Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 82

Mordekai na Esta

Mordekai na Esta

TURUDI kwenye miaka michache kabla Ezra hajaenda Yerusalemu. Mordekai na Esta (Esiteri) ni Waisraeli wenye vyeo vya juu katika ufalme wa Ajemi. Esta ndiye malkia, na Mordekai binamu yake ni wa pili kwa mfalme katika mamlaka. Na tuone hayo yalivyotokea.

Wazazi wa Esta walikufa wakati alipokuwa mtoto mdogo sana, Mordekai akamlea. A·has·ueʹro, mfalme wa Ajemi, ana jumba la kifalme mjini Shuʹshani, naye Mordekai ni mmoja wa watumishi wake. Basi, siku moja Vashʹti mke wa mfalme anakataa kumtii, hivyo mfalme anachagua mke mwingine awe malkia wake. Unajua anachagua mwanamke gani? Esta msichana mrembo.

Wamwona mtu huyu mwenye kiburi anayeinamiwa na watu? Ni Hamani. Ana cheo cha juu katika Ajemi. Hamani anataka Mordekai, unayeona ameketi hapa, amwinamie pia. Lakini Mordekai anakataa. Haoni yafaa kumwinamia mtu huyo mbaya. Hilo linamkasirisha sana Hamani. Basi anafanya hivi.

Hamani anamwambia mfalme uongo juu ya Waisraeli. “Ni watu wabaya wasiotii sheria zako,’ asema. ‘Wanapaswa kuuawa.’ A·has·ueʹro hana habari kwamba Esta mkewe ni Mwisraeli. Basi amsikiliza Hamani, na kuagiza sheria itungwe Waisraeli wauawe siku fulani.

Mordekai anapopata habari ya sheria hiyo, anaona vibaya sana. Anampelekea Esta ujumbe huu: ‘Lazima umwambie mfalme, na kumwomba atuokoe.’ Ni kinyume cha sheria katika Ajemi kumwona mfalme bila kuitwa. Lakini Esta aingia bila kuitwa. Mfalme amnyoshea fimbo yake ya dhahabu, maana yake asiuawe. Esta anamwalika mfalme na Hamani kwenye karamu. Wakiwa huko mfalme amwuliza Esta anachotaka mfalme ampe. Esta asema atamwambia ikiwa yeye na Hamani watakuja kwenye karamu nyingine kesho yake.

Katika karamu hiyo Esta amwambia mfalme hivi: ‘Watu wangu na mimi tutauawa.’ Mfalme anakasirika. ‘Nani anathubutu kufanya hivyo?’ auliza.

‘Mtu huyo, adui huyo, ndiye huyu Hamani mbaya!’ Esta asema.

Sasa mfalme akasirika kweli kweli. Anaamuru Hamani auawe. Kisha, mfalme anampa Mordekai cheo cha pili katika mamlaka. Ndipo Mordekai anahakikisha sheria mpya itungwe kuruhusu Waisraeli wapiganie uhai wao siku ambayo wangeuawa. Kwa kuwa sasa Mordekai ana cheo, watu wengi wanasaidia Waisraeli, nao wanaokolewa na adui zao.

Kitabu cha Biblia cha Esta (Esiteri).