Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 20

Muujiza wa Pili Huko Kana

Muujiza wa Pili Huko Kana

MARKO 1:14, 15 LUKA 4:14, 15 YOHANA 4:43-54

  • YESU AHUBIRI KWAMBA “UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA”

  • AMPONYA MVULANA AKIWA MBALI

Baada ya kukaa siku mbili Samaria, Yesu anaelekea kwenye eneo lake la nyumbani. Amekuwa na kazi nyingi ya kuhubiri huko Yudea, lakini harudi Galilaya ili kupumzika. Badala yake, anaanza huduma kubwa zaidi katika eneo alilolelewa. Hatazamii kupokewa vema huko, kwa sababu kama Yesu alivyosema, “nabii haheshimiwi katika nchi yake.” (Yohana 4:44) Badala ya kukaa pamoja naye, wanafunzi wake wanarudi nyumbani kwa familia zao na kazi zao za zamani.

Yesu anaanza kuhubiri ujumbe gani? Ujumbe huu: “Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na muwe na imani katika habari njema.” (Marko 1:15) Watu wanaitikiaje? Kwa kweli, Wagalilaya wengi wanampokea Yesu vizuri, na wanamheshimu. Hawafanyi hivyo kwa sababu tu ya ujumbe wake. Baadhi ya watu kutoka Galilaya walikuwa kwenye Pasaka huko Yerusalemu miezi kadhaa iliyopita na waliona miujiza ya kushangaza ambayo Yesu alifanya.—Yohana 2:23.

Yesu anaanzia wapi huduma yake kuu huko Galilaya? Inaonekana ni huko Kana, ambako pindi fulani aligeuza maji kuwa divai katika karamu ya harusi. Akiwa huko mara hii ya pili, Yesu anapata habari kwamba mvulana fulani ni mgonjwa sana, karibu kufa. Ni mwana wa ofisa wa serikali ya Herode Antipa, mfalme ambaye baadaye anaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa. Ofisa huyo anasikia kwamba Yesu ametoka Yudea na kuja Kana. Basi mwanamume huyo anasafiri kutoka nyumbani kwake huko Kapernaumu kwenda Kana ili kumtafuta Yesu. Ofisa huyo mwenye huzuni anamwomba hivi: “Bwana, twende kabla mwanangu hajafa.”—Yohana 4:49.

Yesu anajibu kwa maneno ambayo lazima yanamshtua mwanamume huyo: “Rudi nyumbani; mwanao yuko hai.” (Yohana 4:50) Ofisa wa Herode anamwamini Yesu na anaanza safari ya kurudi nyumbani. Akiwa njiani anakutana na watumwa wake, ambao wameharakisha kuja kumwambia habari njema. Naam, mwanawe yuko hai na amepona! ‘Alipata nafuu wakati gani?’ anawauliza, huku akijaribu kuunganisha matukio.

“Alipona homa jana saa saba,” wanajibu.—Yohana 4:52.

Yule ofisa anatambua kwamba huo ndio wakati hasa ambao Yesu alisema, “Mwanao yuko hai.” Baada ya hapo, mwanamume huyo, ambaye ni tajiri hivi kwamba ana watumwa, yeye pamoja na nyumba yake yote wanakuwa wanafunzi wa Kristo.

Kwa hiyo Yesu anafanya miujiza mara mbili huko Kana, kugeuza maji kuwa divai na baadaye kumponya mvulana akiwa umbali wa kilomita 26. Bila shaka, anafanya miujiza mingine pia. Lakini muujiza huu wa kuponya ni muhimu kwa sababu unaonyesha kwamba amerudi Galilaya. Kwa kweli yeye ni nabii anayekubaliwa na Mungu, lakini nabii huyu ‘ataheshimiwa kwa kadiri gani katika nchi yake’?

Hilo litaonekana wazi Yesu anapoelekea nyumbani huko Nazareti. Ni nini kinachomsubiri huko?