walioachiliwa walipata tena kazi ya kimwili.—Ona Zaburi 37:25, 28.

Pascasie alikuwa mmoja wa wale waliovumilia majaribu kwa shangwe. Mume wake alifadhaishwa na marufuku juu ya Mashahidi wa Yehova, akampeleka katika kituo cha polisi ili ashikwe. Hata ingawa hakuwa amebatizwa, alifungwa pamoja na akina dada. Alihukumiwa kifungo cha miaka kumi. Ijapokuwa alihuzunika kuacha watoto wake nyumbani, alitambua kwamba ilikuwa ni lazima kuteseka kwa ajili ya ibada ya kweli. Alifanya maendeleo ya kiroho gerezani na akawa miongoni mwa wale waliobatizwa baada ya kufunguliwa. Lakini ilikuwa shangwe ya ziada kama nini wakati aliporudi nyumbani na kupata kwamba mume wake alikuwa tayari kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova! Kwa kweli uthabiti wake umethawabishwa, kwa vile mume wake amekuwa ndugu yake wa kiroho, jambo linalounganisha familia nzima katika ibada ya kweli.

Mapema katika 1990, katika sehemu nyingine ya nchi, shtaka lililoahirishwa katika 1985 lilifufuliwa tena na ndugu wanne wakafungwa jela miaka kumi kila mmoja. Lakini kwa furaha, jambo hilo halikuathiri sehemu nyinginezo, ambapo makusanyiko ya mzunguko na mitaala ya shule ya painia ingeweza kufanywa. Mwangalizi wa eneo la dunia pia alizuru kwa mara ya kwanza, na chakula kingi zaidi cha kiroho katika Kinyarwanda kikafanya wahubiri wawe wa kiroho zaidi. Kwa kuongezea, ndugu zetu walifunguliwa kwa amri ya rais baada ya wao kuwa gerezani miezi sita.

Uvamizi wa ghafula mwishoni mwa 1990 ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda pia. Msimamo wa kutokuwamo wa ndugu zetu kwa kupatana na kanuni ya Biblia ya Yohana 17:14, kwamba “wao si sehemu ya ulimwengu,” ukafanya wapinzani wa zamani watambue kwamba watu wa Yehova si maadui wa mtu yeyote. Mapema katika 1991, njaa kali ilileta mahangaiko zaidi na kufanya msaada wa chakula uhitajiwe kwa ajili ya Rwanda, hasa sehemu ya kusini mwa nchi hiyo. Hivi karibuni, makusanyiko ya mzunguko yamefanywa peupe. Akina ndugu wanatumaini kwamba siku moja watapata uhuru kamili wa kidini pamoja na kutambuliwa kisheria nchini Rwanda, lakini kwa wakati huu wanaendelea kusaidia wengi wanaotafuta kweli miongoni mwa idadi ya watu inayozidi kuongezeka katika Rwanda.

Kuamshwa kwa Mambo ya Kitheokrasi Nchini Uganda Kujapokuwa Matatizo

Vile “vita vya ukombozi” vilileta mabadiliko katika 1979. Uporaji wa mali, jeuri, na mateso yalifanya msaada uhitajiwe, barua na mawasiliano ya simu yalikatishwa. Lakini serikali mpya ilichukua mamlaka, na gazeti la Times la Uganda la Novemba 19, 1979 lilitangaza kuondolewa kwa marufuku juu ya Mashahidi pamoja na kurudishwa kwa uhuru wa ibada, chini ya kichwa “Wamishonari Wanaweza Kurudi.”

Mfululizo mpya wa makusanyiko ya mzunguko ukafanywa ukihudhuriwa na watu 241. Lakini uchumi ulikuwa umeharibika, na uhai haukuwa na maana. Watu wengi walikuwa na silaha, nao wanajeshi wa zamani wakawa wahalifu. Mifyatuko ya bunduki ilikuwa inasikika karibu kila usiku. Barabara hazikuwa salama kusafiri.

Ofisi ya tawi ya Nairobi ilipendezwa sana kujenga na kutia moyo akina ndugu kwa kutafuta ndugu wajasiri wa kuleta fasihi nchini Uganda. Kumbuka kwamba, watu walikuwa na silaha, na mara nyingi wanajeshi waliishi maisha ya namna mbili, ya kuwa majambazi usiku. Iliwabidi hao waliojitolea wapitie njia ndefu ya msitu ulioko kati ya Jinja na Kampala ambayo ilijulikana sana kwa uvamizi. Mara nyingi watu waliendesha gari mwendo wa kasi sana mpaka wafike sehemu iliyokuwa na watu.

