Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 26

“Hakuna Hata Mmoja Wenu Atakayepotea”

“Hakuna Hata Mmoja Wenu Atakayepotea”

Paulo avunjikiwa meli, aonyesha imani kubwa na upendo kwa watu

Matendo 27:1–28:10

1, 2. Paulo anaelekea wapi, na huenda anafikiria nini?

 “UTAENDA kwa Kaisari.” Bado mtume Paulo anakumbuka maneno hayo ya Gavana Festo. Paulo amekaa gerezani kwa miaka miwili, kwa hiyo safari ndefu ya kwenda Roma, angalau itampa nafasi ya kuona mazingira mapya. (Mdo. 25:12) Hata hivyo, Paulo anakumbuka mengi zaidi kuhusu safari zake nyingi za baharini mbali na upepo mwanana wenye kuburudisha na maji mengi ya bahari yanayofikia upeo wa macho. Kwa kuwa wakati huu anapelekwa kwa Kaisari, huenda anajiuliza maswali mengi.

2 Paulo amekuwa katika “hatari baharini” mara nyingi, mara tatu ameokoka baada ya meli kuvunjika. Hata wakati fulani alikaa usiku na mchana baharini. (2 Kor. 11:25, 26) Isitoshe, safari hii ni tofauti kabisa na safari zake za umishonari alipokuwa huru. Wakati huu atasafiri akiwa mfungwa, tena anaenda mbali, kilomita zaidi ya 3,000, kutoka Kaisaria hadi Roma. Je, atafika salama? Hata ikiwa atafika salama, je, atahukumiwa kifo? Kumbuka kwamba anaenda kuhukumiwa na serikali kuu katika ulimwengu wa Shetani wakati huo.

3. Paulo aliazimia kufanya nini, nasi tutazungumzia nini katika sura hii?

3 Kutokana na habari ambazo umesoma kuhusu Paulo, unafikiri atakata tamaa na kujihurumia akifikiria mambo yatakayompata? Hapana! Anajua atakabili hali nyingi ngumu, ijapokuwa hajui ni hali gani hususa zitakazompata. Kwa nini apoteze shangwe ya huduma yake kwa sababu ya kuhangaikia mambo asiyoweza kubadili? (Mt. 6:27, 34) Paulo anajua mapenzi ya Yehova ni kwamba atumie kila nafasi anayopata kuhubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu, hata mbele ya watawala wa serikali. (Mdo. 9:15) Paulo aliazimia kutimiza mgawo wake, hata hali ziweje. Hilo ndilo linalopaswa kuwa azimio letu pia. Hivyo basi, acheni tuandamane na Paulo katika safari hiyo ya pekee tukifikiria jinsi tunavyoweza kufuata mfano mzuri aliotuwekea.

“Pepo Zilizokuwa Zikivuma Kinyume Nasi” (Mdo. 27:1-7a)

4. Paulo alianza safari yake katika meli ya aina gani, na ni nani waliosafiri pamoja naye?

4 Paulo na wafungwa wengine walitiwa mikononi mwa ofisa Mroma anayeitwa Yulio. Ofisa huyo aliamua wapande meli ya kibiashara iliyokuwa imefika Kaisaria. Ilikuwa imetoka Adramitiamu, bandari iliyo upande wa magharibi wa pwani ya Asia Ndogo, ng’ambo ya jiji la Mitilene katika kisiwa cha Lesbos. Meli hiyo ingesafiri kuelekea kaskazini kisha kuelekea magharibi, ikitua sehemu mbalimbali ili kupakua na kupakia shehena. Meli hizo hazikukusudiwa kubeba abiria, hasa wafungwa. (Ona sanduku lenye kichwa “ Safari za Baharini na Njia Zilizotumiwa na Wafanyabiashara.”) Jambo linalotia moyo ni kwamba Paulo hakuwa Mkristo pekee katikati ya kikundi hicho cha wahalifu. Waamini wengine wawili, Aristarko na Luka, walikuwa pamoja naye. Luka ndiye aliyeandika masimulizi hayo. Hatujui iwapo waandamani hao wawili walilipa nauli ili kusafiri au walikuwa watumishi wa Paulo.​—Mdo. 27:1, 2.

