HADITHI YA 108
Wakienda Damasko
UNAMJUA yule aliyelala chini? Ni Sauli. Kumbuka, ni yule aliyeangalia mavazi ya wale watu waliompiga Stefano mawe. Tazama nuru ile inayong’aa sana! Kuna nini?
Baada ya Stefano kuuawa, Sauli anaongoza katika kutafuta wafuasi wa Yesu awaumize. Anaingia kila nyumba akiwavuta nje na kuwatupa gerezani. Wanafunzi wengi wanakimbilia miji mingine na kuanza kutangaza “habari njema” huko. Lakini Sauli anakwenda kwenye miji mingine akatafute wafuasi wa Yesu. Sasa anakwenda Damasko. Lakini, akiwa njiani, ajabu hii yatokea:
Ghafula nuru kutoka angani inang’aa kuzunguka Sauli. Anaanguka chini, kama unavyoona hapa. Kisha sauti yasema: ‘Sauli, Sauli! Kwa nini unaniumiza?’ Watu walio pamoja na Sauli wanaiona nuru na kusikia sauti, lakini hawafahamu maana yake.
‘Wewe nani, Bwana?’ Sauli auliza. ‘Mimi Yesu, ambaye unaumiza,’ sauti yasema. Yesu anasema hivyo kwa sababu Sauli anapoumiza wafuasi wa Yesu, Yesu anaona kama ni yeye anaumizwa.
Sasa Sauli anauliza: ‘Nitafanya nini, Bwana?’
‘Amka uingie Damasko,’ Yesu asema. ‘Na huko utaambiwa la kufanya.’ Sauli anapoamka na kufungua macho yake, hawezi kuona kitu. Amepofuka! Basi watu walio naye wanamwongoza kwa mkono kuingia Damasko.
Sasa Yesu anamwambia mwanafunzi wake mmoja katika Damasko hivi: ‘Amka, Anania. Nenda kwenye barabara inayoitwa Nyofu. Ukifika nyumbani kwa Yuda uliza mtu anayeitwa Sauli. Nimemchagua awe mtumishi wangu wa pekee.’
Anania anatii. Anapomkuta Sauli, anamwekea mikono yake na kusema: ‘Bwana amenituma ili upate kuona tena na kujazwa roho takatifu.’ Mara hiyo kitu kama magamba kinaanguka katika macho ya Sauli, anaona tena.
Sauli anatumiwa sana awahubiri watu wa mataifa mengi. Anajulikana kuwa mtume Paulo, ambaye tutajifunza habari zake nyingi. Lakini kwanza, na tuone jambo ambalo Mungu anamtuma Petro afanye.