Mmishonari mmoja alikuwa analala kwa ndugu mmoja mjini Mbale wakati aliposikia watu wakivunja gari lake lililokuwa nje. Aliwaacha waibe chochote walichotaka kwa sababu aling’amua kwamba huenda walikuwa na silaha. Asubuhi walipata kwamba magurudumu mawili, na gurudumu la spea na kioo cha mbele, vyote vilikuwa vimeibwa. Alifunga safari ya kwenda kilometa 240 hadi Kampala akiwa ameazima magurudumu mawili yaliyokwisha na bila kioo cha mbele cha kumlinda na mvua. Barabara hiyo ilipitia ile sehemu ndefu ya msitu hatari. Lakini mambo yakaenda sawa—magurudumu hayakutoboka, ila tu kulikuwa na upepo mwingi na mvua iliyompiga usoni!

Kilele kipya cha wahubiri 175 kilifikiwa katika Desemba 1980. Mwaka uliofuata ulianza kwa mkusanyiko wa wilaya uliofanywa Lugogo Stadium mjini Kampala, watu 360 wakihudhuria. Watu walijifunza kweli kujapokuwa jeuri nyingi yenye kuendelea, na kufikia Julai, kulikuwa na wahubiri 206 nchini, wakiangusha wastani wa magazeti 12.5 kila mwezi.

Kulikuwa na uhitaji mkubwa wa msaada kwa kuwa kulikuwa na mzee mmoja tu kwa makutaniko manane nchini Uganda. Hivyo, ikaamuliwa ombi lifanywe tena ili wamishonari wakubaliwe kuingia nchini. Kufikia Septemba 1982, Ari Palviainen na Jeffrey Welch, wamishonari wawili waseja walikuwa wamefika Kampala huku michafuko ikiendelea. Kafyu ya saa 12:30 za jioni ilikuwa ingali iko, na mifyatuko ya risasi na vita vya bunduki vilikuwa ni mambo ya kawaida usiku. Baadhi ya wahubiri walipotea, ikadhaniwa kwamba walikuwa wamekufa lakini walitokea tena. Wengine hawakuonekana tena. Kwa ujumla, wahubiri wanane Waganda walikufa kufuatia mchafuko wa vita ya 1979.

Vyeti vya kuruhusu wamishonari vilikubaliwa katika Februari 1983, na kufikia Aprili wa mwaka huo, makao ya mishonari yalifunguliwa katika eneo salama na kuanza kutumiwa na wahitimu wa Gileadi wanne wajasiri kutia ndani Heinz na Marianne Wertholz. Ule upole na staha ya Biblia ya Waganda ilifanya wamishonari hao wasahau matatizo ya kiuchumi, barabara mbovu, ukosefu wa usalama, na usumbufu wa usiku. Ilikuwa kawaida kuwa na mafunzo ya Biblia 10 au 15 kila mmoja. Kulikuwa na mwezi mmoja ambao wamishonari hao wanne waliangusha magazeti 4,084!

“Ndiye Yule!”

Katika kijiji kimoja kilichokuwa sehemu za ndani za Uganda, mtu mmoja wa makamo alipata kile kitabu Kweli na mara hiyo akang’amua kwamba alikuwa na kitu cha thamani sana. Alikisoma chote kwa kurudia tena na tena, kisha akaanza kutolea ushahidi kila mtu aliyekutana naye. Hata alijitangaza mwenyewe kuwa shahidi wa Yehova ingawa hakuwa amekutana na mmoja wao na alijua kwamba hakukuwa na yeyote katika eneo hilo.

Aling’amua kwamba lazima atafute “ndugu zake.” Hivyo siku moja alifunga safari kwa baiskeli kuelekea Kampala kutafuta Mashahidi wa Yehova. Alipoona misalaba katika makanisa, alijua kwamba Mashahidi hawawezi kupatikana humo. Watu ambao aliuliza walijua Mashahidi wa Yehova lakini hawakujua wanaishi wapi hasa. Akiwa anakata tamaa, akaingia kwa duka la kuuza vitabu na kuuliza juu ya Mashahidi. Mtunza fedha akajibu kwamba mara kwa mara Mashahidi hupitia hapo wakiwa na magazeti yao, lakini hakujua wanaishi wapi. “Wakija tena,” akasema mtu yule aliyependezwa, “tafadhali uwape anwani yangu. Ni lazima wanitembelee.”