5. Paulo alifurahia ushirika gani alipokuwa Sidoni, nasi tunajifunza nini?

5 Baada ya kukaa siku nzima baharini, wakiwa wamesafiri kilomita 110 hivi kuelekea upande wa kaskazini, meli hiyo ilitia nanga Sidoni, katika pwani ya Siria. Yaonekana Yulio hakumtendea Paulo kama alivyokuwa akiwatendea wafungwa, huenda ni kwa sababu Paulo alikuwa raia wa Roma naye hakuwa ameshtakiwa na kuthibitishwa kuwa na hatia. (Mdo. 22:27, 28; 26:31, 32) Yulio alimruhusu Paulo ashuke na kwenda kuwatembelea Wakristo wenzake. Lazima ndugu na dada hao waliliona kuwa pendeleo kubwa kumsaidia mtume huyo baada ya kufungwa kwa muda mrefu! Je, kuna pindi zozote unazoweza kuonyesha ukarimu kama huo kwa upendo nawe utiwe moyo pia?​—Mdo. 27:3.

6-8. Safari ya Paulo kutoka Sidoni hadi Kinido ilikuwaje, na huenda alipata nafasi gani ya kuhubiri?

6 Kisha, meli ikang’oa nanga kutoka Sidoni, na kusafiri kandokando ya pwani, ikapita Kilikia, karibu na Tarso, jiji la nyumbani kwa Paulo. Luka hataji vituo vingine, ijapokuwa anataja hali ya anga ambayo haikuwa shwari, anaposema ‘pepo zilikuwa zikivuma kinyume nasi.’ (Mdo. 27:4, 5) Haikosi Paulo alitumia kila nafasi ili kuhubiri habari njema. Bila shaka aliwahubiria wafungwa wenzake na wengine waliokuwa kwenye meli hiyo, kutia ndani mafundi wa mitambo na askari, na pia watu wengine wowote aliokutana nao meli ilipotia nanga katika bandari mbalimbali. Je, sisi hutumia kila nafasi tunayopata ili kuhubiri?

7 Baada ya muda, meli hiyo ilifika Mira, bandari iliyo katika pwani ya kusini ya Asia Ndogo. Huko Paulo na wenzake walipanda meli nyingine, ambayo ingewafikisha Roma. (Mdo. 27:6) Siku hizo, Misri ilikuwa ghala ya Roma, na meli za nafaka kutoka Misri zilikuwa zikitia nanga Mira. Yulio alipata mojawapo ya meli hizo na kuwapandisha askari na wafungwa. Lazima meli hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko ile ya kwanza. Ilikuwa na shehena kubwa ya ngano na abiria 276—mafundi wa mitambo, wafungwa, na huenda watu wengine waliokuwa wakielekea Roma. Bila shaka, katika meli hiyo, Paulo alipata eneo jipya la kuhubiri, naye hakusita kufanya hivyo.

8 Kituo kilichofuata ni Kinido, kusini magharibi mwa Asia Ndogo. Kwa kawaida meli zingeweza kusafiri umbali huo kwa siku moja ikiwa hali ya hewa ni shwari. Hata hivyo, kama Luka anavyoripoti, “baada ya kusafiri polepole kwa siku kadhaa, tukafika kwa shida huko Kinido.” (Mdo. 27:7a) Bahari ilizidi kuchafuka. (Ona sanduku lenye kichwa “ Pepo Hatari za Mediterania.”) Wazia hali ya watu waliokuwa katika meli hiyo huku wakikabili pepo zenye nguvu na bahari iliyochafuka.

“Tukirushwarushwa kwa Nguvu na Dhoruba” (Mdo. 27:7b-26)

9, 10. Ni hali gani ngumu zilizotokea karibu na Krete?

9 Kapteni wa meli hiyo alipanga kuendelea na safari kuelekea upande wa magharibi kutoka Kinido, hata hivyo, Luka anasema “upepo ulituzuia kusonga mbele.” (Mdo. 27:7b) Meli ilipoanza kwenda mbali na nchi kavu, ilipoteza mkondo, kisha upepo mkali kutoka kaskazini magharibi ukaisukuma, huenda kwa kasi sana. Kama vile meli hiyo ilivyolindwa na kisiwa cha Kipro awali kutokana na pepo zilizokuwa zikivuma kinyume, ililindwa pia na kisiwa cha Krete. Baada ya meli hiyo kupita rasi ya Salmone upande wa mashariki wa Krete, kukawa na utulivu kiasi. Kwa nini? Kwa sababu meli hiyo ilikuwa upande wa kusini wa kisiwa hicho, na hivyo ililindwa kutokana na zile pepo kali. Wazia furaha ya muda waliokuwa nayo watu katika meli hiyo! Hata hivyo, maadamu meli bado ilikuwa baharini, mafundi wa mitambo hawangeweza kupuuza majira ya baridi kali yaliyokuwa yakikaribia. Walikuwa na wasiwasi.

