Upendo Unatuchochea Kusaidia Majanga Yanapotokea
Wakati wa shida, Mashahidi wa Yehova huwasaidia waamini wenzao na watu wengine pia. Wanafanya hivyo kwa sababu ya upendo, alama inayowatambulisha Wakristo wa kweli.—Yohana 13:35.
Ifuatayo ni orodha ndogo ya misaada iliyotolewa katika kipindi cha miezi 12 iliyoishia katikati ya mwaka 2012. Orodha hiyo haitii ndani utegemezo wa kiroho na kihisia ambao kwa kawaida hutolewa wakati wa kutoa misaada. Halmashauri za Kutoa Misaada zilizowekwa rasmi na ofisi za tawi ziliandaa msaada wote uliotolewa. Kuongezea hilo, makutaniko yalisaidia kutoa misaada hiyo.
Japani: Mnamo Machi 11, 2011, tetemeko la ardhi ambalo hatimaye lilisababisha tsunami iliyowaathiri watu wengi sana lilitokea katika eneo la kaskazini ya Japani. Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote walitoa michango mingi ya kifedha, mali, na walitumia maarifa ya ujenzi waliyonayo ili kusaidia kujenga upya majengo yaliyobomolewa na tsunami. Angalia video yetu kuhusu shughuli za kutoa msaada baada ya tetemeko la ardhi nchini Japani.
Brazili: Mafuriko, maporomoko ya ardhi, na matope yalisababisha vifo vya mamia ya watu. Ili kukabiliana na hali hiyo, Mashahidi wa Yehova walituma katika miji iliyoathirika tani 42 za chakula, chupa 20,000 za maji, tani 10 za nguo, na tani 5 za vifaa vya kufanyia usafi, na pia dawa na vitu vingine.
Kongo (Brazzaville): Wakati ghala la kuhifadhia silaha lilipolipuka, nyumba 4 za Mashahidi wa Yehova zilibomolewa na nyumba nyingine 28 za Mashahidi ziliharibiwa. Wale walioathiriwa walipewa chakula na nguo, na Mashahidi wa eneo hilo waliwapa mahali pa kukaa wale walioathiriwa na janga hilo.
Kongo (Kinshasa): Waathirika wa kipindupindu walipewa dawa. Wale walioathiriwa na mvua kubwa walipewa nguo. Wale walio katika kambi za wakimbizi walipewa msaada wa matibabu, mbegu za kupanda, na tani moja ya nguo.
Venezuela: Mvua kubwa ilisababisha mafuriko na maporomoko ya matope. Halmashauri za kutoa misaada ziliwasaidia Mashahidi 288 walioathiriwa. Nyumba mpya zaidi ya 50 zilijengwa. Zaidi ya hayo, halmashauri za kutoa misaada zinawasaidia wale ambao nyumba zao ziko karibu kuzama kwa sababu ya kuongezeka kwa maji ya Ziwa Valencia.
Filipino: Kimbunga kilisababisha mafuriko katika sehemu fulani za nchi. Ofisi ya tawi ilituma vyakula, na Mashahidi wa eneo hilo walifanya kazi ya kusafisha baada ya maji kupungua.
Kanada: Kufuatia moto mkubwa uliowaka msituni jijini Alberta, Kutaniko la Slave Lake lilipokea mchango mkubwa kutoka kwa Mashahidi katika eneo hilo ili kuwasaidia kusafisha. Kwa sababu hawakuhitaji kiasi hicho kikubwa cha pesa, kutaniko lilichangia zaidi ya nusu ya mchango waliopokea ili kuwasaidia waathirika wengine wa majanga mahali pengine duniani.
Côte d’Ivoire: Wale waliohitaji msaada walipewa vitu walivyohitaji, mahali pa kulala, na dawa kabla, wakati, na baada ya vita vilivyotokea nchini Côte d’Ivoire.
Fiji: Kwa sababu ya mafuriko mabaya zaidi yaliyosababishwa na mvua kubwa, karibu familia192 za Mashahidi wa Yehova zilipoteza mashamba yao, ambayo ndiyo chanzo chao cha chakula na mapato. Mashahidi hao walipewa msaada wa chakula.
