Hamia kwenye habari

Mnara wa Mlinzi—Gazeti Lisilo na Kifani

Mnara wa Mlinzi—Gazeti Lisilo na Kifani

Gazeti la Mnara wa Mlinzi linasambazwa kwa wingi zaidi kuliko gazeti lingine lolote ulimwenguni. Nakala zaidi ya 42,000,000 za kila toleo huchapishwa. Gazeti la Amkeni! ni la pili, nakala 41,000,000 za kila toleo huchapishwa. Magazeti hayo mawili huchapishwa na Mashahidi wa Yehova nayo husambazwa katika nchi 236.

Vipi magazeti mengine? Kulingana na The Association of Magazine Media, gazeti la Marekani linaloongoza kwa mauzo huchapishwa na AARP, shirika linalowalenga watu wenye umri wa miaka zaidi ya 50. Nakala zaidi ya 22,400,000 za gazeti hilo husambazwa. Nakala 14,000,000 hivi za gazeti la ADAC Motorwelt la Ujerumani husambazwa, na nakala 5,400,000 za gazeti Gushi Hui (hadithi) la China huchapishwa.

Kuhusu magazeti ya habari, Yomiuri Shimbun la Japan ndilo linaloongoza. Kwa kawaida nakala zaidi ya 10,000,000 huchapishwa.

Pia, machapisho ya Mashahidi wa Yehova yanatia fora katika tafsiri. Gazeti la Mnara wa Mlinzi linatafsiriwa katika lugha zaidi ya 190, nalo gazeti la Amkeni! linatafsiriwa katika lugha zaidi ya 80. Kwa kulinganishwa, Reader’s Digest huchapishwa katika lugha 21, ingawa habari zilizomo hutofautiana ikitegemea nchi.

Tofauti na magazeti mengine yaliyotajwa hapa, Mnara wa Mlinzi na Amkeni! hugharimiwa kwa michango ya hiari, hayana matangazo ya biashara, wala hayauzwi.

Kusudi la Mnara wa Mlinzi ni kufafanua mafundisho ya Biblia, hasa kuhusu Ufalme wa Mungu. Limekuwa likichapishwa tangu mwaka wa 1879. Amkeni! huzungumzia mambo mbalimbali, kama vile mimea au viumbe na sayansi, lengo likiwa kuwasaidia watu wamwamini Muumba. Pia, hukazia jinsi Biblia inavyoweza kutusaidia maishani leo.