Utangulizi
“Nililelewa katika kijiji kidogo katika mkoa wa kaskazini,” asimulia Dauda kutoka Sierra Leone. “Pindi moja, nilipokuwa mvulana, kulitokea mabishano juu ya shamba kati ya familia yangu na familia nyingine. Familia zote mbili zilidai kuwa shamba lile lile ni lao. Ili kumaliza jambo hilo, mganga wa kienyeji aliitwa. Alimpa mtu mwingine kioo, kisha akamfunika kwa kitambaa cheupe. Upesi mtu huyo aliyefunikwa kwa kitambaa akaanza kutetemeka na kutoa jasho. Huku akitazama katika kioo kile, alipaaza sauti: ‘Namwona mzee akikaribia! Amevaa mavazi meupe. Ni mrefu na ni mzee, ana mvi, naye atembea akiinama kidogo.’
“Alikuwa akimfafanua Babu! Ndipo akaanza kulia bila kuzuilika na kupaza sauti hivi: ‘Ikiwa hamwamini ninayosema, njooni mtazame nyinyi wenyewe!’ Bila shaka, hakuna yeyote kati yetu aliyekuwa na ujasiri wa kufanya hivyo! Mganga huyo wa kienyeji akamtuliza kwa kumnyunyizia mchanganyo wa kimizungu wenye majani na maji, alioushika mkononi ukiwa ndani ya kibuyu.
“Akinena kupitia kwa mtu huyo mwenye kioo, ‘Babu’ alisema shamba lilikuwa la familia yetu. Akamwambia nyanya (bibi) yangu kwamba anapaswa alime shamba hilo bila wasiwasi. Ile familia nyingine ikakubali hukumu hiyo. Suala hilo likamalizwa.”
Mambo kama hayo ni ya kawaida sehemu za Afrika ya Magharibi. Hapa, kama ilivyo katika sehemu nyingine za ulimwengu, mamilioni ya watu huamini kwamba wafu huendelea kuishi katika ulimwengu wa roho, ambako wanaweza kuona na kuwa na uvutano juu ya maisha ya watu duniani. Je, imani hiyo ni ya kweli? Je, wafu wako hai kweli? Ikiwa sivyo, ni nani hao ambao hudai kuwa roho za wafu? Kujua majibu sahihi ya maswali hayo ni jambo la muhimu sana. Ni jambo linalohusu uhai na kifo.