Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 23

“Nisikilizeni Ninapojitetea”

“Nisikilizeni Ninapojitetea”

Paulo anaitetea kweli mbele ya umati wenye vurugu na mbele ya Sanhedrini

Matendo 21:18–23:10

1, 2. Kwa nini Paulo amerudi Yerusalemu, na atakabili hali gani ngumu?

 YERUSALEMU! Kwa mara nyingine tena Paulo anatembea katika barabara za jiji hilo zenye watu wengi. Jiji hilo ni la pekee katika historia ya watu wa Yehova. Wakazi wengi wa jiji hilo hujivunia historia hiyo ya pekee. Paulo anajua kwamba Wakristo wengi katika jiji hilo wanazingatia kupita kiasi historia hiyo, na si rahisi kwao kukubali njia mpya ya kumwabudu Yehova. Paulo aliamua kutembelea jiji hilo si tu kwa sababu ya uhitaji wa kimwili waliokuwa nao, bali pia uhitaji wa kiroho wa ndugu katika jiji hilo. (Mdo. 19:21) Ameazimia kabisa kulitembelea jiji hilo licha ya hatari zilizopo.

2 Paulo atakabili hali gani katika jiji la Yerusalemu? Kwanza, kuna uvumi usio wa kweli kumhusu miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Hata hivyo, atakabili changamoto kubwa zaidi kutoka kwa adui za Kristo. Watatoa mashtaka ya uwongo dhidi ya Paulo, watampiga, na kujaribu kumuua. Yote hayo yatampa Paulo nafasi ya kujitetea. Unyenyekevu, ujasiri na imani yake katika kushughulikia hali hizo ngumu ni mfano mzuri kwa Wakristo leo. Jinsi gani? Acheni tuone.

“Wakaanza Kumtukuza Mungu” (Mdo. 21:18-20a)

3-5. (a) Paulo alihudhuria mkutano gani jijini Yerusalemu, na ni mambo gani yaliyozungumziwa? (b) Tunajifunza nini kutokana na mkutano huo wa Paulo na wazee jijini Yerusalemu?

3 Siku ya pili baada ya kufika Yerusalemu, Paulo na wenzake walienda kuwaona wazee wenye madaraka kutanikoni. Hakuna yeyote kati ya mitume anayetajwa; huenda kufikia wakati huo walienda kutumikia katika maeneo mengine. Hata hivyo, Yakobo ndugu ya Yesu bado alikuwa huko. (Gal. 2:9) Inawezekana kwamba Yakobo alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, ambapo “wazee wote walikuwapo,” pamoja na Paulo.​—Mdo. 21:18.

4 Paulo aliwasalimu wazee “na kuanza kusimulia kirefu mambo ambayo Mungu alifanya miongoni mwa mataifa kupitia huduma yake.” (Mdo. 21:19) Wazia jinsi habari hizo zilivyowatia moyo! Leo, sisi pia hufurahia ripoti za maendeleo ya kazi katika nchi nyingine.​—Met. 25:25.

5 Katika mazungumzo hayo, haikosi Paulo alitaja michango aliyoleta kutoka Ulaya. Lazima ndugu hao waliokuwa wakimsikiliza Paulo waliguswa moyo sana kuona jinsi ndugu zao katika sehemu nyingine wanavyowahangaikia. Baada ya kuisikiliza ripoti ya Paulo, masimulizi yanasema: “[Wazee hao] wakaanza kumtukuza Mungu”! (Mdo. 21:20a) Leo pia, wengi ambao wamekumbwa na majanga au magonjwa huchochewa sana wakati ambapo waabudu wenzao wanatoa misaada na kuwafariji.

Bado Wengi “Wanafuata Sheria kwa Bidii” (Mdo. 21:20b, 21)

6. Paulo alijulishwa tatizo gani?

6 Kisha wazee wakamweleza Paulo kwamba kuna tatizo Yudea ambalo linamhusu. Walisema: “Ndugu, unaona jinsi ambavyo maelfu ya Wayahudi wamekuwa waamini, na wote wanafuata Sheria kwa bidii. Lakini wamesikia uvumi kukuhusu kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wote kati ya mataifa kuiasi sheria ya Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zilizowekwa.” aMdo. 21:20b, 21.

7, 8. (a) Wakristo wengi wa Yudea walikuwa na maoni gani? (b) Kwa nini maoni yao hayakuwafanya waasi imani?

