Hamia kwenye habari

Vijana Wasaidiwa Kukabiliana na Unyanyasaji Shuleni

Vijana Wasaidiwa Kukabiliana na Unyanyasaji Shuleni

Hivi karibuni, Hugo, mwenye umri wa miaka kumi, alipokea Tuzo ya Diana kutoka kwenye shirika la kutoa msaada la Uingereza kwa kuwasaidia wanafunzi wenzake shuleni kukabiliana na unyanyasaji.

Hugo alisema hivi: “Nimepata tuzo hii kwa sababu nilitazama video ya vibonzo kwenye ubao inayoitwa Mshinde Mnyanyasaji Bila Kutumia Ngumi. Nilifaulu kuwasaidia wanafunzi wenzangu kukabiliana na unyanyasaji kwa sababu ya yale niliyojifunza kutoka kwenye video hiyo inayopatikana kwenye tovuti ya jw.org.”

“Kila siku, watoto hunyanyaswa ulimwenguni pote . . . , lakini . . . unaweza kumshinda mnyanyasaji bila kutumia ngumi.” (Maelezo mafupi kutoka video Mshinde Mnyanyasaji Bila Kutumia Ngumi)

Hugo aliwaonyesha walimu wake video hiyo ya Mshinde Mnyanyasaji. Kwa kuwa walifurahia kuitazama, walifanya mpango tovuti ya jw.org ipatikane kwa wanafunzi wote. Wanafunzi wengi wenye umri wa kati ya miaka minane na kumi kwenye shule ya Hugo sasa wanatumia kwa ukawaida tovuti ya jw.org. Wanasema tovuti hiyo imewasaidia kukabiliana na matatizo ya kunyanyaswa na pia kujibu maswali kama, Nawezaje kupata marafiki wa kweli?

Hatua Zinazofaa Zawafaidi Vijana

Katika shule nyingine huko Uingereza, Elijah, mwenye umri wa miaka nane alikuwa akinyanyaswa. Yeye na familia yake walitazama video ya Mshinde Mnyanyasaji. Walifanya mazoezi pamoja kuhusu jambo la kusema na la kufanya anaponyanyaswa. Hilo lilimpa Elijah uhakika wa kushughulika na tatizo hilo kwa mafanikio. Baadaye, wakati wa juma la kupinga unyanyasaji, mwalimu mkuu wa shule ya Elijah aliwaonyesha wanafunzi wote video hiyo.

Unyanyasaji ni tatizo la ulimwenguni pote, si nchini Uingereza tu, na video hiyo ya vibonzo kwenye ubao inawasaidia vijana kila mahali.

Nchini Marekani, Ivie, mwenye umri wa miaka kumi, alimwogopa mwanafunzi mwenzake ambaye alimnyanyasa. Baada ya kutazama video ya Mshinde Mnyanyasaji, Ivie alipata ujasiri wa kumkabili msichana huyo. Alizungumza na mwalimu wake pia, ambaye alimsaidia. Mwanafunzi huyo aliomba msamaha, na sasa yeye na Ivie wana uhusiano mzuri.

Mashahidi wa Yehova wanahangaikia hali nzuri ya vijana. Tutaendelea kuchapisha mashauri yanayofaa ili kuwasaidia kukabiliana na matatizo ya kila siku kama unyanyasaji.