HADITHI YA 62
Matata Katika Nyumba ya Daudi
BAADA ya Daudi kuanza kutawala katika Yerusalemu, Yehova analipa jeshi lake ushindi mwingi juu ya adui zao. Yehova alikuwa ameahidi kuwapa Waisraeli nchi ya Kanaani. Na sasa, kwa msaada wa Yehova, nchi yote waliyoahidiwa inakuwa yao.
Daudi ni mtawala mzuri. Anampenda Yehova. Basi baada ya kuuteka Yerusalemu, kwanza anapeleka sanduku la agano huko. Tena anataka kujenga hekalu aweke sanduku humo.
Daudi anapokuwa mzee kidogo, anafanya kosa baya. Daudi anajua kwamba ni vibaya kuchukua kitu cha mwingine. Lakini usiku mmoja, anapokuwa katika dari ya jumba lake la kifalme, anamwona mwanamke mzuri sana. Jina lake ni Bath-sheba, na mume wake ni Uriya, mmoja wa askari zake.
Daudi anamtaka Bath-sheba sana sana. Basi anaagiza aletwe kwenye jumba lake la kifalme. Mume wake amekwenda vitani. Daudi analala naye, kisha anaona amepata mimba. Daudi anapata wasiwasi mwingi. Anampelekea Yoabu mkuu wa jeshi ujumbe ili Uriya awekwe mbele ya pigano ambapo atauawa. Uriya anapokufa, Daudi anamwoa Bath-sheba.
Yehova anamkasirikia Daudi sana. Anamtuma Nathani mtumishi wake akamwambie dhambi zake. Unamwona hapa Nathani akizungumza na Daudi. Daudi anatubu makosa aliyofanya, kwa hiyo Yehova hamwui. Lakini Yehova anasema: ‘Kwa kuwa umefanya mabaya haya, utakuwa na matata mengi nyumbani mwako.’ Na Daudi anapata matata wee!
Kwanza, mwana wa Bath-sheba anakufa. Kisha Am’noni mzaliwa wa kwanza wa Daudi amchukua Tamari dada yake wakiwa peke yao na kumlala kinguvu. Absalomu mwana wa Daudi anakasirika sana hata anamwua Am’noni. Baadaye, Absalomu anapendwa na watu wengi, na kujifanya mfalme. Mwishowe, Daudi anashinda Absalomu katika kupigana, naye auawa. Ndiyo, Daudi amepata matata mengi.
Wakati huo, Bath-sheba anazaa mwana mwingine jina lake Sulemani. Daudi anapokuwa mzee na mgonjwa, Adoniya mwanawe, anataka kujifanya mfalme. Kwa hiyo Daudi anaagiza kuhani Sadoki amwage mafuta kichwani pa Sulemani, kuonyesha kwamba Sulemani atakuwa mfalme. Mara baada ya hayo, Daudi anakufa akiwa na miaka 70. Alitawala kwa miaka 40, lakini sasa Sulemani ndiye mfalme wa Israeli.