Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 33

Kuvuka Bahari Nyekundu

Kuvuka Bahari Nyekundu

TAZAMA tukio hili! Yule ni Musa akiwa na fimbo imenyoshwa juu ya Bahari Nyekundu. Wale walio pamoja naye salama upande mwingine ni Waisraeli. Lakini Farao na jeshi lake lote wanazama katika bahari. Na tuone ilivyokuwa.

Kama tulivyojifunza, Farao aliwaambia Waisraeli waondoke Misri Mungu alipokwisha kuleta pigo la 10 juu ya Wamisri. Wanaume Waisraeli karibu 600,000 wakaondoka, pia wanawake na watoto wengi. Pia, hesabu kubwa ya watu wengine, waliokuwa wamemwamini Yehova, wakaondoka pamoja na Waisraeli. Wote walichukua kondoo na mbuzi na ng’ombe zao wakaenda nazo.

Kabla ya kuondoka, Waisraeli waliwaomba Wamisri wawape mavazi na vitu vya dhahabu na fedha. Wamisri hao waliogopa sana, kwa sababu ya lile pigo la mwisho lililowapata. Basi wakawapa Waisraeli kila kitu walichowaomba.

Baada ya siku chache Waisraeli wakafika kwenye Bahari Nyekundu. Wakapumzika huko. Wakati huo, Farao na watu wake walianza kuhuzunika kwa vile wamewafukuza Waisraeli. ‘Tumeacha watumwa wetu wakaenda!’ wakasema.

Hivyo Farao akabadili tena nia yake. Upesi akatayarisha gari lake la vita na jeshi lake. Kisha akaanza kuwafuatia Waisraeli akiwa na magari ya pekee 600, pia magari mengine yote ya Misri.

Waisraeli walipomwona Farao na jeshi lake wakiwafuata, waliogopa sana. Hakukuwa na njia ya kukimbilia. Ile Bahari Nyekundu ilikuwa upande wao mmoja na Wamisri upande mwingine. Lakini Yehova aliweka wingu kati ya watu wake na Wamisri. Hivyo Wamisri hawakuweza kuwaona Waisraeli wawashambulie.

Kisha Yehova akamwambia Musa anyoshe fimbo yake juu ya Bahari Nyekundu. Alipoinyosha, Yehova akafanya upepo wenye nguvu wa mashariki uvume. Yale maji ya bahari yalitengana, yakasimama pande mbili.

Ndipo Waisraeli wakaanza kutembea katika bahari katika nchi kavu. Ilichukua saa nyingi ili mamilioni ya watu pamoja na wanyama wao wapite salama katika bahari kwenda upande mwingine. Mwishowe Wamisri waliweza kuwaona Waisraeli tena. Watumwa wao walikuwa wakikimbia! Basi wakaingia haraka katika bahari wakiwafuata.

Walipoingia, Mungu alifanya magurudumu ya magari yao yatoke. Wamisri wakaanza kuogopa na kupaza sauti hivi: ‘Yehova anawapigania Waisraeli. Na tuondoke huku!’ Lakini walikuwa wamechelewa.

Wakati huo ndipo Yehova alipomwambia Musa anyoshe fimbo yake juu ya Bahari Nyekundu, kama ulivyoona katika picha. Musa alipofanya hivyo, zile kuta zilianza kurudi na kuwafunika Wamisri na magari yao. Jeshi lote lilikuwa limewafuata Waisraeli katika bahari. Hakuna hata mmoja wa Wamisri hao aliyeokoka!

Lo! watu wote wa Mungu walifurahi kwa vile walivyookoka! Wanaume wakaimba wimbo wa kumshukuru Yehova, wakisema: ‘Yehova amepata ushindi mtukufu. Amewatupa farasi na wanaowapanda baharini.’ Miriamu dada ya Musa akachukua matari yake, nao wanawake wote wakamfuata wakiwa na matari yao. Na walipokuwa wakicheza kwa furaha, waliimba wimbo ule ule walioimba wanaume wakisema: ‘Yehova amepata ushindi mtukufu. Amewatupa farasi na wanaowapanda baharini.’