Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 73

Msamaria Athibitika Kuwa Jirani wa Kweli

Msamaria Athibitika Kuwa Jirani wa Kweli

LUKA 10:25-37

  • JINSI YA KUURITHI UZIMA WA MILELE

  • MSAMARIA MWENYE UJIRANI

Yesu akiwa bado karibu na Yerusalemu, baadhi ya Wayahudi wanakuja kuzungumza naye. Baadhi yao wanataka kujifunza kutoka kwake, wengine wanataka kumjaribu. Mmoja wao aliye na ujuzi wa Sheria, anauliza swali hili: “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”—Luka 10:25.

Yesu anatambua kwamba lengo la mtu huyo si kujifunza. Huenda anajaribu kumfanya Yesu ajibu kwa njia itakayowakasirisha Wayahudi. Yesu anatambua kwamba tayari mtu huyo ana maoni fulani hususa. Basi, kwa hekima anajibu kwa njia inayomfanya mtu huyo afunue kile anachofikiria.

Yesu anamuuliza: “Ni mambo gani yameandikwa katika Sheria? Wewe unasomaje?” Mtu huyo ameisoma Sheria ya Mungu, basi jibu lake linategemea Sheria. Ananukuu andiko la Kumbukumbu la Torati 6:5 na Mambo ya Walawi 19:18, na kusema: “‘Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote kwa nafsi yako yote kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote’ na ‘umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’” (Luka 10: 26, 27) Je, hilo ndilo jibu sahihi?

Yesu anamwambia mtu huyo: “Umejibu vizuri; endelea kufanya hivyo nawe utapata uzima.” Lakini je, mazungumzo yanaishia hapo? Mtu huyo hataki tu majibu ya kawaida; anataka “kujionyesha kuwa mwadilifu,” na kuthibitishiwa kwamba maoni yake ni sahihi na hivyo anawatendea wengine kwa njia inayofaa. Basi anauliza: “Kwa kweli, jirani yangu ni nani?” (Luka 10:28, 29) Swali hilo linaloonekana kuwa rahisi lina maana kubwa. Jinsi gani?

Wayahudi wanaamini kwamba neno “jirani” linawahusu tu wale wanaofuata desturi za Wayahudi, na huenda ikaonekana kwamba andiko la Mambo ya Walawi 19:18 linaunga mkono jambo hilo. Kwa kweli, Myahudi anaweza kudai kwamba ni “kinyume cha sheria” kushirikiana na mtu asiye Myahudi. (Matendo 10:28) Basi mtu huyu na labda baadhi ya wanafunzi wa Yesu wanajiona kuwa waadilifu ikiwa wanawatendea Wayahudi wenzao kwa fadhili. Lakini wanaweza kumtendea bila fadhili mtu asiye Myahudi; yeye si “jirani.”

Yesu anawezaje kusahihisha maoni hayo bila kumuudhi mtu huyo na Wayahudi wengine? Anafanya hivyo kwa kusimulia hadithi: “Mtu fulani alikuwa akishuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko akavamiwa na wezi, wakamvua nguo, wakampiga, kisha wakamwacha akiwa karibu kufa.” Yesu anaendelea: “Ikatukia kwamba kuhani fulani alikuwa akishuka katika barabara hiyo, lakini alipomwona yule mtu akapita upande mwingine wa barabara. Vivyo hivyo, Mlawi alipofika mahali hapo na kumwona, akapita upande mwingine wa barabara. Lakini Msamaria fulani aliyekuwa akisafiri kwenye barabara hiyo alipomwona, akamsikitikia.”—Luka 10:30-33.

Bila shaka mtu ambaye Yesu anamsimulia hadithi hii anajua kwamba makuhani wengi na Walawi wanaosaidia hekaluni huishi Yeriko. Wanaporudi kutoka hekaluni, wanateremka kwenye barabara yenye urefu wa kilomita 23. Barabara hiyo ni hatari, kwa sababu ina wezi. Kuhani na Mlawi wakimkuta Myahudi mwenzao ambaye anahitaji msaada, je, hawapaswi kumsaidia? Katika hadithi hii, Yesu anasema kwamba hawakumsaidia. Alisaidiwa na Msamaria, mtu wa jamii inayodharauliwa na Wayahudi.—Yohana 8:48.

Yule Msamaria alimsaidiaje Myahudi aliyejeruhiwa? Yesu anaendelea kusimulia: “Akamkaribia akayamwagia majeraha yake mafuta na divai, kisha akayafunga. Akampandisha kwenye punda wake akampeleka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. Siku iliyofuata akamlipa msimamizi wa nyumba hiyo dinari mbili, akamwambia: ‘Mtunze, nami nitakulipa gharama zozote za ziada nitakaporudi.’”—Luka 10:34, 35.

Baada ya Mwalimu Mkuu, Yesu, kusimulia hadithi hiyo, anamuuliza yule mtu swali hili linalochochea fikira: “Kati ya watu hao watatu, unafikiri ni nani aliyekuwa jirani ya mtu aliyevamiwa na wezi?” Labda yule mtu anaona vigumu kujibu “ni Msamaria,” basi anajibu: “Ni yule aliyemtendea kwa rehema.” Kisha Yesu anaweka wazi jambo kuu la hadithi hiyo, kwa kumsihi: “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”—Luka 10:36, 37.

Hiyo ni njia ya kufundisha yenye matokeo sana! Ikiwa Yesu angemwambia tu mtu huyo kwamba pia watu wasio Wayahudi ni jirani zake, je, mtu huyo na Wayahudi wengine waliokuwa wakisikiliza wangekubali? Huenda hawangekubali. Hata hivyo, kwa kusimulia hadithi fupi, akitumia habari ambazo wasikilizaji wanazifahamu, jibu la swali “Kwa kweli, jirani yangu ni nani?” limekuwa wazi. Mtu anayethibitika kuwa jirani wa kweli ni yule anayeonyesha upendo na fadhili kama Maandiko yanavyotuagiza tufanye.