10 Luka anasema hivi kwa usahihi: “Tukasafiri kwa shida kandokando ya pwani [ya Krete], tukafika mahali panapoitwa Bandari Nzuri.” Hata hivyo, bado haikuwa rahisi kuendesha meli hiyo. Mwishowe, walitia nanga katika ghuba ndogo inayodhaniwa kuwa ilikuwa katika eneo la pwani, kabla tu ya kugeuka kuelekea kaskazini. Walikaa hapo muda gani? Luka anasema walikaa “muda mrefu,” hata hivyo, hawakuwa na wakati wa kupoteza, kwa sababu Septemba na Oktoba ni miezi hatari kusafiri.​—Mdo. 27:8, 9.

11. Paulo aliwapa wenzake ushauri gani, hata hivyo waliamua kufanya nini?

11 Huenda abiria fulani walimwomba Paulo ushauri kwa sababu alikuwa na uzoefu wa kusafiri katika Bahari ya Mediterania. Alipendekeza wasitishe safari, kwa kuwa ikiwa wangeendelea, wangepatwa na “madhara na hasara kubwa,” na huenda baadhi yao wangepoteza uhai. Hata hivyo, nahodha na mwenye meli walitaka kuendelea na safari, huenda kwa kuwa walitaka kufika haraka mahali salama zaidi. Walimsadikisha Yulio, na wengi wao wakakubaliana wajaribu kufika Feniki, bandari iliyokuwa mbali kidogo katika pwani hiyo. Huenda ilikuwa bandari kubwa na nzuri zaidi, mahali ambapo wangeweza kukaa wakati wa majira ya baridi kali. Kwa hiyo, upepo mwanana ulipoanza kupunga kutoka upande wa kaskazini, meli ikang’oa nanga.​—Mdo. 27:10-13.

12. Baada ya kuondoka Krete, meli ilikumbwa na nini, nao mafundi wa mitambo walifanya nini ili kujaribu kuepuka msiba?

12 Kisha mambo yakawa mabaya zaidi: kukazuka “upepo mkali” kutoka kaskazini mashariki. Kwa muda fulani, walifichwa na “kisiwa kidogo kinachoitwa Kauda,” kilomita 65 hivi kutoka Bandari Nzuri. Hata hivyo, bado meli hiyo ilikuwa hatarini, ingeweza kusukumwa upande wa kusini na kugonga ukingo wa bahari kwenye pwani ya Afrika. Wakihofia hali hiyo, mabaharia hao wakaivuta mashua ndogo iliyokuwa ikikokotwa na meli yao. Haikuwa rahisi kwa sababu inawezekana ilikuwa imejaa maji. Kisha wakajaribu kuikaza meli isivunjike, wakipitisha kamba au minyororo chini yake ili kushikilia mbao zake pamoja. Kisha wakashusha vifaa vya kuendeshea, tanga na kamba za mlingoti, na kung’ang’ana kuielekeza meli hiyo katika upepo huo hadi dhoruba ipite. Wazia jinsi tukio hilo lilivyokuwa lenye kuogopesha! Hata baada ya kufanya yote hayo, bado meli hiyo iliendelea ‘kurushwarushwa kwa nguvu na dhoruba.’ Siku ya tatu, wakatupa ayari majini, huenda ili kuiwezesha meli hiyo kuelea vizuri.​—Mdo. 27:14-19.

13. Hali ilikuwaje katika meli ya Paulo wakati wa dhoruba?

13 Wote walikuwa na hofu kubwa. Hata hivyo, Paulo na wenzake walijipa moyo. Bwana alikuwa amemhakikishia Paulo kwamba atatoa ushahidi Roma, na baadaye malaika akamthibitishia ahadi hiyo. (Mdo. 19:21; 23:11) Hata hivyo, dhoruba hiyo iliendelea kwa majuma mawili, usiku na mchana. Kwa sababu ya mvua iliyokuwa ikinyesha daima na mawingu mazito yaliyozuia nuru ya jua na nyota, kapteni wa meli hangeweza kuona mbali wala kujua wako wapi. Wasafiri hata hawakuweza kula chakula. Isitoshe, ni nani angeweza kula katika mazingira hayo ya baridi, mvua, kichefuchefu, na woga?

14, 15. (a) Alipokuwa akizungumza na wasafiri wenzake, kwa nini Paulo aliwakumbusha ushauri wake wa awali? (b) Tunaweza kujifunza nini kutokana na ujumbe wa tumaini ambao Paulo alitangaza?

