Sayari Yenye Uhai Tele
Hakungekuwa na uhai duniani ikiwa si kwa sababu ya “matukio” hususa, ambayo baadhi yake hayakujulikana au kueleweka vizuri mpaka katika karne ya 20. Matukio hayo yanatia ndani:
-
Mahali dunia ilipo katika kundi-nyota linaloitwa Kilimia na vilevile katika mfumo wa jua, hali kadhalika mzunguko wa dunia, mwinamo wake, mwendo wake inapozunguka, na mwezi wake usio wa kawaida
-
Ugasumaku na angahewa zinazoikinga dunia
-
Mizunguko ya asili ambayo husafisha na kurekebisha hewa na maji ya dunia
Unapotafakari kila moja kati ya mambo hayo, jiulize, ‘Je, yote hayo yalijitokeza yenyewe tu au yalibuniwa kwa kusudi fulani?’
“Anwani” Sahihi ya Dunia
Unapoandika anwani yako, unatia ndani habari gani? Huenda ukaandika jina la nchi, mji, au hata mtaa. Vivyo hivyo, tuseme kwamba kundi-nyota la Kilimia ndilo “nchi” ya dunia, nao mfumo wa jua—yaani, jua na sayari zinazolizunguka—ndio “mji” wa dunia, kisha mzunguko wa dunia katika mfumo wa jua tuuite “mtaa” wa dunia. Kwa sababu ya hatua ambazo zimepigwa katika ulimwengu wa kisayansi, wanasayansi wa leo wameweza kuelewa mengi sana kuhusu faida za dunia kuwa mahali pa pekee ilipo katika ulimwengu mzima.
Kwanza kabisa, “mji” wetu, yaani, mfumo wa jua, uko mahali panapofaa kabisa katika kundi-nyota la Kilimia—si karibu sana na kitovu wala mbali sana. Mahali hapo, au “eneo linalokalika,” kama wanasayansi fulani wanavyopaita, pana kiwango sahihi cha kemikali zinazohitajika ili kutegemeza uhai. Tungekuwa nje zaidi, kemikali hizo zingekuwa chache mno; na kama tungekaribia ndani zaidi, tungekuwa katika mazingira hatari kwa sababu ya miale hatari na mambo mengine. “Tunakaa eneo bora zaidi,” lasema gazeti Scientific American.1
“Mtaa” bora: “Mtaa” wa dunia katika “mji” wetu, yaani, mzunguko wetu katika mfumo wetu wa jua, ni mtaa “bora.” Ikiwa umbali wa kilomita milioni 150 kutoka kwenye jua, dunia inazunguka katika eneo bora kabisa, mahali ambapo viumbe vyenye uhai haviwezi kuganda kwa baridi wala kuteketea kwa moto. Isitoshe, kwa kuwa mzingo wa dunia ni karibu mviringo, kwa mwaka mzima tunabaki karibu umbali uleule kutoka kwenye jua.
Jua nalo ni “kiwanda bora cha umeme.” Linategemeka, lina ukubwa unaofaa, nalo huandaa kiasi cha kutosha cha nguvu zinazohitajiwa. Ndiyo sababu jua huitwa “nyota ya pekee sana.”2
“Jirani” mzuri kabisa: Ikiwa ungeombwa uchague “jirani” wa dunia, hungepata
jirani mzuri kuliko mwezi. Kipenyo chake ni robo moja hivi ya kipenyo cha dunia. Kwa hiyo, kwa kulinganishwa na miezi mingine katika mfumo wetu wa jua, mwezi unaozunguka dunia ni mkubwa isivyo kawaida kwa kulinganishwa na miezi inayozunguka sayari zingine. Je, imetokea hivyo kwa nasibu tu? Haielekei.Kwanza kabisa, mwezi ndio husababisha kujaa na kupwa kwa maji ya bahari, jambo ambalo ni muhimu sana katika mazingira ya dunia. Pia, mwezi huisaidia dunia kuzunguka katika mhimili wake pasipo kuyumbayumba. Pasipo mwezi wetu wa pekee, dunia ingeyumbayumba kama pia, huenda hata kupinduka juu chini! Hali ya hewa, kujaa na kupwa kwa bahari, na mabadiliko mengine yangesababisha madhara makubwa.