Wakati uo huo wamishonari wawili walikuwa wakifanya ziara za kurudia kwa wale walioonyesha kupendezwa; hata hivyo, hawakupata yeyote nyumbani. Wakaangalia maandishi yao tena na kupata jina la yule mtunza fedha na kusema hivi: “Naam, tumzuru tena.”

Mapainia hao walipofika kwenye duka lile la vitabu, yule mtunza fedha akawaambia hivi: “Kulikuwa na mtu aliyekuwa akiwatafuta.” Akaangalia nje ya duka na kuelekeza kule barabarani na kuongeza hivi, “Kwa kweli ndiye yule!”

Muda si muda wamishonari Wazungu wakakutana na yule mtu aliyependezwa. Akawakumbatia wote wawili! Na bila shaka akawa mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii. Upesi baadaye Jumba la Ufalme ndogo likajengwa katika kijiji alimoishi, na tangu ajitoe wakfu na kubatizwa, amekuwa ndugu kwa maana halisi.

Vita Vyazuka Tena!

Maisha yalikuwa ya kuogofya kwa watu wengi nchini Uganda. Hakukuwa na usalama. Watu walichukuliwa na wanajeshi na kutoweka kabisa maishani. Bei za bidhaa zilipanda juu sana. Kwa mfano, bei ya mkate ilipanda kwa asilimia 1,000 kutokea 1974 hadi 1984! Wengine waliacha kuhesabu pesa wakati wa kununua vitu na badala ya hivyo wakapima kwa rula rundo la noti!

Kutoridhika kwa watu kukatokeza vita vya kuvizia nchini. Hatimaye chama cha National Resistance Movement kikanyakua utawala baada ya vita vya miezi mingi. Wakati huohuo, wanajeshi waliokuwa wakitoroka walipora mali na kuwapiga watu risasi ovyo-ovyo.

Vita vilitokea nje tu ya makao ya mishonari. Kesho yake, kufyatuliana risasi kukaanza wakati wamishonari walipokuwa wakienda kwenye mikutano ya Kikristo. Risasi zilipita juu ya vichwa vyao, lakini hakuna aliyeumia. Kisha wakapata wageni wasioalikwa Jumapili alasiri: wanajeshi wenye kutoroka wakipora mali. Wanajeshi hao walikasirika kwamba mlango wa mbele ulikuwa umefungwa. Lakini kiongozi wao alipoona vitambulisho vya wamishonari, mara hiyo alibadilika na kuwa mwenye urafiki, na hakugusa vitu vya wamishonari. Kwa sikitiko, watu hao walichukua mavazi kadhaa na matandiko lakini bila kuchukua chochote cha thamani zaidi.

Walipokuwa wakiondoka, waliwashauri wamishonari hao kwamba wavuruge nyumba nzima kwa kutoa mapazia dirishani, wakiondoa vitu kwenye masanduku ya kabati, na kutupa vitu huku na huku sakafuni ili hali hiyo itoe wazo la kwamba nyumba hiyo tayari ilikuwa imeporwa. Jambo hilo likafanya kazi kwa vile hakuna kitu cha maana kilichoibwa na mtu yeyote. Kabla ya hali kutulia na huku vita vikiwaka moto kuwazunguka, wamishonari walikaa ndani ya chumba kidogo cha kuwekea vitu mchana kutwa na usiku kucha. Chumba hicho ndicho kilichokuwa salama katika nyumba nzima. Katika msukosuko huo wote, walihisi ulinzi wa Yehova na kile kifungo cha upendo wa udugu wao.

Ndugu Waganda wana hadithi nyingi za kueleza juu ya jinsi mkono wa Yehova ulivyowalinda. Wengine wanaweza kuonyesha mashimo ya risasi ukutani au kwenye mavazi yao. Painia wa pekee mmoja alilala chini kifudifudi kwa zaidi ya saa tano, huku risasi zikipita juu yake kutoka kwa wanajeshi wa serikali upande huu na waasi upande ule mwingine. Alijipata amezungukwa na wafu wengi wakati mambo yalipotulia.