7 Miaka 20 baada ya Sheria ya Musa kuondolewa, kwa nini bado Wakristo wengi walikuwa wakiishikilia kwa bidii? (Kol. 2:14) Mwaka wa 49 W.K., mitume na wazee jijini Yerusalemu waliyatumia makutaniko barua wakieleza kwamba waamini kutoka kwa mataifa hawahitaji kutahiriwa wala kuwa chini ya Sheria ya Musa. (Mdo. 15:23-29) Hata hivyo, barua hiyo haikutaja waamini Wayahudi, ambao wengi kati yao hawakuelewa kwamba Sheria ya Musa haitumiki tena.

8 Je, kutoelewa kwa waabudu hao Wayahudi kulimaanisha kwamba hawakustahili kuendelea kuwa Wakristo? Hapana. Si kwamba walikuwa waabudu wa miungu ya kipagani awali, na sasa walikuwa wakiendeleza mapokeo ya dini zao za zamani. Sheria hiyo ambayo ilikuwa muhimu sana kwa waamini hao Wayahudi, ilitoka kwa Yehova. Sheria yenyewe haikuwa na ubaya wowote, wala haikuwa ya kikatili. Tofauti ni kwamba Sheria hiyo ilikuwa sehemu ya agano la kale, nao Wakristo walikuwa chini ya agano jipya. Kwa hiyo, ibada safi haikutegemea tena kuendelea kulishikilia agano la Sheria. Wakristo Waebrania waliokuwa wakishikilia Sheria kwa bidii hawakuelewa vizuri utendaji wa kutaniko la Kikristo. Walihitaji kupatanisha maoni yao na kweli iliyokuwa ikifunuliwa hatua kwa hatua. bYer. 31:31-34; Luka 22:20.

“Uvumi Walioambiwa Kukuhusu si wa Kweli” (Mdo. 21:22-26)

9. Paulo alifundisha nini kuhusu Sheria ya Musa?

9 Namna gani ule uvumi wa kwamba Paulo alikuwa akiwafundisha Wayahudi kati ya mataifa “wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zilizowekwa”? Paulo alikuwa mtume kwa Watu wa Mataifa, naye aliposhughulika nao, aliunga mkono uamuzi uliopitishwa wa kwamba Watu wa Mataifa hawahitaji kufuata matakwa ya Sheria. Pia, alifafanua kwa nini ni kosa kwa mtu yeyote kujaribu kuwalazimisha waabudu wa Mataifa watahiriwe ili tu kuonyesha kwamba wanaiheshimu Sheria ya Musa. (Gal. 5:1-7) Katika majiji aliyotembelea, Paulo aliwahubiria habari njema Wayahudi pia. Bila shaka, aliwaeleza waliokuwa tayari kumsikiliza kwamba kifo cha Yesu kiliondolea mbali Sheria na kwamba uadilifu ungepatikana kwa imani, bali si kwa kushika Sheria.​—Rom. 2:28, 29; 3:21-26.

10. Paulo alionyesha usawaziko jinsi gani kuhusu Sheria na tohara?

10 Hata hivyo, Paulo alielewa hisia za wale waliokuwa wakiendelea kufuata baadhi ya desturi za Kiyahudi, kama vile kutofanya kazi siku ya Sabato au kutokula vyakula fulani. (Rom. 14:1-6) Naye hakuweka sheria kuhusu tohara. Paulo alimtahiri Timotheo ili Wayahudi wasiwe na shaka kumhusu Timotheo, ambaye baba yake alikuwa Mgiriki. (Mdo. 16:3) Suala la tohara lilikuwa la kibinafsi. Paulo aliwaambia Wagalatia: “Kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna faida yoyote, bali imani inayotenda kupitia upendo ina faida.” (Gal. 5:6) Hata hivyo, kutahiriwa ili tu kutimiza Sheria au kudai kwamba lazima mtu atahiriwe ili apate kibali cha Yehova ni kukosa imani.

11. Wazee walimwagiza Paulo afanye nini, na huenda ni nini kilichohusika? (Ona pia maelezo ya chini.)

11 Ijapokuwa uvumi uliokuwa umeenea haukuwa wa kweli, bado uliwasumbua waamini Wayahudi. Ndiyo sababu wazee walimwagiza Paulo: “Tuna wanaume wanne waliojiwekea nadhiri. Nenda pamoja na watu hawa ukajitakase kisherehe pamoja nao na kuwagharimia, ili wanyolewe vichwa vyao. Ndipo kila mtu atajua kwamba uvumi walioambiwa kukuhusu si wa kweli, bali unatembea kwa utaratibu, na pia unashika Sheria.” cMdo. 21:23, 24.

