Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 15

Afanya Muujiza Wake wa Kwanza

Afanya Muujiza Wake wa Kwanza

YOHANA 2:1-12

  • HARUSI HUKO KANA

  • YESU ABADILI MAJI KUWA DIVAI

Siku tatu zimepita tangu Nathanaeli awe kati ya wanafunzi wa kwanza wa Yesu. Yesu na baadhi ya wanafunzi hao wa kwanza wanaelekea kaskazini kwenye wilaya ya Galilaya, eneo lao la nyumbani. Wanaenda katika mji wa Kana, mji alikozaliwa Nathanaeli. Mji wa Kana uko milimani, upande wa kaskazini wa Nazareti, ambako Yesu alilelewa. Wamealikwa kwenye karamu ya harusi huko Kana.

Mama ya Yesu amekuja pia kwenye harusi. Akiwa rafiki wa familia ya wale wanaofunga ndoa, inaonekana Maria anasaidia kuwahudumia wageni wengi waliopo. Basi anatambua haraka kwamba kuna upungufu, naye anamwambia Yesu: “Hawana divai.”—Yohana 2:3.

Ni wazi, Maria anadokeza kwamba Yesu afanye jambo fulani kuhusu upungufu huo wa divai. Akitumia msemo unaoonyesha kwamba anakataa, Yesu anamjibu: “Mwanamke, jambo hilo linatuhusuje mimi na wewe?” (Yohana 2:4) Akiwa Mfalme aliyechaguliwa na Mungu, matendo ya Yesu yanaongozwa na Baba yake wa mbinguni, bali si familia au marafiki. Kwa hekima Maria anaacha mambo mikononi mwa mwanawe, na anawaambia hivi wale wanaohudumu: “Fanyeni lolote atakalowaambia.”—Yohana 2:5.

Kuna mitungi sita ya maji, na kila mmoja una uwezo wa kubeba zaidi ya lita 40. Yesu anawaagiza wahudumu: “Ijazeni mitungi hiyo maji.” Kisha Yesu anawaambia: “Choteni kidogo na kumpelekea msimamizi wa karamu.”—Yohana 2:7, 8.

Msimamizi anafurahishwa na ubora wa divai hiyo lakini hana habari kwamba imeandaliwa kimuujiza. Anamwita bwana harusi na kumwambia: “Kila mtu hutoa divai nzuri kwanza, kisha hutoa divai hafifu wakati ambapo watu wameingiwa na kileo. Lakini wewe umehifadhi divai nzuri mpaka sasa.”—Yohana 2:10.

Huu ndio muujiza wa kwanza ambao Yesu anafanya. Wanafunzi wake wapya wanapoona muujiza huo, imani yao inaimarishwa. Baadaye, Yesu, mama yake, na ndugu zake wa kambo wanasafiri hadi mji wa Kapernaumu ulio kwenye ufuo wa kaskazini magharibi wa Bahari ya Galilaya.