Mwinamo na mzunguko barabara wa dunia: Majira ya kila mwaka, hali-joto, na hali-hewa tofauti-tofauti hutegemea mwinamo wa dunia wa nyuzi 23.4 hivi. Kitabu kimoja chasema: “Yamkini mwinamo wa sayari yetu ni ‘barabara kabisa.’”—Rare Earth—Why Complex Life Is Uncommon in the Universe.3
Jambo jingine “barabara kabisa” ni urefu wa mchana na usiku, unaotegemea mzunguko wa dunia. Ikiwa dunia ingekuwa ikizunguka polepole kuliko inavyozunguka, siku zingekuwa ndefu zaidi nao upande wa dunia unaokabili jua ungeteketea huku upande wa pili ukiganda kwa baridi. Kwa upande mwingine, ikiwa dunia ingezunguka kasi kuliko inavyozunguka, siku zingekuwa fupi zaidi, zenye urefu wa saa chache tu, nao mzunguko huo wa kasi ungetokeza pepo zenye nguvu zinazovuma daima na kusababisha madhara makubwa.
Ngao za Dunia
Anga la nje ni mahali hatari penye miale na vimondo vingi. Hata hivyo, dunia yetu huonekana kana kwamba inasafiri katikati ya “uwanja wa kulenga-shabaha” bila kupatwa na madhara yoyote. Kwa nini? Kwa sababu dunia inalindwa na ngao ya ajabu—ugasumaku wenye nguvu na angahewa kabambe.
Ugasumaku wa dunia: Ndani katikati ya dunia kuna donge kubwa linalozunguka la chuma kilichoyeyuka. Hilo hutokeza ugasumaku mkubwa na wenye nguvu zinazofika anga la nje. Ngao hiyo hutulinda dhidi ya miale hatari kutoka katika anga la nje na pia dhidi ya nguvu hatari za jua. Nguvu hizo zinatia ndani chembechembe zenye nishati zinatoka kwenye jua kwa nguvu; miwako ya jua, ambayo kwa dakika chache hutokeza nguvu zinazoweza kulinganishwa na mabilioni ya mabomu ya hidrojeni;
mabilioni ya tani ya mata zinazotupwa angani kunapotokea milipuko katika kile kinachoonekana kama taji la nuru kulizunguka jua, kinachoitwa korona. Mara kwa mara uthibitisho wa ulinzi huo wa ugasumaku huonekana katika anga la juu karibu na ncha-sumaku za dunia, wakati ambapo miwako na milipuko katika korona inatokeza maonyesho yenye kupendeza ya rangi mbalimbali yanayoitwa orora.Angahewa la dunia: Mbali na kutuandalia hewa ya kupumua, blanketi inayotuzunguka ya gesi mbalimbali hutupa ulinzi. Tabaka la nje la angahewa, linaloitwa tabakastrato, lina oksijeni ya aina fulani inayoitwa ozoni, ambayo hufyonza asilimia 99 ya miale hatari ya urujuani. Kwa hiyo, tabaka la ozoni hulinda aina nyingi za viumbe—kutia ndani wanadamu na mimea ambayo hutokeza oksijeni tunayopumua—dhidi ya miale hatari. Kiwango cha ozoni kwenye tabakastrato hubadilika-badilika kulingana na ukali wa miale ya urujuani. Kubadilika-badilika huko huifanya kuwa ngao murua.
Angahewa hutulinda pia dhidi ya vifusi vinavyoanguka kila siku kutoka katika anga la nje—mamilioni ya vitu, vidogo kwa vikubwa. Vingi kati ya vitu hivyo, huteketea vinapoingia kwenye angahewa la dunia, vikitokeza nuru nyangavu inayoitwa vimondo. Wakati huohuo, ngao za dunia hazizuii miale ambayo ni muhimu kwa uhai, kama vile ile inayotokeza joto na nuru. Angahewa hutapanya vizuri joto duniani, na wakati wa usiku huhifadhi joto kama blanketi.
Angahewa na ugasumaku wa dunia kwa kweli ni vitu vya ajabu ambavyo bado havieleweki kikamili. Twaweza kusema vivyo hivyo kuhusu mizunguko inayotegemeza uhai duniani.
