Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 61

Daudi Anafanywa Mfalme

Daudi Anafanywa Mfalme

TENA Sauli anajaribu kumkamata Daudi. Anachukua askari wake bora zaidi 3,000 na kwenda kumtafuta. Daudi anapojua hivyo, anatuma wapelelezi ajue mahali ambapo Sauli na watu wake wamepiga kambi walale usiku. Ndipo Daudi anawaambia watu wake hivi: ‘Ni nani atakayekwenda pamoja nami kenye kambi ya Sauli?’

‘Mimi,’ Abishai anajibu. Abishai ni mwana wa Seruya dada yake Daudi. Wakati Sauli na watu wake wamelala, Daudi na Abishai wanaingia kambini kimya-kimya. Wanachukua mkuki na mtungi wa Sauli. Hakuna mtu anayeona wala kuwasikia kwa sababu wote wamelala sana.

Ebu mwone sasa Daudi na Abishai. Wamekwisha kwenda mbali, nao wako salama juu ya kilima. Daudi anampazia sauti mkuu wa jeshi la Israeli hivi: ‘We-e Abneri, sababu gani humlinda bwanako, mfalme? Tazama! Mkuki na mtungi wake viko wapi?’

Sauli anaamka. Aitambua sauti ya Daudi, kisha auliza: ‘Ni wewe, Daudi?’ Unaweza kumona Sauli na Abneri chini kule?

‘Ndiyo, bwanangu mfalme,’ Daudi amjibu Sauli. Naye Daudi auliza hivi: ‘Kwa nini wataka kunikamata? Nimefanya ubaya gani? Mkuki wako huu, Ee mfalme. Mtume mmoja wa watu wako aje auchukue.’

‘Nimekosa,’ Sauli anakubali. ‘Nimetenda kipumbavu.’ Ndipo Daudi anakwenda zake, naye Sauli anarudi kwake. Lakini Daudi anajisemesha hivi: ‘Siku fulani Sauli ataniua mimi. Yanipasa nikimbie niende kwenye nchi ya Wafilisti.’ Anafanya hivyo. Daudi anapumbaza Wafilisti na kuwafanya waamini yuko upande wao.

Wakati fulani baadaye Wafilisti wanakwenda kupigana na Israeli. Huko vitani, Sauli na Yonathani wanauawa. Hilo lamhuzunisha Daudi sana, naye anaandika wimbo mzuri, akiimba hivi: ‘Naona huzuni kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani. Jinsi nilivyokupenda!’

Baada ya hayo Daudi anarudi Israeli kwenye mji Hebroni. Kwatokea vita kati ya watu wanaochagua Ishboshethi mwana wa Sauli, awe mfalme, na watu wegine wanaotaka Daudi awe mfalme. Lakini Mwishowe watu wa Daudi wanashinda. Sasa Daudi ni mwenye miaka 30 anapofanywa kuwa mfalme. Anatawala katika Hebroni kwa miaka saba na nusu.

Wakati wafika wa Daudi na watu wake kwenda kuteka mji mzuri unaoitwa Yerusalemu. Yoabu, mwana mwingine wa Seruya, dada yake Daudi, anaongoza vita. Basi Daudi anamfanya Yoabu kuwa mkuu wa jeshi lake. Sasa Daudi anaanza kutawala katika mji wa Yerusalemu.