Usalama Zaidi na Shangwe Mpya

Katika miezi iliyofuata, hali ya usalama ikawa bora, na mambo ya kustaajabisha yakatukia. Kwa mfano, wamishonari walipokuwa wakirudi nyumbani, walikuwa wakipita nyumba kubwa ya ofisa mmoja wa cheo cha juu iliyokuwa ikilindwa nyakati zote na wanajeshi wenye kubadilika-badilika tabia hivi kwamba watu waliogopa kusumbuliwa nao. Hata wamishonari wenyewe wasiwasi wao ulipungua kila baada ya kupita mahali hapo na wageni waliotembelea makao ya mishonari wakawa wachache. Lakini chini ya serikali mpya, ghafula nyumba hiyo ikapatikana ikodiwe wakati uleule ambao wamishonari walikuwa wanahama makao yao. Upesi wakajipata wanaishi katika ile nyumba waliyoogopa kupita, wakifurahia kula chakula cha jioni nje katika ua mkubwa katika upepo mwanana wa jioni wa kitropiki. Ikiwa mtu angedokeza jambo hilo mwaka mmoja uliopita, hakuna mtu angeliamini hilo!

Kazi mjini Kampala ilisitawi. Sehemu nyingi za jiji hazikuwa zimehubiriwa kwa muda wa zaidi ya miaka kumi, na kulikuwa kazi nyingi ya kufanya. Ndugu Waganda waliongeza utendaji wao, wakifikia wastani wa saa 14.3 za utumishi kila mhubiri kwa mwezi wakati wa mwaka wa 1987.

Kifungo cha ukaribu cha upendo kikafanyizwa miongoni mwa Mashahidi hao. Walikuwa na nia ya kufanya dhabihu kwa njia nyingi wajapokuwa na vitu vichache vya kimwili. (Yn. 13:34, 35) Ilibidi wengi waweke akiba ya mapato ya miezi mingi ili waweze kuhudhuria mkusanyiko wa wilaya. Nyakati zote walikuwa wakikaribishana na kusaidia wamishonari wakiwa na tatizo lolote. Bila shaka Yehova aliwasaidia kwa njia nyingi, na mara nyingi ilihitaji “muujiza” ili makusanyiko yafanywe, nyakati nyingine bila vikuza sauti au hata bila viti.

Baada ya makao ya mishonari kufunguliwa katika Kampala na Jinja, makao ya tatu yalifunguliwa katika sehemu nyingine ya jiji la Kampala. Sasa Uganda ina makutaniko 18, kilele cha wahubiri 820, kilele cha waliohudhuria Ukumbusho cha 3,204, na zaidi ya mapainia wa pekee na wa kawaida 140. Majumba ya Ufalme yamejengwa Jinja, Tororo, Mbale, na Kampala. Hata hivyo, hali bado si rahisi kwa ajili ya kutoa ushahidi, na hakuna hakika ya wakati ujao.

Upinzani ulianza tena tangu 1989, ukianza kwa maneno ya makasisi, ukifuatwa na makala zenye kuchambua za magazeti, kufutiliwa bila sababu kwa vyeti vilivyokubaliwa vya kujenga, kukataa kutoa idhini kwa makusanyiko katika maeneo fulani, na kuingilia mambo kwingi kwa maofisa waliopashwa habari vibaya. Baada ya muda, mashirika yote yaliombwa yajiandikishe upya, na kuandikishwa kwa International Bible Students Association kulikataliwa. Wamishonari wengi walilazimika kuondoka nchini. Yajapokuwa mambo hayo yote, mikusanyiko ya wilaya katika Desemba 1990 ilifanywa kwa mafanikio. Maofisa fulani wakuu wamethibitika kuwa wenye kusaidia sana na wenye kufikiri vizuri, wakitoa tumaini la kwamba karibuni wamishonari wote wataweza kurudi Uganda na kuendelea na kazi yao ya kufundisha. Kuna uwezekano mkubwa wa kupata wengi katika shamba hili, na akina ndugu wanaomba Bwana wa mavuno atume wafanyakazi zaidi.—Mt. 9:37, 38.

Kenya Yajitayarishia Mpanuko Mkubwa Zaidi

Huku tengenezo la Yehova likisonga mbele ulimwenguni pote na kukiwa na ongezeko la daima kotekote katika Afrika Mashariki, wakati ulikuwa umefika wa kutumia tekinolojia bora zaidi nchini Kenya. Kulikuwa na msisimko kama nini katika ofisi ya tawi mwaka wa 1984 wakati kompyuta ya kwanza kati ya mbili ya aina ya IBM ilipofika kutoka ofisi ya tawi ya Ujerumani!

