SURA YA 23
Kwa Nini Tunakuwa Wagonjwa?
UNAJUA mtu yeyote ambaye ni mgonjwa?— Labda hata wewe huwa mgonjwa wakati mwingine. Unaweza kupata mafua, au kuumwa na tumbo. Watu wengine ni wagonjwa sana. Hata hawawezi kusimama bila msaada. Inakuwa hivyo hasa watu wanapozeeka sana.
Kila mtu huwa mgonjwa wakati mwingine. Je, unajua kwa nini watu wanakuwa wagonjwa, wanazeeka, na kufa?— Siku moja mtu ambaye hakuweza kutembea aliletwa mbele ya Yesu, naye Yesu akaonyesha ni kwa nini watu wanakuwa wagonjwa na kufa. Hebu nikusimulie habari hiyo.
Yesu alikuwa katika nyumba moja katika mji ulio karibu na Bahari ya Galilaya. Watu wengi walikuja kumwona. Walikuwa wengi mpaka hakukuwa na nafasi ya kuingia ndani ya nyumba hiyo. Hata mtu hangeweza kukaribia mlangoni. Na bado watu waliendelea kumiminika! Watu fulani wakamleta mtu aliyepooza ambaye hakuweza kutembea. Ilibidi watu wanne wambebe kitandani.
Unajua ni kwa nini walitaka kumletea Yesu mtu huyo mgonjwa?— Waliamini kwamba Yesu anaweza kumsaidia kwa kumponya kutokana na ugonjwa huo. Ijapokuwa nyumba ile ilijaa kabisa, je, unajua jinsi walivyoweza kumpeleka mtu huyo mbele za Yesu?—
Picha unayoona hapa inaonyesha jinsi walivyofanya. Kwanza, walimbeba mpaka kwenye paa. Ilikuwa paa tambarare. Kisha wakatoboa shimo kubwa kwenye paa. Halafu wakamteremsha huyo
mgonjwa kupitia shimo hilo akiwa kitandani mpaka ndani ya chumba kile. Kwa kweli watu hao walikuwa na imani sana.Watu wote waliokuwamo walishangaa walipoona jambo hilo. Mtu huyo aliyepooza aliteremshwa katikati yao. Je, Yesu alikasirika alipoona jambo hilo?— Hata kidogo! Alifurahi kuona kwamba wana imani. Akamwambia yule aliyepooza: “Dhambi zako zimesamehewa.”
Watu wengine wakafikiri Yesu hakufanya vizuri kwa kusema hivyo. Hawakufikiri kwamba anaweza kusamehe dhambi. Ili kuonyesha kwamba kwa kweli anaweza kusamehe dhambi, Yesu akamwambia mtu huyo: ‘Simama, chukua kitanda chako, uende nyumbani.’
Yesu aliposema hayo, mtu huyo akapona! Akawa mzima. Sasa angeweza kusimama na kutembea bila kusaidiwa na mtu yeyote. Watu walioona mwujiza huo walishangaa. Hawakuwa wamewahi kuona ajabu kama hiyo maishani mwao! Walimsifu Yehova kwa kuwapa Mwalimu Mkuu ambaye aliweza kuwaponya.—Mwujiza huo unatufundisha nini?— Tunajifunza kwamba Yesu ana nguvu za kusamehe dhambi na kuponya magonjwa. Lakini tunajifunza pia jambo lingine la maana sana. Tunajifunza kwamba watu wanakuwa wagonjwa kwa sababu ya dhambi.
Kwa sababu sisi sote tunakuwa wagonjwa wakati mwingine, je, hiyo inamaanisha kwamba sisi ni wenye dhambi?— Ndiyo, Biblia inasema kwamba sisi sote tumezaliwa tukiwa wenye dhambi. Je, unajua kuzaliwa na dhambi ni nini?— Inamaanisha tumezaliwa bila ukamilifu. Wakati mwingine tunakosea bila kukusudia. Je, unajua ni kwa nini sote tuna dhambi?—
Tumezaliwa na dhambi kwa sababu mtu wa kwanza, Adamu, hakumtii Mungu. Alifanya dhambi alipovunja amri ya Mungu. Nasi sote tukapata dhambi kutoka kwa Adamu. Je, unajua jinsi tulivyopata dhambi kutoka kwake? Hebu nijaribu kukueleza kwa njia rahisi.
Labda umeona mtu akioka mkate katika mkebe. Mkate huo utakuwaje iwapo mkebe unaotumiwa una alama ya kugongwa?
Unajua?— Mikate yote itakayookwa katika mkebe huo itakuwa na alama ileile ya kugongwa, sivyo?—Adamu alikuwa kama huo mkebe, nasi ni kama mikate. Akawa asiyekamilika alipovunja amri ya Mungu. Ni kama alipata alama mbaya. Kwa hiyo angekuwa na watoto wa aina gani?— Wote wangepata alama ileile ya kutokamilika.
Watoto wengi hawazaliwi na kutokamilika ambako unaweza kuona wazi. Kwa mfano, wengi hawazaliwi bila mkono au mguu. Lakini hali yao ya kutokamilika ni mbaya sana hivi kwamba wanakuwa wagonjwa na baadaye wanakufa.
Kama tunavyojua, watu wengine wanakuwa wagonjwa mara nyingi kuliko wengine. Kwa nini hivyo? Je, ni kwa sababu wamezaliwa na dhambi nyingi zaidi?— La, kila mtu anazaliwa na kiasi kilekile cha dhambi. Sisi sote tunazaliwa tukiwa wasio wakamilifu. Hatimaye, kila mmoja wetu anakuwa na ugonjwa fulani. Hata watu wanaojaribu kutii sheria zote za Mungu na kuepuka kutenda mabaya wanaweza kuwa wagonjwa.
Basi, ni kwa nini watu wengine huwa wagonjwa mara nyingi zaidi?— Kuna sababu nyingi. Labda hawana chakula cha kutosha. Au hawali chakula kinachofaa. Labda wanapenda sana kula keki na peremende. Sababu nyingine ni kwamba labda wao huenda kulala wakiwa wamechelewa sana na hivyo hawapati usingizi wa kutosha. Au huenda hawavai nguo zinazowakinga na mvua. Watu wengine wana miili
dhaifu sana ambayo haiwezi kupigana na magonjwa, hata wakijaribu kujitunza.Je, kuna wakati ambapo magonjwa hayatakuwapo? Je, dhambi itapata kuondolewa?— Yesu alimfanyia nini yule mtu aliyepooza?— Yesu alimsamehe dhambi zake akamponya. Yesu alipofanya hivyo, alionyesha jinsi atakavyofanya siku moja kwa wote wanaojaribu sana kufanya yaliyo mema.
Tukionyesha kwamba hatutaki kufanya dhambi, na kwamba tunachukia mabaya, Yesu atatuponya. Wakati ujao, atatuondolea kutokamilika kwetu. Atafanya hivyo akiwa Mfalme wa Ufalme wa Mungu. Dhambi haitaondolewa kutoka kwetu mara moja. Itachukua muda fulani kuondolewa. Kisha dhambi yote itakapoondolewa, hatutakuwa wagonjwa tena. Sisi sote tutakuwa na afya kamilifu. Itakuwa baraka iliyoje!
Kwa habari zaidi kuhusu namna ambavyo dhambi inaathiri kila mtu, soma Ayubu 14:4; Zaburi 51:5 (50:7, “Dy”); Waroma 3:23; 5:12; na 6:23.