Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 65

Ufalme Unagawanywa

Ufalme Unagawanywa

UNAJUA sababu gani mtu huyu anapasua vazi lake vipande vipande? Yehova alimwambia alipasue. Mtu huyu ni Ahiya, nabii wa Mungu. Unajua nabii ni nani? Ni mtu anayeambiwa mapema na Mungu mambo yatakayotokea.

Hapa Ahiya anasema na Yeroboamu. Yeroboamu ni mtu ambaye Sulemani ameweka asimamie kazi yake ya kujenga. Ahiya anapokutana na Yeroboamu hapa njiani, Ahiya anafanya jambo geni. Anachukua vazi jipya alilokuwa akivaa na kulipasua vipande 12. Anamwambia Yeroboamu hivi: ‘Chukua vipande 10.’ Unajua sababu Ahiya anampa Yeroboamu vipande 10?

Ahiya anaeleza kwamba Yehova atamnyang’anya Sulemani ufalme. Anasema kwamba Yehova atampa Yeroboamu makabila 10. Maana yake Rehoboamu mwana wa Sulemani ataachiwa makabila mawili tu ya kutawala.

Wakati Sulemani anaposikia Ahiya alivyomwambia Yeroboamu, anakasirika sana. Anajaribu kumwua Yeroboamu. Lakini Yeroboamu anakimbilia Misri. Muda mfupi Sulemani anakufa. Alitawala kwa miaka 40 lakini sasa Rehoboamu mwanawe anafanywa mfalme. Huko Misri Yeroboamu anasikia kwamba Sulemani amekufa, basi anarudi Israeli.

Rehoboamu si mfalme mzuri. Anatendea watu vibaya kuliko Sulemani babaye. Yeroboamu na wanaume wengine wakubwa wanamwendea Mfalme Rehoboamu na kumwomba awatendee watu vizuri zaidi. Lakini Rehoboamu anakataa kusikiliza. Anazidi kuwa mbaya kuliko zamani. Basi watu wanamfanya Yeroboamu mfalme wa makabila 10, lakini makabila mawili ya Benyamini na Yuda yanataka Rehoboamu aendelee kuwa mfalme wao.

Yeroboamu hataki watu wake waende Yerusalemu kuabudu katika hekalu la Yehova. Basi anafanya ndama wawili wa dhahabu na kuwaagiza watu wa makabila 10 waabudu. Upesi nchi inajaa uhalifu na jeuri.

Pia matata yanatokea katika ufalme wa makabila mawili. Muda usiozidi miaka mitano baada ya Rehoboamu kuwa mfalme, mfalme wa Misri anakuja kuupiga Yerusalemu. Anachukua mali nyingi katika hekalu la Yehova. Basi hali ya kwanza ya hekalu inaendelea kwa muda mfupi tu.