Hapo mwanzoni kila mmoja alitatanishwa na mashine hizo mpya, lakini kwa msaada wa Yehova na vitabu vya maelekezo ya kuzitumia, haikuchukua muda mrefu kuanza kutumia kompyuta hizo. Kompyuta ziliwezesha kuingiza maandishi na kuyaweka katika disketi, ambazo zingeweza kupelekwa kwenye ofisi za tawi zinazochapa ng’ambo. Jambo hilo liliwezesha mambo mengine mengi mapya kufanywa. Sasa haikuwa lazima kupokezana maandishi mara mbili au tatu kati ya Uingereza na Kenya kabla ya Mnara wa Mlinzi la Kiswahili kuchapwa. Sasa Mnara wa Mlinzi la Kiswahili linachapwa sawia na Mnara wa Mlinzi la Kiingereza, na makutaniko yote ya Kenya yanaweza kujifunza habari ileile ya Biblia katika juma lilelile moja.

Ongezeko la daima katika wahubiri liliambatana na ukuzi kuelekea hali ya kiroho thabiti yenye kuonekana wazi. Mashahidi waliongeza wakati wao katika utumishi, wakidumisha jicho sahili, linalokazia masilahi ya Ufalme. Wengi walitia bidii zaidi kusaidia watoto wao wengi kupitia funzo la familia la Biblia. Wazee wapya wamewekwa, na ndugu vijana wengi zaidi wamefikia kustahili kuwa watumishi wa huduma. Wengi wamekuwa wenye uaminifu-maadili katika majaribio ya kutokuwamo kwa Kikristo. Wengine wamejidhabihu kifedha ili wawe na Majumba ya Ufalme yao wenyewe.

“Washika Ukamilifu” Mkusanyiko wa 1985

Mwishoni mwa 1985, Kenya ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoteuliwa kuwa na mkusanyiko wa kimataifa wa pekee kukiwa na wageni kutoka ng’ambo. Karibu wageni 2,000 walikuja. Ingawa wajumbe hao wageni walifurahia mandhari ya Kenya na wanyama wengi, wote walikubali kwamba mambo makuu ya ziara yao yalikuwa ni mkusanyiko na huduma ya shambani, ambayo katika hiyo ndugu wenyeji waliandamana nao.

Watu wa Nairobi walipoona wazungu hao wote wakiwa na waongozi wao wenyeji, hilo lilitokeza pilikapilika. Wageni hao vilevile walivutiwa na kupendezwa ambako Wakenya walionyesha katika Biblia na pia vikundi vya watoto wadogo waliokuwa wakiwafuata kila waendapo.

Wageni hao walifurahia sana kuona maelfu ya watoto wadogo wanaosikiliza kwa uangalifu katika mkusanyiko. Zaidi ya watu 8,000 walijaa Jamhuri Park mjini Nairobi, huo ukiwa ndio mkusanyiko mkubwa zaidi ambao umepata kufanywa. Jambo la pekee kwa wahudhuriaji lilikuwa kuwapo kwa ndugu wawili wa Baraza Linaloongoza, Theodore Jaracz na Albert Schroeder.

Wafanyakazi wa ofisi ya tawi waliongezeka katika miaka iliyofuata, na wamishonari zaidi wakaja Kenya. Wamishonari hao walithawabishwa na watoto wengi wa kiroho. Kwa mfano, kutaniko la Eldoret lilikua kutoka wahubiri 45 hadi kufikia 129 kwa miaka minne tu kwa msaada wa wamishonari. Masilahi ya Ufalme yaliendelea kusonga mbele huku roho ya upainia ikizidi kuongezeka. Zaidi ya saa milioni 1.5 zilitumiwa shambani katika 1987, na wahubiri zaidi ya 4,000 walikuwa wakitenda, kila mmoja akitumia saa 16.4 kwa wastani kila mwezi.

Hudhurio la Ukumbusho liliongezeka kufikia 15,683, na watu 466 walibatizwa pia. Zaidi ya 1,000 kwa wastani walikuwa wakifanya utumishi wa upainia kila mwezi, na zaidi ya 500 kati yao walikuwa mapainia wa kawaida. Majumba ya Ufalme mapya yalijengwa, na ramani za jengo jipya la kusanyiko ambalo lingekuwa viungani mwa jiji la Nairobi zilichorwa. Kwa mara ya kwanza kulikuwa na wahubiri zaidi ya 10,000 chini ya uangalizi wa ofisi ya tawi, kutia ndani na mapainia wa kawaida 1,000. Ndipo jambo la kushtusha likatukia.