Ghana: Watu walioathiriwa na mafuriko katika eneo la mashariki mwa nchi walipewa chakula, mbegu, na makazi ya muda.
Marekani: Vimbunga viliharibu kidogo nyumba 66 za Mashahidi wa Yehova katika majimbo matatu na kuharibu kabisa nyumba 12 za Mashahidi. Hata hivyo, wengi wa wamiliki wa nyumba hizo walikuwa na bima, hivyo walipewa pesa ili kuwasaidia wajenge nyumba zao tena.
Argentina: Mashahidi wa Yehova waliwasaidia watu wanaoishi kusini mwa Argentina, wote ambao majivu ya volkano yaliharibu kwa kiasi fulani nyumba zao.
Msumbiji: Zaidi ya watu 1,000 waliokumbwa na ukame walipewa chakula.
Nigeria: Mashahidi wa Yehova 24 ambao walijeruhiwa katika ajali mbaya sana walipewa msaada wa pesa. Pia, msaada ulitolewa kwa watu wengi wanaoishi kaskazini mwa Nigeria, ambao waliachwa bila makao kwa sababu ya mapigano ya kidini na kikabila.
Benin: Watu waliokumbwa na mafuriko mabaya sana walipewa dawa, mavazi, vyandarua, maji safi, na mahali pa kulala.
Jamhuri ya Dominika: Baada ya kukumbwa na kimbunga Irene, Mashahidi wa Yehova walisaidia kurekebisha nyumba na mahitaji mengine ya kimwili.
Ethiopia: Watu wanaoishi katika maeneo mawili yenye ukame na eneo moja linalokumbwa na mafuriko, walisaidiwa pesa ili kukidhi mahitaji yao.
Kenya: Watu waliokumbwa na ukame walipewa msaada wa pesa.
Malawi: Watu wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Dzaleka walipewa msaada.
Nepal: Maporomoko ya ardhi yaliiharibu vibaya nyumba ya Shahidi mmoja. Shahidi huyo alipewa nyumba ya muda na kisha kusaidiwa na kutaniko lake.
Papua New Guinea: Watu fulani waliteketeza nyumba nane za Mashahidi. Mipango ilifanywa ili nyumba hizo zijengwe upya.
Romania: Baadhi ya Mashahidi walipoteza nyumba zao kwa sababu ya mafuriko. Msaada ulitolewa ili waweze kuzijenga upya.
Mali: Michango ilitolewa kutoka nchi jirani ya Senegal kwa ajili ya watu waliokuwa na tatizo la chakula kwa sababu ya mavuno mabaya yaliyosababishwa na ukame.
Sierra Leone: Madaktari ambao ni Mashahidi kutoka nchini Ufaransa waliwatibu Mashahidi wa Yehova ambao zamani waliishi katika maeneo yaliyokumbwa na vita.
Thailand: Mafuriko mabaya sana yalisababisha uharibifu mkubwa katika majimbo kadhaa. Timu za kutoa msaada zilikarabati na kusafisha nyumba 100 na Majumba ya Ufalme 6.
Jamhuri ya Cheki: Baada ya mafuriko kuharibu nyumba kadhaa nchini Jamhuri ya Cheki, Mashahidi kutoka nchi jirani ya Slovakia walisaidia katika shughuli za kutoa msaada.
Sri Lanka: Sehemu kubwa ya kazi ya kutoa msaada katika maeneo yaliyokumbwa na tsunami imekamilika.
Sudan: Mashahidi wa Yehova ambao walilazimika kuhama makazi yao kwa sababu ya mapigano nchini Sudan walitumiwa chakula, nguo, viatu, na makaratasi ya plastiki.
Tanzania: Familia 14 zilipoteza mali zao mafuriko makubwa yalipotokea. Mashahidi wa Yehova katika maeneo hayo walichangia nguo na vyombo vya nyumbani. Nyumba moja ilijengwa upya.
Zimbabwe: Ukame umesababisha eneo fulani nchini Zimbabwe likumbwe na njaa. Watu walioathiriwa wamepewa chakula na pesa.
Burundi: Wakimbizi wamepewa msaada unaotia ndani matibabu.