14 Paulo akasimama. Akawakumbusha ushauri aliowapa ijapokuwa hakuwa akiwalaumu na kusema, ‘Si niliwaambia.’ Hata hivyo, mambo yaliyowapata yalionyesha wazi kwamba hawapaswi kamwe kupuuza maneno yake. Kisha akasema: “Sasa ninawahimiza mjipe moyo, kwa maana hakuna hata mmoja wenu atakayepotea, meli tu ndiyo itakayopotea.” (Mdo. 27:21, 22) Lazima maneno hayo yaliwasisimua sana waliokuwa wakimsikiliza! Bila shaka Paulo pia alifurahi sana kwa kuwa Yehova alimpa ujumbe wenye tumaini wa kuwaambia wengine. Tunapaswa kukumbuka kwamba Yehova anajali uhai wa kila mtu. Kila mtu ni mwenye thamani machoni pake. Mtume Petro aliandika: “Yehova . . . hataki yeyote aangamizwe bali hutaka wote wafikie toba.” (2 Pet. 3:9) Hivyo basi, tunapaswa kuwatangazia watu wengi iwezekanavyo ujumbe wa tumaini wa Yehova! Uhai wa watu uko hatarini.

15 Inaelekea Paulo aliwahubiria wengi katika meli hiyo kuhusu “tumaini la ahadi iliyotolewa na Mungu.” (Mdo. 26:6; Kol. 1:5) Sasa, meli yao ikikaribia kuvunjika, Paulo angeweza kutoa msingi thabiti wa tumaini lililo karibu zaidi. Aliwaambia: “Usiku huu malaika wa Mungu ambaye mimi ni mali yake . . . , alisimama kando yangu akasema, ‘Usiogope, Paulo. Utasimama mbele ya Kaisari, na, tazama! Mungu amekupa wale wote wanaosafiri pamoja nawe.’” Kisha Paulo akawahimiza: “Basi jipeni moyo, kwa maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa kama nilivyoambiwa. Hata hivyo, ni lazima tutupwe kwenye ufuo wa kisiwa fulani.”​—Mdo. 27:23-26.

“Wote Wakafika Salama Kwenye Nchi Kavu” (Mdo. 27:27-44)

“Akamshukuru Mungu mbele yao wote.”—Matendo 27:35

16, 17. (a) Paulo alitumia nafasi gani kutoa sala, na matokeo yalikuwa nini? (b) Mambo aliyotabiri Paulo yalitimiaje?

16 Baada ya majuma mawili yenye kutia hofu, na baada ya meli kusukumwa na upepo kilomita 870 hivi, mabaharia hao walianza kuona ishara za mabadiliko, huenda hata walianza kusikia mawimbi yakigonga nchi kavu. Walishusha nanga kutoka kwenye tezi ili wasichukuliwe na mawimbi nao wakaanza kuielekeza meli nchi kavu endapo wangeweza kuifikisha pwani. Kisha, wakajaribu kuondoka melini lakini wakazuiwa na askari. Paulo akamwambia ofisa wa jeshi pamoja na askari hao: “Watu hawa wasipobaki katika meli, ninyi hamwezi kuokoka.” Sasa, meli ikiwa imara kiasi, Paulo aliwahimiza wale chakula, akiwahakikishia tena kwamba wataokoka. Kisha Paulo “akamshukuru Mungu mbele yao wote.” (Mdo. 27:31, 35) Kwa kutoa sala hiyo ya shukrani, Paulo aliwawekea mfano mzuri Luka, Aristarko, na Wakristo wa leo. Je, sala unazotoa mbele za wengine ni zenye kutia moyo na kuwafariji wengine?

17 Baada ya Paulo kutoa sala, “wote wakajipa moyo, nao pia wakaanza kula.” (Mdo. 27:36) Kisha, wakaanza kupunguza uzito kwa kutupa baharini shehena ya ngano, na hivyo kuiwezesha meli kuelea zaidi inapokaribia pwani. Kulipopambazuka, wakakata nanga, wakafungua amari za makasia ya mtambo wa usukani, na kutweka tanga la mbele ili waweze kuiongoza meli hadi pwani. Omo ya meli ikakwama, huenda katika mchanga au matope, nayo tezi ikaanza kuvunjika kwa sababu ya mawimbi. Askari fulani walitaka kuwaua wafungwa ili yeyote kati yao asitoroke, lakini Yulio akaingilia kati na kuwazuia. Akawahimiza wote waogelee au kuelea juu ya mbao hadi nchi kavu. Aliyotabiri Paulo yakatimia—wote 276 wakaokoka. Ndiyo, “wote wakafika salama kwenye nchi kavu.” Hata hivyo, walikuwa wapi?​—Mdo. 27:44.