Marufuku Nyingine

Upesi baada ya kumalizwa kwa makusanyiko ya mzunguko yaliyozungumzia majaribu ya imani, na wakati ambapo mipango ilikuwa inafanywa kwa ajili ya “Tumaini Katika Yehova” Mikusanyiko ya Wilaya, tumaini hilo liliwekwa katika jaribu kali. Siku ya Novemba 19, 1987, taarifa ya kisheria yenye tarehe ya Novemba 9 ilitokea katika gazeti rasmi la Kenya Gazette ikitaarifu juu ya kufutwa kwa usajili wa Association of Jehovah’s Witnesses in East Africa ambalo limekuwa likitenda kwa zaidi ya miaka 25. Amri hiyo iliruhusu siku 21 za kukamilisha mambo na kugawanya mali yao kati ya washirika. Alasiri iyo hiyo, barua kutoka kwa msajili mkuu ilithibitisha uamuzi huo uliochukuliwa. Hakuna sababu zozote zilizotolewa.

Kesho yake asubuhi, gazeti mojawapo liliripoti jambo hilo likiwa jambo dogo katika ukurasa wa 5, bali si kama kichwa kikuu kama ilivyokuwa kwa ile marufuku ya 1973. Lakini mashirika ya habari ya nchi za nje yalipiga simu mara hiyo na kisha yakatangaza habari hiyo ya kushtua. Mara hiyo jitihada zilifanywa za kuwaona maofisa wa serikali, lakini hao ama walishughulika mno na ziara ya mgeni mashuhuri ama hawakutaka kuzungumzia jambo hilo.

Ushauri wa kisheria ulitafutwa, na baada ya sala nyingi, rufani ilikatwa. Siku ya Novemba 27 hakimu mmoja aliamua kwamba kesi hiyo ingeweza kusikilizwa, jambo lililorudishia Shirika hilo uhalali mpaka uamuzi ufikiwe na mahakama. Hivyo, mikutano na utendaji wa mahubiri uliendelea waziwazi kotekote Kenya, ukitoa kitulizo cha muda kwa wakati huo.

Vipi juu ya mikusanyiko? Imani ilihitajiwa ili kuendelea mbele na mipango, lakini ilikuwa ni furaha kama nini kupata kibali kwa mambo yote yaliyohitajiwa! Baada ya matatizo kidogo, mahali pa kufanya mikusanyiko palipatikana, na hivyo “Tumaini Katika Yehova” Mikusanyiko ya Wilaya yote mitatu ilifanywa katika mwezi wa Desemba. Hudhurio nchini kote lilifikia jumla ya watu 10,177 na 288 wakabatizwa.

Baada ya hapo, hali ilionekana kuwa ya kawaida. Mashahidi walijua wazi kwamba mambo sasa yalibaki mikononi mwa Yehova hasa juu ya wakati ujao wa ofisi ya tawi na kazi nchini Kenya.

Hali ya kisheria imebaki katika hali hiyo ya kungojea kwa miaka mingi, huku mahakama ikiahirisha kesi hiyo mara nyingi. Jambo hilo lilitokeza visa vingi katika sehemu mbalimbali, ambapo maofisa pasipo kujua uhalali wetu, walishika akina ndugu, wakakawiza vyeti vya kutoa ruhusa, au kuzuia makusanyiko ya mzunguko yasifanywe. Wakati uo huo makasisi wa Jumuiya ya Wakristo wameendelea kujiingiza zaidi na zaidi katika siasa, jambo ambalo limesaidia wengi kuona tofauti kati ya makasisi na Mashahidi watiifu kwa sheria na wenye kupenda amani.

Matokeo yamekuwa ni maongezeko zaidi ya wapiga mbiu ya Ufalme. Karibu na wakati wa Ukumbusho wa 1991, kulikuwa na wahubiri karibu 6,000 nchini, na 19,644 walihudhuria mwadhimisho huo. Majumba ya Kusanyiko yamejengwa katika Nairobi na Nanyuki, mji ulio katika ikweta. Ongezeko hilo la wahubiri limeweka mzigo mkubwa zaidi kwenye ofisi ya tawi, na kufanya familia ya Betheli iongezeke kuwa na washiriki 38, na kuna uhitaji mkubwa wa kupanua jengo lililopo.

Kutazama Wakati Ujao kwa Tumaini Katika Yehova

Nafasi hairuhusu kutaja matukio mengine mengi ya maana na maono ya kusisimua katika Afrika Mashariki. Waaminifu wengine wengi wamejitumikisha kwa ajili ya habari njema na kupatwa na mabaya wakiwa watumishi wa Mungu wa kweli. Wengi wamechukua madaraka mazito na kama ilivyokuwa kwa Paulo, wamehangaikia maekutaniko kwa miaka mingi. (2 Kor. 11:28) Matatizo ya kiuchumi, ya kisheria, na ya kisiasa yaendelea. Suluhisho la kudumu kwa matatizo hayo yote litaletwa na Ufalme wa Yehova pekee, na kwa wakati huu, kazi kubwa ya kukusanya ingali inabaki kutimizwa.