12. Paulo alionyeshaje kwamba alikuwa tayari kubadilika kulingana na hali na kufuata maagizo ya wazee wa Yerusalemu?

12 Paulo angeweza kushikilia msimamo wake na kudai kwamba tatizo si uvumi ulioenea kumhusu, bali ni maoni ya waamini hao Wayahudi kuhusu Sheria ya Musa. Badala ya kufanya hivyo, alikuwa tayari kubadilika kulingana na hali maadamu kufanya hivyo hakungevunja viwango vya Mungu. Mapema alikuwa ameandika hivi: “Kwa wale walio chini ya sheria nilikuwa kama aliye chini ya sheria, ingawa mimi mwenyewe siko chini ya sheria, ili niwapate wale walio chini ya sheria.” (1 Kor. 9:20) Katika kisa hiki, Paulo aliamua kufuata maagizo ya wazee wa Yerusalemu na kuwa “kama aliye chini ya sheria.” Kwa kufanya hivyo, alituwekea kielelezo kizuri cha kufuata maagizo ya wazee badala ya kuamua kufanya mambo kwa njia yetu.​—Ebr. 13:17.

Ikiwa hakuna kanuni za Kimaandiko zilizohusika, Paulo alikuwa tayari kubadilika kulingana na hali. Je, wewe hufanya hivyo?

“Hafai Kuishi!” (Mdo. 21:27–22:30)

13. (a) Kwa nini baadhi ya Wayahudi walisababisha mvurugo hekaluni? (b) Paulo aliokolewaje?

13 Mambo hayakwenda vizuri hekaluni. Kadiri siku za nadhiri zilivyokuwa zinakaribia kwisha, Wayahudi kutoka Asia walimwona Paulo, wakamshtaki kwa uwongo kwamba amewaingiza Watu wa Mataifa hekaluni, na kusababisha mvurugo. Kama kiongozi wa jeshi la Roma hangeingilia kati, Paulo angepigwa na kuuawa. Hata hivyo, kiongozi huyo akamfunga. Tangu siku hiyo, Paulo alikaa gerezani kwa zaidi ya miaka minne kabla ya kufunguliwa. Nazo hatari zilizomkabili hazikuwa zimeisha. Kiongozi alipowauliza Wayahudi kwa nini walimshambulia Paulo, umati huo ulitoa mashtaka mbalimbali. Kwa sababu kulikuwa na vurugu, kiongozi huyo hangeweza kusikia chochote. Ilibidi Paulo aondolewe hapo. Paulo na askari jeshi wa Roma walipokaribia kuingia katika makao ya askari jeshi, Paulo alimwambia kiongozi huyo: “Nakuomba uniruhusu nizungumze na watu hawa.” (Mdo. 21:39) Kiongozi alikubali, naye Paulo akaitetea imani yake kwa ujasiri.

14, 15. (a) Paulo aliwaeleza Wayahudi nini? (b) Kiongozi wa jeshi la Roma alichukua hatua gani ili kujua kwa nini Wayahudi wana hasira kali hivyo?

14 Paulo alianza kwa kusema: “Nisikilizeni ninapojitetea.” (Mdo. 22:1) Paulo alihutubia umati huo kwa Kiebrania, jambo lililowatuliza. Aliwaeleza kwa unyoofu kwa nini yeye ni mfuasi wa Kristo. Kwa ustadi, Paulo alitoa hoja ambazo Wayahudi hao wangeweza kuthibitisha ikiwa wangetaka. Paulo alikuwa amesomea miguuni pa Gamalieli, aliyejulikana sana, naye alikuwa amewanyanyasa wafuasi wa Kristo, kama vile baadhi ya watu katika umati huo wanavyojua. Hata hivyo, alipokuwa njiani kuelekea Damasko aliona maono. Katika maono hayo, Kristo aliyekuwa amefufuliwa alizungumza naye. Watu waliokuwa wakisafiri na Paulo waliona nuru nyangavu na kusikia sauti, lakini hawakuelewa maana ya maneno yaliyosemwa. (Mdo. 9:7; 22:9) Kisha, Paulo aliyekuwa amepofushwa na maono hayo, aliongozwa na wenzake hadi Damasko. Akiwa huko Anania, aliyejulikana na Wayahudi wa eneo hilo, alimponya Paulo kimuujiza.

