Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 19

Yakobo Ana Jamaa Kubwa

Yakobo Ana Jamaa Kubwa

EBU tazama jamaa hii kubwa. Hawa ni wana 12 wa Yakobo. Ana binti pia. Unajua majina ya watoto hao? Na tujifunze majina yao.

Lea alizaa Reubeni, Simeoni, Levi na Yuda. Raheli alipoona kwamba hakuzaa watoto, alihuzunika. Basi akampa Yakobo Bilha, mtumishi wake naye Bilha akazaa wana wawili walioitwa Dani na Naftali. Kisha Lea pia akampa Yakobo Zilpa mtumishi wake, naye Zilpa akazaa Gadi na Asheri. Mwishowe Lea akazaa wana wengine wawili, Isakari na Zebuloni.

Halafu Raheli alizaa mtoto. Akamwita jina Yusufu. Baadaye tutajifunza mengi juu ya Yusufu, kwa sababu akawa mtu mkubwa sana. Hao ndio wana 11 wa Yakobo alipokuwa anakaa na Labani baba ya Raheli.

Yakobo pia alikuwa na mabinti fulani, lakini Biblia inataja jina la mmoja tu, Dina.

Ukafika wakati ambapo Yakobo aliamua kumwacha Labani arudi Kanaani. Akakusanya jamaa yake kubwa na kondoo wake wengi na ng’ombe, akaanza safari ndefu.

Muda kidogo Yakobo na jamaa yake waliporudi Kanaani, Raheli alizaa mwana mwingine. Alizaa walipokuwa katika safari. Raheli alipata taabu kisha akafa alipokuwa akizaa. Lakini mtoto huyo mchanga alipona. Yakobo akamwita Benyamini.

Tunataka tuyakumbuke majina ya wana 12 wa Yakobo kwa sababu taifa zima la Israeli lilitokana nao. Makabila 12 ya Israeli yanaitwa kwa majina ya wana 10 wa Yakobo na wana wawili wa Yusufu. Isaka alikaa miaka mingi baada ya kuzaliwa watoto hao wa kiume, na bila shaka alifurahi sana kuwa na wajukuu wengi sana. Lakini na tuone yaliyompata Dina, mjukuu wake.