SURA YA 81
Yesu na Baba Ni Kitu Kimoja, Lakini Yeye Si Mungu
-
“MIMI NA BABA NI KITU KIMOJA”
-
YESU APINGA MADAI KWAMBA YEYE NI MUNGU
Yesu amekuja Yerusalemu kwa ajili ya Sherehe ya Wakfu (au Hanuka). Sherehe hiyo ni ya kukumbuka kuwekwa wakfu tena kwa hekalu. Zaidi ya karne moja mapema, Mfalme Msiria Antioko wa Nne Epifane, alijenga madhabahu juu ya madhabahu kuu katika hekalu la Mungu. Baadaye, wana wa kuhani Myahudi walikomboa Yerusalemu na kuliweka wakfu tena hekalu kwa Yehova. Tangu wakati huo, kila mwaka sherehe hufanywa tarehe 25 ya Kislevu, mwezi unaolingana na mwishoni mwa Novemba na mwanzoni mwa Desemba.
Ni majira ya baridi kali. Yesu anatembea hekaluni katika safu ya nguzo za Sulemani. Akiwa hapo, Wayahudi wanamzunguka na kumuuliza: “Utaendelea kutuhangaisha mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, tuambie waziwazi.” (Yohana 10:22-24) Yesu atawajibuje? Anawaambia hivi: “Niliwaambia, na bado hamwamini.” Yesu hajawaambia moja kwa moja kwamba yeye ndiye Kristo, kama alivyomwambia mwanamke Msamaria kwenye kisima. (Yohana 4:25, 26) Hata hivyo, amefunua yeye ni nani aliposema: “Mimi nimekuwapo kabla Abrahamu hajakuwapo.”—Yohana 8:58.
Yesu anataka watu wajiamulie wenyewe kwamba yeye ndiye Kristo kwa kulinganisha mambo anayofanya na mambo yaliyotabiriwa kwamba yangefanywa na Kristo. Ndiyo sababu nyakati nyingine aliwaambia wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Masihi. Lakini sasa anawaambia moja kwa moja Wayahudi hao wenye chuki: “Kazi ninazofanya katika jina la Baba yangu, zinatoa ushahidi kunihusu. Lakini hamwamini.”—Yohana 10:25, 26.
Kwa nini hawaamini kwamba Yesu ndiye Kristo? Yesu anasema: “Hamwamini, kwa sababu ninyi si kondoo wangu. Kondoo wangu husikiliza sauti yangu, nami ninawajua, nao hunifuata. Mimi ninawapa uzima wa milele, nao hawataharibiwa kamwe, wala hakuna atakayewanyakua kutoka mkononi mwangu. Kile ambacho Baba yangu amenipa ni chenye thamani kuliko vitu vingine vyote.” Kisha Yesu anawaambia jinsi alivyo na uhusiano wa karibu pamoja na Baba yake, anaposema: “Mimi na Baba ni kitu kimoja.” (Yohana 10:26-30) Yesu yuko hapa duniani na Baba yake yuko mbinguni, basi hamaanishi kwamba kihalisi yeye na Baba yake ni kitu kimoja. Badala yake wana kusudi moja, wana muungano.
Wayahudi wanakasirishwa sana na maneno ya Yesu, hivi kwamba wanaokota mawe ili wamuue. Lakini jambo hilo halimwogopeshi Yesu. Anawauliza: “Niliwaonyesha kazi nyingi nzuri kutoka kwa Baba. Kati ya kazi hizo, ni ipi inayofanya mtake kunipiga mawe?” Wanamjibu hivi: “Tunakupiga mawe, si kwa sababu ya kazi njema, bali umekufuru; kwa maana . . . wewe . . . unajifanya mungu.” (Yohana 10:31-33) Yesu hajawahi kamwe kudai kwamba yeye ni mungu, basi kwa nini wanaleta shtaka hilo?
Yesu anasema kwamba ana nguvu ambazo Wayahudi wanaamini ni za Mungu peke yake. Kwa mfano, kuhusu “kondoo” alisema hivi: “Mimi ninawapa uzima wa milele,” jambo ambalo wanadamu hawawezi kufanya. (Yohana 10:28) Wayahudi hawazingatii kuwa Yesu amekiri waziwazi kwamba alipokea mamlaka kutoka kwa Baba yake.
Akipinga shtaka lao la uwongo, Yesu anauliza: “Je, haijaandikwa katika Sheria yenu [kwenye Zaburi 82:6], ‘Mimi nilisema: “Ninyi ni miungu”’? Ikiwa aliwaita ‘miungu’ wale ambao neno la Mungu lilikuja dhidi yao . . . je, mnaniambia mimi ambaye Baba alinitakasa na kunituma ulimwenguni, ‘Unakufuru,’ kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’?”—Yohana 10:34-36.
Naam, Maandiko yanawaita hata mahakimu wa kibinadamu wasio na haki, “miungu.” Basi Wayahudi hawa wanawezaje kumlaumu Yesu anaposema “Mimi ni Mwana wa Mungu”? Anataja jambo ambalo linapaswa kuwasadikisha: “Kama sifanyi kazi za Baba yangu, msiniamini. Lakini ikiwa ninazifanya, hata ingawa hamniamini mimi, basi iweni na imani katika kazi hizo, ili mjue na kuendelea kujua kwamba Baba yuko katika muungano nami, nami niko katika muungano na Baba.”—Yohana 10:37, 38.
Wayahudi wanaposikia maneno hayo, wanajaribu kumkamata Yesu lakini anaponyoka tena. Anaondoka Yerusalemu na kuvuka Mto Yordani na kwenda eneo ambalo Yohana alianza kuwabatiza watu miaka minne iliyopita. Inaonekana eneo hilo haliko mbali na mahali ambapo Bahari ya Galilaya inaishia upande wa kusini.
Umati unamjia Yesu na kusema: “Yohana hakufanya ishara hata moja, lakini mambo yote aliyosema kumhusu mtu huyu yalikuwa ya kweli.” (Yohana 10:41) Basi Wayahudi wengi wanamwamini Yesu.