“Fadhili Zinazopita za Kawaida” (Mdo. 28:1-10)

18-20. Watu wa Malta walionyesha jinsi gani “fadhili zinazopita za kawaida,” na Mungu alifanya muujiza gani kupitia Paulo?

18 Waokokaji hao walijikuta katika kisiwa cha Malta, upande wa kusini wa Sisili. (Ona sanduku lenye kichwa “ Kisiwa cha Malta Kilikuwa Wapi?”) Watu wa kisiwa hicho wanaozungumza lugha ya kigeni walionyesha “fadhili zinazopita za kawaida.” (Mdo. 28:2) Waliwasha moto kwa ajili ya watu hao wasiowajua waliofika pwani wakiwa wamelowa na kutetemeka kwa sababu ya baridi. Moto huo uliwasaidia kujipasha joto. Hali hiyo pia ilitokeza muujiza.

19 Paulo alijitolea kusaidia kazi. Alikusanya kuni kadhaa, na kuzitia motoni. Alipokuwa akifanya hivyo, nyoka mwenye sumu akatokea, akamuuma, na kujifunga mkononi mwake. Wenyeji hao wa Malta walidhani ni adhabu kutoka kwa Mungu. a

20 Wenyeji waliomwona nyoka huyo akimuuma Paulo walifikiri “atavimba.” Kulingana na kitabu kimoja, neno la lugha ya awali linalotumiwa hapa ni “neno la kitiba.” Haishangazi kuona “Luka, daktari mpendwa” akitumia neno hilo katika masimulizi yake. (Mdo. 28:6; Kol. 4:14) Vyovyote vile, Paulo alimkung’uta nyoka huyo, naye hakupatwa na madhara yoyote.

21. (a) Ni habari gani hususa, au sahihi, tunazopata katika masimulizi ya Luka? (b) Paulo alifanya miujiza gani, nayo ilikuwa na matokeo gani kwa wenyeji wa Malta?

21 Publio, tajiri mwenye mashamba alikuwa akiishi katika eneo hilo. Huenda alikuwa mwakilishi mkuu wa Roma katika kisiwa cha Malta. Luka anamwita “mkuu wa kisiwa hicho,” akitumia jina la cheo linalopatikana katika vitabu viwili vya Kimalta. Aliwakaribisha Paulo na wenzake kwa siku tatu. Hata hivyo, baba ya Publio alikuwa mgonjwa. Kwa mara nyingine tena, Luka anafafanua hali yake kwa usahihi. Anataja ugonjwa hususa aliokuwa nao akisema kwamba “alikuwa amelala kitandani akiugua homa na ugonjwa wa kuhara damu.” Paulo alisali na kuweka mikono yake juu yake, naye akapona. Wakiwa wamevutiwa sana na muujiza huo, wenyeji wa kisiwa hicho wakaleta wagonjwa wengine waponywe, nao wakaleta zawadi kwa ajili ya mahitaji ya Paulo na wenzake.​—Mdo. 28:7-10.

22. (a) Profesa mmoja amesema nini kuhusu masimulizi ya Luka ya safari ya kwenda Roma? (b) Tutazungumzia nini katika sura inayofuata?

22 Habari kuhusu safari ya Paulo tuliyozungumzia kufikia sasa ni sahihi na kweli. Profesa mmoja alisema: “Masimulizi ya Luka . . . ni mojawapo ya masimulizi yaliyo wazi zaidi katika Biblia nzima. Mambo mbalimbali yanayotajwa kuhusu safari za baharini katika karne ya kwanza ni sahihi kabisa na hali zinazozungumziwa za upande wa mashariki wa Mediterania ni sahihi kabisa,” hivi kwamba lazima ziliandikwa kwa kutegemea daftari ya matukio ya kila siku ya mtu aliyekuwa katika safari hiyo. Yawezekana kwamba Luka alinakili mambo hayo alipokuwa akisafiri na mtume Paulo. Ikiwa alifanya hivyo, basi Luka alikuwa na mengi ya kuandika katika sehemu inayofuata ya safari hiyo. Paulo angepatwa na nini baada ya kufika Roma? Tutaona katika sura inayofuata.

a Kwa kuwa wenyeji waliwajua nyoka hao, yaonekana kwamba nyoka hao walikuwako katika kisiwa cha Malta nyakati hizo. Leo, hawapatikani huko. Huenda sababu ikawa kwamba kadiri ambavyo miaka imepita, kumekuwa na mabadiliko ya mazingira. Au nyoka hao waliisha kwa sababu ya ongezeko la watu kwenye kisiwa hicho.