Ishara ya Watchtower—Imeonekana Brooklyn kwa Miaka Mingi
Kwa zaidi ya miaka 40, ishara hiyo yenye maneno mekundu yenye kimo cha futi 4.6 iliyotundikwa juu ya makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova imekuwa jambo la kawaida kwa wakazi wa New York City, wengi wao hutazama ishara hiyo iliyo na saa ili kujua saa na kipimo cha joto.
Eboni, ambaye anaweza kuona ishara hiyo akiwa chumbani kwake huko Brooklyn, alisema hivi: “Inafurahisha kutazama nje ya dirisha ili kujua saa na kipimo cha joto kabla sijaenda kazini. Ishara hiyo hunisaidia kutunza wakati na kuvalia kulingana na hali ya hewa.”
Je, ishara hiyo iliyo na saa na kipima-joto itaendelea kuwapo kwa miaka mingine 40? Huenda isiwepo. Kwa kuwa kuna mipango ya kuhamisha makao makuu ya ulimwenguni pote ya Mashahidi wa Yehova hadi sehemu ya kaskazini ya New York, wale watakaonunua jengo hilo wataamua ikiwa wataiacha ishara hiyo au la.
Miaka 70 iliyopita, kulikuwa na ishara iliyowekwa na wamiliki wa jengo hilo. Baada ya kununua jengo hilo katika mwaka wa 1969, Mashahidi wa Yehova waliibadili na ikawa ishara ya Watchtower ambayo ipo hadi leo.
Ishara hiyo inahitaji kukarabatiwa mara mwa mara. Kadiri miaka imepita, vijana wengi wameifanyia ukarabati uliohitajiwa wakati wowote ule, iwe mchana au usiku.
Mwanamume mmoja aliyekuwa akifanya kazi usiku anakumbuka tukio hili: “Jioni mmoja, tulipokea simu kutoka kwa mkurugenzi wa habari wa kituo fulani cha televisheni. Alituarifu kwamba saa iliyokuwa kwenye ishara hiyo ilikuwa si sahihi kwa sekunde 15. Alitaka tuirekebishe ili aweze kuionyesha katika kipindi chake usiku huo. Mara moja, fundi aliyekuwa bado na usingizi alianza kurekebisha tatizo hilo.”
Ili ifanye kazi kwa njia nzuri na kwa usahihi, ishara hiyo imefanyiwa mabadiliko mara kadhaa. Katikati ya miaka ya 1980, sehemu ya kuonyesha kipimo cha joto ilibadilishwa ili kuonyesha vipimo vya Selsiasi na Farenhaiti.
Katika mwaka wa 2009, balbu za ishara hiyo ambazo hazikuwa na mwangaza wa kutosha ziliondolewa na nyingine zenye mwangaza kwa kutosha zikawekwa. Balbu hizo zilipunguza gharama ya ukarabati kwa dola 4,000 (za Marekani) kwa mwaka. Leo, ishara hiyo hutumia kiwango kidogo sana cha umeme ikilinganishwa na zamani.