Idadi ya watu katika sehemu hii ya dunia imekuwa maradufu katika miaka 20 iliyopita. Kufikia Agosti wa 1991, nchi zote chini ya ofisi ya tawi zilikuwa na jumla ya wahubiri 15,970. Ofisi ya tawi inataarifu hivi: “Tunajua kwamba Yehova anajua kondoo wake na twasali kwamba ‘neno la [Yehova] liendelee’ kabla ya mwisho unaokuja kwa kasi na wakati ambapo eneo hili zuri la dunia, likiwa na maajabu yalo yote ya uumbaji, litakuwa sehemu ya paradiso halisi ya duniani pote.”—2 The. 3:1.

[Maelezo ya Chini]

^ Utawala wa kikoloni ulipoisha katika Afrika, majina ya nchi nyingi zinazotajwa hapa yalibadilika. Rhodesia ya Kaskazini ilikuja kuwa Zambia; Rhodesia ya Kusini ikawa Zimbabwe; Tanganyika ikawa Tanzania; Urundi ikawa Burundi; Nyasaland ikawa Malawi; na Kongo ya Ubelgiji ikawa Zaire.

^ Masimulizi ya maisha ya George Nisbet yalitokea katika toleo la Agosti 1, 1974 la Mnara wa Mlinzi (Kiingereza).

^ Masimulizi ya maisha yake yalitokea katika toleo la Mei 1, 1985, la Mnara wa Mlinzi (Kiingereza).

^ Kwa maelezo zaidi ona masimulizi ya historia ya Afrika Kusini katika Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova cha 1976, (Kiingereza).

^ Barbara Hardy alikufa katika Februari 1988 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

^ Mara nyingi jina la kwanza la mtu ndilo hutumiwa katika Ethiopia.

[Chati katika ukurasa wa 206]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa.)

Kenya 8,000

1950 3

1960 108

1970 947

1980 2,266

1991 6,300

Kilele cha Wahubiri

2,000

1950

1960 5

1970 132

1980 317

1991 1,256

Wast. Mapainia

[Chati katika ukurasa wa 207]

(Ona mpangilio kamili kataka nakala iliyochapishwa.)

Nchi Tisa Zilizo Chini ya Tawi la Kenya

17,000

1950 119

1960 865

1970 2,822

1980 5,263

1991 15,970

Kilele cha Wahubiri

4,000

1950 1

1960 49

1970 296

1980 599

1991 3,127

Wast. Mapainia

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 66]

(Ona mpangilio kamili kataka nakala iliyochapishwa.)

Bahari Nyekundu

Ghuba ya Adeni

YEMEN

SUDAN

Naili

Omdurman

Khartoum

Eritrea

Asmara

DJIBOUTI

ETHIOPIA

Addis Ababa

SOMALIA

Mogadishu

KENYA

Nairobi

Mombasa

IKWETA

Ziwa Viktoria

UGANDA

Kampala

ZAIRE

RWANDA

BURUNDI

TANZANIA

Zanzibar

Dar es Salaam

Mbeya

MALAWI

ZAMBIA

Bahari ya Hindi

USHELISHELI

MADAGASKA

[Sanduku]

KENYA

Jiji Kuu: Nairobi

Lugha Rasmi: Kiswahili na Kiingereza

Dini Kubwa: Imani tofauti-tofauti

Idadi ya Watu: 24,000,000

Ofisi ya Tawi: Nairobi

[Picha katika ukurasa wa 69]

Wachungaji wachanga nchini Kenya

[Picha katika ukurasa wa 71]

Kenya, makao ya wanyama wanaopendeza

[Picha katika ukurasa wa 74]

Olga Smith na watoto wake wawili wakiaga mume wake, Gray na ndugu yake Frank mwanzoni mwa safari yao ya meli kuelekea Afrika Mashariki

Frank Smith akiwa Nairobi, karibu na katikati ya mji katika 1931

Gray Smith akitoa ushahidi nchini Kenya mwaka 1931

[Picha katika ukurasa wa 76]

David Norman na Robert Nisbet wakiwa Durban, Afrika Kusini, mwaka wa 1931, kabla tu ya kuondoka kwa meli kuelekea Dar es Salaam

