Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 6

Mwana Mzuri na Mbaya

Mwana Mzuri na Mbaya

TAZAMA Kaini na Habili sasa. Wote wawili wamekuwa wakubwa. Kaini amekuwa mkulima. Anakuza nafaka na matunda na mboga.

Habili amekuwa mwenye kufuga kondoo. Anapenda kuchunga kondoo wadogo. Wamekuwa kondoo wakubwa, na upesi Habili ana kundi zima la kondoo wa kuchunga.

Siku moja Kaini na Habili walimletea Mungu zawadi. Kaini analeta chakula alichokuza. Na Habili analeta kondoo bora zaidi. Yehova anapendezwa na Habili na zawadi yake. Hapendezwi na Kaini na zawadi yake. Unajua sababu?

Si kwa sababu zawadi ya Habili ni bora kuliko ya Kaini tu. Habili ni mtu mzuri. Anampenda Yehova na ndugu yake. Kaini ni mbaya; hapendi ndugu yake.

Basi Mungu anamwambia Kaini kwamba ni lazima ageuze njia zake. Kaini anakataa. Anakasirika sana kwa sababu Mungu anampenda Habili kuliko yeye. Kwa hiyo Kaini anamwambia Habili hivi, ‘twende kule shambani.’ Halafu, wakiwa huko peke yao, Kaini anampiga Habili ndugu yake. Anampiga sana na kumwua. Kaini alifanya vibaya sana, sivyo?

Ijapo Habili alikufa, Mungu anamkumbuka. Habili alikuwa mtu mzuri, naye Yehova hasahau mtu kama huyo. Kwa hiyo, siku moja Yehova Mungu atamfufua Habili hatakufa tena. Atakaa milele hapa duniani. Je! itakuwa vizuri kujua watu kama Habili?

Lakini Mungu hapendi watu kama Kaini. Kaini alipokwisha kumwua ndugu yake, Mungu alimpa adhabu ya kumfukuzia mbali na jamaa yake. Kaini alipoondoka kukaa sehemu nyingine ya dunia, alichukua mmoja wa dada zake, akawa mke wake.

Kisha Kaini na mke wake wakaanza kuzaa watoto. Wana na binti wengine wa Adamu na Hawa waliolewa, nao wakazaa watoto. Upesi kukawa watu wengi duniani. Na tujifunze habari zao.