Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HADITHI YA 111

Mvulana Aliyelala Usingizi

Mvulana Aliyelala Usingizi

MAMA WEE! Haya ni mambo gani? Mvulana aliye chini ameumizwa vibaya? Tazama! mmoja wa watu wanaotoka nyumbani ni Paulo! Unamwona Timotheo pia? Mvulana huyo alianguka kutoka dirisha?

Ndivyo ilivyokuwa. Paulo alikuwa akitolea wanafunzi hotuba katika Troa. Alijua kwamba hangewaona tena kwa muda mrefu kwa sababu kesho yake angeondoka kwa meli. Hivyo akaendelea kuzungumza wee mpaka saa sita za usiku.

Basi, mvulana huyo Eutiko aliketi penye dirisha, akalala usingizi. We! akaanguka kutoka dirishani, orofa tatu mpaka chini! Basi unajua sababu gani watu hawa wana wasiwasi. Watu wanapomwinua mvulana, amekufa kitambo!

Paulo anapoona mvulana amekufa, anamlalia na kumkumbatia. Kisha anasema: ‘Msitie shaka. Yuko salama!’ Na ni kweli! Ni mwujiza! Paulo amemfufua! Watu wengi wanaanza kufurahi.

Wote wanapanda juu tena na kula chakula. Paulo anaendelea kuzungumza mpaka asubuhi. Lakini Eutiko halali usingizi tena! Ndipo Paulo, Timotheo na wasafiri wenzao wanapanda meli. Unajua wanaenda wapi?

Sasa Paulo anamalizia safari yake ya tatu ya kuhubiri, anarudi nyumbani. Katika safari hii Paulo alikuwa amekaa miaka mitatu katika mji wa Efeso peke yake. Hii ni safari yake ndefu sana kuliko ile ya pili.

Baada ya kutoka Troa, meli inasimama kidogo Mileto. Kwa kuwa Efeso ni mwendo wa kilomita chache, Paulo anapeleka habari ili wazee katika kundi waje Mileto aweze kusema nao mara ya mwisho. Wakati wa meli kuondoka unapofika, wanahuzunika sana kumwona Paulo akienda!

Mwishowe meli yarudi Kaisaria. Paulo anapokaa huku katika nyumba ya mwanafunzi Filipo, nabii Agapo anamwonya Paulo. Anasema kwamba Paulo atafungwa akifika Yerusalemu. Na kwa hakika, inakuwa hivyo. Ndipo akiisha kuwa gerezani muda wa miaka miwili katika Kaisaria, Paulo anapelekwa Roma akahukumiwe mbele ya Kaisari mtawala wa Roma. Na tuone yanayotokea katika safari ya kwenda Roma.