Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 81

Kuutumainia Msaada wa Mungu

Kuutumainia Msaada wa Mungu

Maelfu ya watu wanafunga safari ndefu kutoka Babeli kwenda Yerusalemu. Lakini wanapofika, Yerusalemu umeharibiwa sana. Hakuna anayeishi huko. Inawapasa Waisraeli wajenga upya kila kitu.

Kwanza wanajenga madhabahu. Hapo ni mahali wanapoweza kumtolea Yehova zawadi za wanyama. Miezi michache baadaye Waisraeli wanaanza kujenga hekalu. Lakini adui wanaoishi katika nchi jirani hawataki Waisraeli walijenge. Basi wanajaribu kuwaogopesha waache. Mwishowe, adui hao wanamshauri mfalme mpya wa Ajemi atunge sheria ya kuzuia kazi ya kujenga.

Miaka yapita. Sasa imekuwa miaka 17 tangu Waisraeli waliporudi kutoka Babeli. Yehova anatuma manabii wake Hagai na Zekaria wawaambie watu waanze kujenga tena. Watu hao wanautumainia msaada wa Mungu, nao wanawatii manabii hao. Wanaanza kujenga tena, ijapo sheria inawakataza.

Basi Tatenai Mwajemi, mkuu wa serikali, anakuja kuwauliza Waisraeli kama wana ruhusa ya kujenga hekalu. Waisraeli wanamwambia kwamba Mfalme Koreshi aliwaambia: ‘Nendeni, Yerusalemu, mkamjengee Yehova, Mungu wenu hekalu.’

Tatenai anapeleka barua Babeli na kuuliza kama kweli Koreshi ambaye sasa amekufa, alisema hivyo. Upesi mfalme mpya wa Ajemi anarudisha majibu. Majibu ya barua yanakubali. Basi mfalme anaandika hivi: ‘Waacheni Waisraeli wamjengee Mungu wao hekalu. Nawaamuru mwasaidie.’ Hekalu linamalizika baada ya miaka minne hivi. Waisraeli wanafurahi sana.

Miaka mingine mingi yapita. Sasa ni karibu miaka 48 tangu hekalu hilo lilipomalizika. Watu wa Yerusalemu ni maskini, na mji umeharibika pamoja na hekalu la Mungu. Huko Babeli, Ezra anajua kuna uhitaji wa kutengeneza hekalu la Mungu.

Ezra anakwenda kumwona Ar·ta·ksase (Artasasta), mfalme wa Ajemi. Mfalme huyo mzuri anampa Ezra zawadi nyingi apeleke Yerusalemu. Ezra anawaomba Waisraeli walio Babeli wamsaidie kwenda. Wanachukua fedha na dhahabu nyingi na vitu vingine vya bei.

Ezra anahangaika, kwa sababu njiani kuna watu wabaya. Labda watu hao watawanyang’anya fedha na dhahabu na kuwaua. Basi Ezra anakusanya watu, kama unavyoona katika picha. Kisha wanamwomba Yehova awalinde katika safari yao ndefu ya kurudi Yerusalemu.

Yehova awalinda. Na baada ya miezi minne ya kusafiri, wanafika salama Yerusalemu. Yehova anaweza kulinda wale wanaotumainia msaada wake, sivyo?