15  Paulo alisema kwamba baada ya kurudi Yerusalemu, Yesu alimtokea tena akiwa hekaluni. Waliposikia hilo, Wayahudi wakakasirika sana na kuanza kupiga kelele wakisema: “Mwondoeni duniani mtu kama huyu, hafai kuishi!” (Mdo. 22:22) Ili kumwokoa Paulo, kiongozi wa jeshi akaagiza apelekwe ndani ya kambi ya askari jeshi. Akitaka kujua ni kwa nini Wayahudi hao wana hasira kali hivyo kumwelekea Paulo, kiongozi huyo akaamuru ahojiwe huku akipigwa mijeledi. Paulo aliamua kutumia ulinzi wa kisheria na kusema kwamba yeye ni raia wa Roma. Leo pia, waabudu wa Yehova hutumia ulinzi wa kisheria kutetea imani yao. (Ona sanduku lenye kichwa “ Sheria ya Waroma na Raia wa Roma,” na “ Kesi za Kisheria Katika Siku Zetu.”) Baada ya kusikia kwamba Paulo ni raia wa Roma, kiongozi huyo alihitaji kutafuta njia nyingine ya kupata habari. Siku iliyofuata, alimleta Paulo mbele ya mkutano wa pekee wa mahakama kuu ya Wayahudi inayoitwa Sanhedrini.

“Mimi Ni Farisayo” (Mdo. 23:1-10)

16, 17. (a) Eleza kilichotokea Paulo alipokuwa akijitetea mbele ya Sanhedrini. (b) Alipopigwa, Paulo alionyeshaje unyenyekevu?

16 Paulo alianza kujitetea mbele ya mahakama hiyo kwa kusema: “Wanaume, akina ndugu, nimetenda kwa dhamiri safi kabisa mbele za Mungu mpaka leo hii.” (Mdo. 23:1) Kabla hajasema zaidi, “kuhani mkuu Anania akawaagiza wale waliosimama kando yake wampige kofi mdomoni.” (Mdo. 23:2) Alimdharau sana! Tendo hilo lilionyesha chuki aliyokuwa nayo. Ni kana kwamba alisema Paulo ni mwongo hata kabla ya kumsikiliza! Si ajabu Paulo alisema: “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa. Je, unaketi kunihukumu kulingana na Sheria na wakati uleule unaivunja Sheria hiyo kwa kuamuru nipigwe?”​—Mdo. 23:3.

17 Baadhi ya wale waliokuwa wamesimama hapo wakashangazwa—si na yule aliyempiga Paulo, bali na jibu la Paulo! Wakamuuliza: “Je, unamtukana kuhani mkuu wa Mungu?” Jibu la Paulo lilionyesha kwamba yeye ni mnyenyekevu na pia anaiheshimu Sheria. Alisema: “Akina ndugu, sikujua yeye ni kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’” d (Mdo. 23:4, 5; Kut. 22:28) Paulo akabadili njia yake. Akijua kwamba washiriki wa mahakama hiyo ni Mafarisayo na Masadukayo, akasema: “Wanaume, akina ndugu, mimi ni Farisayo, mwana wa Mafarisayo. Ninahukumiwa kwa sababu ya tumaini la ufufuo wa wafu.”​—Mdo. 23:6.

Kama Paulo alivyofanya, sisi hujaribu kuweka msingi mzuri wa mazungumzo tunapozungumza na watu wenye imani tofauti

18. Kwa nini Paulo alijiita Farisayo, nasi tunaweza kufuata mfano wake jinsi gani?

18 Kwa nini Paulo anajiita Farisayo? Kwa sababu alikuwa “mwana wa Mafarisayo” kutoka katika familia ya Kifarisayo. Kwa hiyo, machoni pa wengi alionwa kuwa Farisayo. e Hata hivyo, je, imani ya Paulo kuhusu ufufuo ilikuwa sawa na ya Mafarisayo? Mafarisayo waliamini nafsi haifi, na kwamba nafsi ya waadilifu huishi tena katika miili ya binadamu. Bila shaka, Paulo hakuamini hivyo bali aliamini ufufuo uliofundishwa na Yesu. (Yoh. 5:25-29) Hata hivyo, sawa na Mafarisayo, Paulo aliamini kwamba kuna tumaini la ufufuo. Kwa upande mwingine, Masadukayo hawakuamini kuna ufufuo. Tunaweza kufuata mfano wake tunapowahubiria Wakatoliki au Waprotestanti. Tunaweza kuwaambia sisi pia tunaamini kuna Mungu. Ingawa wanaamini Utatu, sisi tunamwamini Mungu anayetajwa katika Biblia. Hivyo, sote tunaamini kwamba kuna Mungu.

