HADITHI YA 78
Mwandiko wa Mkono Ukutani
KUNA nini hapa? Watu wanakula karamu kubwa. Mfalme wa Babeli amealika wageni elfu wa heshima. Wanatumia vikombe vya dhahabu na fedha na mabakuli yaliyochukuliwa katika hekalu la Yehova huko Yerusalemu. Lakini, ghafula, vidole vya mkono wa mtu vinatokea hewani na kuanza kuandika ukutani. Kila mtu anaogopa.
Belshaza (Belsasari), mjukuu wa Nebukadreza, ndiye mfalme sasa. Anapaza sauti watu wake wa akili waletwe. ‘Mtu anayeweza kusoma mwandiko huu na kuniambia maana yake,’ mfalme asema, ‘atapewa zawadi nyingi na kufanywa mtawala wa tatu wa maana zaidi katika ufalme.’ Lakini hakuna mtu anayeweza kuusoma mwandiko ukutani, wala kutoa maana yake.
Mama ya mfalme anasikia kelele naye anaingia katika jumba la chakula. ‘Tafadhali usiogope sana,’ amwambia mfalme. ‘Kuna mtu katika ufalme wako anayejua miungu mitakatifu. Babu yako Nebukadreza alipokuwa mfalme alimfanya mkuu wa watu wake wote wa akili. Jina lake Danieli. Agiza akaitwe, naye atakuambia maana yote hiyo.’
Basi mara hiyo Danieli analetwa. Baada ya kukataa kupokea zawadi, Danieli anaanza kueleza kwa nini wakati mmoja Yehova alimwondoa Nebukadreza babu ya Belshaza asiwe mfalme. ‘Alikuwa na kiburi sana,’ Danieli asema. ‘Naye Yehova akamwadhibu.’
‘Lakini wewe,’ Danieli amwambia Belshaza, ‘ulijua yote yaliyompata, na bado una kiburi kama Nebukadreza. Umechukua vikombe na mabakuli katika hekalu la Yehova na kuvinywea. Umesifu miungu ya miti na mawe, nawe hukumheshimu Muumba Mkuu wetu. Ndiyo sababu Mungu amepeleka mkono huo uandike maneno haya.
‘Haya ndiyo maandishi,’ Danieli asema: ‘MEʹNE, MEʹNE, TEʹKEL na PARʹSIN.’
‘MEʹNE maana yake Mungu amezihesabu siku za ufalme wako na kuumaliza. TEʹKEL maana yake umepimwa katika vipimo na kuonekana hufai kitu. PARʹSIN maana yake ufalme wako wamepewa Wamedi na Waajemi.’
Hata hivi Danieli anaposema, Wamedi na Waajemi wamekwisha anza kushambulia Babeli. Wanauteka mji na kumwua Belshaza. Mwandiko huo ukutani watimizwa usiku uo huo! Lakini jambo gani litawapata Waisraeli sasa? Upesi tutajua, lakini kwanza na tuone linalompata Danieli.