Je dunia yetu ilijikuta tu ikiwa na ngao mbili kabambe?
Mizunguko Inayotegemeza Uhai
Ikiwa nyumba ingekatiwa maji, madirisha yafungwe hivi kwamba hewa isiingie wala kutoka, na mifumo ya maji taka izibwe, muda si muda nyumba hiyo haingekalika. Lakini fikiria hili: Hivyo ndivyo dunia yetu ilivyo. Hatupati hewa na maji safi kutoka katika anga la nje, wala takataka zetu hazichukuliwi na kupelekwa katika anga la nje. Hivyo basi, dunia imewezaje kutegemeza uhai na kukalika kwa muda wote huo? Jibu ni: mizunguko yake, kama vile mizunguko ya maji, kaboni, oksijeni, na nitrojeni inayofafanuliwa na kuonyeshwa hapa kwa njia sahili.
Mzunguko wa maji: Maji ni muhimu kwa uhai. Pasipo maji, kila mmoja wetu angekufa baada ya siku chache. Mzunguko wa maji huandaa maji safi duniani pote. Mzunguko huo una hatua tatu. (1) Nguvu za jua huyainua maji hadi angani yakiwa mvuke. (2) Maji hayo safi yaliyotoneshwa hufanyiza mawingu. (3) Nayo mawingu, hutokeza mvua, mvua ya mawe, au theluji ambazo hunyesha, kisha huinuka tena zikiwa mvuke, na hivyo kukamilisha mzunguko wa maji. Ni kiasi gani cha maji kinachorejelezwa kila mwaka? Kulingana na makadirio, ni maji ya kutosha kufunika kila sehemu ya uso wa dunia kwa kina cha karibu mita moja.4
Mizunguko ya kaboni na oksijeni: Kama ujuavyo, ili kuendelea kuishi unahitaji kupumua, kutwaa oksijeni na kutoa kaboni dioksidi. Lakini kwa kuwa kuna mabilioni ya watu na wanyama wanaofanya vivyo hivyo, mbona angahewa letu haliishiwi na oksijeni na kulemewa na kiwango cha kaboni dioksidi? Jibu ni: mzunguko wa oksijeni. (1) Katika mchakato wa ajabu unaoitwa usanidimwanga, mimea hutwaa kaboni dioksidi tunayotoa na kuitumia pamoja na nguvu za nuru ya jua ili kutokeza kabohidrati na oksijeni. (2) Tunapopumua oksijeni, tunakamilisha mzunguko huo. Yote hayo hutendeka kwa njia safi, yenye ustadi, na kimyakimya.
Mzunguko wa nitrojeni: Uhai duniani hutegemea pia kutokezwa kwa molekuli mahuluku kama vile protini. (A) Ili kutokeza molekuli hizo, nitrojeni inahitajika. Jambo la kupendeza ni kwamba, asilimia 78 ya angahewa letu ni gesi ya nitrojeni. Radi huibadili nitrojeni kuwa mchanganyiko ambao mimea inaweza kufyonza. (B) Kisha mimea hutumia michanganyiko hiyo na kufanyiza molekuli mahuluku. Hivyo, wanyama wanaokula mimea hiyo hunufaika kutokana na nitrojeni hiyo. (C) Hatimaye, mimea na wanyama wanapokufa, michanganyiko ya nitrojeni humeng’enywa na bakteria. Mchakato huo wa kuoza huiachilia huru nitrojeni irudi kwenye udongo na angahewa, na hivyo kuukamilisha mzunguko.
Urejelezi Kamili!
Kila mwaka, wanadamu, pamoja na hatua za kitekinolojia ambazo wamepiga, hutokeza takataka zenye sumu zisizoweza kurejelezwa. Hata hivyo, dunia hurejeleza takataka zake zote kikamili, ikitumia uhandisi-kemikali wa kiwango cha juu sana.
Unafikiri mifumo ya urejelezi ya dunia ilitoka wapi? “Ikiwa kwa kweli mifumo ya ikolojia ya Dunia ilijitokeza yenyewe, haingeweza kufikia kiwango cha upatano kamili hivyo wa kimazingira,” asema M. A. Corey, mwandishi wa masuala ya kidini na sayansi.5 Je, unakubaliana na maoni yake?