19. Kwa nini kulikuwa na vurugu mahakamani?

19 Maneno ya Paulo yalitokeza mgawanyiko. Simulizi hilo linasema: “Kukawa na vurugu, na baadhi ya waandishi wa chama cha Mafarisayo wakasimama na kuanza kubishana kwa ukali, wakisema: “Hatuoni kosa lolote katika mtu huyu, lakini ikiwa roho au malaika alizungumza naye—.’” (Mdo. 23:9) Wazo la kwamba huenda Paulo alikuwa ameongea na malaika, liliwachukiza sana Masadukayo ambao hawakuamini malaika! (Ona sanduku lenye kichwa “ Masadukayo na Mafarisayo.”) Vurugu hizo zilikuwa kubwa sana hivi kwamba yule kiongozi akalazimika kumwokoa tena mtume huyo. (Mdo. 23:10) Hata hivyo, bado Paulo alikuwa hatarini. Ni nini kitakachompata mtume huyo? Tutaona katika sura inayofuata.

a Ili kushughulikia mahitaji ya kiroho ya idadi kubwa ya Wakristo Wayahudi, lazima kulikuwa na makutaniko mengi yaliyokuwa yakikutana katika nyumba za watu binafsi.

b Miaka michache baadaye, mtume Paulo aliandika barua yake kwa Waebrania, ambamo alithibitisha ubora wa agano jipya. Katika barua hiyo, alionyesha wazi kwamba kuanzishwa kwa agano jipya kuliondolea mbali agano la kale. Mbali na kutoa hoja zenye kusadikisha ambazo Wakristo Wayahudi wangeweza kutumia kuwajibu Wayahudi waliowapinga, hoja za Paulo ziliimarisha imani ya baadhi ya Wakristo waliokuwa wakishikilia kupita kiasi Sheria ya Musa.​—Ebr. 8:7-13.

c Wasomi fulani wanadokeza kwamba watu hao walikuwa wameweka Nadhiri. (Hes. 6:1-21) Ni kweli kwamba Sheria ya Musa, iliyotumika kuweka nadhiri hizo, haikuwa ikitumika tena. Hata hivyo, huenda Paulo aliona kwamba hakuna ubaya kwa watu hao kutimiza nadhiri waliyoweka kwa Yehova. Kwa hiyo, haingekuwa vibaya kulipa gharama zao na kuandamana nao. Hatujui ni nadhiri ya aina gani iliyowekwa, hata hivyo, haielekei kwamba Paulo angeshiriki kutoa dhabihu ya mnyama (kama Wanadhiri walivyofanya), akiamini kwamba ingesafisha dhambi za mtu. Dhabihu kamilifu ya Kristo ilikuwa imeondolea mbali uwezo wa dhabihu hizo kusafisha dhambi. Vyovyote vile, tuna hakika kwamba Paulo hangekubali kufanya chochote ambacho kingechafua dhamiri yake.

d Watu fulani wamesema kwamba inawezekana Paulo hakuwa akiona vizuri kwa hiyo hakumtambua kuhani mkuu. Au huenda alikuwa mbali na Yerusalemu kwa muda mrefu sana hivi kwamba hakumjua kuhani mkuu wa wakati huo. Au kwa sababu ya umati wa watu uliokuwapo labda Paulo hangeweza kuona ni nani aliyetoa amri apigwe.

e Mwaka wa 49 W.K., mitume na wazee walipokuwa wakijadiliana ikiwa Watu wa Mataifa wanapaswa kushika Sheria ya Musa, baadhi ya Wakristo waliokuwako waliitwa “baadhi ya wale wa madhehebu ya Mafarisayo ambao sasa walikuwa waamini.” (Mdo. 15:5) Inaonekana kwa kiasi fulani waamini hao walikuwa bado wakihusianishwa na asili yao ya Kifarisayo.