[Picha katika ukurasa wa 79]

George Nisbet, Gray na Olga Smith, pamoja na Robert Nisbet wakivuka Mto Limpopo na kutua njiani inayoelekea

[Picha katika ukurasa wa 88]

Kukutana tena kwa “wakale” kunywa kahawa na chai karibu na Nairobi: kutoka kushoto ni Muriel Nisbet, Margaret Stephenson, Vera Palliser, Mary Whittington, na William Nisbet

[Picha katika ukurasa wa 93]

Ingilizi Caliopi pamoja na Mary Girgis, katika Khartoum, Sudan

[Picha katika ukurasa wa 96]

Wamishonari wa Gileadi: Dean Haupt na Haywood Ward katika Addis Ababa

[Picha katika ukurasa wa 99]

Ofisi ndogo ya tawi ya Ethiopia katika Addis Ababa katika 1953

[Picha katika ukurasa wa 105]

Hosea Njabula na mke wake, Leya, walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutangaza habari njema katika Tanzania

[Picha katika ukurasa wa 107]

Watu tisa kati ya wale waliojifunza kweli kusini mwa Tanzania wakati wa miaka ya 1930. Kutoka kushoto kwenda kulia: Andrew Chungu, Obeth Mwaisabila, Timothy na Ana Kafuko, Leya Nsile, Joram Kajumba, Jimu Mwaikwaba, Stela na Semu Mwasakuna

[Picha katika ukurasa wa 108]

Thomson Kangale, mwalimu mwenye subira wa ndugu zake wa Afrika Mashariki

[Picha katika ukurasa wa 123]

George Kadu na Margaret Nyende wakumbuka siku za mapema katika Uganda, waliposikia kweli zaidi ya miaka 35 iliyopita

[Picha katika ukurasa wa 131]

Makao ya wamishonari ya kwanza Kenya na ofisi ya tawi ya Nairobi ilifunguliwa Februari 1, 1963

[Picha katika ukurasa wa 139]

Katika mwaka wa 1965, ofisi ya tawi ya pili ya Kenya katika Nairobi ilikuwa kwenye orofa, na iliyo chini ni picha ya upande wa nyuma wa ofisi ya tawi ya tatu katika mwaka wa 1970 kabla ya kupanuliwa

[Picha katika ukurasa wa 141]

Lamond Kandama, painia wa pekee mtendaji katika Zambia, Tanzania, na Kenya kwa miaka zaidi ya 50, pamoja na Esinala na Stanley Makumba, ambao wametumikia kwa zaidi ya miaka 40 katika utumishi wa pekee katika Uganda na Kenya, sana-sana katika kazi ya kusafiri

[Picha katika ukurasa wa 142]

John na Kay Jason, wakiwa Betheli ya Nairobi, wametumikia zaidi ya miaka 50 kila mmoja katika utumishi wa wakati wote

[Picha katika ukurasa wa 157]

Kikundi cha Wanyarwanda chenye furaha baada ya kubatizwa kwao

[Picha katika ukurasa wa 158]

Anna Nabulya, mmoja wa wahubiri wastahimilivu nchini Uganda

[Picha katika ukurasa wa 169]

Gebregziabher Woldetnsae, mwangalizi aliyejitumikisha hadi kifo chake

[Picha katika ukurasa wa 177]

Nyuso tunazotumaini kuona katika ufufuo. Wote waliuawa kwa sababu ya uaminifu wao kwa habari njema. Kutoka juu kushoto: Ayele Zelelew, Hailu Yemiru, Wubie Ayele, Kaba Ayana, Gebreyohanes Adhanom, Adera Teshome, Wondimu Demera, Kasa Gebremedhin, Eshetu Mindu

[Picha katika ukurasa wa 192]

Gaspard Rwakabubu, Joseph Koroti, na Ferdinand I’Mugarula baada ya wao kufunguliwa kutoka gerezani mjini Kigali, walifurahia kuhudhuria mkusanyiko wa kimataifa katika Nairobi mwaka wa 1985

[Picha katika ukurasa wa 199]

Kusanyiko la mzunguko, Mbale, Uganda, 1987

[Picha katika ukurasa wa 201]

Ofisi ya tawi na makao ya Betheli ya sasa ya Kenya mjini Nairobi baada ya upanuzi

[Picha katika ukurasa wa 202]

Bernard Musinga alitumia miaka 20 katika Afrika Mashariki katika kazi ya kusafiri na alikuwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi kabla ya kurudi kwao Zambia